Na Lucas Mboje, Iringa;
KAMISHNA Jenerali wa Jeshi la
Magereza Magereza nchini, Phaustine Kasike ametoa rai kuwa ili kupunguza
msongamano magerezani ni vema jamii ikaacha kufanya matukio mbalimbali ya
uhalifu hapa nchini.
Rai hiyo imetolewa leo na Kamishna
Jenerali Kasike wakati akitoa ufafanuzi mbele ya wanahabari wa Mkoani Iringa
kuhusu madai ya uwepo wa msongamano wa wafungwa katika magereza mbalimbali
yaliyopo nchini ambapo ameeleza kuwa si kweli kwamba magereza yote yana
msongamano bali msongamano uliopo magerezani ni kwenye baadhi ya magereza yenye
kuhifadhi mahabusu.
Amesema suala la msongamano
limekuwa ni tatizo kubwa ambapo takwimu za Jeshi la Magereza zinaonesha kuwa
idadi ya mahabusu waliopo magerezani ni wengi na hali hiyo inatokana na wingi
wa matukio ya uhalifu kwenye eneo husika na kule ambako hakuna uhalifu mwingi
basi nako kwenye magereza hakuna msongamano mkubwa wa wafungwa/mahabusu.
Ameongeza kuwa Jeshi la Magereza
litaendelea kushirikiana na vyombo vya haki jinai ikiwemo Jeshi la Polisi,
Mahakama na Ofisi ya DPP ili kuhakikisha kuwa kunakuwa na usukumaji wa kesi
mbalimbali za mahabusu waliopo magerezani.
“Tutajitahidi kuendelea
kushirikiana kwa pamoja katika jukwaa letu la haki jinai ili kuangalia namna
bora zaidi ya kuweza kutatua tatizo la ucheleweshaji wa kesi za mahabusu
waliopo magerezani”. Amesema Jenerali Kasike.
Kuhusu uhamisho wa Gereza Iringa
kwenda eneo la la Mlolo, Kamishna Jenerali Kasike amesema tayari Jeshi hilo
limekwishaanza kutekeleza maelekezo ya Serikali ambapo hivi sasa lipo katika
mchakato wa kuhamishwa kadri hali ya kibajeti itakavyoruhusu.
“Tumekwishaanza ufyatuaji wa
tofali za ujenzi wa nyumba za maafisa na askari sambamba na ujenzi wa mabweni
ya wafungwa unaendelea katika eneo hilo hivyo Gereza Iringa litahamishiwa
katika eneo la Mlolo ili kupisha huduma za kijamii”. Amesisitiza Jenerali
Kasike.
Mkuu wa Jeshi la Magereza nchini, CGP. Phaustine
Kasike yupo mkoani Iringa kwa ziara ya
kikazi ambapo leo ametembelea magereza ya Iringa na Pawaga. Ziara hizi ni mwendelezo
wa ziara zake za kikazi zenye lengo la
kukagua magereza yote Tanzania Bara na kuzungumza na Maafisa na askari pamoja
na kujua changamoto mbalimbali wanazokutana nazo wakati wakitekeleza majukumu
yao.
Kamishna Jenerali wa Magereza, Phaustine Kasike
akiwasili katika Gereza la Iringa leo Novemba 9, 2018 tayari kwa ziara yake ya
kikazi yenye lengo la kukagua shughuli mbalimbali za uendeshaji wa Jeshi hilo.
Kamishna
Jenerali wa Magereza, Phaustine Kasike akikagua moja la ghala la kuhifadhia
mpunga unaozalishwa katika Gereza la Kilimo Pawaga.
.
Kamishna Jenerali wa Magereza, Phaustine Kasike akizungumza na Mahabusu na
Wafungwa wa Gereza Iringa(hawapo pichani) alipofanya ziara ya kikazi leo
Novemba 9, 2018.
Kamishna Jenerali wa Magereza, Phaustine Kasike
akikagua maandalizi ya shamba ya kilimo cha mpunga katika eneo la Gereza la
Pawaga Mkoani Iringa. Gereza Pawaga limepewa malengo ya kulima ekari 375 za
mpunga ili kuwezesha mpango wa kujitosheleza kwa chakula cha wafungwa.
Mkuu wa Magereza Mkoa wa Iringa, Kamishna Msaidizi
wa Magereza, Hassan Mkwanda akimuongoza Kamishna Jenerali wa Magereza,
Phaustine Kasike kutembelea maeneo mbalimbali ya Gereza la Wilaya Iringa.
Askari wa vyeo mbalimbali wa Gereza Pawaga
wakifuatilia kwa makini maelekezo ya Kamishna Jenerali wa Magereza
alipotembelea gereza hilo leo Novemba 9, 2018.
Kitalu cha mbegu za mpunga ikiwa ni sehemu ya
maandalizi ya Kilimo mpunga katika eneo la Gereza la Pawaga Mkoani Iringa.
Gereza Pawaga limepewa malengo ya kulima ekari 375 za mpunga ili kuwezesha
mpango wa kujitosheleza kwa chakula cha wafungwa. (Picha na Jeshi la Magereza).