Mojawapo ya Jukumu la Jeshi la Magereza ni kuwapeleka mahakamani mahabusu na kuwarudisha magerezani.

Gadi ya askari Wanawake na Wanaume wa Jeshi la Magereza katika Maadhimisho ya Sherehe za Kitaifa.

Ng'ombe bora wa Nyama na Maziwa ni sehemu ya miradi ya Uzalishaji inayoendeshwa na kusimamiwa na Jeshi la Magereza nchini.

Sehemu ya Mashamba makubwa yanayoendeshwa na Jeshi la Magereza: Shughuli za Kilimo cha Mashamba makubwa, madogo na bustani za mboga mboga ni moja ya shughuli za Magereza katika kuwafunza wafungwa namna ya kujitegemea mara wamalizapo vifungo vyao.

Baadhi wa wafungwa katika Kiwanda cha Ushonaji nguo cha Gereza Kuu Ukonga wakiwa kazini: Shughuli za Ushonaji wa nguo ni moja ya eneo ambalo wafungwa hupata huduma za urekebishwaji kwa vitendo.

Thursday, December 31, 2015

Kamishna Jenerali wa Magereza nchini asisitiza utendaji kazi wenye tija

Kamishna Jenerali wa Magereza Nchini, John Casmir Minja akitoa hotuba kwa Watumishi wa Jeshi la Magereza(hawapo pichani) kwenye Baraza la kufunga Mwaka 2015 na kuukaribisha Mwaka mpya 2016. Baraza hilo limefanyika Desemba 31, 2015 katika Ofisi za Makao Makuu ya Jeshi la Magereza, Jijini Dar es Salaam.
Askari wa vyeo mbalimbali wa Jeshi la Magereza wakimsikiliza Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza wakati akitoa hotuba yake kwenye Baraza la kufunga Mwaka 2015 na kuukaribisha Mwaka mpya wa 2016.
Maafisa Waandamizi wa Jeshi la Magereza wakiwa timamu kumpokea Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza, John Casmir Minja(hayupo pichani) wakati akiwasili tayari kwa kulihutubia Baraza la kufunga Mwaka 2015 na kuukaribisha Mwaka mpya wa 2016.
Maafisa ngazi ya juu wa Jeshi la Magereza wakifuatilia kwa makini hotuba fupi aliyoitoa Kamishna Jenerali wa Magereza, John Casmir Minja.


Na Lucas Mboje, Dar es Salaam

WATUMISHI wa Jeshi la Magereza wametakiwa kuzingatia utendaji kazi wenye tija mahala pa kazi na kuacha kufanya kazi kwa mazoea(Business as usual).

Rai hiyo imetolewa na Kamishna Jenerali wa Magereza nchini, John Casmir Minja wakati akizungumza kwenye Baraza la kufunga Mwaka 2015 na kuukaribisha Mwaka mpya 2016 katika Ofisi za Makao Makuu ya Jeshi hilo Jijini, Dar es Salaam. 

Jenerali Minja amewaagiza Watumishi wote wa Jeshi hilo kuhakikisha kuwa wanawajibika kwenye maeneo yao ya kazi ili kufikia ufanisi uliotarajiwa pamoja na kutumia vizuri rasilimali za Ofisi kwa manufaa yaliyokusudiwa.

"Utekelezaji wenu wa kazi za kila siku lazima uwe na tija na uendane sambamba na kasi ya Serikali ya Awamu ya Tano ili kufikia ufanisi unaotarajiwa". Alisema Jenerali Minja.

Aidha Jenerali Minja amezungumzia baadhi ya mafanikio yaliyopatikana kwa Mwaka 2015 ambayo ni pamoja na kukamilika kwa Sera ya Taifa ya Magereza ambayo italiwezesha Jeshi hilo kutekeleza mpango wake wa Maboresho ya maeneo mbalimbali, kusainiwa kwa Mkataba na Kampuni ya Poly Teknology ya China itakayojenga nyumba 9,500 za Makazi ya Maafisa na Askari, kusainiwa kwa Mkataba wa Magari 9,05 na Kampuni ya Ashok Leyland ambapo magari hayo yanatarajiwa kupokelea mapema mwakani.

Mafanikio mengine ni pamoja na Usajili wa kudumu wa Chuo cha Urekebishaji ambapo Chuo hicho kitatoa elimu stahiki ya Urekebishaji itakayotambulika ndani na nje ya Nchi, Jeshi la Magereza limepeleka Maafisa wake kwenye shughuli za Ulinzi wa Amani kwenye nchi mbalimbali zenye migogoro, Jeshi limeingia ubia na Wawekezaji mbalimbali katika miradi ya Kilimo, uchimbaji madini ya chokaa, ujenzi wa maduka makubwa(shopping Malls) katika Mikoa ya Morogoro na Kilimanjaro ambapo miradi hiyo itakuwa na manufaa makubwa kwa Jeshi.

Vilevile Jeshi limefanikiwa kuandaa Maandiko mbalimbali ikiwemo andiko la kujitosheleza kwa chakula na miradi minane ambayo miradi hiyo ikiwezeshwa inaweza kuongeza thamani za mali zinazozalishwa na Jeshi hilo.

