Mojawapo ya Jukumu la Jeshi la Magereza ni kuwapeleka mahakamani mahabusu na kuwarudisha magerezani.

Gadi ya askari Wanawake na Wanaume wa Jeshi la Magereza katika Maadhimisho ya Sherehe za Kitaifa.

Ng'ombe bora wa Nyama na Maziwa ni sehemu ya miradi ya Uzalishaji inayoendeshwa na kusimamiwa na Jeshi la Magereza nchini.

Sehemu ya Mashamba makubwa yanayoendeshwa na Jeshi la Magereza: Shughuli za Kilimo cha Mashamba makubwa, madogo na bustani za mboga mboga ni moja ya shughuli za Magereza katika kuwafunza wafungwa namna ya kujitegemea mara wamalizapo vifungo vyao.

Baadhi wa wafungwa katika Kiwanda cha Ushonaji nguo cha Gereza Kuu Ukonga wakiwa kazini: Shughuli za Ushonaji wa nguo ni moja ya eneo ambalo wafungwa hupata huduma za urekebishwaji kwa vitendo.

Saturday, May 21, 2016

Katibu mkuu mambo ya ndani ya nchi atunuku vyeo kwa maafisa 327 wa jeshi la magereza, chuo cha magereza kiwira, mkoani Mbeya

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Meja Jenerali Rwegasira akiwa katika Jukwaa akipokea Salaam ya heshima kutoka kwa Gwaride Maalum lililoandaliwa na Wahitimu wa Mafunzo ya Uongozi Daraja la Pili katika sherehe za kufunga Mafunzo hayo ya Maofisa wa Jeshi la Magereza, Chuo cha Magereza Kiwira kilichopo, Rungwe Mbeya(kushoto) ni Kamishna Jenerali wa Magereza, John Casmir Minja.
Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani, Meja Jenerali Rwegasira akikagua moja ya Gadi ya Wanaume inayoundwa Gwaride rasmi la sherehe hizo.
Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Meja Jenerali Rwegasira akimvisha cheo cha Mkaguzi Msaidizi wa Magereza mmoja wa Wanafunzi Wahitimu kwa niaba ya Wahitimu wote wa Mafunzo ya Uongozi Daraja la Pili. Mwanafunzi huyo amefanya vizuri katika Mafunzo hayo.
Onesho Maalum la kujihami kutoka kwa Askari wa Jeshi la Magereza katika namna ya kupambana na adui yeyote wanapokuwa wakitekeleza majukumu yao. 
Kamishna Jenerali wa Magereza Nchini, John Casmir Minja(kushoto) akifurahia jambo na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya nchi(katikati). Kulia ni Mkuu wa Chuo cha Magereza Kiwira, SACP. Stanford Ntirundura.
Askari Wanafunzi ambao wanaendelea na Mafunzo yao ya Awali wakifuatilia sherehe hizo za kufunga Mafunzo ya Uongozi Daraja la Pili.
Maafisa Wandamizi wa Jeshi la Magereza kutoka Makao Makuu ya Jeshi la Magereza wakiteta jambo mara baada ya kufungwa rasmi kwa Mafunzo ya Uongozi Daraja la Pili(kulia) ni ACP. Solomon Urio(katikati) ni ACP. Lazaro nyanga(kushoto) ni ACP. Ismail Mlawa.
(Picha zote na Lucas Mboje).


Na; Lucas Mboje, Rungwe

JUMLA ya Askari 327 wa Jeshi la Magereza, kati yao wanaume 257 na wanawake 81 wametunukiwa  cheo cha Mkaguzi Msaidizi wa Magereza baada ya kuhitimu mafunzo ya Uongozi daraja la Pili kozi namba 1 katika Chuo cha Magereza Kiwira, Wilayani Rungwe Mkoa wa Mbeya.

Cheo hicho wametunukiwa na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya nchi, Meja Jenerali Projest Rwegasira katika Sherehe za ufungaji wa mafunzo hayo zilizofanyika katika Viwanja vya Chuo hicho leo Mei 20, 2016.

Akizungumza katika sherehe hizo Meja Jenerali Rwegasira amesema Askari na Maafisa wa Jeshi la Magereza nchini wanatakiwa kufanya kazi kwa kuzingatia Haki za Binadamu na Utawala Bora kila wakati wanapotekeleza majukumu yao ya kazi.

Jenerali Rwegasira amesema Maafisa hao wahitimu wakazingatie elimu waliyopewa wakati wa mafunzo ili wakawe mfano kipindi cha utendaji kazi wao ikiwa ni pamoja na kuhamasisha na kuwaongoza wenzao ambao hawakupatiwa elimu kama yao.

Aidha, amewaasa kutowatesa Wafungwa walioko magerezani bali kuwahudumia kwa kuzingatia kanuni na taratibu za uendeshaji wa magereza kwani Wafungwa ni Binadamu kama watu wengine ispokuwa tu wameikosea jamii.

