Banner

Banner

Friday, July 11, 2025

CGP. JEREMIAH KATUNGU AWAVISHA VYEO VIPYA MAAFISA 839 WA JESHI LA MAGEREZA

Mkuu wa Jeshi la Magereza nchini CGP Jeremiah Yoram Katungu,leo Julai 11, 2025 amewavisha vyeo vipya maafisa 29 wa Magereza Makao Makuu,  ikiwa ni miongoni mwa maafisa 839 waliopandishwa vyeo kwa kada mbalimbali katika Jeshi la Magereza Tanzania  bara, kwa mwaka 2024/2025.

Akizungumza katika hafla hiyo ya uvalishaji vyeo CGP. Katungu  amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan, kwa kuliwezesha Jeshi la Magereza kutekeleza majukumu yake na kutoa kibali cha upandishaji vyeo  kwa Maafisa hao. 

Aidha, CGP. Katungu amewapongeza maafisa wote walio panda vyeo nchi nzima na kuwataka kufanya kazi kwa uweledi,uadilifu huku akieleza kuwa ni matarajio ya Jeshi na Serikali kwaujumla kuwa watatekeleza majukumu yao kwa ufanisi mkubwa na kutanguliza mbele maslahi na ustawi wa Jeshi la Magereza na Taifa kwaujumla.

Kwaupande wake Kamishna wa Sheria na Uendeshaji wa Magereza CP. Nicodemus Tenga, amewapongeza Maafisa wote waliopandishwa vyeo na kuwataka wakatafute suluhisho la matatizo yaliyopo katika sehemu zao za kazi ili kuleta ufanisi wakiutendaji katika Jeshi.

Akitoa neno la shukrani kwaniaba ya wote waliopandishwa vyeo, Kamishna Msaidizi wa Magereza (ACP) Elmas Mgimwa, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuridhia kibali cha upandishaji vyeo pamoja na Tume ya Utumishi wa Jeshi la Polisi, Magereza, Zimamoto na Uokoaji na Uhamiaji na uongozi mzima wa Jeshi la Magereza kwa kuwapendekeza.

Maafisa hao wamepandishwa vyeo kuanzia Julai 07, 2025 kwa mujibu wa Muundo wa Maendeleo ya Utumishi wa Jeshi la Magereza wa mwaka 2015 na kuzingatia Ikama ya Jeshi.

Wednesday, April 16, 2025

WAKUU WA MAGEREZA MIKOA NA MAGEREZA YOTE NCHINI WAPONGEZWA UTEKELEZAJI MATUMIZI YA NISHATI SAFI


Mkuu wa Jeshi la Magereza nchini (CGP) Jeremiah Yoram Katungu amewapongeza wakuu wa Magereza mikoa na Magereza yote nchini kwa utekelezaji wa agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia.


Pongezi hizo amezitoa Aprili 15, 2025 kwenye kikao kazi kilichofanyika katika Ukumbi wa mikutano wa Makao Makuu ya Jeshi la Magereza Msalato jijini Dodoma.


"Ninayo furaha Magereza yote nchini tumeachana na matunizi ya kuni na sasa tunatumia nishati safi ya kupikia" Alisema CGP Katungu.


Pia, CGP. Katungu amewataka kutorudi nyuma katika matumizi ya kuni, badala yake waendelee kutumia nishati safi ya kupikia kama Serikali ilivyoagiza.


Aidha, CGP. Katungu, amewaeleza Wakuu wa Magereza mikoa na Magereza kuwa Jeshi la Magereza limefanya ushirikiano na taasisi ya Elimu na Mafunzo ya ufundi stadi (VETA) na hivi karibuni imeweza kutunuku vyeti wafungwa 201.


Vilevile, Jeshi la Magereza linaendelea na mazungumzo na Chuo cha Uhasibu Arusha ili kuanza kutoa masomo kwa njia ya mtandao(online) kwa kuanzia na masomo ya ujasiliamali kwa wafungwa magerezani.