Aidha Jenerali Minja alieleza changamoto mbalimbali ambazo Jeshi hilo linakabilianazo ambazo ni ufinyu wa bajeti, uhaba na uchakavu wa vyombo vya usafiri, ukosefu wa zana za kilimo, mabadiliko ya hali ya hewa hivyo kuathiri Uzalishaji, tatizo la miundombinu ya magereza na msongamano magerezani hali inayopelekea kwa kiasi fulani kuathiri utekelezaji wa majukumu ya Jeshi hilo.

Kamishna Jenerali wa Magereza, John Minja ametoa Salaam za kheri ya Mwaka mpya 2016 kwa Watumishi wote wa Jeshi hilo na kuwataka kufanya kazi kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu zinazotawala uendeshaji wa Jeshi la Magereza.

(Picha zote na Lucas Mboje wa Jeshi la Magereza)

    Hotuba ya Kamishna Jenerali wa Magereza John C. Minja ya kufunga mwaka 2015 na kuukaribisha mwaka 2016


    Bofya hapa kupata hotuba kamili ya Kamishina Jenerali wa Magereza John C. Minja kwa watumishi wa Jeshi la Magereza Tanzania Bara wakati wa baraza la kufunga mwaka 2015 na kuukaribisha mwaka 2016 makao makuu ya magereza tarehe 31 Desemba 2015.

    Thursday, December 24, 2015

    Mwili wa afisa wa gereza kuu Ukonga waagwa leo Ukonga jijini, Dar es Salaam

    Maafisa wa Jeshi la Mageereza wameubeba mwili wa Marehemu Mkaguzi wa Magereza, Morice Peter wakiuingiza nyumbani kwake kabla ya kutoa heshima za mwisho leo Desemba 24, 2015 katika Viwanja vya Gereza Kuu Ukonga Jijini Dar es Salaam.
    Mke wa Marehemu Mkaguzi wa Magereza, Morice Peter(vazi jeupe) akiwa kwenye majonzi makubwa wakati wa kuaga mwili wa mwenzi wake. Marehemu ameagwa leo katika Viwanja vya Gereza Kuu Ukonga Jijini Dar es Salaam kabla ya kusafirishwa kwa mazishi nyumbani kwao Mkoani Morogoro.
    Mkaguzi wa Magereza, Seleman Sued wa Gereza Kuu Ukonga, Jijini Dar es Salaam akisoma Wasifu wa Mkaguzi wa Magereza Morice Peter aliyefariki juzi Desemba, 2015 katika Hospitali ya Dar Group, Jijini Dar es Salaam.
    Baadhi ya Maofisa wa Jeshi la Magereza waliohudhuria katika hafla ya kuaga mwili wa Marehemu Mkaguzi wa Magereza, Morice Peter.
    Mke wa Marehemu Mkaguzi wa Magereza, Dorice Peter(kulia) akipewa msaada ndugu wa karibu wakati wa kusindikiza mwili kuelekea kwenye gari tayari kwa safari ya kuelekea Mkoani Morogoro kwenye mazishi.
    Ndugu na jamaa waliojitokeza kuuaga mwili wa Marehemu Mkaguzi wa Jeshi la Magereza, Morice Peter aliyekuwa akihudumu katika Gereza Kuu Ukonga, Jijini Dar es Salaam. Mkaguzi Morice Peter amefariki juzi Desemba 22, 2015 baada ya kuugua muda mrefu katika Hospitali ya Dar Group Jijini Dar es salaam

    (Picha na Lucas Mboje wa Jeshi la Magereza).

    Saturday, December 19, 2015

    Waziri Kitwanga, Dkt. Mwakyembe watembelea Magereza Makuu jijini Dar, waahidi kuboresha huduma kwa wafungwa na mahabusu


    Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga (kushoto) akisalimiana na Kamshina Jenerali wa Jeshi la Magereza,. John Minja wakati alipokuwa anawasili Gereza la Mahabusu Keko kwa ziara ya kikazi. Mwenye mawani ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Mbarak Abdulwakil, kushoto kwake ni Naibu Katibu Mkuu, John Mngodo.

    Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga  akikagua gadi maalumu iliyoandaliwa na Maafisa na Askari wa Gereza Keko alipofanya ziara ya kikazi ya kutembelea Magereza Makuu ya Mkoa wa Dar es Salaam. 

    Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga akizungumza na mahabusu na wafungwa waliopo Gereza la Wanawake Segerea, jijini Dar es Salaam alipofanya ziara katika Gereza hilo kujifunza shughuli mbalimbali za uendeshaji wa Magereza. Kulia kwake ni Waziri wa Sheria na Katiba, Dkt. Harrison Mwakyembe. Kulia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Mbarak Abdulwakil, Kushoto ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Sheria na Katiba, Maimuna Tarishi. Wapili kulia ni Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza, CGP John Minja. 

    Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga (watatu kushoto) na Waziri wa Sheria na Katiba, Dkt. Harrison Mwakyembe (wapili kushoto) wakikagua  jiko linalotumia gesi asilia kupikia vyakula vya wafungwa katika Gereza la Mahabusu Keko, jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza, CGP John Minja. 

    Msafara wa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga ukiwasili katika lango Kuu la Gereza Kuu Segerea, jijini Dar es Salaam kwa ziara ya kikazi kujifunza shughuli mbalimbali za uendeshaji wa Magereza. 

    Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga (wapili kushoto) na Waziri wa Sheria na Katiba, Dkt. Harrison Mwakyembe (kushoto) wakitoka Gereza la Wanawake Segerea baada ya kuzungumza na Mahabusu na Wafungwa wa Gereza hilo lililopo jijini Dar es Salaam.

    Waziri wa Sheria na Katiba, Dkt. Harrison Mwakyembe (kushoto) akiangalia bidhaa zinazotengenezwa na wafungwa wa kike wa Gereza la Wanawake Segerea ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa program ya urekebishaji magerezani. Pembeni yake ni Mkuu wa Gereza Kuu Segerea, Kamishna Msaidizi wa Magereza, Abdalah Kiangi. Kulia ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga. 

    Waziri wa Sheria na Katiba, Dkt. Harrison Mwakyembe (kushoto aliyevaa suti) akipokea heshima kutoka gadi maalumu iliyoandaliwa na Maafisa na Askari wa Chuo cha Taaluma ya Urekebishaji cha Jeshi la  Magereza mara baada ya kumaliza kufanya ziara ya kikazi ya kutembelea Magereza Makuu ya Mkoa wa Dar es Salaam. 

    Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga akitoa majumuisho kwa waandishi wa habari mara baada ya kumaliza ziara ya kutembelea Magereza ya Mkoa wa Dar es Salaam. Katika ziara yake hiyo Waziri Kitwanga aliambatana na Waziri wa Sheria na Katiba, Dkt. Harrison Mwakyembe (katikati). Kulia ni Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza, CGP John Minja. 

    Picha zote na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

    Wednesday, December 16, 2015

    Maafisa magereza nchini wametakiwa kuacha kufanya kazi kwa mazoea

    Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya ndani ya nchi, Mhe. Mbarak Abdulwakil akihutubia  kwenye Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Maafisa Waandamizi wa Jeshi la Magereza uliofanyika leo Desemba 16, 2015 katika Ukumbi wa Bwalo Kuu la Maafisa Magereza, Ukonga jijini Dar es Salaam.
    Maafisa Waandamizi wa Jeshi la Magereza kutoka vituo mbalimbali hapa nchini wakifuatilia hotuba ya mgeni rasmi kama wanavyoonekana katika picha.
    Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza, John Casmir Minja akitoa maelezo ya awali kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi kufungua rasmi  Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Maafisa Waandamizi wa Jeshi la Magereza uliofanyika leo Desemba 16, 2015 katika Ukumbi wa Bwalo Kuu la Maafisa Magereza, Ukonga jijini Dar es Salaam.
    Meza Kuu wakiwa kwenye Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Maafisa Waandamizi wa Jeshi la Magereza.

    Kamishna Jenerali wa Magereza, John Casmir Minja(wa kwanza kulia) akiteta pamoja na Makamishna wa Jeshi la Magereza kabla ya kumpokea mgeni rasmi(wa kwanza kulia) ni Naibu Kamishna wa Magereza Mstaafu, John Nyoka.
    Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya ndani ya nchi, Mhe. Mbarak Abdulwakil akiwa katika picha ya pamoja na Wajumbe wa  Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Maafisa Waandamizi wa Jeshi la Magereza (walisimama). Wa Pili tatu kushoto ni Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza, John Casmir Minja(wa tatu kulia) ni Kamishna wa Huduma za Urekebishaji, Deonice Chamulesile(wa pili kulia) ni Kamishna wa Fedha na Utawala wa Magereza, Gaston Sanga(wa pili kushoto) ni Kamishna wa Sheria na Uendeshaji wa Magereza, Dkt. Juma Malewa.

    (Picha zote na Lucas mboje wa Jeshi la Magereza).


    Na Lucas Mboje wa Jeshi la Magereza;

    MAAFISA wa Magereza nchini wametakiwa kuacha kufanya kazi kwa mazoea na badala yake wafanye kazi kulingana na kauli mbiu ya Rais wa awamu ya tano, Dkt. John Magufuli.

    Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, wakati akifungua Mkutano wa Maafisa Waandamizi wa Jeshi la Magereza nchini,  Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani, Mbarak  Abdulwakil alisema kila kiongozi afanye kazi kwa bidii na maarifa ili utendaji wake ulete tija mahala pa kazi.

    "Nadhani kila mmoja anafahamu kauli mbiu ya Mhe. Rais wa awamu ya tano ya "hapa kazi tu", na amekuwa akisisitiza kuwataka viongozi wenye dhamana na kila Mtanzania kufanya kazi kwa bidii na kuacha kufanya  kazi kwa mazoea kwani huu ni wakati wa kazi tu, " alisema.

    Vile vile, Bw. Abdulwakil aliwataka katika mkutano huo kujadili kwa kina mada maalum itakayowasilishwa na Kamishana Jenerali wa Magereza na kuweka mikakati ya kuongeza uzalishaji katika sekta za Kilimo, Mifugo na Viwanda.

    "Kwa vile Jeshi la Magereza ni mdau mkubwa wa uzalishaji hasa katika sekta za Kilimo, Mifugo na Viwanda vidogo vidogo, nawaasa katika mkutano huu mjadili kwa kina na mapana hatimaye mtoke na mkakati wa namna mtakavyoongeza uzalishaji katika sekta hizo " alisema.

