Mojawapo ya Jukumu la Jeshi la Magereza ni kuwapeleka mahakamani mahabusu na kuwarudisha magerezani.

Gadi ya askari Wanawake na Wanaume wa Jeshi la Magereza katika Maadhimisho ya Sherehe za Kitaifa.

Ng'ombe bora wa Nyama na Maziwa ni sehemu ya miradi ya Uzalishaji inayoendeshwa na kusimamiwa na Jeshi la Magereza nchini.

Sehemu ya Mashamba makubwa yanayoendeshwa na Jeshi la Magereza: Shughuli za Kilimo cha Mashamba makubwa, madogo na bustani za mboga mboga ni moja ya shughuli za Magereza katika kuwafunza wafungwa namna ya kujitegemea mara wamalizapo vifungo vyao.

Baadhi wa wafungwa katika Kiwanda cha Ushonaji nguo cha Gereza Kuu Ukonga wakiwa kazini: Shughuli za Ushonaji wa nguo ni moja ya eneo ambalo wafungwa hupata huduma za urekebishwaji kwa vitendo.

Wednesday, December 31, 2014

Kamishna Jenerali wa Magereza John Minja ahutubia baraza la kufunga mwaka 2014 na kuukaribisha mwaka mpya 2015, makao makuu ya Magereza, D'Salaam

 
Kamishna Jenerali wa Magereza, John Casmir Minja akitoa hotuba yake fupi katika Baraza la kufunga Mwaka 2014 na kuukaribisha Mwaka Mpya 2015 katika Ofisi za Makao Makuu ya Magereza(kulia) ni Kamishna wa Sheria na Uendeshaji wa Magereza, Dkt. Juma Malewa(kushoto) ni Mnadhimu Mkuu wa Jeshi la Magereza, Kamishna Mwandamizi Msaidizi wa Magereza, Mmeta Manyala.

Baadhi ya Maafisa na Askari wa Jeshi la Magereza kutoka Ofisi ya Makao Makuu ya Magereza pamoja na Mkoa wa Dar es Salaam wakisikiliza kwa makini hotuba ya Kamishna Jenerali wa Magereza.

Kamishna wa Sheria na Uendeshaji wa Magereza, Dkt. Juma Malewa akitoa neno la shukrani kwa Kamishna Jenerali wa Magereza, John Casmir Minja(katikati) mara baada ya kutoa hotuba fupi katika Baraza la kufunga Mwaka 2014 na kuukaribisha Mwaka Mpya 2015.

Maafisa na Askari wa Jeshi la Magereza kutoka Ofisi ya Makao Makuu ya Magereza pamoja na Mkoa wa Dar es Salaam wakiwa wamesimama kwa ajili ya kuwakumbuka na kuwaombea kwa Mwenyezi Mungu Watumishi wenzao ambao wametangulia mbele ya haki kwa mwaka huu 2014.


Na Inspekta Lucas Mboje, Jeshi la Magereza
Kamishna Jenerali wa Magereza Nchini, John Casmir Minja amewaasa Maafisa na Askari wa Jeshi la Magereza nchini kuzingatia Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo katika utendaji wao wa kazi za kila siku ili kuleta ufanisi kazini.

Kamishna Jenerali John Minja ameyasema hayo leo wakati wa Baraza la Kufunga Mwaka 2014 na kuukaribisha Mwaka 2015 lililowahusisha baadhi ya Maafisa na Askari kutoka Makao Makuu ya Jeshi la Magereza pamoja na Magereza Mkoa wa D'Salaam.

Aidha, amewataka Maofisa, Askari na Watumishi wote kuacha tabia ya kufanya kazi kwa mazoea bali wawe wabunifu kwa kutumia raslimali zilizopo kwenye maeneo yao ya kazi ili kukabiliana na changamoto mbalimbali zilizopo.

" Kila mmoja wenu atimize wajibu wake katika eneo lake la kazi kwa bidii, ari na moyo wa kujituma ili kuliwezesha Jeshi kupata ufanisi unaotarajiwa". Alisisitiza Jenerali Minja.