Pia, CGP Katungu amewataka watumishi wote wa Jeshi la Magereza kudumisha upendo, mshikamano miongoni mwao kwaajili ya maendeleo ya Taifa.


Kwa upande wake,Kamishna wa Sheria na Uendeshaji wa Magereza, (CP)Nicodemus Tenga 

amewataka wakuu hao wa Magereza mikoa na Magereza yote nchini kukusanya taarifa za wafungwa wenye sifa zitakazowezesha kujadiliwa katika Bodi za Parole kwa kuwa mchakato wa kumjadili mfungwa huanzia katika Kamati za urekebishaji ya Gereza, ili wafungwa wenye sifa ya kunufaika na mpango huo wanatakiwa wapatiwe.


Akitoa neno la shukrani kwa niaba ya Wakuu wa Magereza mikoa na Magereza yote nchini, Mkuu wa Magereza Mkoa wa Mwanza Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP) Masud Kimolo, alimshukuru Mkuu wa Jeshi la Magereza (CGP) Jeremiah Katungu nakuahidi maelekezo yote ambayo ameyatoa watayatekeleza na kufanya kazi kwa weledi wa hali ya juu kwa manufaa ya Jeshi na Taifa kwa ujumla.

Saturday, March 29, 2025

WAHITIMU WA KOZI YA UONGOZI WA JESHI LA MAGEREZA WATAKIWA KUONESHA WELEDI KAZINI


Naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Waziri wa Nishati, Mhe. Dotto Biteko (Mb), ametoa Wito kwa  Wahitimu wa Kozi ya Uongozi wa Ngazi ya Juu (GO'S) Jeshi la Magereza, kutumia maarifa waliyopata kuboresha utendaji kazi, kudumisha nidhamu, sambamba na kuleta magaeuzi chanya ndani ya jeshi.

Mhe. Biteko amezungumza hayo katika hafla ya kufunga Kozi namba 27 ya Uongozi wa juu iliyofanyika katika viwanja vya Chuo Cha Taaluma ya Sayansi ya Urekebishaji Tanzania (TCTA) jijini Dar es Salaam, Machi 28, 2025 ambapo aliwapongeza wahitimu kwa hatua waliyoifikia na kuwakumbusha kuwa kupandishwa cheo ni ishara ya kuongezewa majukumu makubwa zaidi.

"Serikali inatarajia kuona mnakuwa chachu ya mabadiliko katika Jeshi la Magereza kwa kufanya kazi kwa bidii, uadilifu, na kuhakikisha haki inatendeka kwa mujibu wa Sheria," alisema Mhe. Biteko.

Naibu Waziri Mkuu, Alisisitiza kuwa Jeshi la Magereza lina jukumu kubwa la kuwahudumia watu waliokosea, lakini lengo kuu ni kuwasaidia kurekebisha tabia zao ili wawe raia wema wanaporejea kwenye jamii. Aliwataka wahitimu kuhakikisha wanazingatia utu, weledi na kuzingatia Sheria, taratibu na kanuni za kazi.

Kwa Upande wake, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Daniel Sillo amesisitiza dhamira ya Serikali ya kuleta mageuzi katika Taasisi za Haki Jinai kama sehemu ya juhudi za kuboresha mifumo ya utoaji haki nchini.

Aliongeza kuwa hatua hiyo inatokana na maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye aliunda Tume Maalum ya Kuboresha Taasisi za Haki Jinai ili kutathmini changamoto zilizopo na kupendekeza njia bora za kuimarisha Sekta hiyo.

Naye, Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza (CGP) Jeremiah Katungu, amesema kuwa, Jeshi kwa kushirikiana na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) lilizindua mpango wa kurasimisha ujuzi wa wafungwa, ambapo jumla ya wafungwa 201 wamepatiwa vyeti rasmi. Lengo la mpango huo ni kuhakikisha ujuzi walioupata Magerezani unatambulika rasmi ili kuwawezesha kupata ajira au kujiajiri mara baada ya kumaliza vifungo vyao.