Mojawapo ya Jukumu la Jeshi la Magereza ni kuwapeleka mahakamani mahabusu na kuwarudisha magerezani.

Gadi ya askari Wanawake na Wanaume wa Jeshi la Magereza katika Maadhimisho ya Sherehe za Kitaifa.

Ng'ombe bora wa Nyama na Maziwa ni sehemu ya miradi ya Uzalishaji inayoendeshwa na kusimamiwa na Jeshi la Magereza nchini.

Sehemu ya Mashamba makubwa yanayoendeshwa na Jeshi la Magereza: Shughuli za Kilimo cha Mashamba makubwa, madogo na bustani za mboga mboga ni moja ya shughuli za Magereza katika kuwafunza wafungwa namna ya kujitegemea mara wamalizapo vifungo vyao.

Baadhi wa wafungwa katika Kiwanda cha Ushonaji nguo cha Gereza Kuu Ukonga wakiwa kazini: Shughuli za Ushonaji wa nguo ni moja ya eneo ambalo wafungwa hupata huduma za urekebishwaji kwa vitendo.

Friday, March 23, 2018

JESHI LA MAGEREZA LAJIPANGA KUJITOSHELEZA KWA CHAKULA CHA WAFUNGWA



Na Lucas Mboje - Jeshi la Magereza;

Mkuu wa Jeshi la Magereza nchini, Kamishna Jenerali Dkt. Juma Malewa, amesema Jeshi hilo limeanza kufanyia kazi agizo la Rais John Magufuli la kuhakikisha wanajitosheleza kwa chakula na kulisha wafungwa.

Amesema hatua hiyo itaondoa utaratibu wa wafungwa kupelekewa chakula kutoka nje, kwa kuwa watakuwa wanakula wanachokizalisha wakiwa magerezani.

Jenerali Dkt. Malewa alisema hayo katika mkutano wa maafisa waandamizi wa Jeshi la Magereza kutoka maeneo mbalimbali kuweka mkakati wa namna ya kufanikisha agizo hilo la Rais alilolitoa akiwa mkoani Dodoma hivi karibuni.

Rais Magufuli alilitaka jeshi hilo kuhakikisha linawatumia wafungwa kuzalisha chakula kwa ajili ya kuwalisha badala ya kutegemea ruzuku ya serikali kwa chakula.

Alisema kwa sasa Jeshi hilo lina uwezo wa kujitosheleza kwa chakula kwa asilimia 30, kutokana na vifaa vichache vilivyopo, lakini wanatarajia kupokea na kuongeza vifaa zaidi yakiwamo matrekta ili kuongeza nguvu zaidi ya uzalishaji na kufikia asilimia 100 ya kujitosheleza kwa chakula.

“Zoezi hili halitawezekana kutekelezwa kwa haraka sana, itatuchukua kama miaka miwili hadi mitatu kulifanikisha, lakini kwa kutumia nguvu kazi tuliyonayo na vifaa, tutamudu kulitekeleza,” alisema Kamishna Jenerali wa Magereza.

Malewa alibainisha mkakati wa kuhakikisha Magereza inatumika kama chuo cha mafunzo kwa kuwafundisha wafungwa mbinu mbalimbali za kilimo ili wote watumike vyema na kwa ufanisi katika kuboresha sekta ya kilimo.

Hata hivyo, alikiri kuwapo changamoto ya nguvu kazi kama baadhi ya wafungwa wakiwamo waliohukumiwa kunyongwa na mahabusu ambao kisheria hawapaswi kuwa nje ya Magereza, ingawa wanakula magerezani.

Kuhusu agizo la Rais la kuitaka Magereza kuwa sehemu ya ukuzaji wa uchumi kupitia sekta ya viwanda, alisema hilo wameanza kulitekeleza kivitendo kwa kuanzisha kiwanda cha sukari katika Gereza la Mbigiri, kinachojengwa kwa ubia kwa kushirikiana na mashirika ya Hifadhi za taifa ya NSSF na PPF pamoja na kiwanda cha viatu kilichopo Magereza Karanga mkoani Kilimanjaro na kwamba kinajengwa kingine hivyo kuwa viwili eneo moja.

