Wednesday, August 5, 2015

Banda la Jeshi la Magereza kuwanufaisha wananchi wa Lindi njia bora za kisasa za ufugaji mifugo, maonesho ya wakulima nanenane kitaifa.


 Ng'ombe wa maziwa kutoka Gereza Kingolwira, Morogoro katika Banda la Jeshi la Magereza ambalo linatoa elimu ya Ufugaji wa kisasa wa ng'ombe wa maziwa kwa Wananchi wa Mikoa ya Lindi na Mtwara wanapotembelea Banda hilo. Maziwa yanayozalishwa katika Mashamba ya Mifugo ya Jeshi la Magereza hutumika kwa ajili ya Lishe ya Wafungwa, watoto wa Wafungwa na kuuzwa kwa Watumishi wa Jeshi la Magereza na Wananchi wengine.
 Ng'ombe Dume aina ya Boran ambaye hutumika kuboresha vinasaba vya ng'ombe bora wa nyama. Ng'ombe huyu amekuwa kivutio kikubwa kwa Wananchi wengi wanapotembelea katika Banda hili la Jeshi la Magereza ili kujifunza Stadi za Ufugaji bora wa ng'ombe wa maziwa na nyama kupitia teknolojia ya Uhamilishaji wa Mifugo.
 Mshiriki wa Maonesho ya Wakulima Nane Nane Kitaifa Mkoani Lindi, Mtaalamu wa Mifugo Koplo wa Magereza, Henry akiandaa vifaa vya teknolojia ya Uhamilishaji wa Mifugo kabla ya kuanza kutoa elimu hiyo kwa Wananchi mbalimbali wanapotembelea katika Banda la Jeshi la Magereza.
 
 Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mwantumu Mahiza(wa pili kulia) akipata maelezo ya Kitaalam kuhusu Ufugaji wa kisasa wa ng'ombe wa maziwa kutoka kwa Mkuu wa Banda la Jeshi la Magereza, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Magereza, Mlasani Kimaro(wa kwanza kulia). Kushoto ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wakulima Kitaifa, Bw. Engelbert Moyo.


 Na; Lucas Mboje, Lindi

Wananchi mbalimbali wa Mikoa ya Lindi na Mtwara wanaotembelea katika Banda la Jeshi la Magereza Maonesho ya Wakulima Nane Nane Kitaifa wananufaika na elimu inayotolewa bure na Maafisa Mifugo wa Jeshi hilo kuhusiana na njia bora na za Kisasa za Ufugaji wa ng'ombe wa maziwa na nyama.

Akizungumza umuhimu wa elimu hiyo kwa Wananchi, Mkuu wa Banda la Jeshi la Magereza, Mlasani Kimaro amesema lengo kubwa la kutoa elimu hiyo kwa Wananchi ni kusaidia kuboresha vipato vyao sambamba na kuondokana na Ufugaji wa kizamani usiokuwa na tija.

"Tunatoa elimu hiyo bure kwa Wananchi wote wanaotembelea katika Banda letu ili waweze kuzitumia mbinu hizo za kisasa kufuga kisasa hususani kupitia teknolojia hii ya Uhamilishaji Mifugo hivyo kuboresha vipato vyao na kujiletea Maendeleo katika jamii zao". Alisema Kamanda Kimaro.

Aidha, ametoa wito kwa Wananchi wa Mikoa ya Lindi na Mtwara kutumia fursa hiyo kutembelea Banda la Jeshi la Magereza, lililopo katika Viwanja vya Maonesho ya Wakulima Nane Nane Kitaifa, Mkoani Lindi ambalo Mwaka huu limejielekeza kwenye elimu ya Ufugaji wa kisasa.

Jeshi la Magereza nchini lina mashamba makubwa yanayofuga ng'ombe wa nyama na maziwa ambapo kwa upande wa ng'ombe wa nyama ni aina ya "Tanzania Shorthorn Zebu" na Boran.

Miongoni mwa mashamba makubwa yanayofuga ng'ombe wa nyama na maziwa ni pamoja na Gereza la Ubena - Pwani, Mbigiri - Morogoro, Mgumu - Mara, Kitengule - Kagera, Kingurungundwa - Lindi, Namajani - Mtwara, Majimaji - Ruvuma na King'ang'a - Dodoma.

Ng'ombe wa maziwa ni Magereza ya Kingolwira - Morogoro, Isupilo - Iringa, Mugumu - Mara, Arusha, Songwe - Mbeya, Mollo - Rukwa na Kitengule - Kagera ni miongoni mwa mashamba makubwa yanayomilikiwa na Jeshi la Magereza yanayohusika na Ufugaji wa ng'ombe wa maziwa. Aidha, Mikoa yote nchini kuna magereza yanafuga idadi ndogo ya ng'ombe wa nyama kwa ajili ya nyama ya kulisha wafungwa, ziada huuziwa Askari na Wananchi wengine.

Maonesho ya Wakulima Nane Nane Kitaifa yamefunguliwa Agosti 04, 2015 na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mizengo Kayanza Pinda ambapo kauli mbiu ya Mwaka huu ni "Matokeo Makubwa Sasa" - Tuchague Viongozi Bora kwa Maendeleo ya Wakulima na Wafugaji.

(Picha zote na Lucas Mboje wa Jeshi la Magereza).