Sunday, November 18, 2018
KATIBU MKUU WA MAMBO YA NDANI, MEJA JENERALI JACOB KINGU AKAGUA MABORESHO YA KIWANDA CHA VIATU GEREZA KUU KARANGA MOSHI
2:01 PM
Katibu
Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani, Meja Jenerali Jacob Kingu akisalimiana na Maafisa wa Jeshi la Magereza Mkoani
Kilimanjaro mara baada ya kuwasili katika ziara Maalum ya kukagua maboresho
mbalimbali katika Kiwanda cha Viatu cha Gereza Kuu Karanga Moshi jana Novemba 17, 2018. Kushoto kwake ni Kamishna
Jenerali wa Magereza, Phaustine Kasike.
Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya
Ndani ya nchi, Meja Jenerali Jacob Kingu(meza kuu) akitoa maelekezo kwa
Kaimu Mkuu wa Kiwanda hicho, Mrakibu Msaidizi wa Magereza, Hamis
Nyaku(aliyesimama). Kushoto ni Kamishna Jenerali wa Magereza, Phaustine Kasike
Katibu Mkuu Wizara
ya Mambo ya Ndani ya nchi, Meja Jenerali Jacob Kingu na Kamishna Jenerali wa
Magereza, Phaustine Kasike wakiangalia Buti za aina mbalimbali za Jeshi zinazotengenezwa
katika Kiwanda cha Viatu Karanga Moshi.
Sehemu
ya viatu aina mbalimbali ikiwemo viatu vya maafisa na Buti za Jeshi zinazotengenezwa
katika Kiwanda cha Viatu Karanga Moshi kwa ajili ya Jeshi la Polisi nchini. Jeshi
la Polisi limetengenezewa viatu aina ya buti pea elfu kumi (10,000) na pea elfu
tano (5,000) za viatu vya maafisa zenye thamani ya Tsh. 1, 237, 666, 600/=, tayari
buti zimekabidhiwa kwa Jeshi hilo na hivi sasa kiwanda kinamalizia utengenezaji
wa viatu vya maafisa wa Jeshi la Polisi.
Maafisa
Masoko wa Kiwanda cha viatu Karanga Moshi wakivipanga viatu vya kiraia aina
mbalimbali vinavyotengenezwa katika kiwanda hicho kama inavyoonekana katika
picha.
Katibu
Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya nchi, Meja Jenerali Jacob Kingu akipata
maelezo ya kitaalam juu ya utengenezaji wa Buti za Jeshi kutoka kwa Mtaalam wa
utengenezaji viatu wa Jeshi la Magereza
(Picha zote na Jeshi la Magereza).
KATIBU MKUU MAMBO YA NDANI NA CGP KASIKE WATEMBELEA KIWANDA CHA SAMANI CHA JESHI LA MAGEREZA CHA ARUSHA KILICHOTEKETEA KWA MOTO
1:27 PM
Na
Lucas Mboje, Arusha
KATIBU Mkuu
Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Meja
Jenerali Jacob Kingu pamoja na Kamishna Jenerali wa Magereza nchini, Phaustine
Kasike leo wametembelea Kiwanda cha Samani cha Arusha, mali ya Jeshi la
Magereza ili kujionea athari mbalimbali iliyosababishwa na ajali ya moto
iliyotokea juzi Novemba 16, 2018.
Akizungumza
eneo la tukio Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Meja Jenerali Jacob
Kingu amesema kuwa ni vyema taasisi mbalimbali nchini pamoja na wananchi
wakachukua tahadhali za majanga ya moto ili kuepusha hasara zinazoweza
kujitokeza kufuatia majanga hayo.
Amesema
kuwa Wizara yake itaendelea kuliwezesha Jeshi la Zimamoto na Uokoaji vifaa vya
kisasa ili liweze kukabiliana na majanga ya moto pindi yanapojitokeza.
Aidha,
Katibu Mkuu huyo, Meja Jenerali Kingu amelitaka Jeshi la Magereza kuhakikisha
kuwa linafanya jitihada za haraka za kurejesha shughuli za uzalishaji katika
kiwanda hicho ikiwemo kufanyia matengenezo baadhi ya mashine zilizoteketezwa na moto.
