Mojawapo ya Jukumu la Jeshi la Magereza ni kuwapeleka mahakamani mahabusu na kuwarudisha magerezani.

Gadi ya askari Wanawake na Wanaume wa Jeshi la Magereza katika Maadhimisho ya Sherehe za Kitaifa.

Ng'ombe bora wa Nyama na Maziwa ni sehemu ya miradi ya Uzalishaji inayoendeshwa na kusimamiwa na Jeshi la Magereza nchini.

Sehemu ya Mashamba makubwa yanayoendeshwa na Jeshi la Magereza: Shughuli za Kilimo cha Mashamba makubwa, madogo na bustani za mboga mboga ni moja ya shughuli za Magereza katika kuwafunza wafungwa namna ya kujitegemea mara wamalizapo vifungo vyao.

Baadhi wa wafungwa katika Kiwanda cha Ushonaji nguo cha Gereza Kuu Ukonga wakiwa kazini: Shughuli za Ushonaji wa nguo ni moja ya eneo ambalo wafungwa hupata huduma za urekebishwaji kwa vitendo.

Friday, July 31, 2015

Tanzia

 Marehemu SACP Aneth Laurent

Kamishna Jenerali wa Magereza John C. Minja anasikitika kutangaza kifo cha Mkuu wa Magereza  Mkoa wa Shinyanga Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Magereza (SACP)  Aneth Laurent kilichotokea jana tarehe 30 Julai,2015 katika Hosptali ya Rufaa Bungando jijini Mwanza.

Kaminshna Jenerali anatoa pole kwa watumishi wote wa Jeshi la Magereza nchini, familia na wale wote walioguswa na msiba huu kwa namna tofauti tofauti.

Jeshi la Magereza kwa kushirikiana na familia ya marehemu linaendelea kuratibu shughuli za msiba ambapo mwili wa marehemu unatarajiwa kusafirishwa kwa ndege kutoka Mwanza kuja Dar es salaam na taratibu za mazishi zitatolewa baadae.

Mungu ailaze Roho ya Marehemu mahali pema peponi.

Amina

UTENZI

KWAHERI KAMANDA ANETH
1.    Mchunga wangu ameniandalia mema yote,
    Aneth Laurent mchunga wako alikuandalia mema yote,
    Kwa kuwa yeye ndiye mwenye kuchunga uzima wote,
    Atakuandalia raha kamili huko mbinguni uliko.

2.    Ulifanya kazi yako ya kupigana na Shetani,
    Umeshinda, tena umeshinda sana,
    Ameona usisubiri ili shetani akirudi akushinde,
    Umepita katika uvuli wa mauti na hutaogopa kamwe.

3.    Ulikuwa kioo, mhimili wa familia,
    Hatukuwahi kukuona unagombana au kumchukia mtu,
    Ulikuwa mtenda haki, mtetea haki,
    Hukukaa kimya pale ulipoona haki haitendeki.

4.    Ulikuwa mpiganaji, mpambanaji usiyechoka,
    Kila wakati ulifuata maelekezo ya viongozi wako,
    Kwa unyenyekevu mkubwa uliwaongoza walio chini yako,
    Katu heshima hukuwavunjia,wakubwa kwa wadogo.

5.    Ulifanya kazi usiku na mchana,
    Ili kuhakikisha Jeshi letu mbele linasonga,
    Kitengo Uliongoza, cha Mipango kwa uadilifu mkubwa,
    Sote tulijivunia, uwepo wapo idarani.

6.     Kiongozi wa Mkoa usiyetetereka, Shinyanga umeongoza
    Umetuacha bila kutuaga, amani tunakuombea,
    Na lako tabasamu umeondoka, vichekesho vyako pia
    Umeondoka na utani wako na heshima yako.

7.    Vai na Karo mama ametuacha,
    Sunday, dada ametutoka,
    Pamela na David mama ametutoka tutakimbilia wapi,
    Mjukuu bibi hatutamwona tena,
    Amemfuata Beatrisi dada yake.

8.    Yosefu na Mwasiti rafiki yetu mpenzi kaondoka,
    Masunga, Novati, Ambayuu, Mmassy, Mwambashi,
    Makwaiya, Kaswaka, Mwamgunda,
    Kipenzi chetu hayupo tena, kwa heri Massawe wetu.

9.    Tunakuaga kipenzi chetu leo,
    Wizara itakukumbuka, Idara zote hazitakusahau,
    Jeshi la Magereza daraja limebomoka,
    Tumwombee kwa kuwa amemaliza kazi yake duniani.

