Banner

Banner

Saturday, December 31, 2016

KAIMU KAMISHNA JENERALI WA MAGEREZA DKT. JUMA MALEWA AWAASA MAOFISA MAGEREZA KUTIMIZA WAJIBU WAO KWA UFANISI

 
Na Lucas Mboje, Dar es Saam
KAIMU Kamishna Jenerali wa Magereza nchini, Dkt. Juma Malewa(pichani) amewaasa Maafisa na Askari wa Jeshi la Magereza  nchini kuzingatia  kuwa utendaji wao wa kazi za kila siku uende sambamba na kasi ya Serikali ya Awamu ya tano ili kuleta ufanisi unaotarajiwa.
 
KAIMU Kamishna Jenerali, Dkt. Malewa ameyasema hayo jana wakati wa Baraza la Kufunga Mwaka 2016 na kuukaribisha Mwaka 2017 lililowahusisha baadhi ya Maafisa na Askari kutoka Ofisi ya Makao Makuu ya Jeshi la Magereza, Chuo cha Taaluma ya Urekebishaji Ukonga, Kikosi Maalum cha Kutuliza Ghasia Magerezani pamoja na Magereza ya Mkoa wa D'Salaam.

Aidha, amewataka Maofisa na Askari wa Jeshi hilo kudumisha nidhamu wanapokuwa wakitekeleza majukumu yao ya kazi  ikiwemo kutekeleza mara moja Amri mbalimbali zinazotolewa na Viongozi wao wa Jeshi.
 
"Kila mmoja wenu atimize wajibu wake katika eneo lake la kazi kwa bidii, ari na moyo wa kujituma ili kuliwezesha Jeshi letu kupata ufanisi unaotarajiwa". Alisisitiza Kaimu Jenerali Dkt. Malewa.
 
Wakati huo huo Kaimu Kamishna Jenerali wa Magereza nchini, Dkt. Juma Malewa  pia ametumia fursa hiyo kuelezea baadhi ya mafanikio mbalimbali yaliyopatikana kwa Mwaka uliopita 2016 ambapo Jeshi la Magereza limeweza kupata jumla ya leseni 102 za uchimbaji wa madini ya ujenzi kama vile chokaa, mawe, kokoto, mchanga na Murram katika maeneo mbalimbali ya magereza. Pia katika mwaka 2016 Jeshi limeweza kujenga nyumba 129 kwa njia ya kujitolea ambapo nyumba 231 zipo katika hatua mbalimbali ya ukamilishaji.
 
Aidha, Ujenzi wa nyumba 320 za makazi ya askari katika eneo la Gereza Ukonga maandalizi ya ujenzi yanaendelea na ujenzi wa nyumba hizo ni kufuatia ziara ya Rais Magufuli  Novemba 29 mwaka huu  ambapo alipokea taarifa ya uhaba wa nyumba za kuishi askari wa jeshi hilo na akaagiza Jeshi la Magereza lipatiwe Tsh. bilioni 10 haraka ili kupunguza tatizo hilo.
 
Shirika la Magereza na Mfuko wa hifadhi ya Jamii wa PPF wameingia Makubaliano ya Mkataba wa ubia katika mradi wa ujenzi wa Kiwanda kipya cha kusakata ngozi pamoja na uwekezaji wa mashine za kisasa za kutengnezea bidhaa za ngozi katika Kiwanda cha Viatu cha Gereza Karanga, Moshi.
Chuo cha Maafisa Magereza Ukonga kimepata Ithibati na hivyo kuwa na hadhi ya kuwa Chuo cha Taaluma ya Urekebishaji na mapema mwakani kinatarajia kudahili wanafunzi 30 katika fani ya Taaluma ya Urekebishaji ngazi ya cheti. 
 
Pamoja na Mafanikio hayo, Kaimu Kamishna Jenerali Dkt. Malewa ameelezea changamoto mbalimbali zinazolikabili Jeshi hilo ikiwemo ufinyu wa bajeti, makazi duni ya maofisa na askari, uhaba wa vitendea kazi, ukosefu wa pembejeo pamoja na madeni ya wabuni na watumishi wa jeshi hilo.
 
