Sunday, January 27, 2019
GEREZA KITETE – NKASI LAANZA UZALISHAJI WA ZAO LA MAHARAGE
10:02 PM
Na ASP.
Lucas Mboje, Nkasi
KATIKA
kuelekea kwenye mpango wa kujitosheleza kwa chakula cha wafungwa magerezani Gereza
la Kilimo Kitete – Nkasi limeanza uzalishaji wa maharage ambapo katika msimu
huu wa mwaka 2018/2019 tayari limelima zao hilo.
Akizungumza
leo mara baada ya kutembelea Gereza hilo, Kamishna Jenerali wa Magereza nchini,
Phaustine Kasike amesema kuwa ameridhishwa na hatua mbalimbali zinazoendelea
katika kufanikisha mpango mkakati wa uzalishaji wa chakula kwa wingi katika
maeneo yakimkakati pamoja na uwepo wa changamoto mbalimbali ikiwemo mabadiliko
ya hali ya hewa na vitendea kazi.
“Ni
lazima tuhakikishe kuwa jukumu hili tulilopewa linatekelezwa ipasavyo hivyo,
Mkuu wa Gereza pamoja na timu yako hakikisheni mnaongeza bidii ya kazi kwa
kutumia rasilimali zilizopo ikiwemo nguvu kazi ya wafungwa ili kufikia malengo
ya hekari 300 za zao la maharge mlizopewa kwani msimu bado unaruhusu”. Alisema
Kamishna Jenerali Kasike.
Aidha,
Kamishna Jenerali Kasike amesema kuwa Jeshi litaangalia uwezekano wa
kuliwezesha Gereza Kitete zana mbalimbali za kilimo kama vile trekta, ambazo
zitarahisisha kufanikisha malengo ya kimkakati ili kuongeza uzalishaji wa
chakula cha wafungwa.
Ameongeza
kuwa Gereza Kitete - Nkasi ni miongoni mwa magereza 10 ya kimkakati ambayo
tayari yameainishwa katika mpango mkakati wa Jeshi la Magereza katika
kujitosheleza kwa chakula cha wafungwa. Magereza mengine ni Songwe, Mollo, Arusha,
Idete, Kiberege, Kitengule, Pawaga, Kitai na Gereza Ludewa.
Katika
hatua nyingine, Kamishna Jenerali Kasike amewaasa viongozi wa Jeshi hilo pamoja
na watendaji waliopewa dhamana ya kusimamia vitengo(Ugavi na Uhasibu) katika
vituo vyao kuzingatia suala la uadilifu na amewataka kujiepushe na vitendo
vyote vya ubadhilifu wa mali za umma ili kuwezesha kufikia malengo
yaliyokusudiwa.
Kwa
upande wake, Mkuu wa Gereza Kitete, SP. Job Lwesya alisema kuwa katika msimu wa Kilimo wa mwaka 2018/2019
gereza hilo limelima ekari 114 za maharage na kwa sasa linaendelea na
maandalizi ya mashamba mengine ili kufikia malengo waliyopewa ya kulima hekari
300 za maharage.
Aidha,
aliongeza kuwa gereza hilo linayo ardhi
ya kutosha na yenye rutuba hivyo wamejipanga kimkakati katika kuhakikisha kuwa
wanazalisha mazao mbalimbali kwa wingi kwa ajili ya chakula wafungwa.
Gereza
Kitete - Nkasi lina eneo lenye ukubwa wa ekari 3,742 ambazo zinafaa kwa kilimo
cha mazao mbalimbali ya chakula ikiwemo zao la maharage, mahindi na Alizeti.
Gereza hilo lilianzishwa rasmi mwaka 1989 kwa lengo la kuwahifadhi wahalifu
pamoja na kuwapatia wafungwa programu za urekebishaji ili wamalizapo vifungo
vyao waweze kuwa raia wema.
Thursday, January 24, 2019
KAMISHNA JENERALI WA MAGEREZA, PHAUSTINE KASIKE AWASILI JIJINI MBEYA LEO TAYARI KWA ZIARA YA KIKAZI KATIKA BAADHI YA MIKOA YA NYANDA ZA JUU KUSINI
11:33 PM
Kamishna Jenerali wa Magereza nchini, Phaustine
Kasike(kulia vazi la kiraia) akiwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa
Songwe leo Januari 24, 2019 tayarri kwa ziara ya kikazi katika baadhi ya mikoa
ya nyanda za juu kusini ikiwemo Mbeya, Songwe, Rukwa, Katavi na Ruvuma.
Kutoka kulia ni Mkuu wa Gereza
Kuu Ruanda Mbeya, SSP Lugona Msomba, Mkuu wa Chuo cha Mafunzo ya awali ya Uaskari
Magereza – Kiwira, ACP. Mathias Mkama, Mkuu wa Chuo cha Ufundi
Ruanda Mbeya, SSP. Enock Lupyuto kwa pamoja wakiteta jambo kabla ya mapokezi ya
Mkuu wa Jeshi la Magereza nchini leo Januari 24, 2019 jijini Mbeya.
