Friday, July 31, 2015

Tanzia

 Marehemu SACP Aneth Laurent

Kamishna Jenerali wa Magereza John C. Minja anasikitika kutangaza kifo cha Mkuu wa Magereza  Mkoa wa Shinyanga Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Magereza (SACP)  Aneth Laurent kilichotokea jana tarehe 30 Julai,2015 katika Hosptali ya Rufaa Bungando jijini Mwanza.

Kaminshna Jenerali anatoa pole kwa watumishi wote wa Jeshi la Magereza nchini, familia na wale wote walioguswa na msiba huu kwa namna tofauti tofauti.

Jeshi la Magereza kwa kushirikiana na familia ya marehemu linaendelea kuratibu shughuli za msiba ambapo mwili wa marehemu unatarajiwa kusafirishwa kwa ndege kutoka Mwanza kuja Dar es salaam na taratibu za mazishi zitatolewa baadae.

Mungu ailaze Roho ya Marehemu mahali pema peponi.

Amina

UTENZI

KWAHERI KAMANDA ANETH
1.    Mchunga wangu ameniandalia mema yote,
    Aneth Laurent mchunga wako alikuandalia mema yote,
    Kwa kuwa yeye ndiye mwenye kuchunga uzima wote,
    Atakuandalia raha kamili huko mbinguni uliko.

2.    Ulifanya kazi yako ya kupigana na Shetani,
    Umeshinda, tena umeshinda sana,
    Ameona usisubiri ili shetani akirudi akushinde,
    Umepita katika uvuli wa mauti na hutaogopa kamwe.

3.    Ulikuwa kioo, mhimili wa familia,
    Hatukuwahi kukuona unagombana au kumchukia mtu,
    Ulikuwa mtenda haki, mtetea haki,
    Hukukaa kimya pale ulipoona haki haitendeki.

4.    Ulikuwa mpiganaji, mpambanaji usiyechoka,
    Kila wakati ulifuata maelekezo ya viongozi wako,
    Kwa unyenyekevu mkubwa uliwaongoza walio chini yako,
    Katu heshima hukuwavunjia,wakubwa kwa wadogo.

5.    Ulifanya kazi usiku na mchana,
    Ili kuhakikisha Jeshi letu mbele linasonga,
    Kitengo Uliongoza, cha Mipango kwa uadilifu mkubwa,
    Sote tulijivunia, uwepo wapo idarani.

6.     Kiongozi wa Mkoa usiyetetereka, Shinyanga umeongoza
    Umetuacha bila kutuaga, amani tunakuombea,
    Na lako tabasamu umeondoka, vichekesho vyako pia
    Umeondoka na utani wako na heshima yako.

7.    Vai na Karo mama ametuacha,
    Sunday, dada ametutoka,
    Pamela na David mama ametutoka tutakimbilia wapi,
    Mjukuu bibi hatutamwona tena,
    Amemfuata Beatrisi dada yake.

8.    Yosefu na Mwasiti rafiki yetu mpenzi kaondoka,
    Masunga, Novati, Ambayuu, Mmassy, Mwambashi,
    Makwaiya, Kaswaka, Mwamgunda,
    Kipenzi chetu hayupo tena, kwa heri Massawe wetu.

9.    Tunakuaga kipenzi chetu leo,
    Wizara itakukumbuka, Idara zote hazitakusahau,
    Jeshi la Magereza daraja limebomoka,
    Tumwombee kwa kuwa amemaliza kazi yake duniani.

10.    Aneth Laurent Balibusha,
    Ulipigana vita vitakatifu hapa duniani,
    Mambo ya dunia si kitu nakuambia yana uongo ndani,
    Yesu mwema, Yesu Mwokozi umwonee huruma,
    Angalia machozi umponye salama,
    Apumzike kwa Amani.  AMINA

Na Alexander Mmasy
Makao Makuu ya Magereza