10.    Aneth Laurent Balibusha,
    Ulipigana vita vitakatifu hapa duniani,
    Mambo ya dunia si kitu nakuambia yana uongo ndani,
    Yesu mwema, Yesu Mwokozi umwonee huruma,
    Angalia machozi umponye salama,
    Apumzike kwa Amani.  AMINA

Na Alexander Mmasy
Makao Makuu ya Magereza


Thursday, July 9, 2015

Taarifa ya mafanikio ya Jeshi la Magereza katika kipindi cha Serikali ya awamu ya nne(mwaka 2005-2015)

Bofya hapa kupata taarifa ya mafanikio ya Jeshi la Magereza katika kipindi cha Serikali ya awamu ya nne(mwaka 2005-2015)

Sunday, July 5, 2015

Waziri wa mambo ya ndani ya Nchi mhe. Mathias Chikawe azindua rasmi huduma za "Duty Free Shop" gereza kuu Lilungu, mkoani Mtwara


Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Mathias Chikawe(kulia) akifurahia kwenye jiwe la Msingi mara tu baada ya kuzindua rasmi duka hilo lenye bidhaa zisizo na tozo la Kodi(wa pili kushoto) ni Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza Nchini, John Casmir Minja(kushoto) ni Mkurugenzi wa Transit Military Shop, Bw. Alfazar Meghji. Uzinduzi huo umefanyika Julai 5, 2015 katika Viwanja vya Gereza Kuu Lilungu, Mkoani Mtwara.
Bidhaa mbalimbali zinazopatikana katika Magereza "Duty Free Shop" ya Gereza Kuu Lilungu, Mkoani Mtwara kama inavyoonekana katika picha. Duka hilo limezinduliwa rasmi na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Mathias Chikawe(hayupo pichani).
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Mathias Chikawe akitoa hotuba fupi ya uzinduzi wa Magereza "Duty Free Shop" Gereza Kuu Lilungu, Mkoani Mtwara leo Julai 5, 2015 katika Viwanja vya Lilungu, Mkoani Mtwara.
Muonekano wa nje wa Magereza "Duty Free shop" ya Gereza Kuu Lilungu, Mkoani Mtwara kabla ya kuzinduliwa rasmi leo Julai 5, 2015.
Maafisa Waandamizi wa Jeshi la Magereeza kutoka Mikoa ya Lindi na Mtwara wakifuatilia kwa makini hotuba ya Mgeni rasmi kwenye uzinduzi wa Magereza "Duty Free Shop" Gereza Kuu Lilungu, Mkoani Mtwara.
Kamishna Jenerali wa Magereza nchini, John Casmir Minja(kulia) akiteta jambo na Mkuu wa Wilaya ya Newala, Mhe. Christopher Magala(kushoto) kwenye hafla ya ufunguzi rasmi wa Magereza "Duty Free Shop Gereza Kuu Lilungu, Mkoani Mtwara.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Mathias Chikawe(katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Maafisa na Askari wa Jeshi la Magereza kutoka Mikoa ya Lindi na Mtwara kwenye uzinduzi wa Magereza "Duty Free Shop" Gereza Kuu Lilungu, Mkoani Mtwara(wa tatu kushoto) ni Kamishna Jenerali wa Magereza, John Casmir Minja(wa tano kulia) ni Mkuu wa Magereza Mkoani Mtwara, Kamishna Msaidizi wa Magereza, Mussa Kaswaka(wa pili kushoto) Mkuu wa Wilaya ya Newala, Mhe. Christopher Magala(wa kwanza kushoto) ni Mkurugenzi wa Transit Military Shop, Alfazar Meghji.


Na, Lucas Mboje, Mtwara

Maafisa na Askari wa Jeshi la Magereza nchini wametakiwa kutumia fursa ya maduka yenye bidhaa nafuu "Duty Free Shop" zilizofunguliwa katika Magereza mbalimbali ili kupata vifaa vya ujenzi na kujenga makazi yaliyobora na ya kudumu kabla ya kustaafu Utumishi wao Jeshini.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Mathias Chikawe alipokuwa akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa Magereza "Duty Free Shop" ya Gereza Kuu Lilungu, Mkoani Mtwara.

Amesema kuwa Maafisa na Askari wakitumia vizuri fursa ya maduka haya kwa kununua bidhaa za vifaa vya ujenzi itasaidia kukwepa aibu inayowapata baadhi ya Maafisa na Askari baada ya kustaafu hivyo kukosa nyumba za kuishi wakitegemea kujenga kwa kutumia Mafao baada ya kustaafu.

"Serikali iliidhinisha utaratibu wa Maafisa na askari wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama kusogezewa Huduma hizo za bidhaa muhimu katika maeneo yao kwa gharama nafuu kwa lengo la kuwapunguzia makali ya maisha". Alisema Waziri Chikawe.

Kwa upande wake Kamishna Jenerali wa Magereza, John Casmir Minja amesema kuwa Jeshi la Magereza limejipanga kuhakikisha kuwa linasambaza huduma hizo nchi nzima kwa ajili ya kutoa huduma kwa Maafisa na askari nchini.

Hadi sasa Jeshi hilo limekwisha kuzindua "Duty Free Shops" Nane katika Mikoa ifuatayo Dar es Salaam - Ukonga na Keko, Mwanza - Butimba, Tabora - Uyui, Kingolwira - Morogoro, Mbeya - Ruanda, Dodoma - Isanga na Mtwara - Lilungu.

Friday, July 3, 2015

Jeshi la Magereza laibuka mshindi wa kwanza katika utengenezaji wa samani maonesho ya 39 ya biashara kimataifa,"Sabasaba", mwaka 2015

Muonekano wa Samani za Ofisi ambazo hutengenezwa kwa Ustadi mkubwa katika Viwanda mbalimbali vinavyoendeshwa na Jeshi la Magereza zikiwa tayari zimekamilika kwa matumizi ya kiofsi kama inavyoonekana katika picha.


