Na ASP.
Lucas Mboje, Nkasi
KATIKA
kuelekea kwenye mpango wa kujitosheleza kwa chakula cha wafungwa magerezani Gereza
la Kilimo Kitete – Nkasi limeanza uzalishaji wa maharage ambapo katika msimu
huu wa mwaka 2018/2019 tayari limelima zao hilo.
Akizungumza
leo mara baada ya kutembelea Gereza hilo, Kamishna Jenerali wa Magereza nchini,
Phaustine Kasike amesema kuwa ameridhishwa na hatua mbalimbali zinazoendelea
katika kufanikisha mpango mkakati wa uzalishaji wa chakula kwa wingi katika
maeneo yakimkakati pamoja na uwepo wa changamoto mbalimbali ikiwemo mabadiliko
ya hali ya hewa na vitendea kazi.
“Ni
lazima tuhakikishe kuwa jukumu hili tulilopewa linatekelezwa ipasavyo hivyo,
Mkuu wa Gereza pamoja na timu yako hakikisheni mnaongeza bidii ya kazi kwa
kutumia rasilimali zilizopo ikiwemo nguvu kazi ya wafungwa ili kufikia malengo
ya hekari 300 za zao la maharge mlizopewa kwani msimu bado unaruhusu”. Alisema
Kamishna Jenerali Kasike.
Aidha,
Kamishna Jenerali Kasike amesema kuwa Jeshi litaangalia uwezekano wa
kuliwezesha Gereza Kitete zana mbalimbali za kilimo kama vile trekta, ambazo
zitarahisisha kufanikisha malengo ya kimkakati ili kuongeza uzalishaji wa
chakula cha wafungwa.
Ameongeza
kuwa Gereza Kitete - Nkasi ni miongoni mwa magereza 10 ya kimkakati ambayo
tayari yameainishwa katika mpango mkakati wa Jeshi la Magereza katika
kujitosheleza kwa chakula cha wafungwa. Magereza mengine ni Songwe, Mollo, Arusha,
Idete, Kiberege, Kitengule, Pawaga, Kitai na Gereza Ludewa.
Katika
hatua nyingine, Kamishna Jenerali Kasike amewaasa viongozi wa Jeshi hilo pamoja
na watendaji waliopewa dhamana ya kusimamia vitengo(Ugavi na Uhasibu) katika
vituo vyao kuzingatia suala la uadilifu na amewataka kujiepushe na vitendo
vyote vya ubadhilifu wa mali za umma ili kuwezesha kufikia malengo
yaliyokusudiwa.
Kwa
upande wake, Mkuu wa Gereza Kitete, SP. Job Lwesya alisema kuwa katika msimu wa Kilimo wa mwaka 2018/2019
gereza hilo limelima ekari 114 za maharage na kwa sasa linaendelea na
maandalizi ya mashamba mengine ili kufikia malengo waliyopewa ya kulima hekari
300 za maharage.
Aidha,
aliongeza kuwa gereza hilo linayo ardhi
ya kutosha na yenye rutuba hivyo wamejipanga kimkakati katika kuhakikisha kuwa
wanazalisha mazao mbalimbali kwa wingi kwa ajili ya chakula wafungwa.
Gereza
Kitete - Nkasi lina eneo lenye ukubwa wa ekari 3,742 ambazo zinafaa kwa kilimo
cha mazao mbalimbali ya chakula ikiwemo zao la maharage, mahindi na Alizeti.
Gereza hilo lilianzishwa rasmi mwaka 1989 kwa lengo la kuwahifadhi wahalifu
pamoja na kuwapatia wafungwa programu za urekebishaji ili wamalizapo vifungo
vyao waweze kuwa raia wema.