Kwa
upande wake, Kamishna Jenerali wa Magereza nchini, Phaustine Kasike amevishukru
vyombo vya ulinzi na usalama ikiwemo Jeshi la Zimamoto na Uokoaji pamoja na
Jeshi la Polisi Mkoani Arusha sambamba na wananchi waliojitokeza kusaidia
katika uzimaji wa moto huo ambao umeunguza sehemu ya kiwanda hicho.
“Nawashukru
sana Jeshi la zimamoto na uokoaji Mkoani Arusha, Jeshi la Polisi pamoja na wananchi
kwa kazi kubwa waliyoifanya siku ya tukio kwani niliarifiwa kuwa moto ulikuwa
mkubwa lakini tunashukuru Mungu hatimaye uzimaji ulifanikiwa pamoja na hasara
iliyojitokeza”. Alisema Jenerali Kasike.
Akizungumzia
chanzo cha moto huo na hasara iliyojitokeza, Kamishna Jenerali Kasike amesema
kuwa taarifa za awali zinaonesha kuwa moto huo ulisababishwa na hitilafu ya
umeme ambayo ilisababisha kuteketea kwa baadhi ya mashine za kiwanda hicho
pamoja na uharibu wa nyaraka mbalimbali za ofisi katika jengo la utawala.
Wakati
huo huo, Kamishna Jenerali Phaustine Kasike ameunda Kamati maalum ya Maafisa
watano kutoka Makao Makuu ya Jeshi la Magereza ambayo itachunguza chanzo cha
moto huo pamoja na kuwasilisha taarifa kamili ya hasara iliyojitokeza. Tume
hiyo itaongozwa na Kamishna wa Fedha na Mipango wa Jeshi hilo, Kamishna wa
Magereza, Gideon Nkana.
Kiwanda
cha samani cha Magereza Arusha kilimikishwa rasmi kwa Jeshi la Magereza mwaka
1973 baada ya Azimio la Arusha mwaka 1967 ambapo tangu kipindi hicho kiwanda
hicho kinajishughulisha na utengenezaji wa samani mbalimbali za ofisi na samani
za majumbani. Pia kiwanda hiki hutumika kuwafundisha na kuwarekebisha wafungwa
ili wamalizapo vifungo vyao waweze kujitegemea kupitia ujuzi waliojifunza.
Katibu
Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Meja Jenerali Jacob Kingu akiwasili Novemba 17, 2018 katika Kiwanda cha samani cha Magereza Arusha kukagua sehemu
mbalimbali ambazo moto umeteketeza sehemu ya kiwanda hicho. Kushoto kwake ni
Kamishna Jenerali wa Magereza, Phaustine Kasike.
Mkuu
wa Magereza Mkoa huo, ACP Anderson Kamtiaro akisoma taarifa ya janga la moto
mbele ya Katibu Mkuu Mambo ya ndani ya nchi, Meja Jenerali Jacob Kingu
aliwasili kiwandani kujionea uhabribu mbalimbali uliojitokeza.
Kamishna
Jenerali wa Magereza nchini, Phaustine Kasike akitoa taarifa kwa Katibu Mkuu
Mambo ya ndani ya nchi, Meja Jenerali Jacob Kingu kuhusu hatua mbalimbali
ambazo amezichukua ikiwemo kuunda kamati maalum ya watu watano ambayo
itachunguza tukio la moto katika kiwanda hicho.
Kamishna Jenerali wa Magereza nchini, Phaustine Kasike (wa pili toka kulia) pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Meja Jenerali Jacob Kingu (kulia kwake), wakiangalia moja ya mashine mbalimbali ambazo zimeteketezwa na moto katika kiwanda cha Samani cha Magereza Arusha. Chanzo cha moto huo inasemekana ni hitilafu ya umeme ndani ya kiwanda hicho.
Katibu
Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Meja Jenerali Jacob Kingu (wa kwanza
kushoto) akitoa maelekezo mbalimbali kwa Kamishna Jenerali wa Magereza,
Phaustine Kasike(katikati). Kulia ni Kamishna wa Fedha na Mipango, Kamishna wa
Magereza, Gideon Nkana ambaye ni Kiongozi wa Kamati Maalum ya kuchunguza tukio
hilo.
Jengo
la kiwanda cha samani cha Magereza Arusha ambalo limeteketea kwa moto.
