Mojawapo ya Jukumu la Jeshi la Magereza ni kuwapeleka mahakamani mahabusu na kuwarudisha magerezani.

Gadi ya askari Wanawake na Wanaume wa Jeshi la Magereza katika Maadhimisho ya Sherehe za Kitaifa.

Ng'ombe bora wa Nyama na Maziwa ni sehemu ya miradi ya Uzalishaji inayoendeshwa na kusimamiwa na Jeshi la Magereza nchini.

Sehemu ya Mashamba makubwa yanayoendeshwa na Jeshi la Magereza: Shughuli za Kilimo cha Mashamba makubwa, madogo na bustani za mboga mboga ni moja ya shughuli za Magereza katika kuwafunza wafungwa namna ya kujitegemea mara wamalizapo vifungo vyao.

Baadhi wa wafungwa katika Kiwanda cha Ushonaji nguo cha Gereza Kuu Ukonga wakiwa kazini: Shughuli za Ushonaji wa nguo ni moja ya eneo ambalo wafungwa hupata huduma za urekebishwaji kwa vitendo.

Sunday, March 29, 2015

Askari magereza aliyekamatwa na fedha bandia afukuzwa kazi

Jeshi la Magereza nchini limemfukuza kazi askari wake wa Gereza Bariadi, Mkoani Shinyanga (pichani) kwa kosa la kupatikana na fadha za bandia kinyume na Sheria za Nchi.

Kwa mujibu wa taarifa rasmi iliyotolewa jana Machi 28, 2015 na kusainiwa na Kamishna Jenerali wa Magereza nchini, John Casmir Minja, askari Na. B. 6499 Wdr. Edmund Masaga amefukuzwa kazi kwa fedheha kuanzia Machi 28, 2015 kwa kosa la kulidhalilisha Jeshi mbele ya Umma kinyume na Kanuni 22(xlix) ya Kanuni za Utumishi wa Jeshi la Magereza za Mwaka 1997.

Aidha, Kamishna Jenerali wa Magereza nchini, John Casmir Minja amekemea vikali vitendo hivyo kwani ni kinyume cha Maadili na Utendaji ndani ya Jeshi la Magereza huku akiwataka askari wote wa Jeshi la Magereza nchini kutenda kazi zao kwa uadilifu na uaminifu mkubwa.


Imetolewa na; Lucas Mboje, Mkaguzi wa Magereza,
Afisa Habari wa Jeshi la Magereza,
Makao Makuu ya Jeshi la Magereza,
DAR ES SALAAM
Machi 29, 2015.

Saturday, March 21, 2015

Kamishna Jenerali wa Magereza avisha vyeo maafisa wa jeshi la Magereza, jijini Dar es Salaam

Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza(CGP), John Casmir Minja akimvisha cheo cha Kamishna Msaidizi wa Magereza, Afisa Mwandamizi kutoka Makao Makuu ya Jeshi la Magereza, Jeremiah Katungu katika hafla ya uvishaji vyeo kwa Maafisa waliopandishwa vyeo ngazi mbalimbali(jana) Machi 20, 2015 katika Viwanja ya Chuo cha Maafisa Magereza Ukonga, Jijini Dar es Salaam.
Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza nchini, John Casmir Minja akikagua Gadi Maalum ya Heshima iliyoandaliwa na Maafisa wa Jeshi la Magereza katika hafla ya uvishaji vyeo kwa Maafisa waliopandishwa vyeo ngazi mbalimbali(jana) Machi 20, 2015 katika Viwanja vya Chuo cha Maafisa Magereza Ukonga, Dar es Salaam.
Bendi ya Jeshi la Magereza ikipita mbele ya Mgeni rasmi Kamishna Jenerali wa Magereza, John Casmir Minja(hayupo pichani) kutoa heshima baada ya zoezi la uvishaji vyeo Maafisa 77 wa vyeo mbalimbali kukamilika
Maafisa wa Jeshi la Magereza Nchini pamoja na Wageni Waalikwa wakifuatilia kwa makini hotuba ya Mgeni rasmi, Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza, John Casmir Minja(hayupo pichani) katika hafla ya zoezi la uvishaji vyeo kwa Maafisa 77 wa Mkoa wa Dar es Salaam.
Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza nchini, John Casmir Minja(katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Maafisa Wanawake vyeo mbalimbali(waliosimama nyuma) baada ya zoezi la uvishaji vyeo hivyo Chuo cha Maafisa Magereza Ukonga, Jijini Dar es Salaam(wa pili kushoto) ni Kamishna Huduma za Urekebishaji, Injinia Dionice Chamulesile(wa pili kulia) ni Kamishna wa Sheria na Uendeshaji wa Magereza, Dkt. Juma Malewa(wa kwanza kulia) ni Kamishna wa Fedha na Utawala, Gaston Sanga(wa kwanza kushoto) ni Mkuu wa Chuo cha Maafisa Magereza Ukonga, Kamishna Msaidizi wa Magereza, Erasmus Kundy. 