    Kwa upande wake,Kamishna Jenerali wa Magereza, John Minja amesema Jeshi la Magereza limejipanga vyema kutekeleza maelekezo mbalimbali ambayo yalitolewa na Rais wa Awamu ya tano, Mhe. John Magufuli ambayo ni pamoja na kuanzisha miradi ya kibiashara ili kuipunguzia  Serikali mzigo wa kuwahudumia wafungwa na mahabusu magerezani.

    "Kuna mashamba 11 yametengwa ili kuzalisha kibiashara hivyo kuipunguzia Serikali mzigo na pia tumeainisha na miradi ya ufugaji" alisema Minja.

    Kamishna Jenerali Minja alisema kuwa Jeshi hilo linakabiliwa na matatizo mbalimbali ikiwamo madeni ya Wazabuni, ukosefu wa Ofisi za Wakuu wa Magereza Mikoa, Migogoro ya Ardhi na wananchi wanaoishi jirani na vituo vya magereza pamoja na Msongamano wa wafungwa magerezani.

    Mkutano huu ni wa kwanza kufanyika tangu Uongozi wa Serikali ya awamu ya tano uingie Madarakani chini ya Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli mapema mwanzoni mwa mwezi Novemba, 2015.

    Akizungumza kuhusu mkutano huo alisema ni mkutano wa kila mwaka kwa ajili ya kutathimini kwa pamoja utendaji wa Jeshi katika maeneo yote na kuweka mikakati ya kukabiliana na matatizo yaliyopo, kurekebisha dosari zilizojitokeza na kujiwekea malengo ya kuboresha utendaji wa kazi kwa ujumla katika mwaka ujao.

    Tuesday, December 15, 2015

    Naibu katibu mkuu mambo ya ndani aliasa Jeshi la Magereza kupunguza matumizi ya fedha za serikali yasiyo muhimu

    Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya ndani ya nchi, Mhe. John Mngodo akihubia Baraza la Wafanyakazi raia wa Jeshi la Magereza lililofanyika leo Desemba 15, 2015 katika Ukumbi wa Bwalo Kuu la Maafisa Magereza, Ukonga jijini Dar es Salaam.
    Wajumbe wa  Baraza la Wafanyakazi raia wa Jeshi la Magereza kutoka vituo mbalimbali hapa nchini wakifuatilia hotuba ya mgeni rasmi kama wanavyoonekana katika picha.
    Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza, John Casmir Minja akitoa maelezo ya awali kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi kufungua rasmi  Baraza la Wafanyakazi raia wa Jeshi la Magereza lililofanyika leo Desemba 15, 2015 katika Ukumbi wa Bwalo Kuu la Maafisa Magereza, Ukonga jijini Dar es Salaam.
    Maafisa Wandamizi wa Jeshi la Magereza kutoka Mikoa yote Tanzania Bara, Makao Makuu ya Jeshi hilo, Wakuu wa Vyuo vya Magereza wakifuatilia majadiliano katika Baraza hilo.
    Wajumbe wa  Baraza la Wafanyakazi raia wa Jeshi la Magereza wakiwa wameshikana mikono huku wakiimba wimbo Maalum wa Mshikamano Daima “SOLIDARITY FOREVER”.
    Mgeni rasmi Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya ndani ya nchi, Mhe. John Mngodo akiwa katika picha ya pamoja na Wajumbe wa  Baraza la Wafanyakazi raia wa Jeshi la Magereza (walisimama). Wa Pili kushoto ni Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza, John Casmir Minja(wa kwanza kushoto) ni Kamishna wa Huduma za Urekebishaji, Deonice Chamulesile(wa kwanza kulia) ni Kamishna wa Sheria na Uendeshaji wa Magereza, Dkt. Juma Malewa(wa pili kulia) ni Katibu wa Baraza la Wafanyakazi raia wa Jeshi la Magereza, Haikamen Mshida.

    (Picha zote na Lucas mboje wa Jeshi la Magereza).


    Na Lucas Mboje wa Jeshi la Magereza

    JESHI la Magereza limeaswa kuwa na matumizi mazuri ya fedha za umma ambayo ni pamoja na kuokoa fedha ambazo zilitengwa kwa matumizi ambayo siyo ya muhimu sana na fedha hizo kupelekwa katika mambo muhimu zaidi.

    Akizungumza katika ufunguzi wa Baraza la wafanyakazi la Jeshi hilo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya ndani ya Nchi, Mhe. John Mngodo alisema kwa kufanya hivyo Jeshi hilo litakuwa limeunga mkono kauli ya Rais John Magufuli ambapo Rais amekuwa akisisitiza watumishi wa umma kuokoa fedha za Serikali katika mambo ambayo hayana ulazima.

    "Tuzingatie makusanyo ya fedha za Serikali sambamba na kuokoa fedha katika mambo yasiyokuwa ya lazima na kupeleka fedha hizo katika mambo ya muhimu zaidi" Alisema Mngodo.

    Mngodo amewataka pia watumishi hao wa Jeshi la Magereza kuzingatia nidhamu ya matumizi ya fedha na utunzaji wa mali za Serikali.

    Aidha aliwasisitiza watumishi hao kuzingatia mapambano dhidi ya Rushwa mahala pa kazi  kwa kuepuka matendo ya utoaji na upokeaji rushwa kwa kuzingatia kauli ya Rais Magufuli kuwa “Tanzania bila ufisadi inawezekana”  badala yake kufanya kazi kwa bidii ili kuongeza tija mahala pa kazi.