Muonekano
wa baadhi ya mashine pamoja na vifaa mbalimbali na nyaraka nyinginezo za ofisi
zilizoungua kufuatia janga la moto.
Samani
mbalimbali zinazotengenezwa katika kiwanda cha samani cha Magereza Arusha kama
inavyoonekana katika picha zikiwa tayari kwenda sokoni(Picha na Jeshi la Magereza).
Friday, November 16, 2018
MKUU WA JESHI LA MAGEREZA AKUTANA NA RC NJOMBE KABLA YA KUHITIMISHA ZIARA YAKE TAREHE 15/11/2018
10:20 AM
Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Mhe. Christopher Ole
Sendeka akisalimiana na Mkuu wa Jeshi la Magereza nchini (CGP) Phaustine Kasike
alipotembelea Ofisi za Mkuu wa Mkoa
kabla ya kuhitimisha ziara yake ya kikazi, Novemba 15, 2018.
Mkuu
wa Mkoa wa Njombe, Mhe. Christopher Ole
Sendeka akitoa taarifa fupi ya Mkoa wake alipotembelewa na Mkuu wa Jeshi la
Magereza Ofsini kwake.
Kamishna Jenerali wa Magereza Nchini (CGP)
Phaustine Kasike akielezea malengo ya ziara yake ya kikazi mbele ya Mkuu wa
Mkoa wa Njombe alipotembelea Ofisi za Mkoa huo.
Mkuu
wa Jeshi la Magereza, CGP. Phaustine Kasike akiagana na baadhi ya askari wa
Gereza Njombe baada ya kuhitimisha ziara yake ya kikazi Mkoani Njombe.
Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Mhe.
Christopher Ole Sendeka (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Kamishna Jenerali wa Magereza nchini,
Phaustine Kasike(wa pili toka kulia) pamoja na wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na
Usalama ya Mkoa wa Njombe. Wa pili toka kushoto ni Katibu Tawala Mkoa wa
Njombe, Bw. Erick Shitindi ( Picha
na Jeshi la Magereza).
Thursday, November 15, 2018
ZIARA YA CGP KASIKE GEREZA LA WILAYA MAKETE, MKOANI JOMBE
1:34 AM
Mkuu wa Jeshi la Magereza Nchini (CGP) Phaustine
Kasike akizungumza jambo alipotembelea Ofisi za Mkuu wa Wilaya Makete Novemba 14, 2018. Wengine ni Maafisa Waandamizi wa Jeshi hilo.
Baadhi ya Askari wa kike wa Jeshi la Magereza
wakiteta jambo na Kamishna Jenerali wa Magereza nchini, Phaustine Kasike ambapo
askari hao wamempongeza Mkuu wa Jeshi hilo kwa uamuzi wake wa kutembelea magereza
mbalimbali hapa nchini.
Mkuu wa Jeshi la Magereza nchini (CGP) Phaustine
Kasike akiwasili Gereza Makete tayari kwa ziara yake ya kikazi Mkoani Njombe, Novemba 14, 2018.
Kamishna Jenerali wa Magereza, Phaustine Kasike akikagua
maandalizi ya mashamba ya kilimo cha mahindi katika eneo la Gereza Ludewa
mapema leo asbuhi Novemba 14, 2018 kabla
ya kuelekea Gereza Makete kuendelea na ziara yake ya kikazi.
Mkuu wa Gereza Makete, SP. Aloyce
Kayera(kushoto) akisoma taarifa ya Gereza mbele ya Kamishna Jenerali wa
Magereza Nchini (CGP) Phaustine Kasike(kulia) alipotembelea gereza hilo leo
Novemba 14, 2018.
. Mkuu wa Wilaya ya Makete, Mhe. Veronica Kessy
akiagana na Kamishna Jenerali wa Magereza, Phaustine Kasike alipotembelea Ofisi za Mkuu wa Wilaya Makete.
Wednesday, November 14, 2018
GEREZA LUDEWA KUPATIWA TREKTA ILI KUONGEZA UZALISHAJI WA CHAKULA CHA WAFUNGWA
10:04 AM
Na
Lucas Mboje, Ludewa
KAMISHNA
Jenerali wa Magereza nchini, Phaustine Kasike ameahidi kulipatia trekta moja
Gereza la Kilimo Ludewa ili kuongeza uzalishaji wa chakula cha wafungwa.
