Mojawapo ya Jukumu la Jeshi la Magereza ni kuwapeleka mahakamani mahabusu na kuwarudisha magerezani.

Gadi ya askari Wanawake na Wanaume wa Jeshi la Magereza katika Maadhimisho ya Sherehe za Kitaifa.

Ng'ombe bora wa Nyama na Maziwa ni sehemu ya miradi ya Uzalishaji inayoendeshwa na kusimamiwa na Jeshi la Magereza nchini.

Sehemu ya Mashamba makubwa yanayoendeshwa na Jeshi la Magereza: Shughuli za Kilimo cha Mashamba makubwa, madogo na bustani za mboga mboga ni moja ya shughuli za Magereza katika kuwafunza wafungwa namna ya kujitegemea mara wamalizapo vifungo vyao.

Baadhi wa wafungwa katika Kiwanda cha Ushonaji nguo cha Gereza Kuu Ukonga wakiwa kazini: Shughuli za Ushonaji wa nguo ni moja ya eneo ambalo wafungwa hupata huduma za urekebishwaji kwa vitendo.

Thursday, July 28, 2016

WAZIRI MKUU MAJALIWA AKABIDHI HUNDI YA TSH. 85 MILIONI KWA JESHI LA MAGEREZA ZITAKAZOTUMIKA KUTENGENEZEA MADAWATI, JIJINI DAR‏

Waziri Mkuu wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa akimkabidhi mfano wa hundi Afisa Mwandamizi wa Jeshi la Magereza, SACP. John Masunga(kushoto) leo Julai 28, 2016 katika Viwanja vya Shule ya Msingi Chamazi. Waziri Mkuu amelekeza Fedha hizo zitumike kutengeneza madawati ya shule za msingi Majimatitu na Mbande zilizopo Wilayani Temeke.
Waziri Mkuu wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa akiwa ameketi kwenye madawati yaliyotolewa kwa Msaada wa Ubalozi wa Kuwait Nchini Tanzania kama inavyoonekana katika picha(Picha na Lucas Mboje wa Jeshi la Magereza).

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa(Mb) amekabidhi hundi ya Tsh. 85 Milioni kwa Uongozi wa Jeshi la Magereza  ili litengeneze jumla ya madawati  1,703 yatakayotumika katika Shule za Msingi za Majimatitu na Mbande zilizopo Wilaya ya Temeke, Jijini Dar es Salaam.

Hafla ya makabidhiano hayo  yamefanyika  leo tarehe 28 Julai, 2016 katika Viwanja vya Shule ya Msingi Chamazi iliyopo Wilaya ya Temeke, Jijini Dar es salaam ambapo Waziri Mkuu Majaliwa  amekabidhi madawati katika Shule ya Msingi Chamazi yaliyotolewa na Ubalozi wa Kuwait nchini Tanzania na Jumuiya ya Mabohora Tanzania kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri Mkuu Majaliwa  amewashukuru na kuwapongeza Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa kutoa mchango huo na pia amewapongeza wadau wengine ambao wameitikia wito wa Rais Magufuli wa kuchangia madawati kwa lengo la kuondoa tatizo la wanafunzi kukaa chini.

Waziri Mkuu Majaliwa  amesema baada ya kuanza kutekeleza ahadi ya kuondoa ada kwa shule za msingi na sekondari, idadi ya wanafunzi waliojiandikisha kuanza darasa la kwanza katika shule mbali mbali imeongezeka hali iliyosababisha upungufu wa madawati lakini tatizo hilo limetatuliwa kwa kiasi kikubwa hapa nchini.

Aidha,  amelitaka na Jeshi la Magereza kutengeneza madawati hayo mapema iwezekanavyo ili yakamilike haraka na kuanza kutumika katika Shule za Msingi Majimatitu na Mbande kwani shule hizo zinakabiliwa na idadi kubwa ya Wanafunzi hapa Jijini Dar es Salaam.

Hafla hiyo imehudhuriwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Augustine Mahiga, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Ramadhani Mwinyi, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Paul Makonda, Wakuu wa Wilaya zote za Mkoa wa Dar es Salaam, Wakurugenzi wote wa Halmashauri za Mkoa wa Dar es Salaam, Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Dar es Salaam, Wananchi pamoja na wanafunzi wa Shule ya msingi Chamazi.

Lucas Mboje, Mrakibu Msaidizi wa Magereza,
Afisa Habari wa Jeshi la Magereza,
Makao Makuu ya Jeshi la Magereza,
28 Julai, 2016.