Wakati huo huo Kamishna Jenerali wa Magereza Nchini, John Casmir Minja pia ametumia fursa hiyo kuelezea baadhi ya mafanikio mbalimbali yaliyopatikana kwa Mwaka uliopita 2014 ambapo Jeshi la Magereza limepata jumla ya leseni 102 za uchimbaji wa madini ya ujenzi kama vile chokaa, mawe, kokoto, mchanga na Murram katika maeneo mbalimbali ya magereza ambayo ni Gereza Wazo Hill - D’Salaam, Gereza Msalato - Dodoma, Kambi Bahi - Dodoma, Gereza Maweni - Tanga, Gereza Lilungu - Mtwara, Gereza Butimba - Mwanza na Gereza Kalilankulukulu - Katavi. Leseni hizo zitatumika kuingia ubia na wawekezaji wenye nia ya kushirikiana na Jeshi katika uchimbaji wa madini.

Pili, Shirika la Magereza limeeingia Mkataba wa ubia na Kiwanda cha Saruji Wazo (Twiga Cement) katika uchimbaji wa madini ya ujenzi Gereza Wazo Hill. Aidha, Kiwanda hicho katika kutekeleza wajibu kwa jamii wametoa msaada wa mifuko ya saruji 1200 na Tzs.100, 000, 000.00 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za makazi ya askari Gereza Wazo Hill. Pia Shirika la Magereza limeingia makubaliano na Mfuko wa Mafao ya Kustaafu wa GEPF kwa ajili ya ujenzi na uendeshaji wa vituo vya biashara (business malls) kwenye maeneo ya Gereza Kihonda, Morogoro na Gereza Karanga, Moshi.
Tatu, Rasimu ya kwanza ya Sera ya Taifa ya magereza imekamilika na tayari imewasilishwa kwenye mamlaka za juu kwa hatua zaidi. Kukamilika kwa sera hiyo kutawezesha Jeshi kutekeleza Mpango Mkakati wa Sera na Maboresho ya Jeshi kwa ujumla.

Pamoja na Mafanikio hayo, Kamishna Jenerali Minja ameelezea maeneo yatakayopewa kipaumbele kwa Mwaka huu wa 2015 ikiwemo Jeshi litaendeleza jitihada za kuimarisha na kuongeza uzalishaji kwenye miradi mbalimbali ya Jeshi la Magereza. Jitihada hizi ni pamoja kutangaza fursa zilizopo ili kuwavutia wawekezaji mbalimbali wa ndani na nje ya nchi waje kuingia ubia katika miradi hiyo kwa kuleta mitaji na teknolojia, pia Kuendeleza mikakati ya kupunguza msongamano magerezani

Baraza la kufunga Mwaka na kuukaribisha Mwaka unaofuata ni utamaduni wa siku nyingi ambao unaenziwa na Viongozi Wakuu wa Jeshi la Magereza. Baraza la aina hii hufanyika kila Mwaka ambapo Kamishna Jenerali wa Magereza Nchini hupata fursa ya kuongea na Watumishi wote wa Jeshi la Magereza nchini kupitia Baraza hilo lengo ikiwa ni kufanya tathmini ya yale yaliyojiri katika Jeshi kwa kipindi cha Mwaka unaisha kwa kuzungumzia mafanikio na changamoto zilizojitokeza na kutazama matarajio ya Mwaka mpya

Hotuba ya Kamishna Jenerali wa Magereza katika Baraza la Kufunga mwaka 2014 na kuukaribisha Mwaka 2015 kwa Maafisa Magereza Nchini.


Kamishna Jenerali wa Magereza John C. Minja ahutubia watumishi wa Jeshi la Mgereza Tanzania Bara katika Baraza la Kufunga mwaka 2014 na kuukaribisha Mwaka 2015.
Bofya hapa kupata hotuba kamili

Monday, December 29, 2014

Maafisa, Askari na Watumishi wa Jeshi la Magereza wapatiwa mafunzo ya jinsia, Rombo Green View Hotel-Jijini Dar es Salaam