Kamishna
Jenerali Kasike ametoa ahadi hiyo leo wakati akizungumza na uongozi wa Gereza
hilo baada ya kuwasili Wilayani Ludewa katika ziara yake ya kikazi ya kukagua
utendaji kazi wa Jeshi hilo.
Amesema
kuwa Gereza Ludewa ni miongoni mwa magereza 13 ambayo tayari yameainishwa
katika mpango mkakati wa Jeshi la Magereza katika kujitosheleza kwa chakula cha
wafungwa waliopo magerezani hivyo lazima liwezeshwe zana za kilimo.
“Nafahamu kuwa trekta lililopo hapa Gereza
Ludewa ni la muda mrefu na ni chakavu, hivyo nitawapatieni trekta jipya ili
muweze kuongeza uzalishaji wa chakula cha wafungwa”. Alisema Jenerali Kasike.
Pia,
Kamishna Jenerali Kasike amehimiza uongozi wa Gereza hilo kuzingatia suala zima
la uadilifu na amewataka kujiepushe na vitendo vyote vya ubadhilifu wa mali za
umma.
Kwa
upande wake, Mkuu wa Gereza hilo, SSP. Akley Mkude amesema kuwa katika msimu wa Kilimo wa mwaka 2017/2018
gereza hilo lililima ekari 200 za mahindi na kufanikiwa kuvuna gunia zaidi ya
1700 ambazo zitatumika kulisha magereza yote ya Mkoa wa Njombe na Iringa.
Aidha,
ameongeza kuwa malengo ya msimu huu wa
mwaka 2018/2019 ni kulima ekari 700 za mahindi, ekari 40 za maharage, ekari 30
za alizaeti pamoja na bustani ekari 5 za mbogamboga.
Gereza
Ludewa lina eneo lenye ukubwa wa ekari 3500, Gereza hilo linajishughulisha na kilimo
cha mahindi, maharage, alizeti pamoja na bustani za mbogamboga. Pia,
linajishughulisha na miradi ya ufugaji wa ng’ombe, mbuzi, kuku wa kienyeji
pamoja na uhifadhi wa mazingira.
Mkuu wa Jeshi la Magereza nchini (CGP) Phaustine
Kasike akisalimiana na Maofisa na askari wa Gereza Ludewa alipowasili kuendelea
na ziara yake ya kikazi ya kutembelea magereza mbalimbali Mkoani Njombe, Novemba 13, 2018.
Mkuu wa Gereza Ludewa, SSP. Akley
Mkude(kushoto) akimweleza jambo Kamishna Jenerali wa Magereza Nchini (CGP)
Phaustine Kasike(kulia) alipotembelea gereza hilo Novemba 13, 2018. Wengine
ni Maafisa Waandamizi wa Jeshi hilo.
Kamishna
Jenerali wa Magereza Nchini (CGP) Phaustine Kasike akipanda mti wa mparachichi
katika Kambi ya Jeshi la Magereza ya Kidewa iliyopo Mkoani Njombe kabla ya
kuendelea na ziara yake ya kikazi Gereza Ludewa, Novemba 13, 2018.
Ghala la kuhifadhia mahindi yanayozalishwa katika
Gereza Ludewa.
Baadhi ya Askari wa Gereza la Wilaya Ludewa wakimsikiliza Kamishna Jenerali wa Magereza
nchini, Phaustine Kasike(hayupo pichani).
Mkuu
wa Wilaya ya Ludewa, Mhe. Andrea Tsere(wa tatu toka kushoto) akiwa katika picha
ya pamoja na Kamishna Jenerali wa Magereza nchini, Phaustine Kasike(wa pili
toka kulia) pamoja na Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilayani Ludewa( Picha
na Jeshi la Magereza).
Monday, November 12, 2018
WAKUU WA MAGEREZA NCHINI WATAKIWA KUWA WABUNIFU KATIKA UTATUZI WA NYUMBA ZA ASKARI
3:43 PM
Na
Lucas Mboje, Njombe
WAKUU
wa Magereza yote nchini wametakiwa kuwa wabunifu ili kutatua changamoto ya
uhaba wa makazi ya askari kwa kutumia nguvukazi ya wafungwa na rasilimali nyinginezo
zilizopo katika maeneo yao.