    Mngodo katika hotuba yake hiyo aliwataka pia watumishi wa Jeshi hilo waliokuwa kwenye Baraza hilo kuzingatia maadili ya utumishi wa umma wanapodai maslahi yao.

    "Natumia fursa hii kuwataka kila mmoja wenu aliyopo hapa kubeba jukumu la kuhakikisha kuwa maadili ya nidhamu katika utendaji kazi kuwa kama chachu ya kuongeza ufanisi inazingatiwa kila siku," alisema Mngodo.

    Mngodo alisema katika kuleta maendeleo ni muhimu kuwashirikisha wafanyakazi kwa njia mbalimbali ikiwa ni pamoja na mabaraza ya wafanyakazi ili kuweka mikakati ya kuimarisha utendaji kazi na kutatua kero zinazowakabili.

    Awali  akimkaribisha mgeni rasmi, Mwenyekiti wa Baraza hilo ambaye ni Kamishna Jenerali wa Jeshi hilo, John Minja alisema majadiliano ya Kikao hicho yataleta chachu na kuimarisha hali ya watumishi na utendaji kazi  katika Jeshi hilo.

    ‘’Naamini uwepo wenu hapa utakuwa ni chachu katika majadiliano ambao utasaidia kuimarisha hali za watumishi na utendaji kazi katika Jeshi letu la Magereza” alisema Minja.

    Katika Kikao hicho kama ilivyo katika mabaraza ya wafanyakazi, hupokea taarifa za utekelezaji wa Bajeti katika kipindi cha Mwaka 2015/2016 kunaanzia Julai hadi Septemba Mwaka huu ambapo watajadili na kutoa mapendekezo

    Monday, December 14, 2015

    Taarifa kwa vyombo vya habari

    JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
    W1ZARA YA MAMBO YA NDAN1 YA NCH1
    (Jeshi la Magereza)
    Anwani ya Simu :" MAGEREZA"
    Simu namba: (+255) - 022 : 2110314-6
    Fax: (+255)-022: 2113737
    Email: cgp@prisons.go.tz
    UnapoJibu tafadhali taja:

    Ofisi ya Kamishna Jenerali wa Magereza,
    S.L.P. 9190,
    DAR ES SALAAM.


    TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

    Tarehe 16 Desemba 2015 saa 3:00 asubuhi Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya ndani ya Nchi Mhe. Mbarak Abdulwakil atafungua rasmi Mkutano wa Mwaka wa Maafisa Waandamizi wa Jeshi la Magereza Tanzania Bara utakaofanyika katika Bwalo Kuu la Maafisa Magereza Ukonga, Jijini Dar es Salaam.

    Mkutano huo ndio Kikao cha juu kabisa Jeshini ambacho huwahusisha Wakuu wa Magereza wa Mikoa, Maafisa Waandamizi wa Makao Makuu na Wakuu wa Vyuo vya Magereza. Kauli mbiu ya Mkutano huu ni utendaji kazi wenye tija, uadilifu na weledi kazini.

    Madhumuni ya Mkutano huu wa kila mwaka ni kutathmini kwa pamoja utendaji wa Jeshi la Magereza katika maeneo yake yote na kuweka mikakati ya kukabiliana na changamoto zilizopo, kurekebisha dosari zilizojitokeza na kujiwekea malengo ya kuboresha utendaji wa kazi kwa ujumla katika mwaka unaofuata.

    Mada kuu ya Mkutano wa Mwaka huu itatolewa na Kamishna Jenerali wa Magereza ambapo mada hiyo imezingatia Kauli mbiu ya sasa ya Serikali ya Awamu ya Tano.

    Maamuzi na mikakati mbalimbali itakayotolewa na Mkutano huu itakuwa na umuhimu wa pekee katika kuandaa na kutoa miongozo mbalimbali ya utendaji katika kufanikisha utekelezaji wa majukumu ya Jeshi hili.

    Vyombo vya Habari mnakaribishwa kwenye ufunguzi wa Mkutano huo tarehe 16 Desemba, 2015 saa 3:00 asubuhi na pia katika ufungaji siku hiyo saa 9:30 alasiri.

    Imetolewa na kusainiwa na;
    John C. Minja
    KAMISHNA JENERALI WA MAGEREZA
    14 Desemba, 2015.

    Thursday, December 10, 2015

    Rais Dkt. John Pombe Magufuli asemehe wafungwa 2,336 katika kuadhimisha miaka 54 ya uhuru