“Tumeshapata oda za ndani na nje ya nchi, na tukishafunga mashine zaidi za kisasa, tutazalisha viatu kwa wingi sana,” Alisema Dkt. Malewa.

Mkuu wa Magereza Mkoa wa Morogoro, SACP. Ramadhani Nyamka, alisema wamejipanga kutekeleza agizo la Rais kwa kuzalisha kwa wingi, kwani Morogoro ina Magereza 12 na mengi yanajihusisha na uzalishaji wa mazao ya kilimo.

SACP. Nyamka alisema kutokana na kuwa na ardhi yenye rutuba, maji mengi na miundombinu yote muhimu ya kilimo, wanaamini wataweza kufanikiwa.

“Katika Magereza ya Morogoro niseme nguvu kazi inajitosheleza, kwani hatuna wafungwa waliohukumiwa kunyongwa, kwa hiyo tutatumia fursa ya Morogoro kama ghala la Taifa la chakula kulima kwa bidii tujitosheleze na ziada tuhudumie maeneo mengine, yakiwamo mashule,” alisema SACP. Nyamka.

Mrakibu Mwandamizi wa Magereza, Ramadhani Mkele ambaye ni Mkuu wa Gereza Kuu la Arusha, alisema pamoja na kutegemea kilimo cha jembe la mkono kwa kuwatumia wafungwa, wakipata vitendea kazi kama matrekta  wanaweza kupanua zaidi shughuli za kilimo katika gereza hilo.

Kamishna wa Fedha na Utawala wa Magereza, Gaston Sanga akitoa neno fupi kabla ya kumkaribisha Kamishna Jenerali wa Magereza kufungua rasmi kikao kazi hicho.

Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza, Dkt. Juma Malewa akiongoza Kikao Maalum cha kujadili mikakati ya utekelezaji wa Jeshi la Magereza kujitosheleza kwa chakula.

Wajumbe wa Kikao hicho ambao ni Maafisa Waandamizi wa Jeshi la Magereza wakifuatilia kwa makini maelekezo kutoka kwa Kamishna Jenerali wa Magereza, Dkt. Juma Malewa(hayupo pichani).

Washiriki wa Kikao kazi ambao ni Maafisa Waandamizi wa Jeshi la Magereza wakifanya maadiliano mbalimbali katika vikundi kama inavyoonekana katika picha.

Kamishna Jenerali wa Magereza, Dkt. Juma Malewa(katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Wakuu wa Magereza Mikoa yote Tanzania Bara(waliosimama mstari wa nyuma) mara baada ya ufunguzi rasmi wa kikao maalum cha kujadili mikakati ya utekelezaji wa Jeshi la Magereza kujitosheleza kwa chakula. Kikao hicho kimefanyika kwa siku moja 17 Machi, 2018 Mkoani Morogoro.

Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza, Dkt. Juma Malewa, akisalimiana na Kamishna wa Utawala na Fedha wa Magereza, Gaston Sanga  mara baada ya kuwasili kwenye viwanja vya Nanenane, Mkoani Mororogoro tayari kwa Kikao Maalum cha Maafisa Waandamizi wa Jeshi hilo. Kikao hicho kimefanyika kwa siku moja  17 Machi, 2018 Mkoani Morogoro. 



JESHI LA MAGEREZA KUENDESHA MAFUNZO YA UJASIRIAMALI KWA WAFUNGWA

Na Lucas Mboje - Jeshi la Magereza;
Jeshi la Magereza limetiliana saini makubaliano na Asasi ya kiraia katika kuendesha  mafunzo ya ujasiriamali kwa wafungwa vijana wenye umri wa kati ya miaka 18 hadi 30 waliopo magerezani katika Mikoa ya nyanda za juu Kusini ikiwemo Mbeya, Songwe, Iringa, Njombe, Ruvuma, Katavi na Rukwa.