Wito
huo umetolewa leo Novemba 12, 2018 na Kamishna Jenerali wa Magereza nchini,
Phaustine Kasike alipofanya ziara ya kikazi ya kukagua magereza yote ya Mkoa wa
Njombe ambayo yanaendeshwa na Jeshi hilo.
Kamishna
Jenerali Kasike amesema kuwa lazima wakuu wa magereza wawe wabunifu katika
kutatua tatizo hilo la uhaba wa nyumba kwani Jeshi hilo linazo fursa nyingi
ikiwemo nguvu kazi ya wafungwa.
“Mkoa
wa Njombe na mingineyo nchini haipo sababu ya kuwa na tatizo la uhaba wa nyumba
za askari kwani kuna fursa ya kutosha ya kufyatua tofali za kuchoma kwa kuwatumia wafungwa ili kumaliza tatizo
hili nchini”. Amesisitiza Jenerali Kasike.
Aidha,
Kamishna Jenerali Kasike amewataka mafisa na askari wote kuendelea kutimiza
majukumu yao kwa kuzingatia maadili, sheria na kanuni mbalimbali za uendeshaji
wa Jeshi hilo.
Awali,
akisoma taarifa ya Gereza la Wilaya Njombe, Mkuu wa Gereza hilo, SP. Charls
Mihinga amesema kuwa tayari wameanzisha
mradi wa ufyatuaji wa tofali za kuchoma katika kambi ya mdandu ili kumaliza
tatizo la uhaba wa nyumba za watumishi wa gereza hilo.
“Katika
msimu huu tumeweza kufyatua tofali kubwa zipatazo 30,000 ambazo tayari
zimeshachomwa, tofali hizi zitatumika katika ujenzi wa nyumba za askari pamoja
na ujenzi wa Ofisi mpya ya Mkuu wa Magereza Mkoani Njombe”. Alisema SP.
Mihinga.
Pia,
ameongeza kuwa malengo ya baadaye ni
kuifanya kambi hiyo ya Gereza Njombe kuwa na taswira ya uzalishaji wa matofali
kwa wingi kwa ajili ya kufanya biashara na hivyo kuongeza maduhuri serikalini.
Jeshi
la Magereza linakabiliwa na uhaba wa nyumba za kuishi za Maafisa na askari hapa
nchini, mkakati uliopo hivi sasa chini ya uongozi wa Kamishna Jenerali wa
Magereza ni kuhakikisha kuwa tatizo hilo linatatulika kwa kutumia njia ya
ubunifu pamoja na fursa mbalimbali zilizopo ndani ya Jeshi hilo.
Kaimu Mkuu wa Mkoa wa
Njombe ambaye pia ni Katibu Tawala wa Mkoani Njombe Bw. Erick Shitindi
akisalimiana na Mkuu wa Jeshi la Magereza nchini (CGP) Phaustine Kasike
walipokutana Mkoani Njombe alipotembelea
Ofisi za Mkuu wa Mkoa huo kabla ya kuendelea na ziara yake ya kikazi Mkoani
Njombe, leo
Novemba 12, 2018.
Wajumbe
wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Njombe wakimsikiliza Mkuu
wa Jeshi la Magereza Nchini (CGP) Phaustine Kasike(hayupo pichani) alipotembelea
Ofisi za Mkuu wa Mkoa kabla ya kuendelea na ziara yake ya kikazi Mkoani humo.
Baadhi
ya Askari wa Gereza la Wilaya Njombe wakifuatilia maelekezo katika Baraza
lililoongozwa na Kamishna Jenerali wa
Magereza nchini, Phaustine Kasike ambapo askari hao wameelezea changamoto zao
kiutendaji leo Novemba 12, 2018.
Kamishna Jenerali wa Magereza nchini, Phaustine
Kasike(katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Maafisa na askari wa Gereza
Njombe.
Mkuu wa Jeshi la Magereza Nchini (CGP) Phaustine
Kasike(wa kwanza kulia) akizungumza jambo alipotembelea Ofisi za Mkuu wa Mkoa
wa Njombe. Wengine ni Maafisa Waandamizi wa Jeshi hilo.