Kamishna wa Sheria na Uendeshaji wa Magereza, Dkt. Juma Malewa akitoa hotuba fupi kwa niaba ya Kamishna Jenerali wa Magereza katika Ufunguzi wa Mafunzo ya Jinsia kwa Maafisa, Askari na Watumishi raia wa Jeshi la Magereza, leo Desemba 29, 2014 katika Ukumbi wa Rombo Green View Hotel. Mafunzo hayo yanafanyika kwa siku mbili ambapo yatafungwa rasmi kesho Desemba 30, 2014(kushoto) ni Mkuu wa Magereza Mkoani Morogoro, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Magereza, Kato Rugainunura(wa pili kulia) ni Mkuu wa Magereza Mkoani Tanga, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Magereza, Augustino Mboje(kulia) ni Mkuu wa Mafunzo ya Kijeshi wa Magereza, Kamishna Msaidizi wa Magereza, Mbarak Semwenza.
Baadhi ya Maafisa, Askari na Watumishi raia wa Jeshi la Magereza wanaoshiriki Mafunzo ya Jinsia katika Ukumbi wa Rombo Green View Hotel wakisikiliza hotuba ya Mgeni rasmi. Mafunzo hayo yanafanyika kwa siku mbili ambapo yatafungwa rasmi kesho Desemba 30, 2014.
Mshiriki wa Mafunzo ya Jinsia kutoka Makao Makuu ya Magereza, Mkaguzi wa Magereza, Amina Lidenge akijitambulisha kabla ya Ufunguzi rasmi wa Mafunzo ya Jinsia.
Mtoa Mada wa Kwanza kutoka Wizara ya Jamii, Jinsia na Watoto, Bi. Magreth Mussai akiwasilisha Mada yake kuhusiana na dhana ya Jinsia kama anavyoonekana katika picha.
Kamishna wa Sheria na Uendeshaji wa Magereza, Dkt. Juma Malewa(katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Maafisa, Askari na Watumishi raia wa Jeshi la Magereza(waliosimama) mara baada ya Ufunguzi rasmi wa Mafunzo ya Jinsia leo Desemba 29, 2014 katika Ukumbi wa Rombo Green View Hotel, (kushoto) ni Mkuu wa Magereza Mkoani Morogoro, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Magereza, Kato Rugainunura, (wa pili kushoto) ni Mtoa Mada wa Kwanza kutoka Wizara ya Jamii, Jinsia na Watoto, Bi. Magreth Mussai(wa pili kulia) ni Mkuu wa Gereza Kuu la Wanawake Kingolwila, Mrakibu Mwandamizi wa Magereza, Loyce Luhembe, (kulia) ni Mkuu wa Magereza Mkoani Tanga, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Magereza, Augustino Mboje
 
(Picha zote na Lucas Mboje wa Jeshi la Magereza).

Saturday, December 20, 2014

Waliochaguliwa kujiunga na Jeshi la Magereza

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI
(Jeshi la Magereza)
TANGAZO LA KUITWA CHUONI
Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza Tanzania Bara, anawatangazia wafuatao kuwa wamechaguliwa kujiunga na Jeshi la Magereza baada ya kufaulu mitihani ya usaili iliyofanyika kati ya tarehe 10 Desemba, 2014 hadi 17 Desemba, 2014 katika Bwalo Kuu la Maafisa Magereza Ukonga, Jijini Dar es Salaam pamoja na wale wa Kidato cha Nne na Sita waliosailiwa kutoka Kambi mbalimbali za JKT.

Wahusika wote wanatakiwa kuripoti Ofisi za Magereza za Mikoa husika ifikapo tarehe 30 Desemba, 2014 tayari kwa safari ya kwenda Chuo cha Mafunzo ya Awali kilichopo Kiwira Tukuyu Mkoani Mbeya. Mafunzo yatafunguliwa rasmi tarehe 8 Januari, 2015 hivyo mwisho wa kuripoti Chuoni ni tarehe 7 Januari, 2015. Yeyote atakayeshindwa kuripoti kwa tarehe ya mwisho iliyotamkwa kwenye tangazo hili hatapokelewa na atarudishwa kwa gharama zake.