Kamishna Jenerali wa Magereza nchini, Phaustine
Kasike(vazi la kiraia) akisalimiana na Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama
Mkoa wa Mbeya mapema alipowasili katika
Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Songwe leo Januari 24, 2019 kwa ziara ya kikazi
katika baadhi ya mikoa ya nyanda za juu kusini.
Kamishna
Jenerali wa Magereza nchini, Phaustine Kasike(katikati vazi la kiraia) akiteta
jambo na Maafisa Waandamizi wa Jeshi hilo mara baada ya kuwasili jijini Mbeya
kwa ziara ya kikazi(kulia) ni Mkuu wa Magereza Mkoani Mbeya, SACP. Luhende
Makwaia(wa kwanza kushoto) ni Mkuu wa Chuo cha Mafunzo ya awali ya Uaskari
Magereza – Kiwira, ACP. Mathias Mkama(wa pili toka kushoto) ni Mkuu wa Magereza
Mkoani Mbeya, ACP. Lyzek Mwaseba.(Picha zote na Jeshi la Magereza).
Tuesday, January 1, 2019
SALAAM ZA KAMISHNA JENERALI WA MAGEREZA PHAUSTINE KASIKE KWA WATUMISHI WA JESHI HILO KATIKA KUFUNGA MWAKA 2018 NA KUUKARIBISHA MWAKA 2019 TAREHE 31 DEC, 2018
10:14 AM
Na
ASP Deodatus Kazinja
Katika
kufunga mwaka 2018 na kuukaribisha mwaka 2019
Kamishna Jenerali wa Magereza, Phaustine Kasike ameelezea matarajio ya
Jeshi hilo kwa mwaka 2019 kuwa ni pamoja
kuimarisha ushirikiano na wadau mbalimbali zikiwemo asasi za kiraia
katika kutoa huduma kwa wafungwa na mahabusu.
Matarajio
mengine ni pamoja na kuimarisha hali ya
ulinzi na usalama magerezani ikiwa ni pamoja na kusimika mifumo ya kiusalama, kujenga
kiwanda cha seremala mkoani Dodoma ili kuongeza na kuimarisha utengenezaji wa samani, kujenga nyumba 100
mkoani Dodoma kwa ajili ya watumishi wa ofisi ya Makao makuu mkoani humo.
Aidha,
Kamishna Jenerali Kasike ameongeza kuwa matarajio ya mwaka ujao ni Kuanzisha ujenzi wa Jengo la Ofisi ya Makao
Makuu mkoani Dodoma, kuendelea kuhimiza ujenzi wa nyumba kwa njia ya kujitolea
ili kupunguza uhaba wa nyumba za watumishi wa jeshi hilo,
Pia
amesema atahakikisha Shirika la Magereza (Magereza Corporation Sole) linapata
Bodi ili kujiimarisha katika kufanya shughuli za kibiashara.
Ameongeza kuwa Jeshi la Magereza litashirikiana
na Idara ya mahakama katika kukamilisha maandalizi ya uendeshaji wa mashauri
kwa mfumo wa kielektroniki wa ‘video conference’ ili kurahisisha utoaji wa haki
kwa wafungwa na mahabusu kwa wakati.
Kamishna
Jenerali Kasike amehitimisha Salaam za Mwaka Mpya kwa kusisitiza suala la
ufanyaji kazi kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zinazoongoza Jeshi hilo
na amewataka askari kubadili mtazamo wa kiutendaji na kuacha kufanya kazi kwa
mazoea. “Kila mmoja atimize wajibu wake
kikamilifu kwa kutumia uweledi, ubunifu na kutanguliza maslahi ya Taifa mbele”.
Kamishna Jenerali wa Magereza Phaustine Kasike
(kushoto) akiwasili tayari katika Baraza la kufunga mwaka 2018 na kuukaribisha
mwaka 2019 Desemba 31, 2018 Makao Makuu ya Jeshi la Magereza
Kamishna Jenerali wa Magereza Phaustine Kasike
akizungumza na maafisa na askari wa Jeshi la Magereza katika Baraza la kufunga
mwaka 2018 na kuukaribisha mwaka 2019 Desemba 31, 2018 Makao Makuu ya Jeshi
la Magereza
Baadhi ya maafisa, askari na watumishi raia wa Jeshi
la Magereza wakimsilikiliza Kamishna
Jenerali wa Magereza Phaustine Kasike (hayupo pichani)wakati wa Baraza la
kufunga mwaka 2018 na kuukaribisha mwaka 2019 Desemba 31, 2018 Makao Makuu
ya Jeshi la Magereza
Baadhi ya Maafisa wa Jeshi la Magereza wakiwa
wamesimama kwa heshima kuwakumbuka watumishi mbalimbali wa jeshi hilo walioaga
dunia kwa mwaka 2018. (Picha zote na
Jeshi la Magereza)