Mojawapo ya Jukumu la Jeshi la Magereza ni kuwapeleka mahakamani mahabusu na kuwarudisha magerezani.

Gadi ya askari Wanawake na Wanaume wa Jeshi la Magereza katika Maadhimisho ya Sherehe za Kitaifa.

Ng'ombe bora wa Nyama na Maziwa ni sehemu ya miradi ya Uzalishaji inayoendeshwa na kusimamiwa na Jeshi la Magereza nchini.

Sehemu ya Mashamba makubwa yanayoendeshwa na Jeshi la Magereza: Shughuli za Kilimo cha Mashamba makubwa, madogo na bustani za mboga mboga ni moja ya shughuli za Magereza katika kuwafunza wafungwa namna ya kujitegemea mara wamalizapo vifungo vyao.

Baadhi wa wafungwa katika Kiwanda cha Ushonaji nguo cha Gereza Kuu Ukonga wakiwa kazini: Shughuli za Ushonaji wa nguo ni moja ya eneo ambalo wafungwa hupata huduma za urekebishwaji kwa vitendo.

Wednesday, April 26, 2017

MSAMAHA WA RAIS KWA WAFUNGWA KATIKA KUADHIMISHA MIAKA 53 YA MUUNGANO WA TANZANIA, TAREHE 26 APRILI, 2017

Katika kuadhimisha Miaka 53 ya Muungano wa Tanzania tarehe 26 Aprili, 2017 Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutumia madaraka aliyopewa chini ya Ibara ya 45(1)(d) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ametoa msamaha kwa wafungwa wafuatao:-

(i) Wafungwa wote ambao baada ya punguzo la kawaida la moja ya tatu (1/3) linalotolewa chini ya Kifungu 49(1) cha Sheria ya Magereza Sura ya 58, wawe wametumikia nusu (½) ya vifungo vyao vilivyobaki, isipokuwa wafungwa walioorodheshwa katika Ibara ya 2(i – xxi).

(ii) Wafungwa wagonjwa wenye magonjwa kama UKIMWI, Kifua kikuu (TB) na Saratani (Cancer) ambao wako kwenye “terminal stage”. Wafungwa hawa wathibitishwe na Jopo la Waganga chini ya Uenyekiti wa Mganga Mkuu wa Mkoa/Mganga Mkuu wa Wilaya.

(iii) Wafungwa wazee wenye umri wa miaka sabini (70) au zaidi. Umri huo uthibitishwe na Jopo la Waganga chini ya Uenyekiti wa Mganga Mkuu wa Mkoa/Mganga Mkuu wa Wilaya.

(iv) Wafungwa wa kike walioingia na mimba gerezani, pamoja na wale walioingia na watoto wanaonyonya na wasionyonya.

(v) Wafungwa wenye ulemavu wa mwili na akili (Physical disability and mental disability). Ulemavu huo uthibitishwe na Jopo la Waganga chini ya Uenyekiti wa Mganga Mkuu wa Mkoa/Mganga Mkuu wa Wilaya.

2. Aidha, Msamaha huu wa Mheshimiwa Rais hautawahusu wafungwa wafuatao:-

(i) Wafungwa waliohukumiwa adhabu ya kunyongwa.
(ii) Wafungwa waliohukumiwa adhabu ya kunyongwa na adhabu hiyo kubadilishwa kuwa kifungo cha maisha au kifungo gerezani.

(iii) Wafungwa waliohukumiwa kifungo cha maisha gerezani.

(iv) Wafungwa wanaotumikia kifungo kwa makosa ya kujihusisha na usafirishaji na matumizi ya madawa ya kulevya kama vile cocaine, heroin, bhangi n.k.

(v) Wafungwa wanaotumikia kifungo kwa makosa ya kujihusisha na uombaji na upokeaji au utoaji rushwa.

(vi) Wafungwa wanaotumikia kifungo kwa makosa ya unyang’anyi na unyang’anyi wa kutumia silaha au kujaribu kutenda makosa hayo (robbery with violence, armed robbery and attempt robbery).

(vii) Wafungwa wanaotumikia kifungo kwa makosa ya kupatikana na silaha, risasi au milipuko isivyo halali (fire arms, ammunitions and explosives).

(viii) Wafungwa wanaotumikia kifungo kwa makosa ya shambulio la aibu, kunajisi, kubaka na kulawiti au kujaribu kutenda makosa hayo.

(ix) Wafungwa waliopatikana na hatia na kuhukumiwa kifungo kwa kosa la kuwapa mimba wanafunzi wa Shule za Msingi na Shule za Sekondari na ambao walitenda kosa hilo wakiwa na umri wa miaka kumi na nane (18) na kuendelea.

(x) Wafungwa wanaotumikia kifungo kwa makosa ya wizi wa magari na pikipiki, uharibifu wa miundombinu au kujaribu kutenda makosa hayo.

(xi) Wafungwa wanaotumikia kifungo chini ya Sheria ya Bodi ya Parole (Act. No. 25/1994) na Sheria ya Huduma kwa Jamii (Act. No. 6/2002).

(xii) Wafungwa waliopatikana na hatia na kuhukumiwa kifungo kwa makosa ya kutumia vibaya madaraka yao.