"Tuzingatie falsafa ya kwamba mfungwa yupo gerezani kwa ajili ya kutumikia adhabu na si kwa kuongezewa adhani. Kwa kufanya hivyo, Serikali yetu itakuwa inazingatia Utawala wa Sheria na hivyo kuwa Taifa linalozingatia na kuheshimu Haki za Binadamu na Utawala Bora". Alisisitiza Jenerali Rwegasira.

Akizungumza kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi Kamishna Jenerali wa Magereza nchini, John Casmir Minja amesema kuwa changamoto nyingi ambazo kwa kiasi fulani zimeathili utekelezaji wa majukumu ya Jeshi hilo ni pamoja na ufinyu wa bajeti, makazi duni ya maafisa na askari, uhaba wa vitendea kazi na uchakavu wa vyombo vya usafiri.

Kamishna Jenerali Minja ameongeza kuwa tayari Jeshi hilo limechukua hatua mbalimbali za kufanya maboresho kwa lengo la kufanya Jeshi la Magereza kuwa la kisasa katika kutekeleza majukumu yake kisayansi na kwa ufanisi unaotarajiwa.

Thursday, May 19, 2016

Katibu mkuu wizara ya mambo ya ndani ya nchi kufunga mafunzo ya uongozi daraja la pili kwa maafisa wa jeshi la magereza, jijini Mbeya


Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Meja Jenerali Projest Rwegasira kesho tarehe 20 Mei, 2016 saa 3:00
asubuhi anatarajia kufunga Mafunzo ya Uongozi Daraja la Pili katika Chuo cha Magereza, Kiwira Mkoani Mbeya.

Mafunzo hayo ambayo yamechukua muda wa miezi mitatu yalilenga kuwaandaa Maafisa(pichani) kuwa viongozi wa kati katika vituo vya Magereza nchini. Jumla ya wahitimu ni 327, kati yao Wanaume 246 na Wanawake 81, Aidha Wanaume 08 na Wanawake 02 wanatoka Vyuo vya Mafunzo Zanzibar. 

Sherehe hizo, zitajumuisha mambo yafuatayo:- 
* Mgeni Rasmi kukagua Gwaride rasmi lililoandaliwa na wahitimu hao; 
* Mgeni Rasmi kutoa vyeti kwa Wanafunzi waliofanya vizuri katika Mafunzo ya darasani na
  Mafunzo ya mbinu za medani; 
* Mgeni Rasmi kuvisha cheo cha Mkaguzi Msaidizi wa Magereza kwa wahitimu wawili kwa niaba
  ya wahitimu wengine na; 
* Mgeni Rasmi kutoa Hotuba. 

Sherehe za ufungaji wa Mafunzo hayo zinatarajia kukamilika saa 8:00 mchana. Vyombo vya Habari vinakaribishwa 
kwenye sherehe hizo siku ya Ijumaa  tarehe 20 Mei, 2016 kuanzia saa 3:00 asubuhi. 


IMETOLEWA NA KITENGO CHA HABARI NA MAWASILIANO 
MAKAO MAKUU YA JESHI LA MAGEREZA 
Mei 19, 2016

Wednesday, May 18, 2016

Magereza na mavunzo ya ujasiliamali kwa wafungwa






JESHI LA MAGEREZA NCHINI LASAINI MKATABA WA UFUNDISHAJI ELIMU YA UJASILIAMALI KWA WAFUNGWA LEO 18.05.2016-DAR ES SALAAM

Jeshi la Magereza limesaini Mkataba (MoU) na Taasisi isiyo ya Kiserikali ya Technoserve – Tanzania kushirikiana katika ufundishaji wa wafungwa mafunzo ya Ujasiriamali wakiwa wanakaribia kumaliza vifungo vyao magerezani ili stadi hizo ziwasaidie kumudu maisha mapya baada ya kutumikia adhabu zao. 

Programu hii itaendeshwa katika Mkoa wa Mbeya kwa kushirikiana na Mfuko wa “Master Card”  kwa vijana wa kike na kiume wenye umri kati ya miaka 18 hadi 30 hivyo wafungwa walioko katika Magereza yaliyomo Mkoani humo na wengine wenye sifa toka Kanda ya Nyanda za Juu Kusini ili kupata mafunzo kupitia progamu ya uimarishaji wa maendeleo ya vijana vijijini kupitia biashara “STRYDE” inayoendeshwa na Taasisi hiyo.

Takwimu za sasa zinaonesha kwamba kati ya asilimia 30 na 35 ya wafungwa wanaomaliza vifungo vyao hurejea magerezani.Hivyo, mafunzo haya yatalenga kuwafanya  wanapomaliza vifungo vyao waweze kupata maarifa ya kuanzisha shughuli zao wenyewe za kujipatia kipato halali na kuacha vitendo vya uhalifu katika jamii wanamoishi vinavyowafanya kurejea magerezani.

