Na. Sgt. Geofrey Jacka - DODOMA
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Majaliwa Kassim Majaliwa (Mb), leo Novemba 07, 2024 amefanya ziara ya kikazi Gereza Kuu Isanga jijini Dodoma, kwa lengo la kukagua maendeleo ya utekelezaji wa agizo la Serikali kuhusu Matumizi ya Nishati safi ya kupikia Magerezani, ambapo ameeleza kuridhishwa na utekelezaji unaondelea Gerezani hapo.
Akizungumza mara baada ya kukagua Miundombinu hiyo Mhe. Majaliwa amesema, Serikali imeunda Kamati ya Kitaifa ya kusimamia kampeni ya Matumizi ya Nishati safi ya kupikia inayojumuisha Tanzania Bara na Zanzibar na umewekwa mpango kazi wa namna ya kuendesha kampeni huku kukiwa na Mkakati wa miaka kumi kuanzia 2023 hadi 2033 kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wote wanatumia Nishati safi ya kupikia.
"Niwapongeze sana Jeshi la Magereza kwa kuanza kutumia Nishati safi ya kupikia Magerezani, kwani Serikali tumeshaunda Kamati ya kusimamia kampeni ya Matumizi ya Nishati safi na Mpango kazi wa namna ya kuendesha kampeni hiyo ili kufikia 2033 asilimia 80 ya Watanzania wote wawe wameachana na Matumizi ya kuni na kutumia nishati safi ya kupikia, hivyo niwapongeze sana Magereza kwa kuanza teknolojia hii". Alisema Mhe. Majaliwa
Aidha Mhe. Majaliwa amemtaka Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Mhandisi Hamad Masauni, kuhakikisha anasimamia kikamilifu zoezi la matumizi ya Nishati safi ya kupikia kwa Magereza yote Nchini na kutoa taarifa ya ukamilishaji ifikapo Desemba Mwaka huu 2024, huku akieleza kuendelea na zoezi la Ukaguzi wa mara kwa mara kuhakikisha Taasisi zote zinatumia Nishati safi ya kupikia.
Kwaupande wake Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Mhandisi Hamad Masauni amesema anaishukuru Serikali kufuatia ongezeko la bajeti ya Wizara kutoka wastani wa Shilingi Milioni 936 hadi kufikia Trilioni 1.7 ambayo inagusa maeneo mengi ikiwemo kuboresha Miundombinu ya Magereza.
Akitoa ripoti ya utekelezaji wa Mpango wa Matumizi ya Nishati safi ya kupikia Magerezani, Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza (CGP) Jeremiah Yoram Katungu amesema, Jeshi la Magereza linaendelea na utekelezaji wa agizo la Serikali kuhusu Matumizi ya Nishati safi ya kupikia chakula cha Wafungwa na Mahabusu, ambapo mpaka kufikia Novemba 2024 Magereza kadhaa yameanza kutumia nishati safi ikiwemo Gereza Lilungu, Keko, Ukonga, Butimba, Ilagala, Babati, Isanga na Karanga huku maandalizi ya Miundombinu ya Biogas kwa Kambi Kimbiji na Ngara yakiendelea vizuri.
Pia CGP. Katungu amesema umesha fanyika Ununuzi wa jumla ya tani 167 za mkaa mbadala wa rafiki unao zalishwa na STAMICO na kusambazwa katika Magereza 16, lengo likiwa ni kuwezesha matumizi ya Nishati safi, ambapo kwasasa tupo katika hatua ya ukamilishaji wa upatikanaji wa majiko kwa ajili ya utumiaji wa mkaa huo.
Aidha CGP. Katungu amesema, Jeshi la Magereza kwa kushirikiana na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) linaendesha program ya matumizi ya Nishati safi ya kupikia Magerezani ambayo inahusisha jumla ya Vituo 211 yakiwemo Magereza 129, Ofisi za Mikoa 26, vituo vya Magereza 04, Makao Makuu, Bohari Kuu, Hospitali Kuu ya Jeshi, Karakana, Bwawani Sekondari pamoja na Kikosi cha Kutuliza Ghasia na Kambi za Magereza takribani 47 pamoja na Watumishi wote wa Magereza wapatao 15,920.