Mojawapo ya Jukumu la Jeshi la Magereza ni kuwapeleka mahakamani mahabusu na kuwarudisha magerezani.

Gadi ya askari Wanawake na Wanaume wa Jeshi la Magereza katika Maadhimisho ya Sherehe za Kitaifa.

Ng'ombe bora wa Nyama na Maziwa ni sehemu ya miradi ya Uzalishaji inayoendeshwa na kusimamiwa na Jeshi la Magereza nchini.

Sehemu ya Mashamba makubwa yanayoendeshwa na Jeshi la Magereza: Shughuli za Kilimo cha Mashamba makubwa, madogo na bustani za mboga mboga ni moja ya shughuli za Magereza katika kuwafunza wafungwa namna ya kujitegemea mara wamalizapo vifungo vyao.

Baadhi wa wafungwa katika Kiwanda cha Ushonaji nguo cha Gereza Kuu Ukonga wakiwa kazini: Shughuli za Ushonaji wa nguo ni moja ya eneo ambalo wafungwa hupata huduma za urekebishwaji kwa vitendo.

Monday, June 3, 2019

WAZIRI MKUU, KASSIM MAJALIWA AFUNGUA RASMI GEREZA JIPYA LA WILAYA YA RUANGWA, LEO MKOANI LINDI

Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa akisalimiana na Kamishna Jenerali wa Magereza, Phaustine Kasike alipowasili kwenye hafla ya ufunguzi wa Gereza la Wilaya ya Ruangwa leo Juni 3, 2019.

Kamishna Jenerali wa Magereza, Phaustine Kasike akitoa historia fupi ya ujenzi wa Gereza la Wilaya Ruangwa kabla ya kumkaribisha Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa kufungua rasmi Gereza hilo, leo Juni 3, 2019.
Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa akitoa hotuba fupi kabla ya ufunguzi wa Gereza la Wilaya ya Ruangwa. Kushoto ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya nchi, Mhe. Kangi Lugola. 
Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa(kulia) akisoma jiwe la msingi kabla ya ufunguzi wa Gereza la Wilaya ya Ruangwa leo Juni 3, 2019. Kushoto ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya nchi, Mhe. Kangi Lugola.

Baadhi ya Askari wa Gereza Ruangwa wakifuatilia hotuba ya Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa katika hafla ya ufunguzi wa Gereza hilo, leo Juni 3, 2019.

Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa akiongea na wafungwa na mahabusu wa Gereza Ruangwa(hawapo pichani) baada ya uzinduzi wa Gereza hilo leo.

Muonekano wa nje wa Gereza la Wilaya ya Ruangwa  (Picha zote na Kitengo cha Habari na Mawasiliano – Jeshi la Magereza).

WAZIRI MKUU MAJALIWA: KAMILISHENI UJENZI WA MAGEREZA YA WILAYA MPYA

WAZIRI MKUU MAJALIWA: KAMILISHENI UJENZI WA MAGEREZA YA WILAYA MPYA


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameuagiza uongozi wa Jeshi la Magereza nchini ukamilishe mkakati wa ujenzi wa magereza za wilaya kwa wilaya zisizokuwa na magereza.

Ametoa agizo hilo leo (Jumatatu, Juni 3, 2019) wakati akifungua Gereza la wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi. Uzinduzi huo umefanyika kwenye viwanja vya gereza hilo. 

Amesema uwepo wa magereza katika wilaya zote nchini utasaidia kumaliza tatizo la msongamano wa wafungwa na mahabusu kwenye magereza ya jirani.

“Kutokuwepo kwa magereza ya wilaya kunasababisha msongamano wa wafungwa na mahabusu katika magereza ya jirani, pamoja na kuchelewesha upatikanaji wa haki.” Amesema Majaliwa.

Majaliwa amesema kwamba ufunguzi wa gereza la Ruangwa utatatua tatizo la msongamano wa wafungwa na mahabusu katika Gereza la wilaya ya Nachingwea 

Awali wakazi wa wilaya hiyo waliokabiliwa na tuhuma mbalimbali au waliohukumiwa vifungo walikuwa wakipelekwa katika Gereza la wilaya ya Nachingwea.

Amesema kitendo cha kupelekwa Nachingwea kilikuwa kikiwanyima wafungwa na mahabusu fursa ya kuonana na ndugu au mawakili wao kutokana na umbali uliokuwepo.

“Mbali na ndugu na jamaa kushindwa kwenda kuwaona ndugu zao pia Jeshi la Polisi lilikuwa likilaumiwa kuwa linawachelewesha mahubusu kuja kusikiliza mashauri yao.”

Waziri Mkuu amesema uwepo wa gereza hilo katika wilaya ya Ruangwa umeipunguzia Serikali gharama za kuwasafirisha mahabusu na wafungwa kwenda Nachingwea. 

Awali, Waziri waMambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola amesema Gereza la Wilaya ya Ruangwa ni nyenzo muhimu katika kuimarisha ulinzi na usalama wa wilaya hiyo.

Amesema gereza hilo ni chachu ya kuimarika kwa uchumi wa wilaya hiyo kwa kupitia sekta ya kilimo kwani kutakuwa na kambi za kilimo, hivyo wananchi nao watajifunza.  

 “Wananchi msilione gereza hili kama adui kwenu, halijaja kuwafunga bali lipo kwa ajili ya kuimarisha amani, ulinzi na usalama wa wilaya yetu pamoja na kutoa elimu mbalimbali.”
Kwa upande wake, Kamishna Jenerali wa Magereza Phaustine Kasike amesema ujenzi huo umefanywa na kikosi cha ujenzi cha Magereza kwa kutumia nguvukazi ya wafungwa.

Amesema awamu ya kwanza ya ujenzi wa gereza hilo imekamilika na imegharimu sh. bilioni 1.5 hivyo umekamilisha uwepo wa magereza katika wilaya zote za mkoa wa Lindi.

Kamishna huyo amesema ujenzi huo ungefanywa na mkandarasi wa nje ungegharimu sh. bilioni 2.226, hivyo kwa kutumia kikosi cha Magereza wameokoa sh. milioni 635.675.

Amesema kwa sasa gereza hilo lina uwezo wa kuwahifadhi wahalifu 250 hadi 280 na likikamilika itakuwa na uwezo wa kuwahifadhi wahalifu 500.

Kamishna Kasike amesema gereza hilo lina ardhi yenye ukubwa wa ekari 80, ambapo ekari saba zitatumika kwa ajili ya majengo ya gereza, maegezo ya magari na karakana.

“Ekari 56 zitatumika kwa ajili ya ujenzi wa nyumba 100 za makazi, ekari sita ujenzi wa majengo ya huduma kama zahanati na ekari nane zitatumika katika kilimo cha bustani.”

Baadhi ya wananchi waliohudhuria ufunguzi huo wameishukuru Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli kwa kuboresha huduma za jamii.

Mmoja wa wananchi hao Zena Selemani amesema kabla ya ujenzi wa gereza hilo walikuwa wanashindwa kuwatembelea ndugu zao walofungwa katika gereza la Nachingwea.