Mkuu
wa Gereza Njombe, SP. Charles Mihinga(kushoto) akimtembeza Kamishna Jenerali wa
Magereza Nchini (CGP) Phaustine Kasike(kulia) alipotembelea gereza hilo leo
Novemba 12, 2018.( Picha na Jeshi la Magereza)
Friday, November 9, 2018
KAMISHNA JENERALI WA MAGEREZA AASA JAMII KUACHA KUTENDA UHALIFU ILI KUPUNGUZA MSONGAMANO MAGEREZANI
11:21 PM
Na Lucas Mboje, Iringa;
KAMISHNA Jenerali wa Jeshi la
Magereza Magereza nchini, Phaustine Kasike ametoa rai kuwa ili kupunguza
msongamano magerezani ni vema jamii ikaacha kufanya matukio mbalimbali ya
uhalifu hapa nchini.
Rai hiyo imetolewa leo na Kamishna
Jenerali Kasike wakati akitoa ufafanuzi mbele ya wanahabari wa Mkoani Iringa
kuhusu madai ya uwepo wa msongamano wa wafungwa katika magereza mbalimbali
yaliyopo nchini ambapo ameeleza kuwa si kweli kwamba magereza yote yana
msongamano bali msongamano uliopo magerezani ni kwenye baadhi ya magereza yenye
kuhifadhi mahabusu.
Amesema suala la msongamano
limekuwa ni tatizo kubwa ambapo takwimu za Jeshi la Magereza zinaonesha kuwa
idadi ya mahabusu waliopo magerezani ni wengi na hali hiyo inatokana na wingi
wa matukio ya uhalifu kwenye eneo husika na kule ambako hakuna uhalifu mwingi
basi nako kwenye magereza hakuna msongamano mkubwa wa wafungwa/mahabusu.
Ameongeza kuwa Jeshi la Magereza
litaendelea kushirikiana na vyombo vya haki jinai ikiwemo Jeshi la Polisi,
Mahakama na Ofisi ya DPP ili kuhakikisha kuwa kunakuwa na usukumaji wa kesi
mbalimbali za mahabusu waliopo magerezani.
“Tutajitahidi kuendelea
kushirikiana kwa pamoja katika jukwaa letu la haki jinai ili kuangalia namna
bora zaidi ya kuweza kutatua tatizo la ucheleweshaji wa kesi za mahabusu
waliopo magerezani”. Amesema Jenerali Kasike.
Kuhusu uhamisho wa Gereza Iringa
kwenda eneo la la Mlolo, Kamishna Jenerali Kasike amesema tayari Jeshi hilo
limekwishaanza kutekeleza maelekezo ya Serikali ambapo hivi sasa lipo katika
mchakato wa kuhamishwa kadri hali ya kibajeti itakavyoruhusu.
“Tumekwishaanza ufyatuaji wa
tofali za ujenzi wa nyumba za maafisa na askari sambamba na ujenzi wa mabweni
ya wafungwa unaendelea katika eneo hilo hivyo Gereza Iringa litahamishiwa
katika eneo la Mlolo ili kupisha huduma za kijamii”. Amesisitiza Jenerali
Kasike.
Mkuu wa Jeshi la Magereza nchini, CGP. Phaustine
Kasike yupo mkoani Iringa kwa ziara ya
kikazi ambapo leo ametembelea magereza ya Iringa na Pawaga. Ziara hizi ni mwendelezo
wa ziara zake za kikazi zenye lengo la
kukagua magereza yote Tanzania Bara na kuzungumza na Maafisa na askari pamoja
na kujua changamoto mbalimbali wanazokutana nazo wakati wakitekeleza majukumu
yao.
Kamishna Jenerali wa Magereza, Phaustine Kasike
akiwasili katika Gereza la Iringa leo Novemba 9, 2018 tayari kwa ziara yake ya
kikazi yenye lengo la kukagua shughuli mbalimbali za uendeshaji wa Jeshi hilo.
Kamishna
Jenerali wa Magereza, Phaustine Kasike akikagua moja la ghala la kuhifadhia
mpunga unaozalishwa katika Gereza la Kilimo Pawaga.
.
Kamishna Jenerali wa Magereza, Phaustine Kasike akizungumza na Mahabusu na
Wafungwa wa Gereza Iringa(hawapo pichani) alipofanya ziara ya kikazi leo
Novemba 9, 2018.