(xiii) Wafungwa waliowahi kupunguziwa kifungo na Msamaha wa Mhe. Rais na bado wangali wanaendelea kutumikia sehemu ya kifungo kilichobaki.

(xiv) Wafungwa waliopatikana na hatia na kuhukumiwa kwa kosa la kuzuia watoto kupata masomo.

(xv) Wafungwa waliopatikana na hatia na kuhukumiwa kwa kosa la utekaji wa watoto, kupoka na kufanya biashara ya binadamu (Human Trafficking).

(xvi) Wafungwa waliopatikana na hatia na kuhukumiwa kwa kosa la kukutwa na viungo vya binadamu.

(xvii) Wafungwa wanaotumikia vifungo kwa makosa ya kujihusisha kwa namna yoyote ile na nyara za Serikali na ujangili (poachers).

(xviii) Wafungwa wanaotumikia vifungo kwa makosa ya wizi/ubadhirifu wa fedha za Serikali.

(xix) Wafungwa wanaotumikia vifungo kwa makosa ya kutoroka au kujaribu kutoroka chini ya ulinzi halali.

(xx) Wafungwa walioingia gerezani baada ya tarehe 16/03/2017.

(xxi) Wafungwa warejeaji wa makosa/wafungwa waliowahi kufungwa gerezani (Recidivists).

3. Wafungwa 2,219 watafaidika na msamaha huu na wataachiliwa huru. Ni mategemeo ya Serikali kwamba watarejea tena katika jamii kushirikiana na wenzao katika ujenzi wa Taifa na kwamba watajiepusha kutenda makosa ili wasirejee tena gerezani.

Meja Jenerali Projest Rwegasira
KATIBU MKUU
WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI
26/04/2017

Tuesday, April 11, 2017

MAHAFALI YA PILI KIDATO CHA SITA BWAWANI SEKONDARI YAFANA MKOANI PWANI

Kamishna wa Magereza Divisheni ya Fedha na Utawala ambaye ni Mwenyekiti wa Bodi ya Shule ya Sekondari Bwawani, Gaston Sanga akivishwa skafu na mmoja ya wa wanafunzi wa kikundi cha skauti cha shule hiyo mara baada ya kuwasili katika viwanja vya mahafali ya pili ya Kidato cha sita shuleni hapo leo Aprili 11, 2017.
Kamishna wa Magereza Divisheni ya Fedha na Utawala ambaye ni Mwenyekiti wa Bodi ya Shule ya Sekondari Bwawani, Gaston Sanga akikagua kikundi cha skauti cha shule hiyo kama inavyoonekana katika picha.
Kamishna wa Magereza Divisheni ya Fedha na Utawala ambaye ni Mwenyekiti wa Bodi ya Shule ya Sekondari Bwawani, Gaston Sanga akisalimiana na baadhi ya wazazi na wajumbe wa Bodi ya shule hiyo.
Muonekano wa madarasa mapya yaliyojengwa tayari kwa matumizi katika Shule ya Sekondari Bwawani, Mkoani Pwani.
Muonekano wa ndani wa Bweni la Wasichana lililokamilishwa kujengwa tayari kwa matumizi katika Shule ya Sekondari Bwawani, Mkoani Pwani
Maandamano ya wahitimu, wazazi na wageni waalikwa yakiongozwa na kikundi cha Brass Bendi kuelekea katika viwanja vya mahafali ya Kidato ya sita katika Shule ya Sekondari Bwawani, Mkoani Pwani.
Mkuu wa Shule ya Shule ya Sekondari Bwawani, Kamishna Msaidizi wa Magereza, Emmanuel Lwinga akitoa maelezo mafupi kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi katika mahafali hayo.
Mgeni rasmi Kamishna wa Magereza Divisheni ya Fedha na Utawala ambaye ni Mwenyekiti wa Bodi ya Shule hiyo, Gaston Sanga akitoa hotuba fupi kwa niaba ya Kamishna Jenerali wa Magereza, Dkt. Juma Malewa.
Wahitimu wa Kidato cha Sita wakifuatilia kwa makini hotuba ya Mgeni rasmi Kamishna Jenerali wa Magereza aliyewakilishwa na Kamishna wa Magereza Divisheni ya Fedha na Utawala Gaston Sanga.
Mmoja wa wahitimu wa Kidato cha Sita katika Shule ya Sekondari Bwawani iliyopo Mkoani Pwani akipokea cheti cha kuhitimu elimu hiyo.
Baadhi ya Wanafunzi wa Bwawani Sekondari wakionesha ubunifu wa mavazi mbalimbali katika mahafali ya pili ya kidato cha Sita shuleni hapo.
Mgeni rasmi Kamishna wa Magereza Divisheni ya Fedha na Utawala, Gaston Sanga(katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Wahitimu wa Kidato cha Sita(waliosimama) katika Mahafali ya pili ya Shule ya Sekondari Bwawani(wa pili kushoto) ni Kamishna Mkuu wa Magereza Mstaafu Jumanne Mangala, (wa tatu kulia) ni Naibu Kamishna wa Magereza Edith Malya na wa pili kulia ni Mkuu wa Chuo cha Urekebishaji Ukonga, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Magereza, Gideon Nkana

(Picha zote na Jeshi la Magereza).