    Katika kuadhimisha miaka 54 ya Uhuru wa Nchi yetu tarehe 9 Desemba, 2015 Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutumia madaraka aliyopewa chini ya ya Ibara ya 45(1)(d) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ametoa msamaha kwa wafungwa wafuatao:-

    i) Wafungwa wote wamepunguziwa moja ya sita(1/6) ya vifungo vyao zaidi ya punguzo la kawaida linalotolewa chini ya kifungu 49(1) cha Sheria ya Magereza Sura ya 58 isipokuwa wafungwa walioorodheshwa katika Ibara ya 2(i-xix);

    ii) Wafungwa wagonjwa wenye magonjwa kama UKIMWI, KIFUA KIKUU(TB) na SARATANI(CANCER) ambao wako kwenye "terminal stage". Wafungwa ambao wamethibitishwa na Jopo la Waganga chini ya Uenyekiti wa Mganga Mkuu wa Mkoa/Mganga Mkuu wa Wilaya;

    iii) Wafungwa wa wazee wenye umri wa miaka (70) au zaidi ambao umri huo umethibitishwa na Jopo la Waganga chini ya Uenyekiti wa Mganga Mkuu wa Mkoa/Mganga Mkuu wa Wilaya;

    iv) Wafungwa wa kike walioingia na mimba gerezani, pamoja na wale walioingia na watoto wanaonyonyesha na wasionyonya;

    v) Wafungwa wenye ulemavu wa mwili na akili(Physical disability and mental disability) ambao ulemavu huo umethibitishwa na Jopo la Waganga chini ya Uenyekiti wa Mganga Mkuu wa Mkoa/Mganga Mkuu wa Wilaya.

    Aidha, Msamaha huo wa Mheshimiwa Rais hautawahusu wafungwa wafuatao:-
    i) Wafungwa waliohukumiwa adhabu ya kunyongwa;
    ii) Wafungwa waliohukumiwa adhabu ya kunyongwa na adhabu hiyo kubadilishwa kuwa kifungo cha maisha au kifungo gerezani.
    iii)Wafungwa waliohukumiwa kifungo cha maisha gerezani;
    iv) Wafungwa waliohukumiwa kifungo kwa makosa ya kujihusisha na usafirishaji na matumizi ya madawa ya kulevya kama vile cocaine, heroin, bhang;
    v) Wafungwa wanaotumikia kifungo kwa makosa ya kujihusisha na uombaji, upokeaji au utoaji wa rushwa;
    vi) Wafungwa wanaotumikia kifungo kwa makosa ya unyanga'anyi na unyang'anyi wa kutumia silaha au kujaribu kutenda makosa hayo;
    vii) Wafungwa wanaotumikia kifungo kwa makosa ya kupatikana na silaha, risasi au milipuko isivyo halali;
    viii) Wafungwa wanaotumikia kifungo kwa makosa ya shambulio la aibu, kunajisi, kubaka na kulawiti, au kujaribu kutenda makosa hayo;
    ix) Wafungwa waliopatikana na hatia na kuhukumiwa kifungo kwa kosa la kuwapa mimba wanafunzi wa shule za msingi na Shule za Sekondari na ambao walitenda kosa hilo wakiwa na umri wa miaka kumi na nane(18) na kuendelea;
    x) wafungwa wanaotumikia kifungo kwa makosa ya wizi wa magari na pikipiki au kujaribu kutenda makosa hayo;
    xi) Wafungwa wanaotumikia kifungo chini ya Sheria ya Bodi ya Parole(Act. No. 25/1994) na Sheria ya Huduma kwa Jamii(Act. No. 6/2002);
    xii) Wafungwa waliopatikana na hatia na kuhukumiwa kifungo kwa makosa ya kutumia vibaya madaraka yao;
    xiii) Wafungwa waliowahi kupunguziwa kifungo na Msamaha wa Mheshimiwa Rais na bado wangali wanaendelea ksehemu ya kifungo kilichobaki;
    xiv) Wafungwa waliopatikana na hatia na kuhukumiwa kwa kosa la kuzuia watoto kupata masomo;
    xv) Wafungwa waliopatikana na hatia na kuhukumiwa kwa kosa la utekaji wa watoto, kupoka ma kufanya biashara ya binadamu(Human Trafficking);
    xvi) Wafungwa waliopatikana na hatia na kuhukumiwa kwa kosa la kukutwa na viungo vya binadamu pamoja na vitendo vya mashambulizi na ukatili dhidi ya watu wenye ualbino;
    xvii) Wafungwa wanaotumikia vifungo kwa makosa ya kujihusisha na usafirishaji wa nyara za Serikali na ujangili(Poachers);
    xviii) Wafungwa wanaotumikia kifungo kwa makosa ya wizi/ubadhirifu wa fedha za Serikali;
    xix) Wafungwa wanaotumikia vifungo kwa makosa ya kutoroka au kujaribu kutoroka wakiwa chini ya ulinzi halali.

    Wafungwa wapatao 2,336 watanufaika na msamaha huu baada ya kupunguziwa 1/6 ya vifungo vyao ambapo 117 wataachiliwa huru na wafungwa 2,219 watanufaika na kubaki gerezani wakitumikia sehemu ya kifungo kilichobaki. Ni mategemeo ya Serikali kwamba watakaochiliwa huru watarejea tena katika jamii kushirikiana na wenzao katika ujenzi wa Taifa na kwamba watajiepusha kutenda makosa ili wasirejee tena gerezani.


    Imetolewa na kusainiwa na;

    JOHN C. MINJA

    KAMISHNA JENERALI WA MAGEREZA

    9 Desemba, 2015

    Tuesday, December 8, 2015

    Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza nchini aongoza kikao maalumu cha kupitia rasimu ya mpango wa Jeshi la Magereza kujitosheleza chakula, Jijini Dar

    Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza, John Casmir Minja akifungua Kikao Maalum cha Wadau kutoka nje ya Magereza(hawapo pichani) cha kujadili rasimu ya Mpango wa Jeshi la Magereza wa kujitosheleza kwa chakula cha Wafungwa waliopo Magerezani. Kikao hicho kimefanyika leo Desemba 8, 2015 katika Ofisi za Makao Makuu ya Jeshi hilo Jijini Dar es Salaam.