Wahusika wanatakiwa kuzingatia mambo yafuatayo:-
i. Vyeti halisi vya masomo na kuzaliwa, vikiwa na nakala 5 za kila cheti,
ii. Picha za rangi(pass-port size) 5 za hivi karibuni,
iii. Fedha taslim Tzs.90,000/=,
iv. Kalamu za wino, kalamu za risasi na madaftari ya kutosha,
v. Chandarua cheupe cha duara ft 31/2, shuka nyeupe mbili, mto wenye foronya nyeupe zisizo na maua/maandishi,
vi. Cheti cha Afya kutoka Hospitali ya Serikali,
vii. Nguo za kiraia za kutosha, sweta, raba (brown au nyeusi) na soksi,
viii. Kwa wale wenye kadi za bima za afya waje nazo, na
ix. Kila mwanafunzi atajitegemea kwa nauli ya kwenda.

Tangazo hili linapatikana kwenye Mbao za Matangazo zilizopo Bwalo Kuu la Magereza, tovuti ya Magereza kwa anwani ya www.magereza.go.tz sanjari na blog ya Magereza kwa anwani ya www.magereza.blogspot.com


Imetolewa na Kamishna Jenerali wa Magereza.

J.C. Minja
KAMISHNA JENERALI WA MAGEREZA
Bofya hapo chini kuona majina ya waliochaguliwa kwa mchanganuo ufuatao:-

Wanahabari watembelea gereza kuu la wanawake Kingolwira-Morogoro, wampongeza Kamishna Jenerali Minja kwa juhudi kubwa za maboresho ndani ya magereza nchini

Mkuu wa Gereza Kuu la Wanawake Kingolwira, Mrakibu Mwandamizi wa Magereza, Loyce Ruhembe akiwakaribisha Wanahabari ambao wakitembelea gerezani hapo Desemba 19, 2014. Wanahabari hao wapo katika ziara ya kikazi katika miradi mbalimbali ya Uzalishaji mali inayotekelezwa kwa mafanikio makubwa na Jeshi la Magereza(kushoto) ni Mkuu wa Magereza Mkoani Mororogoro, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Magereza, Kato Rugainunula.

Mkuu wa Gereza Kuu la Wanawake Kingolwira - Morogoro, Mrakibu Mwandamizi wa Magereza, Loyce Ruhembe akikabidhi msaada huo kwa Mfungwa wa Kike ambaye ndiye Nyampara Mkuu wa Gereza Kuu la Wanawake Kingolwira - Morogoro. Wafungwa wa Gereza hilo wamewashukru Wanahabari hao kuwatembelea pamoja na msaada huo walioutoa na wameahidi kuwa raia wema mara wamalizapo vifungo vyao.
Msaada wa vitu mbalimbali vya Kibinadamu na vinavyoruhusiwa Magerezani vilivyokabidhiwa na Wanahabari walipotembelea Gereza Kuu la Wanawake Kingolwira - Morogoro Desemba 19, 2014.
Mkuu wa Gereza Kuu la Wanawake Kingolwira - Morogoro, Mrakibu Mwandamizi wa Magereza, Loyce Ruhembe akipokea rasmi msaada wa vitu mbalimbali vilivyotolewa na Wanahabari hao kwa ajili ya Wafungwa wa kike gerezani hapo walipotembelea Gereza hilo Desemba 19, 2014.

Wafungwa wa kike wa Gereza Kuu la Wanawake Kingolwira - Morogoro wakifuma mashuka katika Kiwanda cha Ushonaji cha Gereza hilo. Wafungwa hao wanapitiwa ujuzi wa aina mbalimbali ikiwemo Ushonaji wa nguo ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Programu za Urekebishaji ndani ya Magereza hapa nchini.
Muonekano wa mashuka na mito yake yanayofumwa na Wafungwa Wanawake katika Kiwanda cha Ushonaji cha Gereza Kuu la Wanawake Kingolwira - Morogoro.
Wanahabari wakionja chakula cha Wafungwa katika Gereza Kuu la Wanawake Kingolwira - Morogoro walipotembelea Gereza hilo Desemba 19, 2014(kulia) ni Mwandishi kutoka Gazeti la Habari Leo, Bi. Regina Kumba(kushoto) ni Mwandishi kutoka Gazeti la Daily News, Bw. Finning Simbeye(katikati) ni Mwanahabari kutoka Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa, Bi. Rose Mdami.
Mkuu wa Gereza Kuu la Wanawake Kingolwira - Morogoro, Mrakibu Mwandamizi wa Magereza, Loyce Ruhembe(katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Wanahabari walipotembelea Gereza hilo Desemba 19, 2014. Wa tatu kushoto ni Mkuu wa Magereza Mkoani Morogoro, Kamishna Msaidizi wa Magereza, Kato Rugainunula

(Picha zote na Lucas Mboje wa Jeshi la Magereza).

