Na
Lucas Mboje, Arusha
KATIBU Mkuu
Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Meja
Jenerali Jacob Kingu pamoja na Kamishna Jenerali wa Magereza nchini, Phaustine
Kasike leo wametembelea Kiwanda cha Samani cha Arusha, mali ya Jeshi la
Magereza ili kujionea athari mbalimbali iliyosababishwa na ajali ya moto
iliyotokea juzi Novemba 16, 2018.
Akizungumza
eneo la tukio Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Meja Jenerali Jacob
Kingu amesema kuwa ni vyema taasisi mbalimbali nchini pamoja na wananchi
wakachukua tahadhali za majanga ya moto ili kuepusha hasara zinazoweza
kujitokeza kufuatia majanga hayo.
Amesema
kuwa Wizara yake itaendelea kuliwezesha Jeshi la Zimamoto na Uokoaji vifaa vya
kisasa ili liweze kukabiliana na majanga ya moto pindi yanapojitokeza.
Aidha,
Katibu Mkuu huyo, Meja Jenerali Kingu amelitaka Jeshi la Magereza kuhakikisha
kuwa linafanya jitihada za haraka za kurejesha shughuli za uzalishaji katika
kiwanda hicho ikiwemo kufanyia matengenezo baadhi ya mashine zilizoteketezwa na moto.
Kwa
upande wake, Kamishna Jenerali wa Magereza nchini, Phaustine Kasike amevishukru
vyombo vya ulinzi na usalama ikiwemo Jeshi la Zimamoto na Uokoaji pamoja na
Jeshi la Polisi Mkoani Arusha sambamba na wananchi waliojitokeza kusaidia
katika uzimaji wa moto huo ambao umeunguza sehemu ya kiwanda hicho.
“Nawashukru
sana Jeshi la zimamoto na uokoaji Mkoani Arusha, Jeshi la Polisi pamoja na wananchi
kwa kazi kubwa waliyoifanya siku ya tukio kwani niliarifiwa kuwa moto ulikuwa
mkubwa lakini tunashukuru Mungu hatimaye uzimaji ulifanikiwa pamoja na hasara
iliyojitokeza”. Alisema Jenerali Kasike.
Akizungumzia
chanzo cha moto huo na hasara iliyojitokeza, Kamishna Jenerali Kasike amesema
kuwa taarifa za awali zinaonesha kuwa moto huo ulisababishwa na hitilafu ya
umeme ambayo ilisababisha kuteketea kwa baadhi ya mashine za kiwanda hicho
pamoja na uharibu wa nyaraka mbalimbali za ofisi katika jengo la utawala.
Wakati
huo huo, Kamishna Jenerali Phaustine Kasike ameunda Kamati maalum ya Maafisa
watano kutoka Makao Makuu ya Jeshi la Magereza ambayo itachunguza chanzo cha
moto huo pamoja na kuwasilisha taarifa kamili ya hasara iliyojitokeza. Tume
hiyo itaongozwa na Kamishna wa Fedha na Mipango wa Jeshi hilo, Kamishna wa
Magereza, Gideon Nkana.
Kiwanda
cha samani cha Magereza Arusha kilimikishwa rasmi kwa Jeshi la Magereza mwaka
1973 baada ya Azimio la Arusha mwaka 1967 ambapo tangu kipindi hicho kiwanda
hicho kinajishughulisha na utengenezaji wa samani mbalimbali za ofisi na samani
za majumbani. Pia kiwanda hiki hutumika kuwafundisha na kuwarekebisha wafungwa
ili wamalizapo vifungo vyao waweze kujitegemea kupitia ujuzi waliojifunza.
Katibu
Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Meja Jenerali Jacob Kingu akiwasili Novemba 17, 2018 katika Kiwanda cha samani cha Magereza Arusha kukagua sehemu
mbalimbali ambazo moto umeteketeza sehemu ya kiwanda hicho. Kushoto kwake ni
Kamishna Jenerali wa Magereza, Phaustine Kasike.
Mkuu
wa Magereza Mkoa huo, ACP Anderson Kamtiaro akisoma taarifa ya janga la moto
mbele ya Katibu Mkuu Mambo ya ndani ya nchi, Meja Jenerali Jacob Kingu
aliwasili kiwandani kujionea uhabribu mbalimbali uliojitokeza.
Kamishna
Jenerali wa Magereza nchini, Phaustine Kasike akitoa taarifa kwa Katibu Mkuu
Mambo ya ndani ya nchi, Meja Jenerali Jacob Kingu kuhusu hatua mbalimbali
ambazo amezichukua ikiwemo kuunda kamati maalum ya watu watano ambayo
itachunguza tukio la moto katika kiwanda hicho.
Kamishna Jenerali wa Magereza nchini, Phaustine Kasike (wa pili toka kulia) pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Meja Jenerali Jacob Kingu (kulia kwake), wakiangalia moja ya mashine mbalimbali ambazo zimeteketezwa na moto katika kiwanda cha Samani cha Magereza Arusha. Chanzo cha moto huo inasemekana ni hitilafu ya umeme ndani ya kiwanda hicho.
Katibu
Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Meja Jenerali Jacob Kingu (wa kwanza
kushoto) akitoa maelekezo mbalimbali kwa Kamishna Jenerali wa Magereza,
Phaustine Kasike(katikati). Kulia ni Kamishna wa Fedha na Mipango, Kamishna wa
Magereza, Gideon Nkana ambaye ni Kiongozi wa Kamati Maalum ya kuchunguza tukio
hilo.
Jengo
la kiwanda cha samani cha Magereza Arusha ambalo limeteketea kwa moto.
Muonekano
wa baadhi ya mashine pamoja na vifaa mbalimbali na nyaraka nyinginezo za ofisi
zilizoungua kufuatia janga la moto.
Samani
mbalimbali zinazotengenezwa katika kiwanda cha samani cha Magereza Arusha kama
inavyoonekana katika picha zikiwa tayari kwenda sokoni(Picha na Jeshi la Magereza).