Tuesday, April 24, 2018

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI


MSAMAHA WA RAIS KWA WAFUNGWA KATIKA KUADHIMISHA MIAKA 54
YA MUUNGANO WA TANZANIA TAREHE 26 APRILI, 2018

Katika kuadhimisha Miaka 54 ya Muungano wa Tanzania tarehe  26 Aprili, 2018 Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutumia madaraka aliyopewa chini ya Ibara ya 45(1)(d) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ametoa msamaha kwa wafungwa wafuatao:-

(i)      Wafungwa wote wapunguziwe robo (1/4) ya adhabu zao baada ya punguzo la kawaida la moja ya tatu (1/3) linalotolewa chini ya Kifungu 49(1) cha Sheria ya Magereza Sura ya 58, wafungwa hao  sharti wawe wametumikia robo (1/4) ya adhabu zao gerezani isipokuwa wafungwa walioorodheshwa katika Ibara ya 2(i – xxi).

(ii)        Wafungwa wagonjwa wenye magonjwa kama UKIMWI, Kifua kikuu (TB) na Saratani (Cancer) ambao wako kwenye “terminal stage”. Wafungwa hawa wathibitishwe na Jopo la Waganga chini ya Uenyekiti wa Mganga Mkuu wa Mkoa/Mganga Mkuu wa Wilaya.

(iii)       Wafungwa wazee wenye umri wa miaka sabini (70) au zaidi.  Umri huo uthibitishwe na Jopo la Waganga chini ya Uenyekiti wa Mganga Mkuu wa Mkoa/Mganga Mkuu wa Wilaya.

(iv)       Wafungwa wa kike walioingia na mimba gerezani, pamoja na wale walioingia na watoto wanaonyonya na wasionyonya.

(v)         Wafungwa wenye ulemavu wa mwili na akili (Physical disability and mental disability). Ulemavu huo uthibitishwe na Jopo la Waganga chini ya Uenyekiti wa Mganga Mkuu wa Mkoa/Mganga Mkuu wa Wilaya.

2.      Aidha, Msamaha wa Mheshimiwa Rais hautawahusu wafungwa wafuatao:-

(i)              Wafungwa waliohukumiwa adhabu ya kunyongwa au kwa makosa ya kujaribu kuua (attempt to murder).

(ii)       Wafungwa waliohukumiwa adhabu ya kunyongwa na adhabu hiyo kubadilishwa kuwa kifungo cha maisha au kifungo gerezani.

(iii)           Wafungwa waliohukumiwa kifungo cha maisha gerezani.

(iv)    Wafungwa wanaotumikia kifungo kwa makosa ya kujihusisha na usafirishaji na matumizi ya madawa ya kulevya kama vile cocaine, heroin, bhangi n.k.

(v)     Wafungwa wanaotumikia kifungo kwa makosa ya kujihusisha na uombaji na upokeaji au utoaji rushwa.

(vi)      Wafungwa wanaotumikia kifungo kwa makosa ya unyang’anyi na unyang’anyi wa kutumia silaha au kujaribu kutenda makosa hayo (robbery with violence, armed robbery and attempted robbery).

(vii)    Wafungwa wanaotumikia kifungo kwa makosa ya kupatikana na silaha, risasi au milipuko isivyo halali (fire arms, ammunitions and explosives).

(viii)        Wafungwa wanaotumikia kifungo kwa makosa ya shambulio la aibu, kunajisi, kubaka na kulawiti, ukatili dhidi ya watoto au kujaribu kutenda makosa hayo.

(ix)           Wafungwa waliopatikana na hatia na kuhukumiwa kifungo kwa kosa la kuwapa mimba wanafunzi wa Shule za Msingi na Shule za Sekondari na ambao walitenda kosa hilo wakiwa na umri wa miaka kumi na nane (18) na kuendelea.

(x)             Wafungwa wanaotumikia kifungo kwa makosa ya wizi wa magari na pikipiki, uharibifu wa miundombinu au kujaribu kutenda makosa hayo.

(xi)           Wafungwa wanaotumikia kifungo chini ya Sheria ya Bodi ya Parole (Act. No. 25/1994), Sheria ya Huduma kwa Jamii (Act. No. 6/2002) na Kifungo cha Nje {The Prisons (Extra Mural Penal Employment) Regulation}.

(xii)   Wafungwa waliopatikana na hatia na kuhukumiwa kifungo kwa makosa ya kutumia vibaya madaraka yao na kuhujumu uchumi.

(xiii)     Wafungwa waliowahi kupunguziwa kifungo na Msamaha wa Mhe. Rais na bado wangali wanaendelea kutumikia sehemu ya kifungo kilichobaki.

(xiv)     Wafungwa waliopatikana na hatia na kuhukumiwa kwa kosa la kuzuia watoto kupata masomo.

(xv)     Wafungwa waliopatikana na hatia na kuhukumiwa kwa kosa la utekaji wa watoto, kupoka na kufanya biashara ya binadamu (Human Trafficking).

(xvi)    Wafungwa waliopatikana na hatia na kuhukumiwa kwa kosa la kukutwa na viungo vya binadamu.

(xvii)      Wafungwa wanaotumikia vifungo kwa makosa ya kujihusisha kwa namna yoyote ile na nyara za Serikali na ujangili (poachers).

(xviii)    Wafungwa wanaotumikia vifungo kwa makosa ya wizi/ubadhirifu wa fedha za Serikali.

(xix)   Wafungwa wanaotumikia vifungo kwa makosa ya kutoroka au kujaribu kutoroka chini ya ulinzi halali au kusaidia kutendeka kwa makosa hayo na bado wangali wanatumika adhabu hizo.

(xx)          Wafungwa walioingia gerezani baada ya tarehe 7 Aprili, 2018.

(xxi)        Wafungwa waliowahi kufungwa gerezani (warudiaji) na wale wenye makosa ya kinidhamu gerezani.

3.      Wafungwa 3,319 watafaidika na Msamaha huu ambapo 585 wataachiliwa huru tarehe 26 Aprili, 2018 na 2,734 watabaki gerezani kumalizia sehemu ya kifungo kilichobaki baada ya kupewa msamaha huu. Ni mategemeo ya Serikali kwamba watarejea tena katika jamii kushirikiana na wenzao katika ujenzi wa Taifa na kwamba watajiepusha kutenda makosa ili wasirejee tena gerezani.


Maj. Jen. Projestus Rwegasira
KATIBU MKUU - WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI
26 Aprili, 2018