Friday, March 23, 2018

JESHI LA MAGEREZA LAJIPANGA KUJITOSHELEZA KWA CHAKULA CHA WAFUNGWA



Na Lucas Mboje - Jeshi la Magereza;

Mkuu wa Jeshi la Magereza nchini, Kamishna Jenerali Dkt. Juma Malewa, amesema Jeshi hilo limeanza kufanyia kazi agizo la Rais John Magufuli la kuhakikisha wanajitosheleza kwa chakula na kulisha wafungwa.

Amesema hatua hiyo itaondoa utaratibu wa wafungwa kupelekewa chakula kutoka nje, kwa kuwa watakuwa wanakula wanachokizalisha wakiwa magerezani.

Jenerali Dkt. Malewa alisema hayo katika mkutano wa maafisa waandamizi wa Jeshi la Magereza kutoka maeneo mbalimbali kuweka mkakati wa namna ya kufanikisha agizo hilo la Rais alilolitoa akiwa mkoani Dodoma hivi karibuni.

Rais Magufuli alilitaka jeshi hilo kuhakikisha linawatumia wafungwa kuzalisha chakula kwa ajili ya kuwalisha badala ya kutegemea ruzuku ya serikali kwa chakula.

Alisema kwa sasa Jeshi hilo lina uwezo wa kujitosheleza kwa chakula kwa asilimia 30, kutokana na vifaa vichache vilivyopo, lakini wanatarajia kupokea na kuongeza vifaa zaidi yakiwamo matrekta ili kuongeza nguvu zaidi ya uzalishaji na kufikia asilimia 100 ya kujitosheleza kwa chakula.

“Zoezi hili halitawezekana kutekelezwa kwa haraka sana, itatuchukua kama miaka miwili hadi mitatu kulifanikisha, lakini kwa kutumia nguvu kazi tuliyonayo na vifaa, tutamudu kulitekeleza,” alisema Kamishna Jenerali wa Magereza.

Malewa alibainisha mkakati wa kuhakikisha Magereza inatumika kama chuo cha mafunzo kwa kuwafundisha wafungwa mbinu mbalimbali za kilimo ili wote watumike vyema na kwa ufanisi katika kuboresha sekta ya kilimo.

Hata hivyo, alikiri kuwapo changamoto ya nguvu kazi kama baadhi ya wafungwa wakiwamo waliohukumiwa kunyongwa na mahabusu ambao kisheria hawapaswi kuwa nje ya Magereza, ingawa wanakula magerezani.

Kuhusu agizo la Rais la kuitaka Magereza kuwa sehemu ya ukuzaji wa uchumi kupitia sekta ya viwanda, alisema hilo wameanza kulitekeleza kivitendo kwa kuanzisha kiwanda cha sukari katika Gereza la Mbigiri, kinachojengwa kwa ubia kwa kushirikiana na mashirika ya Hifadhi za taifa ya NSSF na PPF pamoja na kiwanda cha viatu kilichopo Magereza Karanga mkoani Kilimanjaro na kwamba kinajengwa kingine hivyo kuwa viwili eneo moja.

“Tumeshapata oda za ndani na nje ya nchi, na tukishafunga mashine zaidi za kisasa, tutazalisha viatu kwa wingi sana,” Alisema Dkt. Malewa.

Mkuu wa Magereza Mkoa wa Morogoro, SACP. Ramadhani Nyamka, alisema wamejipanga kutekeleza agizo la Rais kwa kuzalisha kwa wingi, kwani Morogoro ina Magereza 12 na mengi yanajihusisha na uzalishaji wa mazao ya kilimo.

SACP. Nyamka alisema kutokana na kuwa na ardhi yenye rutuba, maji mengi na miundombinu yote muhimu ya kilimo, wanaamini wataweza kufanikiwa.

“Katika Magereza ya Morogoro niseme nguvu kazi inajitosheleza, kwani hatuna wafungwa waliohukumiwa kunyongwa, kwa hiyo tutatumia fursa ya Morogoro kama ghala la Taifa la chakula kulima kwa bidii tujitosheleze na ziada tuhudumie maeneo mengine, yakiwamo mashule,” alisema SACP. Nyamka.

Mrakibu Mwandamizi wa Magereza, Ramadhani Mkele ambaye ni Mkuu wa Gereza Kuu la Arusha, alisema pamoja na kutegemea kilimo cha jembe la mkono kwa kuwatumia wafungwa, wakipata vitendea kazi kama matrekta  wanaweza kupanua zaidi shughuli za kilimo katika gereza hilo.

Kamishna wa Fedha na Utawala wa Magereza, Gaston Sanga akitoa neno fupi kabla ya kumkaribisha Kamishna Jenerali wa Magereza kufungua rasmi kikao kazi hicho.

Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza, Dkt. Juma Malewa akiongoza Kikao Maalum cha kujadili mikakati ya utekelezaji wa Jeshi la Magereza kujitosheleza kwa chakula.

Wajumbe wa Kikao hicho ambao ni Maafisa Waandamizi wa Jeshi la Magereza wakifuatilia kwa makini maelekezo kutoka kwa Kamishna Jenerali wa Magereza, Dkt. Juma Malewa(hayupo pichani).

Washiriki wa Kikao kazi ambao ni Maafisa Waandamizi wa Jeshi la Magereza wakifanya maadiliano mbalimbali katika vikundi kama inavyoonekana katika picha.

Kamishna Jenerali wa Magereza, Dkt. Juma Malewa(katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Wakuu wa Magereza Mikoa yote Tanzania Bara(waliosimama mstari wa nyuma) mara baada ya ufunguzi rasmi wa kikao maalum cha kujadili mikakati ya utekelezaji wa Jeshi la Magereza kujitosheleza kwa chakula. Kikao hicho kimefanyika kwa siku moja 17 Machi, 2018 Mkoani Morogoro.

Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza, Dkt. Juma Malewa, akisalimiana na Kamishna wa Utawala na Fedha wa Magereza, Gaston Sanga  mara baada ya kuwasili kwenye viwanja vya Nanenane, Mkoani Mororogoro tayari kwa Kikao Maalum cha Maafisa Waandamizi wa Jeshi hilo. Kikao hicho kimefanyika kwa siku moja  17 Machi, 2018 Mkoani Morogoro.