Picha zote na Lucas Mboje wa Jeshi la Magereza.

Thursday, March 19, 2015

Kamishna jenerali wa magereza nchini kuvisha vyeo maafisa waandamizi wa magereza mkoa wa Dar es Salaam

Kamishna Jenerali wa Magereza Nchini, John Casmir Minja(pichani) kesho tarehe 20 Machi, 2015 saa 8:00 mchana atawavisha vyeo Maafisa wa Jeshi la Magereza wa ngazi mbalimbali wa Mkoa wa Dar es Salaam waliopandishwa vyeo kwa mujibu wa Sheria.

Kwa Mamlaka aliyopewa kisheria na Tume ya Polisi na Magereza ya Mwaka 1990, Kamishna Jenerali wa Magereza Nchini atawavisha vyeo hivyo katika Viwanja vya Chuo cha Maafisa wa Magereza Ukonga, Jijini Dar es Salaam.

Tume ya Polisi na Magereza katika Kikao chake Namba 2/2014/2015 kilichofanyika tarehe 16 Machi, 2015 chini ya Mwenyekiti Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Pereira Ame Silima(Mb) imewapandisha vyeo Maafisa 292 wa ngazi mbalimbali kuanzia tarehe 16 Machi, 2015.

Maafisa hao waliopandishwa vyeo ni Mrakibu Mwandamizi wa Magereza kuwa Kamishna Msaidizi wa Magereza 11, Mrakibu wa Magereza kuwa Mrakibu Mwandamizi wa Magereza 41, Mrakibu Msaidizi wa Magereza kuwa Mrakibu wa Magereza 83 na Mkaguzi Msaidizi wa Magereza kuwa Mkaguzi wa Magereza 157.

Imetolewa na; Inspekta Lucas Mboje, Afisa Habari wa Jeshi la Magereza,
Makao Makuu ya Jeshi la Magereza,
DAR ES SALAAM
19 Machi, 2015.

Tuesday, March 17, 2015

Wafungwa gereza kuu Ukonga, Dar es Salaam mahiri kwa ushonaji wa nguo za aina mbalimbali magereza

Wafungwa wa Gereza Kuu Ukonga, Jijini Dar es Salaam wakikata vitambaa vya nguo kabla ya kuanza kushona nguo za Wafungwa Magerezani. Wafungwa hao hujifunza Stadi mbalimbali za ujuzi ambazo huwasaidia kujipatia kipato mara tu wanapomaliza kifungo chao.
Wafungwa wa Gereza Kuu Ukonga, Jijini Dar es Salaam wakiendelea na ushonaji wa nguo za aina mbalimbali kama wanavyoonekana katika picha. Jeshi la Magereza nchini linatekeleza ipasavyo jukumu lake la Urekebishaji kwa kuwapatia ujuzi wa fani mbalimbali Wafungwa wanapokuwa wakitumikia vifungo vyao Magerezani.
Mkuu wa Kiwanda cha Gereza Kuu Ukonga, Kamishna Msaidizi wa Magereza, Ismail Mlawa akiongea na Wanahabari(hawapo pichani).
Aina za nguo mbalimbali ambazo tayari zimeshonwa kwa Ustadi Mkubwa na Wafungwa wa Gereza Kuu Ukonga Dar es Salaam. Gereza Kuu Ukonga Dar es Salaam limejizolea umaarufu mkubwa hapa nchini kwa kutekeleza ipasavyo Programu mbalimbali za Urekebishaji wa Wafungwa kwa Vitendo.

(Picha zote na Lucas Mboje wa Jeshi la Magereza).

