Mojawapo ya Jukumu la Jeshi la Magereza ni kuwapeleka mahakamani mahabusu na kuwarudisha magerezani.

Gadi ya askari Wanawake na Wanaume wa Jeshi la Magereza katika Maadhimisho ya Sherehe za Kitaifa.

Ng'ombe bora wa Nyama na Maziwa ni sehemu ya miradi ya Uzalishaji inayoendeshwa na kusimamiwa na Jeshi la Magereza nchini.

Sehemu ya Mashamba makubwa yanayoendeshwa na Jeshi la Magereza: Shughuli za Kilimo cha Mashamba makubwa, madogo na bustani za mboga mboga ni moja ya shughuli za Magereza katika kuwafunza wafungwa namna ya kujitegemea mara wamalizapo vifungo vyao.

Baadhi wa wafungwa katika Kiwanda cha Ushonaji nguo cha Gereza Kuu Ukonga wakiwa kazini: Shughuli za Ushonaji wa nguo ni moja ya eneo ambalo wafungwa hupata huduma za urekebishwaji kwa vitendo.

Thursday, June 16, 2016

MAAFISA WA VYOMBO VYA ULINZI NA USALAMA WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI WAASWA KUZINGATIA UTII NA NIZAMU MAHALA PA KAZI JIJINI DAR‏Na Lucas Mboje, Dar es Salaam;

KATIBU Mkuu Wizara ya Mambo ya ndani ya Nchi, Meja Jenerali Projest Rwegasira(pichani) amewataka Maafisa na Askari wote wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama katika Wizara ya Mambo ya ndani ya Nchi kudumisha nidhamu wanapokuwa wakitekeleza majukumu ya kazi za kila siku.

Meja Jenerali Rwegasira ameyasema hayo leo katika hafla ya ufungaji Mafunzo ya Uongozi wa ngazi za juu kwa Maafisa wa Jeshi la Magereza yaliyofanyika katika Chuo cha Taaluma ya Urekebishaji Ukonga, Dar es Salaam.

"Katika muda mfupi niliofanya kazi katika Wizara hii nimeambiwa kuna watumishi wanakataa kwenda kwenye vituo vipya kwasababu ya kutopatiwa fedha za uhamisho, huo ni utovu wa nidhamu," Alisema Jenerali Rwegasira.

Alisisitiza Mtumishi anapopatiwa uhamisho ndani ya Jeshi jambo la kwanza ni Utii kwanza wa Utekelezaji wa Amri hiyo na siyo sababu au madai mengine ambayo ni kinyume na Utendaji wa Taasisi za Kijeshi.

Kwa upande wake Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza nchini, CGP. John Casmir Minja alisema Jeshi hilo limeitikia wito wa kubana matumizi kama inavyosisitizwa na Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Mhe. Joseph Pombe Magufuli ndiyo maana katika hafla hiyo imehusisha Maafisa wachache wa Gwaride ili kupunguza gharama zisizo za Msingi.

"Katika Sherehe za kufunga Mafunzo ya Uongozi kwa mwaka huu Gwaride limepunguzwa kwa kujumuisha Maafisa na Askari wachache zaidi na pia hata Wageni Waalikwa utaona wamekua ni wachache sana ili kuitikia wito wa Rais wa Awamu ya tano kama anavyosisitiza kupunguza matumizi yasiyoyalazima" Alisema Kamishna Jenerali John Casmir Minja.

Aidha, alisema Chuo hicho kina changamoto kadhaa ikiwa ni pamoja na uchakavu wa Miundombinu baada ya kupewa hadhi ya kuwa Chuo cha Taaluma ya Urekebishaji na kwamba anaamini Serikali ya awamu ya tano itazifanyia kazi changamoto hizo.

Hata hivyo Kamishna Jenerali Minja aliwapongeza wahitimu hao kwa kuchangia Tsh. Milioni 2.4 kwaajili ya kuboresha miundombinu ya chuo hicho kwa ridhaa yao ambapo walichangishana fedha hiyo ili kuboresha hali ya chuo hicho.

Jumla ya Wahitimu 98 wa Mafunzo ya Uongozi ngazi za Juu wamehitimu Kozi hiyo na kutunukiwa cheo cha Mrakibu Msaidizi wa Magereza ambapo Idadi hiyo inajumuisha Wahitimu 93 kutoka Tanzania Bara ikiwa Wanaume ni 83 na Wanawake 10 pamoja na Wahitimu 05 kutoka Vyuo vya Mafunzo Zanzibar ambao ni Wanaume 04 na Mwanamke 01.

KATIBU MKUU MAMBO YA NDANI YA NCHI AFUNGA RASMI MAFUNZO YA UONGOZI NGAZI ZA JUU MAAFISA WA JESHI LA MAGEREZA, JIJINI DAR ES SALAAM‏

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Meja Jenerali Projest Rwegasira akimvisha cheo cha Mrakibu Msaidizi wa Magereza mmoja wa Wahitimu wa Mafunzo ya Uongozi ngazi za juu aliyefanya vizuri katika masomo ya Medani kwa niaba ya Wahitimu wote wa kozi hiyo(kulia) ni Kamishna Jenerali wa Magereza, John Casmir Minja akishuhudia tukio hilo la uvishaji cheo.
Maafisa Wandamizi wa Jeshi la Magereza pamoja na Wageni Waalikwa kutoka Taasisi mbalimbali wakifuatilia kwa karibu Gwaride la Wahitimu.
Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza nchini, CGP John Casmir Minja akitoa maelezo mafupi juu ya Uendeshaji wa Jeshi la Magereza kabla ya kumkaribisha Mgeni rasmi Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya ndani ya Nchi, Meja Jenerali Projest Rwegasira(hayupo pichani).
Kamishna Jenerali wa Magereza Nchini, John Casmir Minja(wa pili kulia) akimuongoza Mgeni Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Meja Jenerali Projest Rwegasira kuelekea eneo la hafla ya kufunga rasmi Mafunzo ya Uongozi ngazi za juu wa Jeshi la Magereza(wa kwanza kulia) ni Mkuu wa Chuo cha Taaluma ya Urekebishaji Tanzania, ACP. Erasmus Kundy.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya ndani ya Nchi, Meja Jenerali Projest Rwegasira akikagua Gwaride la Wahitimu kama inavyoonekana katika picha.
Gwaride la Maafisa Wahitimu wa kozi ya Uongozi ngazi ya Juu wa Jeshi la Magereza likijiandaa kupita mbele ya Jukwaa la Mgeni kwa heshima kama wanavyoonekana wakiwa wakakamavu katika picha. Sherehe za kufunga Mafunzo hayo zimefanyika leo Juni 14, 2016 katika Viwanja vya Chuo cha Taaluma ya Urekebishaji Tanzania kilichopo Ukonga, Dar es Salaam.

(Picha zote na Lucas Mboje wa Jeshi la Magereza).