Na; Lucas Mboje wa Jeshi la Magereza

Jeshi la Magereza limeibuka Mshindi wa kwanza kwa upande wa Utengenezaji bidhaa za Samani kwenye Maonesho ya 39 ya Biashara ya Kimataifa yanayoendelea Jijini, Dar es Salaam Maarufu "SABASABA" kwa Mwaka huu 2015.

Akizungumzia ushindi huo Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza Nchini, John Casmir Minja amesema kuwa anajivunia ushindi huo kwani kulikuwa na ushindani mkubwa wa Makampuni mengi yanayoshiriki katika Maonesho haya ya Kibiashara yanayoendelea.

"Nachukua fursa hii kwa dhati kuwapongeza sana Maafisa wote washiriki katika Banda letu la Jeshi la Maonesho kwa kazi nzuri iliyowezesha ushindi huo wa kwanza kwa upande wa Utengenezaji wa Samani Bora". Alisema Jenerali Minja.

Aidha, Jenerali Minja amewaomba Wananchi kutoka maeneo mbalimbali ndani na nje ya Jiji la Dar es Salaam watembelee Banda la Jeshi la Magereza ili waweze kujipatia bidhaa bora pia kuona na kujifunza namna bora ya utengenezaji wa bidhaa mbalimbali.

Kwa upande wao Maofisa wa Jeshi la Magereza wanaoshiriki katika Maonesho haya wameushukru Uongozi wa Jeshi la Magereza kwa kuwawezesha kushiriki kikamilifu hususani kufanikisha maandalizi yote muhimu ya kushiriki katika Maonesho haya ya Biashara yanayoendelea Jijini Dar es Salaam.

Jeshi la Magereza Tanzania limepiga hatua kubwa ya Maboresho juu ya utengenezaji wa bidhaa bora za Samani hivyo kupelekea kuibuka mara kwa mara Mshindi wa kwanza katika Maonesho mbalimbali ya Kibiashara hapa nchini.

Thursday, July 2, 2015

Banda la Jeshi la Magereza lang'ara kwa bidhaa bora maonesho ya 39 ya biashara ya kimataifa 'sabasaba' 2015

Meza ya Chakula iliyotengenezwa kwa Ustadi mahiri katika Kiwanda cha Userelemala kilichopo Gereza Kuu Ukonga, Dar es Salaam. Meza hiyo ina viti vinane imetengenezwa kwa kutumia mbao ya Mninga inauzwa kwa Tsh. 2500,000/=
"Sofa set" yenye uwezo wa kukaliwa na watu saba, sofa hii imetengenezwa pia na Mafundi waliobobea kutoka Kiwanda cha Uselemala kilichopo Gereza Kuu Ukonga, Dar es Salaam kwa kutumia mbao aina ya mninga ambapo inauzwa kwa Tsh. 4,500,000/=
Meza Maalum ya Ofisi iliyotengenezwa kwa kutumia mbao ya mninga inapatikana katika Banda la Maonesho ya 39 ya Biashara ya Kimataifa, Jijini Dar es Salaam. Meza hiyo kwa pembeni ina meza ndogo kwa matumizi ya kiofisi kama ambavyo inaonekana. Aliyeketi ni Afisa Habari wa Jeshi la Magereza nchini, Mrakibu Msaidizi wa Magereza Lucas Mboje akiendelea na majukumu kama anavyoonekana katika picha.
Seti mbalimbali za kapeti za mlangoni ambazo zimetengenezwa kwa kutumia malighafi za mkonge na nazi kama zinavyoonekana katika picha. Kapeti hizo zenye ubora zinauzwa Tsh. 7000/= hadi 15,000/=
Vikoi kutoka Kiwanda cha Ushonaji cha Gereza Kuu Butimba, Mwanzaj vikiwa katika Banda la Jeshi la Magereza katika Maonesho ya 39 ya Biashara ya Kimataifa, kikoi kimoja kinauzwa kwa Tsh. 10,000/= tu
Bidhaa za mianzi zinazotengenezwa kutoka Gereza Njombe, Mkoani Njombe. Stafu Sajin wa Magereza, Shukrani wa Gereza Njombe akielezea namna bidhaa hizo zinavyotengenezwa pia namna Wafungwa wanavyonufaika kupitia Stadi hiyo ya utengenezaji wa bidhaa za mianzi Mkoani Njombe.
Vinyago vya aina mbalimbali kama vinavyoonekana katika picha ambapo vimechongwa kwa kutumia Mti wa Mpingo. Vinyago hivyo imetengenezwa katika Kiwanda cha Gereza Kuu Lilungu, Mkoani Mtwara. Wafungwa wa Gereza Kuu Lilungu wananufaika sana na Stadi hiyo ya uchongaji Vinyago hivyo kujipatia ujuzi na ajira mara wamalizapo vifungo vyao magerezani. Picha zote na Lucas Mboje wa Jeshi la Magereza.