Saturday, March 14, 2015

Mafunzo ya awali ya askari wa magereza kozi na. 27 yaendelea vyema chuo Kiwira, Mbeya

Askari Wanafunzi(Recruits) wa Mafunzo ya Awali ya Uaskari Magereza Kozi Na. 27 wakiendelea na masomo kwa vitendo katika Gwaride la silaha kama wanavyoonekana kikakamavu wakiwa na Walimu wao uwanjani huku silaha zao zikiwa begani.
Askari Wanafunzi wa Mafunzo ya Uaskari Magereza Kozi Na. 27 wakiendelea na somo la Gwaride la Salaam ya Utii wakiwa na silaha kama inavyoonekana katika picha.
Bango Kuu linaloonyesha unapoingia Chuo cha Mafunzo ya Uaskari Magereza kilichopo Kiwira, Mkoani Mbeya.
Askari Wanafunzi wa Mafunzo ya Awali ya Uaskari Magereza wakiendelea na masomo ya Darasani. Katika Mafunzo hayo hujifunza masomo mbalimbali ikiwemo Utawala na Uendeshaji wa Magereza, Sheria zinazoongoza Jeshi la Magereza, Ustawi wa Jamii, Afya, Uraia na Utawala na Uongozi

(Picha zote na Lucas Mboje wa Jeshi la Magereza).

Friday, March 13, 2015

Kamishna Jenerali wa magereza apongezwa kwa kufufua kiwanda cha sabuni gereza kuu Ruanda, Mbeya

Sabuni za kufulia zenye miche minene mirefu(Big Bars) zinazotengenezwa katika Kiwanda cha Sabuni cha Gereza Kuu Ruanda, Mbeya zikiwa tayari kupelekwa kwa watumiaji.

Muonekano wa Sabuni ya kufulia ikiwa bado haijawekwa kwenye mashine maalum ya kukatia vipande vyenye ukubwa tofauti tofauti. Kwa wastani Kiwanda hicho kinauwezo wa kuzalisha katoni 150 hadi 200 kwa siku.

Fundi Mkuu katika Kiwanda cha Sabuni cha Gereza Kuu Ruanda, Mbeya Sajin wa Magereza, George akitoa maelezo ya aina za Sabuni zinazotengenezwa katika mradi wa Sabuni Gereza Kuu Ruanda, Mbeya kama zinavyoonekana katika picha.


Na Lucas Mboje, Mbeya

Kamishna Jenerali wa Magereza Nchini, John Casmir Minja amepongezwa kwa kukifufua Kiwanda cha utengenezaji Sabuni za aina mbalimbali Gereza Kuu Ruanda, Mbeya.

Pongezi hizo zimetolewa na Maofisa na Askari wa Magereza Mkoani Mbeya kutokana na kukiwezesha Kiwanda hicho vifaa na malighafi za utengenezaji sabuni hivyo kukifanya Kiwanda hicho kizalishe sabuni za kutosha kwa Wafungwa waliopo Magerezani Tanzania Bara.

"Tunampongeza sana Kamishna Jenerali Minja hususani kwa kukiwezesha Kiwanda chetu vifaa vya utengenezaji sabuni. Tunaamini kutokana na kasi ya utendaji wake wa kazi ataendeleza juhudi za kukiunga mkono Kiwanda hiki ili kiweze kukidhi mahitaji halisi ya soko la ndani na nje." Walisikika wakisema.

Kiwanda cha Uzalishaji sabuni cha Gereza Kuu Ruanda, Mbeya ni miongoni mwa miradi 23 iliyopo chini ya Shirika la Magereza(Prison Corporation Sole) ambapo mradi huu ulianza shughuli zake za Uzalishaji sabuni mnamo Mwaka 1978.

Madhumuni ya kuanzishwa kwa mradi huu yalilenga zaidi kutimiza majukumu ya msingi ya Jeshi la Magereza hususani utekelezaji wa Programu ya Urekebishaji wa Wafungwa kwa kuwafundisha utengenezaji wa sabuni pia kiwanda hicho kinajiendesha kibishara hivyo kuchangia pato la Taifa.

Kiwanda hicho kinatengeneza Sabuni za aina mbalimbali zikiwemo Sabuni za kufulia zenye miche minene na mifupi, sabuni za kuongea, sabuni za maji kwa ajili ya usafi majumbani pamoja na sabuni za chenga chenga(flex soap).

Malighafi zinazotumika katika Kiwanda hicho ni caustic soda, mafuta ya mawese na mafuta ya mise ambayo hupatikana kwa wingi Wilayani Kyela, Mkoani Mbeya. Kwa wastani Kiwanda hicho kinauwezo wa kuzalisha katoni za sabuni 150 hadi 200 kwa siku.

Tangu kuanzishwa kwa mradi huu kwa kiasi kikubwa kimechangia utoaji elimu ya Ufundi Stadi kwa vitendo kwa Wafungwa katika fani ya za utengenezaji wa sabuni ambapo kuna Wafungwa wengi wamenufaika kupitia mradi huu na wameweza kuanzisha shughuli zao baada ya vifungo vyao kukoma.

