Friday, March 13, 2015

Kamishna Jenerali wa magereza apongezwa kwa kufufua kiwanda cha sabuni gereza kuu Ruanda, Mbeya

Sabuni za kufulia zenye miche minene mirefu(Big Bars) zinazotengenezwa katika Kiwanda cha Sabuni cha Gereza Kuu Ruanda, Mbeya zikiwa tayari kupelekwa kwa watumiaji.

Muonekano wa Sabuni ya kufulia ikiwa bado haijawekwa kwenye mashine maalum ya kukatia vipande vyenye ukubwa tofauti tofauti. Kwa wastani Kiwanda hicho kinauwezo wa kuzalisha katoni 150 hadi 200 kwa siku.

Fundi Mkuu katika Kiwanda cha Sabuni cha Gereza Kuu Ruanda, Mbeya Sajin wa Magereza, George akitoa maelezo ya aina za Sabuni zinazotengenezwa katika mradi wa Sabuni Gereza Kuu Ruanda, Mbeya kama zinavyoonekana katika picha.


Na Lucas Mboje, Mbeya

Kamishna Jenerali wa Magereza Nchini, John Casmir Minja amepongezwa kwa kukifufua Kiwanda cha utengenezaji Sabuni za aina mbalimbali Gereza Kuu Ruanda, Mbeya.

Pongezi hizo zimetolewa na Maofisa na Askari wa Magereza Mkoani Mbeya kutokana na kukiwezesha Kiwanda hicho vifaa na malighafi za utengenezaji sabuni hivyo kukifanya Kiwanda hicho kizalishe sabuni za kutosha kwa Wafungwa waliopo Magerezani Tanzania Bara.

"Tunampongeza sana Kamishna Jenerali Minja hususani kwa kukiwezesha Kiwanda chetu vifaa vya utengenezaji sabuni. Tunaamini kutokana na kasi ya utendaji wake wa kazi ataendeleza juhudi za kukiunga mkono Kiwanda hiki ili kiweze kukidhi mahitaji halisi ya soko la ndani na nje." Walisikika wakisema.

Kiwanda cha Uzalishaji sabuni cha Gereza Kuu Ruanda, Mbeya ni miongoni mwa miradi 23 iliyopo chini ya Shirika la Magereza(Prison Corporation Sole) ambapo mradi huu ulianza shughuli zake za Uzalishaji sabuni mnamo Mwaka 1978.

Madhumuni ya kuanzishwa kwa mradi huu yalilenga zaidi kutimiza majukumu ya msingi ya Jeshi la Magereza hususani utekelezaji wa Programu ya Urekebishaji wa Wafungwa kwa kuwafundisha utengenezaji wa sabuni pia kiwanda hicho kinajiendesha kibishara hivyo kuchangia pato la Taifa.

Kiwanda hicho kinatengeneza Sabuni za aina mbalimbali zikiwemo Sabuni za kufulia zenye miche minene na mifupi, sabuni za kuongea, sabuni za maji kwa ajili ya usafi majumbani pamoja na sabuni za chenga chenga(flex soap).

Malighafi zinazotumika katika Kiwanda hicho ni caustic soda, mafuta ya mawese na mafuta ya mise ambayo hupatikana kwa wingi Wilayani Kyela, Mkoani Mbeya. Kwa wastani Kiwanda hicho kinauwezo wa kuzalisha katoni za sabuni 150 hadi 200 kwa siku.

Tangu kuanzishwa kwa mradi huu kwa kiasi kikubwa kimechangia utoaji elimu ya Ufundi Stadi kwa vitendo kwa Wafungwa katika fani ya za utengenezaji wa sabuni ambapo kuna Wafungwa wengi wamenufaika kupitia mradi huu na wameweza kuanzisha shughuli zao baada ya vifungo vyao kukoma.