Kuhusu maeneo yatakayopewa kipaumbele kwa Mwaka mpya 2017 ni kuwa Jeshi la Magereza litaendeleza jitihada za kuimarisha na kuongeza uzalishaji kwenye miradi ya uzalishaji wa mazao ya Kilimo na mifugo lengo ikiwa ni kujitosheleza kwenye chakula cha wafungwa, kuhakikisha wafungwa wanafanya kazi za uzalishaji mali kwa kiwango chenye tija badala ya kukaa tu magerezani pia kuendeleza mikakati ya kupunguza msongamano magerezani.
 
Baraza la kufunga Mwaka na kuukaribisha Mwaka unaofuata ni utamaduni wa siku nyingi ambao unaenziwa na Viongozi Wakuu wa Jeshi la Magereza ambapo Baraza la aina hii hufanyika kila Mwaka ili Kamishna Jenerali wa Magereza nchini aweze kuongea na Watumishi wote wa Jeshi la Magereza nchini kupitia Baraza hilo lengo ikiwa ni kufanya tathmini ya yale yaliyojiri katika Jeshi kwa kipindi cha Mwaka unaisha kwa kuzungumzia mafanikio na changamoto zilizojitokeza na  kutazama matarajio ya Mwaka mpya.

Friday, December 30, 2016

KAIMU KAMISHNA JENERALI WA MAGEREZA AHUTUBIA BARAZA LA KUFUNGA MWAKA 2016 NA KUUKARIBISHA MWAKA MPYA 2017 JIJINI DAR

Kaimu Kamishna Jenerali wa Magereza, Dkt. Juma Malewa akitoa hotuba yake fupi ya kufunga mwaka 2016 na kuukaribisha mwaka mpya 2017 kwenye Baraza la Maafisa na Askari kutoka vituo mbalimbali vya Magereza Mkoani Dar es Salam Desemba 30, 2016 katika Bwalo Kuu la Maafisa Magereza Ukonga.
Naibu Kamishna wa Magereza, Edith Mallya akimkaribisha Kaimu Kamishna Jenerali wa Magereza, Dkt. Juma Malewa(katikati aliyeketi) kabla ya kuongea na Maafisa na Askari wa Jeshi la Magereza Mkoa wa Dar es Salaam katika Baraza Maalum la kufunga mwaka 2016 na kuukaribisha mwaka mpya 2017(kushoto) ni Mkuu wa Magereza Mkoa wa D ar es Salaam, SACP. Augustine Mboje. Baraza hilo limefanyika Bwalo Kuu la Maafisa Magereza Ukonga, Dar es Salaam Desemba 30, 2016.
Kaimu Kamishna Jenerali wa Magereza, Dkt. Juma Malewa akijibu kero mbalimbali zilizoulizwa na Maafisa na Askari wa Jeshi la Magereza Mkoa wa Dar es Salaam(hawapo pichani) katika Baraza Maalum la kufunga mwaka 2016 na kuukaribisha mwaka mpya 2017
Askari wa Jeshi la Magereza kutoka vituo mbalimbali vya Magereza ya Mkoa wa Dar es Salaam wakisikiliza hotuba ya Kaimu Kamishna Jenerali wa Magereza, Dkt. Juma Malewa(hayupo pichani) katika Baraza Maalum la kufunga mwaka 2016 na kuukaribisha mwaka mpya 2017.
Afisa Utumishi wa Jeshi la Magereza, Mrakibu wa Magereza Elmas Mgimwa akitolea ufafanuzi kuhusiana na masuala ya kiutumishi yaliyoulizwa na Maafisa na Askari wa Jeshi la Magereza Mkoa wa Dar es Salaam(hawapo pichani) katika Baraza hilo.
Baadhi ya Maafisa Waandamizi wa Jeshi la Magereza wakifuatilia kwa umakini mkubwa hotuba ya Kaimu Kamishna Jenerali wa Magereza, Dkt. Juma Malewa kwenye Baraza hilo. 

(Picha zote na Lucas Mboje wa Jeshi la Magereza).