Thursday, March 12, 2015

Magereza Watinga Kilele cha Mlima Kilimanjaro‏

Baadhi ya Maafisa, Askari na Mtumishi raia ambaye pia Mhasibu Mkuu wa Jeshi la Magereza Estomih Hamis  (Mzee wa Magereza Kileleni) wa saba kutoka kushoto wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kuwasili katika kilele cha Mlima Kilimanjaro asubuhi ya Machi 9, 2015 na kutundika bendera ya Jeshi hilo kileleni.
Kiongozi wa Msafara wa Maafisa, Askari na baadhi ya watumishi raia wa Jeshi la Magereza waliopanda mlima Kilimanjaro Kamishna Msaidizi wa Magereza Alexander Mmasy (kushoto) akikabidhi bendera ya Jeshi la Magereza kwa Mnadhimu wa Magereza Mkoani Kilimanjaro Kamishna Msaidizi wa Magereza Dickson Mlay aliyemwakilisha Mkuu wa Magereza Mkoa wa Kilimanjaro katika kupokea msafara wa wapanda mlima wa Jeshi hilo katika Lango la Hifadhi ya Mlima Kilimanjaro la Marangu.
Mkuu wa Gereza Kuu la Karanga Moshi Kamishna Msaidizi wa Magereza Dk. Hasan Mkwiche akipokea cheti kutoka kwa Mkuu wa Hifadhi ya Mlima wa Kilimanjaro Ndugu Erastus Lufungulo (wa kwanza kushoto) ikiwa ni ishara ya kuwa amepanda Mlima Kilimanjaro na kufika kileleni. Dk. Mkwiche ni miongoni wa Maafisa wa Magereza 16 waliofika katika kilele cha Mlima Kilimanjaro cha Uhuru kwa upande wake ikiwa ni mara ya pili kupanda mlima huo kwa mafanikio mara ya kwanza ilikuwa ni mwaka 2011.
Kiongozi wa Msafara wa Maafisa, Askari na baadhi ya watumishi raia wa Jeshi la Magereza waliopanda mlima Kilimanjaro Kamishna Msaidizi wa Magereza Alexander Mmasy akiwa katika uso wa furaha mara alipowasili katika kituo cha Gilman’s kabla ya kuanza safari ya kuelekea kilele cha Mlima huo cha Uhuru. Kushoto ni Mkaguzi wa Magereza Bakari Boi akiwa katika sura ya uchovu baada ya safari ndefu ya usiku kucha kutoka Kituo cha Kibo kuelekea Gilman’s.
Wakaguzi wa Magereza Abas Mikidadi (katikati), Jamhuri Yassin (kushoto), Deodatus Kazinja (aliyekaa kulia) na Bakari Boi wakiwa katika sura za uchovu mara baada ya kuwasili katika Kituo cha Gilman’s  alfajiri ya tarehe 09 Mach, 2015 baada ya safari ndefu na ngumu iliyoanza usiku wa saa tano tarehe 08 Machi, 2015 kutoka Kibo kwenda Gilman’s kabla ya kuhitimisha safari yao katika kilele cha Mlima huo cha Uhuru.
Baadhi ya Maafisa, askari na watumishi raia wa Jeshi la Magereza na wasaidizi wao (guiders)  wakiwa wamepumzika usiku wa manane katikati ya njia ya kutoka Kibo kuelelekea Gilman’s na baadae kilele cha Uhuru. Safari ya kutoka Kibo kwenda Gilman’s  ilianza usiku wa saa 5:13 Machi 8, 2015 na kuhitimishwa Asubuhi ya saa moja Machi 9,2015.
 
Baadhi ya Maafisa na askari wa Jeshi la Magereza wakiwa katika nyuso za furaha baada ya kuwasili katika Kituo cha Horombo kutoka Kituo cha Mandala baada ya kutembea umbali wa kilometa 11 na kulala hapo kabla ya kuanza safari ya kilometa tisa kutoka Horombo kwenda Kibo kesho yake.Kushoto mwenye nguo nyeupe ni Kiongozi wa Msafara Kamishna Msaidizi wa Magereza Alexander Mmasy na aliyeinua Mkono juu ni Mhasibu Mkuu wa Jeshi la Magereza Estomih Hamis (Mzee wa Magereza Kileleni). Hamis ndiye aliyekuwa na umri mkubwa kuliko wote katika kundi la watu 20 unaokaribia kabisa miaka 60.
Kundi la Maafisa, askari na watumishi raia wa Jeshi la Magereza pamoja wa waongoza njia (guiders) kwa pamoja likiwa katika mwendo wa kilometa tisa kutoka Horombo kwenda kituo cha Kibo ambapo liliwasili majira ya saa tisa alasiri na kupumzika kabla ya kuanza safari ya kwenda Gilman’s saa tano usiku.
Baadhi ya  Maafisa, askari na watumishi raia wa Jeshi la Magereza wakiwa  katika picha ya pamoja baada ya kuwasili katika kituo cha Mandala kutoka Lango Kuu la Marangu. Mandala ni kituo kilicho umbali wa takribani kilometa 8 kutoka Marangu na kiko katika mwinuko wa mita 2720 kutoka usawa wa Bahari.
Mkuu wa Magereza Mkoa wa Kilimanjaro Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Magereza Venant Kayombo akikabidhi bendera ya Jeshi la Magereza kwa kiongozi wa Msafara wa wapanda mlima wa Jeshi la Magereza Kamishna Msaidizi wa Magereza Alexander Mmasy katika Lango Kuu la Hifadhi ya Mlima Kilimanaro kabla ya kuanza zoezi la kupanda mlima huo March 6, 2015. 

