Mojawapo ya Jukumu la Jeshi la Magereza ni kuwapeleka mahakamani mahabusu na kuwarudisha magerezani.

Gadi ya askari Wanawake na Wanaume wa Jeshi la Magereza katika Maadhimisho ya Sherehe za Kitaifa.

Ng'ombe bora wa Nyama na Maziwa ni sehemu ya miradi ya Uzalishaji inayoendeshwa na kusimamiwa na Jeshi la Magereza nchini.

Sehemu ya Mashamba makubwa yanayoendeshwa na Jeshi la Magereza: Shughuli za Kilimo cha Mashamba makubwa, madogo na bustani za mboga mboga ni moja ya shughuli za Magereza katika kuwafunza wafungwa namna ya kujitegemea mara wamalizapo vifungo vyao.

Baadhi wa wafungwa katika Kiwanda cha Ushonaji nguo cha Gereza Kuu Ukonga wakiwa kazini: Shughuli za Ushonaji wa nguo ni moja ya eneo ambalo wafungwa hupata huduma za urekebishwaji kwa vitendo.

Tuesday, August 2, 2016

WASIFU WA MAREHEMU KAMISHNA MSTAAFU WA MAGEREZA EGNO KAMILIUS KOMBA‏


KAMISHNA MSTAAFU WA MAGEREZA MAREHEMU EGNO KAMILIUS KOMBA

Marehemu Kamishna Mstaafu wa Magereza EGNO KAMILIUS KOMBA alizaliwa tarehe 20 Oktoba,1947 katika Kijiji cha Mtungu - Kindimba Wilaya ya Mbinga Mkoani Ruvuma. Mwaka 1956 alijiunga na Elimu ya Msingi katika Shule ya Msingi Kindimba na kuhitimu elimu hiyo mwaka1959. Alijiunga na Shule ya Kati (Middle School) ya Litembo mwaka 1960 na kuhitimu mwaka 1963. Alijiunga na Shule ya Sekondari ya Kigonsera mwaka 1964 na kuhitimu Kidato cha Nne mwaka 1967. Mwaka 1968 alijiunga na Shule ya Sekondari Karimjee iliyopo Mkoani Tanga na kuhitimu mwaka 1968.

Marehemu aliajiriwa na Jeshi la Magereza tarehe 02 Agosti, 1972 na kupelekwa kuhudhuria mafunzo ya awali ya Uaskari katika Chuo cha Usalama – Moshi. Marehemu alihitimu mafunzo hayo tarehe 30 Aprili, 1973 na kupangiwa kufanya kazi Gereza Malya, Mkoa wa Shinyanga.

Mwaka 1975 akiwa mwajiriwa wa Jeshi la Magereza, Kamishna mstaafu wa Magereza, Marehemu EGNO KAMILIUS KOMBA alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es salaam kwa ajili ya masomo ya Shahada ya Kwanza katika Uchumi na kuhitimu mwaka 1978.

Marehemu akiwa Jeshini alitunukiwa vyeo mbalimbali kama ifuatavyo:-

Afisa Magereza Daraja la III (PO III)– 30/04/1973 – 31/09/1973

Afisa Magereza Daraja la I (PO I)- 01/09/1973 - 31/06/1976

Afisa Magereza Mkuu (PPO)-01/07/1976 - 30/11/1978

Mrakibu Msaidizi wa Magereza (ASP)- 01/12/1978 - 31/09/1980

Mrakibu Mwandamizi wa Magereza (SSP) - 01/10/1980 -31/12/1996

Kamishna Msaidizi wa Magereza (ACP) - 01/07/1984 -19/09/1989

Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Magereza (SACP)-20/09/1989-30/6/1996

Kamishna wa Magereza (CP) - 01/07/1996 - 30/06/2007 (Alipostaafu kwa umri Mkubwa).


Marehemu alifanya kazi katika vituo vifuatavyo vya Magereza:-

Gereza Malya – Shinyanga - Tarehe 01/05/1973 - 12/05/1974

Makao Makuu ya Magereza - Tarehe 13/05/1974 – 30/06/2007


Katika utumishi wake Jeshini Marehemu pia alitunukiwa nishani mbalimbali kama ifuatavyo:-
• Nishani ya Mstari wa Nyuma ya Vita vya Kagera,
• Nishani ya Utumishi Mrefu Tanzania na,
• Nishani ya Utumishi Uliotukuka.

Katika utendaji wake wa kazi, Marehemu alikuwa na uwezo mkubwa wa kujifunza, kutawala na kuyamudu majukumu yake ya kazi ipasavyo. Viongozi na watumishi wa Jeshi la Magereza tunamlilia mno kwa Utumishi wake uliotukuka na hazina kubwa ya utendaji aliyoondoka nayo kwani hata baada ya kustaafu katika Jeshi la Magereza bado alikuwa akitoa ushauri katika mambo mbalimbali ya Uendeshaji wa Jeshi la Magereza.

Kamishna Mstaafu wa Magereza EGNO KAMILIUS KOMBA alikuwa anasumbuliwa na Ugonjwa wa Moyo hadi umauti ulipomkuta mchana ya tarehe 31 Julai, 2016 nyumbani kwake Mvuti, Chanika Jijini Dar es Salaam. Mwili wa Marehemu unatarajiwa kuzikwa kesho Agosti 3, 2016 Shambani kwake Mvuti, Jijini Dar es Salaam.

MWENYEZI MUNGU AIWEKE PEMA PEPONI ROHO YA MAREHEMU EGNO KAMILIUS KOMBA, AMEN

Monday, August 1, 2016

TANZIA: KAMISHNA MSTAAFU WA MAGEREZA EGNO KAMILIUS KOMBA AFARIKI DUNIA JIJINI DAR‏

Marehemu Kamishna Mstaafu wa Magereza, Egno Kamilius Komba

                                                   …………………………

Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza nchini - CGP. John Casmir Minja anasikitika kutangaza kifo cha aliyekuwa Kamishna Mstaafu wa Sheria na Utawala wa Magereza - CP(Rtd) Egno Kamilius Komba  kilichotokea jana Julai 31, 2016 akiwa nyumbani kwake Mvuti, Chanika Jijini Dar es Salaam.

Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza anatoa pole kwa Watumishi wote wa Jeshi la Magereza nchini, familia ya Marehemu na wale wote walioguswa na msiba huu kwa namna tofauti tofauti.

Jeshi la Magereza kwa kushirikiana na familia ya Marehemu linaendelea kuratibu shughuli za msiba huo na taarifa za mazishi zitatolewa baadaye baada ya taratibu zote kukamilika.

                    Mwenyezi Mungu ailaze roho ya Marehemu mahali pema peponi Amina.