Thursday, December 18, 2014

Ziara ya kikazi ya wanahabari katika ujenzi wa mradi wa kilimo cha umwagiliaji gereza Idete mkoani Morogoro

Waandishi wa Habari kutoka Vyombo mbalimbali vya Daily News, Tanzania Daima, Habari Leo na Michuzi Blogu wakifanya mahojiano na Mkuu wa Gereza Idete(hayupo pichani) walipofanya ziara yao ya kikazi Desemba 17, 2014 kujionea ujenzi wa mradi wa Kilimo cha Umwagiliaji.
Mkuu wa Gereza Idete, Beno Hunja akiwaongoza Waandishi wa Habari kutembelea eneo kunakojengwa mradi wa Kilimo cha Umwagiliaji.
Sehemu ya Mbanio na chanzo Kikuu cha kupokelea maji yatakayotumika katika mradi wa Kilimo cha Umwagiliaji wa Gereza Idete.
Mfereji ambao tayari umekamilika kujengwa katika mradi wa Kilimo cha Umwagiliaji wa Gereza Idete, Mkoani Morogoro.
Wafungwa wa Gereza Idete wakilima shamba kwa kutumia trekta kama inavyoonekana katika picha. Wafungwa hao wamepatiwa ujuzi wa kulima na trekta wakiwa gerezani ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Programu mbalimbali za Urekebishaji zinazofanywa na Jeshi la Magereza hapa nchini. Kwa wastani Wafungwa hao hulima hekari 10 kwa siku.

(Picha zote na Lucas Mboje wa Jeshi la Magereza).

Monday, December 15, 2014

Waandishi wa habari watembelea miradi ya uzalishaji mali ya Jeshi la Magereza mkoani Arusha na Kilimanjaro

Mkuu wa Magereza Mkoani Arusha, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Magereza, Hamis Nkubas akifanya mahojiano maalum Ofsini kwake  na Waandishi wa Habari kutoka Vyombo vya Habari vya Habari Leo, Daily News, Michuzi Media na Gazeti la Tanzania Daima. Waandishi haowameanza ziara leo Desemba 15, 2014 ambapo watatembelea katika miradi mbalimbali ya uzalishaji mali inayotekelezwa kwa mafanikio na Jeshi la Magereza.
Viti vya Ofisi ambavyo vimetengenezwa katika Kiwanda cha Samani Arusha cha Jeshi la Magereza. Viti hivyo vitatumiwa katika Ofisi za Jimbo kwa Waheshimiwa Wabunge wa Bunge la Jamhuri  Muungano wa Tanzania.
Viatu vya ngozi vinavyotengenezwa kwa ustadi mkubwa katika Kiwanda cha Viatu vya ngozi cha Gereza Kuu Karanga Moshi kama vinavyoonekana katika picha.
Waandishi wa Habari wakiangalia viatu vya ngozi vinavyotengenezwa katika Kiwanda cha ngozi cha Gereza Kuu Karaga Moshi(wa pili kushoto) ni Mwandishi kutoka Daily News, Bw. Fining Simbeye(wa tatu kushoto) ni Mwandishi kutoka Gazeti la Tanzania Daima, Bw. Edson Kamkara.
Mkuu wa Magereza Mkoani Kilimanjaro, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Magereza, Venant Kayombo(wa tano kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na Waandishi wa Habari kutoka Magazeti ya Daily News, Tanzania Daima, Habari Leo pamoja na Globu ya Michuzi

(Picha zote na Lucas Mboje wa Jeshi la Magereza).