Saturday, December 24, 2016

WAZIRI MKUU AKAGUA ENEO LA UJENZI WA MAKAZI YA ASKARI MAGEREZA JIJINI DAR, AMPONGEZA KAIMU KAMISHNA JENERALI WA MAGEREZA NAMNA ALIVYOJIPANGA KUSIMAMIA UJENZI

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa(Mb)  akisalimiana na Kaimu Kamishna Jenerali wa Magereza, Dkt. Juma Malewa kabla ya kuongea na Maafisa na askari wa Jeshi la Magereza Mkoa wa Dar es Salaam alipofanya ziara ya kikazi ya kukagua maandalizi ya ujenzi wa nyumba 320 za makazi ya Maafisa na askari wa Jeshi hilo katika eneo la Gereza Kuu Ukonga, Jiji la Dar es Salaam Disemba 24, 2016(wa kwanza kushoto) ni Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni (Mb).
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa(Mb) akikagua Gwaride Maalum la heshima lililoandaliwa na Maofisa na askari wa Jeshi la Magereza kabla ya kukagua eneo la ujenzi wa nyumba 320 za makazi ya Maafisa na askari wa Jeshi hilo katika eneo la Gereza Kuu Ukonga, Jiji la Dar es Salaam Disemba 24, 2016.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa(Mb) akipokea Salaam ya heshima kutoka Gwaride Maalum la heshima lililoandaliwa na Maofisa na askari wa Jeshi la Magereza kabla ya kukagua eneo la ujenzi wa nyumba 320 za makazi ya Maafisa na askari wa Jeshi hilo katika eneo la Gereza Kuu Ukonga, Jiji la Dar es Salaam Disemba 24, 2016.
Kaimu Kamishna Jenerali wa Magereza, Dkt. Juma Malewa akitoa maelezo mafupi kwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim(hayupo pichani) namna Jeshi hilo lilivyojipanga katika kuhakikisha kuwa ujenzi wa nyumba hizo ambazo zinatarajiwa kujengwa katika eneo la Gereza Kuu Ukonga, Jijini Dar es Salaam unakamilika ipasavyo.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa akitoa hotuba fupi kwa  Maafisa na askari wa Jeshi la Magereza  alipofanya ziara ya kikazi ya kukagua maandalizi ya ujenzi wa nyumba 320 za makazi ya askari katika eneo la Gereza Kuu Ukonga, Jiji la Dar es Salaam Disemba 24, 2016.
Baadhi ya Maafisa na askari wa Jeshi la Magereza wakimsikiliza Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa alipofanya ziara ya kikazi ya kukagua maandalizi ya ujenzi wa nyumba 320 za makazi ya askari katika eneo la Gereza Kuu Ukonga, Jiji la Dar es Salaam Disemba 24, 2016.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa akiteta jambo na Naibu Waziri wa Mambo ya ndani ya nchi, Mhandisi Hamad Masauni(kulia).
Meneja Ujenzi wa Mamlaka ya Majengo nchini – TBA, Arch. Humphrey Killo akitoa maelezo ya kitalaam kwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa alipofanya ziara ya kikazi ya kukagua maandalizi ya ujenzi wa nyumba 320 za makazi ya askari katika eneo la Gereza Kuu Ukonga, Jiji la Dar es Salaam Disemba 24, 2016.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa akikagua eneo la ujenzi wa nyumba hizo za makazi ya askari kama inavyoonekana katika picha.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa akiwa katika picha ya pamoja na Maafisa Waandamizi wa Jeshi la Magereza alipofanya ziara ya kikazi ya kukagua maandalizi ya ujenzi wa nyumba 320 za makazi ya askari katika eneo la Gereza Kuu Ukonga, Jiji la Dar es Salaam

(Picha zote na Lucas Mboje wa Jeshi la Magereza).

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametembelea gereza la Ukonga jijini Dar es Salaam na kukagua eneo la ujenzi wa makazi ya askari wa Magereza unaotarajiwa kuanza baada ya wiki tatu zijazo.

Akizungumza na askari wa magereza kabla ya kufanya ukaguzi huo leo (Jumamosi, Desemba 24, 2016) Waziri Mkuu amesema ziara aliyoifanya leo, ni ufuatiliaji wa maagizo ya Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli aliyoitoa wakati alipoenda kukagua gereza hilo.

Novemba 29, mwaka huu, Rais Magufuli alifanya ziara kwenye gereza hilo na kupokea taarifa ya uhaba wa nyumba za kuishi askari wa jeshi hilo zipatazo 9,500 na akaagiza zitafutwe sh. bilioni 10 haraka ili kupunguza tatizo hilo.

Akizungumzia kuhusu ujenzi huo, Waziri Mkuu amesema amefarijika kukuta Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) wako eneo la kazi na wameanza kusafisha eneo hilo.

