Wednesday, December 31, 2014

Kamishna Jenerali wa Magereza John Minja ahutubia baraza la kufunga mwaka 2014 na kuukaribisha mwaka mpya 2015, makao makuu ya Magereza, D'Salaam

 
Kamishna Jenerali wa Magereza, John Casmir Minja akitoa hotuba yake fupi katika Baraza la kufunga Mwaka 2014 na kuukaribisha Mwaka Mpya 2015 katika Ofisi za Makao Makuu ya Magereza(kulia) ni Kamishna wa Sheria na Uendeshaji wa Magereza, Dkt. Juma Malewa(kushoto) ni Mnadhimu Mkuu wa Jeshi la Magereza, Kamishna Mwandamizi Msaidizi wa Magereza, Mmeta Manyala.

Baadhi ya Maafisa na Askari wa Jeshi la Magereza kutoka Ofisi ya Makao Makuu ya Magereza pamoja na Mkoa wa Dar es Salaam wakisikiliza kwa makini hotuba ya Kamishna Jenerali wa Magereza.

Kamishna wa Sheria na Uendeshaji wa Magereza, Dkt. Juma Malewa akitoa neno la shukrani kwa Kamishna Jenerali wa Magereza, John Casmir Minja(katikati) mara baada ya kutoa hotuba fupi katika Baraza la kufunga Mwaka 2014 na kuukaribisha Mwaka Mpya 2015.

Maafisa na Askari wa Jeshi la Magereza kutoka Ofisi ya Makao Makuu ya Magereza pamoja na Mkoa wa Dar es Salaam wakiwa wamesimama kwa ajili ya kuwakumbuka na kuwaombea kwa Mwenyezi Mungu Watumishi wenzao ambao wametangulia mbele ya haki kwa mwaka huu 2014.


Na Inspekta Lucas Mboje, Jeshi la Magereza
Kamishna Jenerali wa Magereza Nchini, John Casmir Minja amewaasa Maafisa na Askari wa Jeshi la Magereza nchini kuzingatia Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo katika utendaji wao wa kazi za kila siku ili kuleta ufanisi kazini.

Kamishna Jenerali John Minja ameyasema hayo leo wakati wa Baraza la Kufunga Mwaka 2014 na kuukaribisha Mwaka 2015 lililowahusisha baadhi ya Maafisa na Askari kutoka Makao Makuu ya Jeshi la Magereza pamoja na Magereza Mkoa wa D'Salaam.

Aidha, amewataka Maofisa, Askari na Watumishi wote kuacha tabia ya kufanya kazi kwa mazoea bali wawe wabunifu kwa kutumia raslimali zilizopo kwenye maeneo yao ya kazi ili kukabiliana na changamoto mbalimbali zilizopo.

" Kila mmoja wenu atimize wajibu wake katika eneo lake la kazi kwa bidii, ari na moyo wa kujituma ili kuliwezesha Jeshi kupata ufanisi unaotarajiwa". Alisisitiza Jenerali Minja.

Wakati huo huo Kamishna Jenerali wa Magereza Nchini, John Casmir Minja pia ametumia fursa hiyo kuelezea baadhi ya mafanikio mbalimbali yaliyopatikana kwa Mwaka uliopita 2014 ambapo Jeshi la Magereza limepata jumla ya leseni 102 za uchimbaji wa madini ya ujenzi kama vile chokaa, mawe, kokoto, mchanga na Murram katika maeneo mbalimbali ya magereza ambayo ni Gereza Wazo Hill - D’Salaam, Gereza Msalato - Dodoma, Kambi Bahi - Dodoma, Gereza Maweni - Tanga, Gereza Lilungu - Mtwara, Gereza Butimba - Mwanza na Gereza Kalilankulukulu - Katavi. Leseni hizo zitatumika kuingia ubia na wawekezaji wenye nia ya kushirikiana na Jeshi katika uchimbaji wa madini.

Pili, Shirika la Magereza limeeingia Mkataba wa ubia na Kiwanda cha Saruji Wazo (Twiga Cement) katika uchimbaji wa madini ya ujenzi Gereza Wazo Hill. Aidha, Kiwanda hicho katika kutekeleza wajibu kwa jamii wametoa msaada wa mifuko ya saruji 1200 na Tzs.100, 000, 000.00 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za makazi ya askari Gereza Wazo Hill. Pia Shirika la Magereza limeingia makubaliano na Mfuko wa Mafao ya Kustaafu wa GEPF kwa ajili ya ujenzi na uendeshaji wa vituo vya biashara (business malls) kwenye maeneo ya Gereza Kihonda, Morogoro na Gereza Karanga, Moshi.
Tatu, Rasimu ya kwanza ya Sera ya Taifa ya magereza imekamilika na tayari imewasilishwa kwenye mamlaka za juu kwa hatua zaidi. Kukamilika kwa sera hiyo kutawezesha Jeshi kutekeleza Mpango Mkakati wa Sera na Maboresho ya Jeshi kwa ujumla.

Pamoja na Mafanikio hayo, Kamishna Jenerali Minja ameelezea maeneo yatakayopewa kipaumbele kwa Mwaka huu wa 2015 ikiwemo Jeshi litaendeleza jitihada za kuimarisha na kuongeza uzalishaji kwenye miradi mbalimbali ya Jeshi la Magereza. Jitihada hizi ni pamoja kutangaza fursa zilizopo ili kuwavutia wawekezaji mbalimbali wa ndani na nje ya nchi waje kuingia ubia katika miradi hiyo kwa kuleta mitaji na teknolojia, pia Kuendeleza mikakati ya kupunguza msongamano magerezani

Baraza la kufunga Mwaka na kuukaribisha Mwaka unaofuata ni utamaduni wa siku nyingi ambao unaenziwa na Viongozi Wakuu wa Jeshi la Magereza. Baraza la aina hii hufanyika kila Mwaka ambapo Kamishna Jenerali wa Magereza Nchini hupata fursa ya kuongea na Watumishi wote wa Jeshi la Magereza nchini kupitia Baraza hilo lengo ikiwa ni kufanya tathmini ya yale yaliyojiri katika Jeshi kwa kipindi cha Mwaka unaisha kwa kuzungumzia mafanikio na changamoto zilizojitokeza na kutazama matarajio ya Mwaka mpya