    Mshauri Mwelekezi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Prof. Beatus Kundy(aliyesimama) akiwasilisha rasimu ya Mpango wa Jeshi la Magereza wa kujitosheleza kwa chakula cha Wafungwa waliopo Magerezani. Jeshi la Magereza limeandaa rasimu hiyo ili kuipunguzia Serikali gharama za kuwalisha wafungwa waliopo magerezani.
    Maafisa Waandamizi wa Jeshi la Magereza wakifuatilia kwa makini uwasilishaji wa Andiko hilo(wa kwanza kulia) ni Kamishna wa Huduma za Urekebishaji, Eng. Deonice Chamulesile(wa pili kulia) ni Kamishna wa Sheria na Uendeshaji wa Magereza, Dkt. Juma Malewa(wa pili kushoto) ni Kamishna wa Fedha na Utawala wa Magereza, Gaston Sanga.
    Mwakilishi kutoka Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika, Bw. Hashim Kimmwe akitoa mchango wake wakati wa kujadili rasimu ya Mpango wa Jeshi la Magereza wa kujitosheleza kwa chakula cha Wafungwa waliopo Magerezani.
    Wataalam wa Jeshi la Magereza walioshiriki kikamilifu katika maandalizi ya Andiko la Mpango wa Jeshi la Magereza kujitosheleza kwa chakula kwa kushirikiana na Mshauri Mwelekezi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wakifuatilia majadiliano ya rasimu hiyo.

    (Picha zote na Lucas Mboje wa Jeshi la Magereza).

    Friday, December 4, 2015

    Magereza kuhamasisha utalii wa ndani katika miaka 54 ya uhuru wa Tanganyika

    Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza John Minja akiwasilia katiki viwanja vya Magereza Mkoa wa Kilimanjaro kwa ajili ya hafla ya kukabishi bendera kwa watumishi 39 wa Jehi hilo wanaotarajia kuadhimisha miaka 54 ya Uhuru wa Tanganyika kwa kupanda Mlima Kilimanjaro.
    Kamishna Jenerali wa Magereza John Minja akikabidhi bendera ya Magereza kwa kiongozi wa Msafara Kamishna Msaidizi wa Magereza Alexander Mmasy leo tarehe 04/12/2015 wakiwa wanajiandaa kupanda Mlima tarehe 06/12/2015 ili ifikapo tarehe 09 siku ya Uhuru wa Tanganyika wawe kileleni
    Kamishna Jenerali  wa Jeshi la Magereza John Minja akitoa nasaha kwa wapanda mlima wa Jeshi la Magereza (Hawapo pichani)
    Baadhi ya wadau wa Magereza Utalii Klabu walio tayari kupanda Mlima Kilimanjaro wakisikiliza kwa makini nasaha za Kamishna Jenerali wa Magereza John Minja katika hafla ya kukabidhiwa bendera ya Jeshi hilo kuipeleka katika Kilele cha Mlima huo.
    Baadhi ya wadau wa Magereza Utalii Klabu walio tayari kupanda Mlima Kilimanjaro wakiimba nyimbo za hamasa baada ya kupokea bendera kutoka kwa Kamishna Jenerali wa Magereza John Minja katika hafla ya kukabidhiwa bendera ya Jeshi hilo kuipeleka katika Kilele cha Mlima huo.
    Wapanda Mlima Kilimanjaro wa Jeshi la Magereza wakiwa katika picha ya pamoja na Mkuu wa Jeshi la Magereza  John Minja (Katikati),wa tatu kulia ni Mkuu wa Magereza Mkoa wa Arusha SACP Hamis Nkubasi, na Mkuu wa Magereza Mkoa wa Kilimanjaro SACP Venant Kayombo,  wa tatu kushoto ni Mnadhimu Mkuu wa Magereza Mkoa
    Baadhi ya wapanda mlima Kilimanjaro walipojumuika na watumishi wa Magereza Mkoa wa Kilimanjaro katika kupata kifungua kinywa katika hafla fupi ya kukabidhiwa bendera kwa watumishi hao wanaotarajia kupanda mlima ifikapo tarehe 06/12/2015
    Mmoja wa waongozaji utalii Mkoani Kilimanjaro akitoa maelezo mafupi kwa wapanda Mlima ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya awali kabla ya kupanda.
    Wadau wa Magereza Utalii Klabu wakiwa katika mazoezi mbalimbali ya kukimbia na kutembea katika viunga vya mji wa Moshi ikiwa ni maandalizi ya kuelekea katika kilele cha Mlima Kilimanjaro ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha miaka 54 ya Uhuru wa Tanganyika sambamba na kuamasisha utalii wa ndani.
    Baada ya mazoezi ya kutembea na kukimbia hufuatiwa na mazoezi ya viuongo ikiwa ni maandalizi ya kuelekea katika kilele cha Mlima Kilimanjaro ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha miaka 54 ya Uhuru wa Tanganyika sambamba na kuamasisha utalii wa ndani.