“Nimefarijika kukuta TBA wako kazini na nimeelezwa hatua inayofuata ni upimaji wa sampuli za udongo kabla hawajaanza kujenga msingi. Nawapongeza TBA kwa kazi nzuri wanazofanya za ujenzi wa nyumba zenye viwango na kwa haraka kama tulivyoona kule Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na nyumba za Magomeni Kota,” amesema.

Waziri Mkuu amesema Serikali inatambua mchango uliofanywa na Serikali ya awamu ya nne katika suala la makazi ya askari kama vile wa Jeshi la Wananchi (JWTZ) na Jeshi la Polisi. “Nia ya Serikali ni kuhakikisha makamanda wote wanapata nyumba nzuri ili waendelee kufanya kazi zao kwa weledi mkubwa wakiwa na uhakika familia zao zimetulia kwenye makazi bora”.

Amesema katika ziara alizozifanya kwenye mikoa mbalimbali, alitembelea magereza ya Isanga, Msalato (Dodoma), Lindi, Singida na Keko (Dar es Salaam) alikuta nyumba za askari hazina viwango na kama zipo zimechakaa sana.

Mapema, akitoa taarifa kuhusu ujenzi wa nyumba hizo, Kaimu Kamishna Jenerali wa Magereza, Juma Malewa alisema wanamshukuru Mheshimiwa Rais kwa kuwapatia fedha za ujenzi wa makazi ya askari na kwamba jeshi hilo litafanya kazi zote zisizo za kitaalamu ili kuokoa fedha za Serikali na badala ya kulipwa watu binafsi, fedha hizo zitatumika kuongeza nyumba zaidi.

“Tumekubaliana na TBA kazi zote zisizohitaji utalaamu kama kufyatua matofali, kubeba mizigo au kufyeka zitafanywa na askari wetu pamoja na wafungwa ili tuokoe gharama zote hizo na badala ya kulipa watu binafsi, fedha hizo zitumike kujenga nyumba nyingine 80,” alisema huku akishangiliwa.

Alisema wamejipanga kufanya kazi hizo kwa saa 24 kila siku ili kuokoa muda ambao TBA walikuwa wameuweka wa kukamilisha ujenzi ndani ya miezi minane.

Alisema wako tayari kuanzisha kambi za ujenzi kwa kutumia wafungwa na askari ili wafanye kazi zisizohitaji utaalamu na fedha zitakazopatikana, badala ya kuwalipa watu binafsi zitumike kujenga nyumba zaidi za askari.

Naye mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa TBA, Bw. Baltazar Kimangano alisema wanataraji kuanza ujenzi ndani ya wiki tatu baada ya kupokea matokeo ya uchunguzi wa sampuli za udongo kutoka taasisi ya BICO ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Alisema wanataraji kujenga majengo (block) manne ya ghorofa sita kila moja ambayo kwa ujumla yatakuwa na nyumba 240 zenye ukubwa wa vyumba viwili vya kulala. Pia watajenga majengo (block) mengine mawili ya ghorofa sita kila moja ambayo yatakuwa na nyumba 80 zenye ukubwa wa vyumba vitatu vya kulala.





IMETOLEWA NA:

OFISI YA WAZIRI MKUU,


2 MTAA WA MAGOGONI,

L. P. 3021,

11410 – DAR ES SALAAM

JUMAMOSI, DESEMBA 24, 2016

Monday, December 19, 2016

JESHI LA MAGEREZA NA WAKALA WA MAJENGO - TBA WAINGIA MAKUBALIANO UJENZI WA NYUMBA 320 ZA ASKARI MAGEREZA MKOA WA DAR ES SALAAM

