Na
Lucas Mboje, Njombe
WAKUU
wa Magereza yote nchini wametakiwa kuwa wabunifu ili kutatua changamoto ya
uhaba wa makazi ya askari kwa kutumia nguvukazi ya wafungwa na rasilimali nyinginezo
zilizopo katika maeneo yao.
Wito
huo umetolewa leo Novemba 12, 2018 na Kamishna Jenerali wa Magereza nchini,
Phaustine Kasike alipofanya ziara ya kikazi ya kukagua magereza yote ya Mkoa wa
Njombe ambayo yanaendeshwa na Jeshi hilo.
Kamishna
Jenerali Kasike amesema kuwa lazima wakuu wa magereza wawe wabunifu katika
kutatua tatizo hilo la uhaba wa nyumba kwani Jeshi hilo linazo fursa nyingi
ikiwemo nguvu kazi ya wafungwa.
“Mkoa
wa Njombe na mingineyo nchini haipo sababu ya kuwa na tatizo la uhaba wa nyumba
za askari kwani kuna fursa ya kutosha ya kufyatua tofali za kuchoma kwa kuwatumia wafungwa ili kumaliza tatizo
hili nchini”. Amesisitiza Jenerali Kasike.
Aidha,
Kamishna Jenerali Kasike amewataka mafisa na askari wote kuendelea kutimiza
majukumu yao kwa kuzingatia maadili, sheria na kanuni mbalimbali za uendeshaji
wa Jeshi hilo.
Awali,
akisoma taarifa ya Gereza la Wilaya Njombe, Mkuu wa Gereza hilo, SP. Charls
Mihinga amesema kuwa tayari wameanzisha
mradi wa ufyatuaji wa tofali za kuchoma katika kambi ya mdandu ili kumaliza
tatizo la uhaba wa nyumba za watumishi wa gereza hilo.
“Katika
msimu huu tumeweza kufyatua tofali kubwa zipatazo 30,000 ambazo tayari
zimeshachomwa, tofali hizi zitatumika katika ujenzi wa nyumba za askari pamoja
na ujenzi wa Ofisi mpya ya Mkuu wa Magereza Mkoani Njombe”. Alisema SP.
Mihinga.
Pia,
ameongeza kuwa malengo ya baadaye ni
kuifanya kambi hiyo ya Gereza Njombe kuwa na taswira ya uzalishaji wa matofali
kwa wingi kwa ajili ya kufanya biashara na hivyo kuongeza maduhuri serikalini.
Jeshi
la Magereza linakabiliwa na uhaba wa nyumba za kuishi za Maafisa na askari hapa
nchini, mkakati uliopo hivi sasa chini ya uongozi wa Kamishna Jenerali wa
Magereza ni kuhakikisha kuwa tatizo hilo linatatulika kwa kutumia njia ya
ubunifu pamoja na fursa mbalimbali zilizopo ndani ya Jeshi hilo.
Kaimu Mkuu wa Mkoa wa
Njombe ambaye pia ni Katibu Tawala wa Mkoani Njombe Bw. Erick Shitindi
akisalimiana na Mkuu wa Jeshi la Magereza nchini (CGP) Phaustine Kasike
walipokutana Mkoani Njombe alipotembelea
Ofisi za Mkuu wa Mkoa huo kabla ya kuendelea na ziara yake ya kikazi Mkoani
Njombe, leo
Novemba 12, 2018.
Wajumbe
wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Njombe wakimsikiliza Mkuu
wa Jeshi la Magereza Nchini (CGP) Phaustine Kasike(hayupo pichani) alipotembelea
Ofisi za Mkuu wa Mkoa kabla ya kuendelea na ziara yake ya kikazi Mkoani humo.
Baadhi
ya Askari wa Gereza la Wilaya Njombe wakifuatilia maelekezo katika Baraza
lililoongozwa na Kamishna Jenerali wa
Magereza nchini, Phaustine Kasike ambapo askari hao wameelezea changamoto zao
kiutendaji leo Novemba 12, 2018.
Kamishna Jenerali wa Magereza nchini, Phaustine
Kasike(katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Maafisa na askari wa Gereza
Njombe.
Mkuu wa Jeshi la Magereza Nchini (CGP) Phaustine
Kasike(wa kwanza kulia) akizungumza jambo alipotembelea Ofisi za Mkuu wa Mkoa
wa Njombe. Wengine ni Maafisa Waandamizi wa Jeshi hilo.
Mkuu
wa Gereza Njombe, SP. Charles Mihinga(kushoto) akimtembeza Kamishna Jenerali wa
Magereza Nchini (CGP) Phaustine Kasike(kulia) alipotembelea gereza hilo leo
Novemba 12, 2018.( Picha na Jeshi la Magereza)