Picha zote na Mkaguzi wa Magereza Deodatus Kazinja

Wednesday, March 4, 2015

Maandalizi ya kupanda mlima kilimanjaro-Maafisa na askari wa Jeshi la Magereza

Baadhi ya Maafisa na Askari wa Jeshi la Magereza wakiwa katika mazoezi ya kukimbia katika viunga vya manispaa ya Moshi ikiwa ni maandalizi ya kupanda mlima Kilimanjaro March 6, 2015. Maafisa hao wameweka kambi katika eneo la Gereza Karanga-Moshi.
Sehemu ya  Maafisa na Askari wa Jeshi la Magereza wakiwa katika mazoezi makali  katika mitaa ya mji wa Moshi ikiwa ni maandalizi ya kupanda mlima Kilimanjaro ifikapo Machi 6,2015. Katikati (mwenye vazi jeupe) ni Kamishna Msaidizi wa Magereza Alexander Mmasy kutoka Makao Makuu ya Magereza, wa kwanza kulia ni Mrakibu Msaidizi wa Magereza Mbezi Ramadhani kutoka Ofisi ya Mkuu wa Magereza Mkoa wa Tanga na wa kwanza kushoto ni Mkaguzi wa Magereza Jamhuri Yassin kutoka Makao Makuu ya Magereza, Dar es salaam.
Baadhi ya Maafisa na Askari wa Jeshi la Magereza wakiwa katika mazoezi ya kutembea  katika viunga vya Manispaa ya Moshi ikiwa ni maandalizi ya kupanda mlima Kilimanjaro mnamo Machi 6, 2015. Kutoka kushoto ni Mkaguzi wa Magereza Vicent Magessa kutoka Gereza Bagamoyo Mkoa wa Pwani, Mkaguzi wa Magereza Tumaini Kihampa na Mkaguzi wa Magereza Jamhuri Yassin wote kutoka Makao Makuu ya Magereza.
Maafisa na Askari na baadhi wa watumishi raia wa  Jeshi la Magereza wakiwa katika mazoezi makali ya kupita katika njia ngumu ikiwa ni maandalizi ya kupanda mlima Kilimanjaro ifikapo Machi 6, 2015. Wa sita kutoka mbele ni Mhasibu Mkuu wa Jeshi la Magereza Estomiah Hamis na wa mwisho ni Mkaguzi wa Magereza Abas Mikidadi
Maafisa na Askari na baadhi wa watumishi raia wa  Jeshi la Magereza wakiwa katika mazoezi makali ya kupita katika njia ngumu ikiwa ni maandalizi ya kupanda mlima Kilimanjaro ifikapo Machi 6, 2015.
Baadhi ya Maafisa na Askari wa Jeshi la Magereza wakiwa katika mazoezi ya viungo  baada ya kutembea na kukimbia katika viunga vya Manispaa ya Moshi ikiwa ni maandalizi ya kupanda mlima Kilimanjaro mnamo Machi 6, 2015.
Baadhi ya Maafisa na Askari wa Jeshi la Magereza wakipata kifungua kinywa baada ya mazoezi mazito ya maandalizi ya kupanda mlima Kilimanjaro ifikapo Machi 6,2015. Maafisa hao wako kambini eneo la Gereza Karanga mjini Moshi.
Baadhi wa washiriki wa Kilimanjaro Marathon Machi 1, 2015 mbio ambazo baadhi ya  Maafisa na Askari wa Jeshi la Magereza walishiriki ikiwa ni maandalizi ya kupanda Mlima Kilimanjaro mnao Machi 6, 2015. 

Picha zote na Mkaguzi wa Magereza Deodatus Kazinja