    Picha zote na Mrakibu Msaidizi wa Magereza Deodatus Kazinja na Koplo Mfaume Abdalah wa Jeshi la Magereza

    Na Deodatus Kazinja
    Katika kuadhimisha miaka 54 ya uhuru wa Tanganyika tarehe 9 Desemba  watumishi  wapatao 39 Jeshi la Magereza wakiwa katika uwiano wa wanaume 30 na wanawake 9  wataadhimisha siku hiyo kwa kupanda mlima Kilimanjaro na kutembelea Mamlaka ya Hifadhi ya Bonde la Ngorongoro.

    Washiriki hawa wanatoka katika vituo vya Makao Makuu ya Magereza, Chuo cha Taaluma ya urekebishaji Ukonga Dar es salaam,  Kikosi Maalum cha Kutuliza Gasia Magereza (KMKGM), Pwani, Dar es salaam, Iringa, Mbeya, Mara, Tabora, Tanga, Kilimanjaro na Arusha ambao kwa gharama zao wameamua kuadhimisha miaka 54 ya uhuru wa Tanganyika kwa kufanya utalii wa ndani.

    Akiongea na waandishi wa habari Kamishna Jenerali wa Magereza nchini John Casmir Minja katika hafula fupi ya kuwakabidhi bendera watumishi hao katika viwanja vya Magereza Mkoa wa Kilimanjaro amesema amefurahishwa mno na uamuzi wa askari hao kwa vile unalitangaza Jeshi la Magereza nje ya mipaka yake.

    Kamishna Minja alisema pia mbali na kulitangaza Jeshi la Magereza unawaweka timamu watumishi hao katika kufanya kazi  zao vizuri ikiwa ni kuunga kauli mbiu ya serikali ya Awamu ya Tano ya Hapa Kazi tu.

    Aidha Kamishna  huyo alitumia fursa hiyo kuishukuru serikali kwa namna ambavyo imekuwa ikijitolea kulisaidia Jeshi la Magereza ambapo alitoa taarifa kuwa tayari mikataba ya kununuliwa magari yapatayo 905 na ujenzi wa nyumba za watumishi zipatazo 9500 imesainiwa na magari yataanza kuingia mapema Januari 2016.

    Kwa upande wake mwenyekiti wa Magereza Utalii Klabu ambaye pia ni Mhasibu Mkuu wa Jeshi la Magereza Ndugu Estomih Hamis mbali na kumshuruku Kamishna Minja akwa namna ambavyo amejitolea katika kufanikisha uanzishwaji wa Klabu hiyo kuelezea dhima nzima ya utalii huo.

     “ Tumeamua kuadhimisha miaka 54 ya uhuru wa Tanganyika kwa mfumo huu  kwa sababu kadhaa. Mosi , ni kuunga mkono jitihada za serikali  za muda mrefu za kuhamasisha utalii wa ndani ambacho ni chanzo kimojawapo cha kuongeza mapato ya ndani ya serikali”

    “Pili, ni kuleta mwamko kwa  watumishi wa umma na watanzania kwa ujumla katika kutembelea vivutio vya utalii vya ndani kuliko ilivyo sasa ambapo sehemu kubwa ya watalii ni wageni kutoka nje ya Tanzania”

    Aidha, ndugu Hamis aliongeza kuwa zoezi  la upandaji mlima Kilimanjaro ni zuri kwa kuimarisha afya za watumishi hivyo kujiepusha na magonjwa kama vile kisukari, shinikizo la damu na utimamu wa mwili na hasa kwa askari wanaotakiwa kuwa hivyo muda wote.

    Tukio la watumishi wa Magereza kupanda mlima Kilimanjaro  litakuwa ni la pili kwa mwaka huu ambapo mara ya mwisho walipanda mlima tarehe 6 March, 2015 wakiwa ni jumla ya watumishi 20 ambapo 16 walifanikiwa kufika kileleni na wanne kurudia njiani kwa sababu mbalimbali.

    Zoezi la upandaji mlima lililopita lilifanyika kwa mafanikio makubwa kiasi cha kuibua hoja y wa unndwaji wa chombo cha pamoja kinachoweza kuratibu shughuli za utalii ndani ya Jeshi la Magereza kwa kuwaunganisha watumishi wote.

    Hoja hiyo ilifanikiwa kwa kuundwa kwa Klabu ya Utalii ya Magereza, klabu ambayo iko katika hatua za mwisho za usajili. Tayari Klabu hiyo inao viongozi wakiongozwa na Mwenyikiti ndugu Hamis, katibu wake akiwa ni Mkaguzi wa Magereza Dominick Mshana na Mweka Hazina ni Mrakibu Msaidizi wa Magereza Erasto Kipingu.

    Nani analipa gharama za utalii huo?
    Akijibu swali hilo katibu wa Klabu hiyo Mkaguzi Mshana alisema kwa hivi sasa watumishi hao wanapanda kwa gharama zao wenyewe kutoka katika mishahara yao ambapo karibu kila mshiriki amechanga wastani wa shilingi 300,000.

    Mshana amesema ni matumaini yake kuwa katika siku za mbeleni kama watapatikana wadhamini gharama hizo zinaweza kupungua sana kutoka mifukoni mwa washiri.

    Aidha amesema gharama za kupanda mlima na kutembelea vivutio vingine kwa ujumla ni kubwa kwa mtu mmoja mmoja lakini kunakuwa na unafuu mkubwa watu wakipanda kama kikundi.