Aidha,  mafunzo haya ya Ujasiriamali yatajikita katika kuwafundisha kilimo biashara, matumizi mazuri ya fedha binafsi, uwezo wa kutumia ujuzi, ubunifu na tafakari ya kina katika kufanya maamuzi, mpango biashara, mawazo ya biashara na uwezo wa kuandaa mpango biashara n.k.

Ushirikiano huu ni mkakati endelevu wa Jeshi la Magereza katika kuboresha Programu za Urekebishaji wa wafungwa magerezani ili wawe raia wema na wenye tija katika jamii na Taifa kwa ujumla. 

Program za Ujasiriamali kwa wafungwa zinaendeshwa pia katika baadhi ya Magereza kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kama vile Dorcas International na New Life in Christ katika Gereza la Karanga – ushonaji viatu, ufumaji na uokaji mikate, Gereza Arusha – uokaji mikate, ufundi seremala na ufumaji. 

Jeshi la Magereza linawakaribisha wadau wa ndani na nje kushirikiana katika urekebishaji wa tabia za wafungwa ili wawe na michango chanya katika jamii na Taifa kwa ujumla.


IMETOLEWA NA KITENGO CHA HABARI NA MAWASILIANO
MAKAO MAKUU YA JESHI LA MAGEREZA
DAR ES SALAAM

Kamishna jenerali wa magereza nchini kuvisha vyeo maafisa wa jeshi la magereza, leo jijini Dar


Kamishna Jenerali wa Magereza Nchini, John Casmir Minja leo tarehe 18 Mei, 2016 saa 8:00 mchana atawavisha vyeo Maafisa wa Jeshi la Magereza wa ngazi mbalimbali wa Mkoa wa Dar es Salaam waliopandishwa vyeo kwa mujibu wa Sheria.

Kwa Mamlaka aliyopewa kisheria na Tume ya Polisi na Magereza ya Mwaka 1990, Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza atawavisha vyeo hivyo katika Viwanja vya Chuo cha Taaluma ya Urekebishaji kilichopo Ukonga, Jijini Dar es Salaam.

Tume ya Polisi na Magereza katika Kikao chake Namba 5/2015/2016 kilichofanyika tarehe 13 Mei, 2016 chini ya Mwenyekiti wake Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Charles Kitwanga(Mb) imewapandisha vyeo Maafisa 310 wa ngazi mbalimbali kuanzia tarehe 16 Mei, 2016.
Maafisa hao waliopandishwa vyeo ni Mrakibu Mwandamizi wa Magereza kuwa Kamishna Msaidizi wa Magereza 45, Mrakibu wa Magereza kuwa Mrakibu Mwandamizi wa Magereza 37, Mrakibu Msaidizi wa Magereza kuwa Mrakibu wa Magereza 90 na Mkaguzi Msaidizi wa Magereza kuwa Mkaguzi wa Magereza 138.

Imetolewa na; Mrakibu Msaidizi wa Magereza, Lucas Mboje, Afisa Habari wa Jeshi la Magereza,Makao Makuu ya Jeshi la Magereza,
                
DAR ES SALAAM
18 Mei, 2016.

Tuesday, May 3, 2016

Katibu wa bunge akutana na viongozi wa jeshi la magereza na SUMA - JKT, jijini Dar, utengenezaji wa madawati ya shule nchini kuanza muda wowote

Katibu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Thomas Kashilila akiongea na Viongozi wa Jeshi la Magereza pamoja na SUMA - JKT kwenye Ofisi za Bunge, Jijini Dar es Salaam kuhusiana na namna walivyojipanga katika kutekeleza jukumu la utengenezaji wa Madawati ya shule hapa nchini.
Katibu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Thomas Kashilila akiongoza mazungumzo na Viongozi wa Jeshi la Magereza pamoja na SUMA - JKT(hawapo pichani).
Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza, CGP John Casmir Minja(wa kwanza kushoto) akiwa pamoja na Maafisa Waandamizi wa Jeshi hilo wakifuatilia kwa makini mazungumzo na Katibu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Thomas Kashilila(hayupo pichani).
Mtendaji Mkuu wa SUMA - JKT, Bregedia Jenerali C. Yateri akifuatilia mazungumzo hayo na Maofisa Watendaji wa Shirika hilo la SUMA - JKT.
Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza, CGP John Casmir Minja akiteta jambo na Mtendaji Mkuu wa SUMA - JKT, Bregedia Jenerali C. Yateri walipokutana leo Mei 3, 2016 katika Ofisi za Bunge, Jijini Dar es Salaam

(Picha zote na Lucas Mboje wa Jeshi la Magereza).