Sunday, July 10, 2016

SHEREHE ZA KUFUNGA MAFUNZO YA AWALI YA UASKARI MAGEREZA ZAFANA CHUO CHA MAGEREZA, KIWIRA MKOANI MBEYA‏

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Meja Jenerali Projest Rwegasira(katikati) katika Jukwaa akipokea Salaam kutoka kwa Gwaride la Wahitimu wa Mafunzo ya Awali ya Uaskari Magereza(hawapo pichani) katika hafla ya kufunga Mafunzo hayo leo Julai 9, 2016 Chuo cha Magereza, Kiwira Mbeya. Kushoto ni Kamishna Jenerali wa Magereza, CGP- John Casmir Minja.
Mgeni rasmi ambaye ni Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Meja Jenerali Projest Rwegasira akikagua Gwaride la Wahitimu wa Mafunzo ya Awali ya Uaskari Magereza, Kozi Na. 28 ya Mwaka 2016.
Wahitimu wa Mafunzo ya Awali ya Uaskari Magereza, Kozi Na. 28 ya Mwaka 2016 wakila  kiapo  cha Utii kwa Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama ambaye ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kama inavyoonekana katika picha wakiwa wakakamavu.
Mgeni rasmi akimkabidhi cheti cha sifa mmoja wa Askari Wahitimu ambaye amefanya vizuri zaidi katika nyanja ya Nidhamu katika kipindi chote cha Mafunzo hayo.
Gadi Maalum ya Gwaride la kunyakua iliyoundwa na Wahitimu wa Mafunzo ya Awali ya Uaskari Magereza wakitoa heshima mbele ya Jukwaa la Mgeni rasmi ambaye ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi(hayupo pichani).
Maafisa Waandamizi wa Jeshi la Magereza wakifuatilia kwa karibu Maonesho mbalimbali katika Uwanja wa Gwaride kwenye hafla ya kufunga Mafunzo hayo.
Wakufunzi kutoka Kikosi Maalum cha Kutuliza Ghasia Magerezani(KMKGM) wakionesha onesho la kijasiri kama inavyoonekana katika picha.
Kamishna Jenerali wa Magereza, CGP - John Casmir Minja akitoa maelezo mafupi kabla ya kumkaribisha Mgeni rasmi kutoa hotuba yake ya kufunga rasmi kwa Mafunzo ya Awali ya Uaskari Magereza katika Chuo cha Magereza, Kiwira Mbeya.

Kamishna Jenerali wa Magereza, CGP - John Casmir Minja(wa pili kulia)akiwa ameongozana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi(wa pili kushoto) mara baada ya sherehe za kufunga Mafunzo ya Awali ya Uaskari Magereza, Chuo cha Magereza, Kiwira Mbeya(wa kwanza kulia) ni Mkuu wa Chuo cha Magereza - Kiwira, SACP. Stanford Ntirundura(Picha zote na Lucas Mboje wa Jeshi la Magereza).

Na; Lucas Mboje, Rungwe
JUMLA ya Wahitimu 1364 wa Mafunzo ya Awali ya Uaskari Magereza wamehitimu kuwa Askari kamili wa Jeshi hilo ambapo kati yao wanaume ni 977 na wanawake 377, Mafunzo hayo yamefungwa rasmi Julai 9, 2016 katika Chuo cha Magereza Kiwira, Wilayani Rungwe Mkoani Mbeya.

Akizungumza katika sherehe za kufunga Mafunzo hayo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Meja Jenerali Projest Rwegasira amesema Askari wote wa Jeshi la Magereza nchini wanatakiwa kufanya kazi kwa kuzingatia Misingi ya Haki za Binadamu na Utawala Bora kila wakati wanapotekeleza majukumu yao ya kazi.

Aidha, Meja Jenerali Rwegasira amewataka  Askari wahitimu wakazingatie elimu waliyopewa wakati wa mafunzo ili kuwezesha kuongezeka kwa ufanisi katika majukumu ya Jeshi la Magereza.
Sambamba na hilo, amewaasa kudumisha nidhamu mahala pa kazi kwani nidhamu ndiyo msingi wa kufanikisha utendaji kazi mahala pa kazi hususani katika Taasisi za Kijeshi.

"Hivyo ili kudumisha utendaji wenu wa kazi, mnapaswa kuzingatia nidhamu katika utekelezaji wenu wa majukumu yenu kulingana na maelekezo mtakayokuwa mnapewa". Alisisitiza Meja Jenerali Rwegasira.

Akizungumza kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi Kamishna Jenerali wa Magereza nchini, John Casmir Minja amesema kuwa changamoto nyingi ambazo kwa kiasi fulani zimeathili utekelezaji wa majukumu ya Jeshi hilo ni pamoja na ufinyu wa bajeti, makazi duni ya maafisa na askari, uhaba wa vitendea kazi na uchakavu wa vyombo vya usafiri.

Kamishna Jenerali Minja ameongeza kuwa tayari Jeshi hilo limechukua hatua mbalimbali za kufanya maboresho kwa lengo la kufanya Jeshi la Magereza kuwa la kisasa katika kutekeleza majukumu yake kisayansi na kwa ufanisi unaotarajiwa.

Friday, July 8, 2016

KATIBU MKUU WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI AWASILI JIJINI MBEYA TAYARI KWA KUFUNGA MAFUNZO YA AWALI YA UASKARI MAGEREZA, CHUO CHA MAGEREZA, KIWIRA‏

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Meja Jenerali Projest Rwegasira akipokea Salaam ya Kijeshi kutoka kwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, SACP. Dhahiri Kidavashari alipowasili leo Julai 8, 2016 katika Uwanja wa Ndege wa Songwe tayari kwa kufunga Mafunzo ya Awali ya Uaskari Magereza kesho Julai 9, 2016 katika Chuo cha Magereza, Kiwira Mkoani Mbeya(kushoto) ni Kamishna Jenerali wa Magereza, CGP - John Casmir Minja.
Kamishna Jenerali wa Magereza, CGP - John Casmir Minja(kulia) akiwa ameongozana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Meja Jenerali Projest Rwegasira walipowasili leo jioni Julai 8, 2016 katika Uwanja wa Ndege wa Songwe, Jijini Mbeya(Picha zote na Lucas Mboje wa Jeshi la Magereza).