Friday, December 12, 2014

Makabidhiano ya mkataba wa makubaliano ya mradi wa ubia wa uchimbaji madini ya chokaa kati ya shirika la Jeshi la Magereza na kampuni ya Twiga Cement yafanyika leo jijini Dar

Kamishna Jenerali wa Magereza John Casmir Minja akimkabidhi Mkataba wa Makubaliano ya mradi uchimbaji madini Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Twiga Cement, Bw. Alphonso Rodrudges. Shirika la Magereza limeingia ubia katika mradi huo na Kampuni ya Twiga Cement katika eneo la Jeshi la Magereza, Wazo Hill lililopo jijini Dar es Salaam ambapo hafla hiyo imefanyika leo Desemba 12, 2014 katika Ofisi za Makao Makuu ya Jeshi la Magereza.
Kamishna Jenerali wa Magereza John Casmir Minja akiwa makini kumsikiliza Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Twiga Cement, Bw. Alphonso Rodrudges(hayupo pichani) kabla ya makabidhiano rasmi ya Mkataba wa Makubaliano ya mradi wa ubia wa uchimbaji madini ya chokaa. Shirika la Magereza limeingia ubia katika mradi huo na Kampuni ya Twiga Cement katika eneo la Jeshi la Magereza, Wazo Hill lililopo jijini Dar es Salaam ambapo hafla hiyo imefanyika leo Desemba 12, 2014 katika Ofisi za Makao Makuu ya Jeshi la Magereza.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Twiga Cement, Bw. Alphonso Rodrudges(kushoto) akifuatilia majadiliano kabla ya makabidhiano rasmi ya Mkataba wa Makubaliano ya mradi wa ubia wa uchimbaji madini ya chokaa.Shirika la Magereza limeingia ubia katika mradi huo na Kampuni ya Twiga Cement katika eneo la Jeshi la Magereza, Wazo Hill lililopo jijini Dar es Salaam(kulia) ni Mkurugenzi wa Fedha wa Kampuni ya Twiga Cement.
Maafisa Waandamizi wa Jeshi la Magereza waliohuhuria hafla hiyo ya makabidhiano rasmi ya Mkataba wa Makubaliano ya mradi wa ubia wa uchimbaji madini ya chokaa(wa kwanza kulia) ni Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Magereza, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Magereza, John Masunga(wa kwanza kushoto) ni Afisa Ugavi Mkuu wa Shirika la Magereza,  Mrakibu wa Magereza, George Wambura

(Picha zote na Lucas Mboje wa Jeshi la Magereza).

Thursday, December 4, 2014

Kuitwa kwenye usaili04 Desemba 2014

KUITWA KWENYE USAILI

Jeshi la Magereza linawatangazia wafuatao kufika kwenye usaili kwa nafasi walizoomba. Usaili huo utafanyika kuanzia tarehe 10/12/2014 mpaka tarehe 17/12/2014 katika Ukumbi wa Bwalo Kuu la Magereza Ukonga Jijini Dar es salaam kuanzia 2:00 asubuhi kwa mujibu wa tarehe za makundi kama yalivyoainishwa. Kwa wale wa kidato cha Nne na Sita waliosailiwa kupitia Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) wasubiri maelekezo mengineyo. Aidha wale ambao hawakuona majina yao hapa wahesabu kuwa hawakufanikiwa.

Waombaji wanatakiwa kuzingatia  yafuatavyo;-

i.    Kuja na Vyeti halisi (Original Certificates) vya elimu na ujuzi

ii.    Kuja naCheti halisi cha kuzaliwa,

iii.    Hati za matokeo ya mitihani (Result Slip/Statements) hazitakubaliwa isipokuwa kwa wahitimu ambao vyeti vyao halisi havijatolewa na vyuo husika wakiwa na barua Maalum ya kuthibitisha kwamba vyeti halisi havijatolewa,

iv.    Wahusika watajitegemea kwa nauli za kuja na kurudi, chakula na malazi kwa kipindi chote cha usaili

Tangazo hili pia linapatikana kwenye Mbao za Matangazo zilizopo Bwalo Kuu la Magereza, tovuti ya magereza kwa anwani ya www.magereza.go.tz, gazeti la Uhuru la tarehe 05 Desemba 2014 sanjari na blog ya magereza kwa anwani ya www.magereza.blogspot.com

Imetolewa na Kamishna Jenerali wa Magereza

J.C.Minja

KAMISHNA JENERALI WA MAGEREZA


Bofya HAPA kupata orodha ya wanaotakiwa kufika kwenye usaili