Monday, December 23, 2019
KAMISHNA JENERALI WA MAGEREZA NCHINI, PHAUSTINE KASIKE AHIMIZA WAFUASI WAKE KUZINGATIA NIDHAMU JESHINI
9:05 AM
Kamishna
Jenerali wa Magereza nchini Phaustine Kasike akizungumza katika kikao na
Maafisa na askari wa vituo vya Magereza Mkoa wa Dar es Salaam ambapo kikao
hicho kilijadili masuala mbalimbali ikiwemo masuala ya utendaji kazi, maadili
ya kazi, nidhamu na mikakati mbalimbali ya Jeshi ikiwemo ya Kilimo, viwanda na
ufugaji. Kikao kazi hicho kimefanyika Bwalo Kuu la Maafisa Magereza, Ukonga
jijini Dar es Salaam.
Baadhi
ya Maafisa Waandamizi wa Jeshi la Magereza kutoka vituo vya Magereza Mkoa wa
Dar es Salaam wakimsikiliza Kamishna Jenerali wa Magereza nchini, Phaustine
Kasike(hayupo pichani) kikao hicho kilijadili masuala mbalimbali ikiwemo
masuala ya utendaji kazi, maadili ya kazi, nidhamu na mikakati mbalimbali ya
Jeshi ikiwemo ya Kilimo, viwanda na ufugaji.
Askari
wa vyeo mbalimbali wa Jeshi la Magereza kutoka katika vituo vya Magereza Mkoa
wa Dar es Salaam wakifuatilia mazungumzo ya kikao kazi na Kamishna Jenerali wa
Magereza nchini Phaustine Kasike Desemba 20, 2019 (Picha zote na Jeshi la Magereza).
Saturday, December 14, 2019
UTEKELEZAJI WA ZOEZI LA KUWAACHILIA HURU WAFUNGWA WANUFAIKA WA MSAMAHA WA RAIS WAKAMILIKA NCHI NZIMA
11:01 AM
Na ASP. Lucas Mboje, Dar es Salaam
JUMLA ya Wafungwa
5,533 katika magereza mbalimbali nchini walionufaika na msamaha wa Rais wakati
wa maadhimisho ya miaka 58 ya Uhuru
wameachiliwa huru magerezani.
Akizungumza
na wanahabari leo jijini Dar es Salaam, Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza,
Phaustine Kasike amesema kuwa utekelezaji wa zoezi la kuwaachiliwa huru
wafungwa wote walionufaika na msamaha wa Rais umekamilika nchi nzima.
“Ni
matarajio yangu kuwa wafungwa walioachiliwa wamejutia makosa yao na wataacha
kutenda uhalifu hivyo kujihusisha na shughuli halali kwa maendeleo yao, familia
zao, jamii na taifa kwa ujumla”, amesisitiza Jenerali Kasike.
Aidha,
Kamishna Jenerali Kasike ameelezea manufaa mbalimbali ya msamaha huo; mosi
kupungua kwa msongamano magerezani, pili, wanufaika wa msamaha kujumuika na
familia zao, tatu, kichocheo cha urekebishaji magerezani kwani msamaha huo
utasaidia kuimarika kwa nidhamu na kurejesha matumaini kwa wanaobakia
magerezani pamoja na wanufaika wa wamsamaha huo kupata fursa ya kujishughulisha
na shughuli za maendeleo uraiani.
“Zipo
changamoto zilizojitokeza katika utekelezaji wa zoezi hili ambapo baadhi ya wafungwa
walionesha kuwa hawako tayari kuungana na jamii zao pamoja na waliosamehewa
kurejea kutenda makosa mara baada ya kuachiwa huru. Hata hivyo nitoe wito kwa
jamii nchini kuwapokea wafungwa hao na kuacha kuwanyanyapaa”, amesema Jenerali
Kasike.
Wakati
huo huo, Kamishna Jenerali Kasike amemshukru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Dkt. John Pombe
Magufuli kwa kutoa msamaha huo ambao ni wa kihistoria hapa nchini. Pia
amewapongeza wanahabari wote nchini kwa namna walivyoshiriki kutoa habari za
zoezi la msamaha huo katika ngazi ya Mkoa na wilaya.
Kwa
mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 45(1) (d) imempa
mamlaka Rais kutoa msamaha kwa wafungwa waliopo magerezani. Kwa kutumia Ibara
hiyo Rais Dkt. John Pombe Magufuli alitoa msamaha kwa wafungwa wakati wa
maadhimisho ya miaka 58 ya Uhuru ambapo kilele chake kilifanyika Mkoani Mwanza
Desemba 9, 2019.
Wednesday, December 11, 2019
WAFUNGWA 79 WA GEREZA KUU BUTIMBA WALIONUFAIKA NA MSAMAHA WA RAIS WAACHILIWA JIJINI MWANZA TAREHE 10 DISEMBA 2019
9:38 AM
Mfungwa mnufaika wa Msamaha wa Rais, William
Dingu akizungumza na Wanahabari(hawapo pichani) baada ya kuachiliwa huru leo.
Mfungwa huyo amemshukru Rais kwa msamha huo, aidha, amelipongeza Jeshi la Magereza kwa kumwezesha
ujuzi wa wa fani ya ujenzi ambao ameupatia gerezani kupitia programu ya
Urekebishaji inayosimamiwa na Jeshi hilo
Baadhi
ya wafungwa wakiume wa Gereza Kuu Butimba walionufaika na Msamaha wa Rais
wakitoka katika lango la Gereza Kuu Butimba tayari kwenda kuungana na familia
zao. Wafungwa hao wamemshukru Rais Magufuli kwa msamaha huo wa kihistoria.
Wafungwa
wa kike Gereza Kuu Butimba – Sehemu ya Wanawake wakitoka gerezani baada ya
Msamaha wa Rais alioutoa jana katika maadhimisho ya miaka 58 ya uhuru. Wafungwa
hao wamemshukru Rais Magufuli kwa msamaha huo na wameahidi kutokurejea katika
uhalifu.
Kamati
ya Ulinzi na Usalama Mkoani Mwanza pamoja na Kamishna Jenerali wa Magereza nchini, Phaustine Kasike
wakishuhudia wafungwa walionufaika na Msamaha wa Rais katika Gereza Kuu Butimba
wakipewa mali zao na nauli ya kwenda kuungana na familia zao Desemba 10,
2019 kabla ya zoezi la uachiliaji wa wafungwa husika wa msamaha huo.
Kamishna
Jenerali wa Magereza nchini, CGP - Phaustine Kasike akitoa taarifa fupi ya
zoezi zima la uachiliaji wa wafungwa walionufaika na msamaha wa Rais katika
mikoa mbalimbali nchini mbele ya wanahabari kutoka vyombo mbalimbali vya Habari
jijini Mwanza Desemba 10, 2019.
Mkuu
wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. John Mongela ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya
Ulinzi na Usalama ya Mkoa huo akizungumza na Wafungwa wa Gereza Kuu Butimba
kabla ya zoezi la uachiliaji wa wafungwa walionufaika na Msamaha wa Rais Desemba 10, 2019. Kushoto ni Kamishna Jenerali wa Magereza nchini, CGP
- Phaustine Kasike.
(Picha
zote na Jeshi la Magereza).