Kamishna Jenerali wa Magereza, Phaustine Kasike
akikagua maandalizi ya shamba ya kilimo cha mpunga katika eneo la Gereza la
Pawaga Mkoani Iringa. Gereza Pawaga limepewa malengo ya kulima ekari 375 za
mpunga ili kuwezesha mpango wa kujitosheleza kwa chakula cha wafungwa.
Mkuu wa Magereza Mkoa wa Iringa, Kamishna Msaidizi
wa Magereza, Hassan Mkwanda akimuongoza Kamishna Jenerali wa Magereza,
Phaustine Kasike kutembelea maeneo mbalimbali ya Gereza la Wilaya Iringa.
Askari wa vyeo mbalimbali wa Gereza Pawaga
wakifuatilia kwa makini maelekezo ya Kamishna Jenerali wa Magereza
alipotembelea gereza hilo leo Novemba 9, 2018.
Kitalu cha mbegu za mpunga ikiwa ni sehemu ya
maandalizi ya Kilimo mpunga katika eneo la Gereza la Pawaga Mkoani Iringa.
Gereza Pawaga limepewa malengo ya kulima ekari 375 za mpunga ili kuwezesha
mpango wa kujitosheleza kwa chakula cha wafungwa. (Picha na Jeshi la Magereza).
MKUU WA JESHI LA MAGEREZA NCHINI, CGP PHAUSTINE KASIKE AANZA ZIARA YA KIKAZI MKOANI IRINGA
5:44 PM
Kaimu
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, ambaye ni Mkuu
wa Wilaya ya Iringa Mjini, Mhe. Richard Kasesela akisalimiana na Mkuu wa Jeshi
la Magereza nchini (CGP) Phaustine Kasike walipokutana Mkoani Iringa alipotembelea Ofisi za Mkuu wa
Mkoa kabla ya kuendelea na ziara yake ya kikazi, leo Novemba 8, 2018.
Kaimu Mkuu
wa Mkoa wa Iringa, ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Iringa Mjini, Mhe. Richard Kasesela(watatu toka kushoto) akiwa katika
picha ya pamoja na Kamishna Jenerali wa
Magereza nchini, Phaustine Kasike(wa tatu toka kulia) pamoja na wajumbe wa
Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Iringa.
Mkuu wa Jeshi la Magereza nchini (CGP) Phaustine Kasike (kushoto) akizungumza na Mkuu wa Magereza Mkoa wa Iringa, Kamishna Msaidizi wa Magereza (ACP) Hassan Mkwanda na Maafisa wengine wa Magereza Mkoani Iringa, muda mfupi alipowasili leo Novemba 8, 2018 Mkoani humo. CGP Kasike yupo mkoani humo kwa ziara ya kikazi yenye lengo la kukagua magereza yote ya Mkoa wa Iringa na kuzungumza na Maafisa na askari pamoja na kujua chamgamoto mbalimbali wanazokutana nazo wakati wakitekeleza majukumu yao.
Wajumbe
wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Iringa wakisalimiana na Mkuu
wa Jeshi la Magereza Nchini (CGP) Phaustine Kasike walipokutana Mkoani Iringa alipotembelea Ofisi za Mkuu wa
Mkoa kabla ya kuendelea na ziara yake ya kikazi.
Baadhi
ya Askari wa Gereza la Wilaya Iringa wakifuatilia maelekezo katika Baraza
lililoongozwa na Kamishna Jenerali wa
Magereza nchini, Phaustine Kasike ambapo askari hao wameelezea changamoto zao
kiutendaji leo Novemba 8, 2018.
Mkuu
wa Magereza Mkoa wa Iringa, Kamishna
Msaidizi wa Magereza (ACP) Hassan Mkwanda
akimkaribisha Kamishna Jenerali wa Magereza Nchini (CGP) Phaustine
Kasike(katikati meza kuu) ili azungumze na baadhi ya Maafisa na askari wa
Gereza Iringa(hawapo pichani, leo Novemba 8, 2018 . Kulia ni ACP. Josephine Semwenda ambaye hivi karibuni
ameteuliwa kuwa Mkuu wa Magereza Mkoa wa
Lindi ( Picha na Jeshi la Magereza).