Hafla ya kutiliana saini makubaliano hayo imefanyika katika Ofisi za Makao Makuu ya Jeshi la Magereza jijini Dar es Salaam na Asasi ya TECHNOSERVE iliwakilishwa na Afisa wake Bw. Monsiapile Kajimbwa.

Akizungumza baada ya kutiliana saini makubaliano hayo, Kamishna Jenerali wa Magereza, Dkt. Juma Malewa amesema kuwa mafunzo hayo ya ujasiriamali yatawapa uwezo wafungwa wa kubaini na kutumia fursa mbalimbali za kiuchumi ikiwemo uwezo wa kubuni na kuandaa mipango ya biashara.

“Mafunzo haya yatawanufaisha sana wafungwa waliopo magerezani katika mikoa hiyo kwani yatawajengea uwezo wa kujitambua pamoja na kujipatia vipato halali badala ya kutenda uhalifu katika jamii.” Alisema Jenerali Malewa.

Ameongeza kuwa mafunzo hayo yatafanyika katika Chuo cha Ufundi cha Magereza Ruanda kilichopo Mkoa wa Mbeya ambapo wafungwa watajifunza nadharia na vitendo katika dhana nzima ya ujasiriamali ikiwemo stadi za utengenezaji sabuni, ushonaji, useremala, ufumaji sambamba na uandaaji wa mipango ya kibiashara.

Meneja Mkazi wa Asasi ya TECHNOSERVE, Bw. Monsiapile Kajimbwa amesema kuwa hatua ya kutiliana saini makubalino hayo ni kuimarisha ushirikiano kati ya Asasi yake na Jeshi la Magereza katika kutoa mafunzo kwa wafungwa ili waweze kupata ujuzi kupitia program hiyo.

Dira ya Jeshi la Magereza ni kuwa Jeshi la kurekebisha wahalifu lenye utaalam wa hali ya juu linaloendeshwa katika kanuni na viwango vilivyowekwa Kitaifa na Kimataifa.


Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza,  Dkt. Juma Malewa(meza kuu mbele) akisaini Mkataba  wa makubaliano baina ya Asasi ya TECHNOSERVE katika mradi wa mafunzo ya ujasiriamali kwa Wafungwa waliopo magerezani. Kulia ni Meneja Mkazi wa Asasi ya hiyo Bw. Monsiapile Kajimbwa akisaini mkataba huo.  Hafla fupi ya  utilianaji saini Mkataba huo Machi 19, 2018 Makao Makuu ya Jeshi la Magereza, Jijini Dar es Salaam.

Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza, Dkt. Juma Malewa(kushoto) na Meneja Mkazi wa Asasi ya TECHNOSERVE, Bw. Monsiapile Kajimbwa(kulia) wakionesha nyaraka za Mkataba wa makubaliano mara baada ya utiliananji wa mkataba huo wa  mradi wa mafunzo ya ujasiriamali kwa Wafungwa waliopo magerezani.

Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza, Dkt. Juma Malewa akipongezana na Meneja Mkazi wa Asasi ya TECHNOSERVE, Bw. Monsiapile Kajimbwa mara baada ya kubadilishana Mkataba wa makubaliano baina ya Asasi hiyo katika mradi wa mafunzo ya ujasiriamali kwa Wafungwa waliopo magerezani.

Maafisa Waandamizi wa Jeshi la Magereza wakishuhudia utiliananji saini wa mkataba huo. Kulia ni Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Magereza, George Mwambashi kutoka Divisheni ya Sheria ya Magereza(kushoto) ni Mrakibu Mwandamizi wa Magereza, Uswege Mwakahesya ambaye ni Mratibu wa Programu za Ujasiriamali katika Jeshi la Magereza  
(Picha zote na Lucas Mboje wa Jeshi la Magereza).