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Majengo – TBA, Arch. Elius Mwakalinga akimkabidhi Mkataba wa Makubaliano ya mradi wa ujenzi wa nyumba 320 Kaimu Kamishna Jenerali wa Magereza, Dkt. Juma Malewa. Hafla hiyo ya uwekaji saini makubaliano hayo ya ujenzi wa nyumba za askari wa Jeshi la Magereza Mkoani Dar es Salaam imefanyika leo Desemba 19, 2016 Jijini, Dar es Salaam katika Ukumbi wa TBA. Ujenzi wa nyumba hizo ni agizo la Rais Magufuli kufuatia ziara yake hivi karibuni ambapo alitoa kiasi cha bilioni 10 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za makazi ya askari wa Jeshi hilo.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Majengo – TBA, Arch. Elius Mwakalinga (kushoto) na Kaimu Kamishna Jenerali wa Magereza, Dkt. Juma Malewa(kulia) kwa pamoja wakisaini Mkataba wa Makubaliano ya ujenzi wa nyumba 320 za Askari wa Jeshi la Magereza Mkoa wa Dar es Salaam katika Ukumbi wa Mikutano wa TBA, leo Desemba 19, 2016 Jijini, Dar es Salaam.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Majengo – TBA, Arch. Elius Mwakalinga na Kaimu Kamishna Jenerali wa Magereza, Dkt. Juma Malewa(kulia) wakionesha nyaraka mbalimbali baada ya hafla fupi ya uwekaji saini wa Mkataba wa Makubaliano ya mradi wa ujenzi wa nyumba 320 za askari wa Jeshi la Magereza Mkoani Dar es Salaam.
Maafisa Waandamizi wa Wakala wa Majengo - TBA wakifuatilia majadiliano kabla ya uwekaji saini wa Mkataba wa Makubaliano ya ujenzi wa nyumba 320 za Askari wa Jeshi la Magereza Mkoa wa Dar es Salaam katika Ukumbi wa Mikutano wa TBA, leo 19 Desemba, 2016 Jijini Dar es Salaam.
Kamishna wa Fedha na Utawala wa Jeshi la Magereza, Gaston Sanga(wa kwanza kushoto) akiwa pamoja na Maafisa Waandamizi wa Jeshi la Magereza wakishuhudia uwekaji saini wa Makubaliano ya ujenzi wa nyumba 320 za Askari wa Jeshi la Magereza Mkoa wa Dar es Salaam katika Ukumbi wa Mikutano wa TBA, leo 19 Desemba, 2016 Jijini Dar es Salaam.

(Picha zote na Lucas Mboje wa Jeshi la Magereza)

Friday, December 9, 2016

RAIS DKT JOHN POMBE MAGUFULI ASAMEHE WAFUNGWA 5,678 MAADHIMISHO YA MIAKA 55 YA UHURU WA TANZANIA BARA LEO 9 DISEMBA, 2016 JIJIJINI DAR

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Katika kuadhimisha miaka 55 ya Uhuru wa Tanzania Bara tarehe  9 Disemba, 2016 Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutumia madaraka aliyopewa chini ya Ibara ya 45(1)(d) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ametoa msamaha kwa wafungwa wafuatao:-

(i)    Wafungwa wote wamepunguziwa moja ya sita (1/6) ya vifungo vyao zaidi ya punguzo la kawaida linalotolewa chini ya kifungu 49(1) cha Sheria ya Magereza Sura ya 58 isipokuwa wafungwa walioorodheshwa katika Ibara ya 2 (i-xx).

(ii)    Wafungwa wagonjwa wenye magonjwa kama UKIMWI, KIFUA KIKUU (TB) na SARATANI (CANCER) ambao wako kwenye “terminal stage”. Wafungwa ambao wamethibitishwa na Jopo la Waganga chini ya Uenyekiti wa Mganga Mkuu wa Mkoa/Mganga Mkuu wa Wilaya.

(iii)    Wafungwa wazee wenye umri wa miaka sabini (70) au zaidi ambao umri huo umethibitishwa na Jopo la Waganga chini ya Uenyekiti wa Mganga Mkuu wa Mkoa/Mganga Mkuu wa Wilaya.

(iv)    Wafungwa wa kike walioingia na mimba gerezani, pamoja na wale walioingia na watoto wanaonyonya na wasionyonya.

(v)    Wafungwa wenye ulemavu wa mwili na akili (Physical disability and mental disability) ambao ulemavu huo umethibitishwa na Jopo la Waganga chini ya Uenyekiti wa Mganga Mkuu wa Mkoa/Mganga Mkuu wa Wilaya.

2.    Aidha, Msamaha huu wa Mheshimiwa Rais hautawahusu wafungwa wafuatao:-

(i)    Wafungwa waliohukumiwa adhabu ya kunyongwa.
(ii)    Wafungwa waliohukumiwa adhabu ya kunyongwa na adhabu hiyo kubadilishwa kuwa kifungo cha maisha au kifungo gerezani.
(iii)    Wafungwa waliohukumiwa kifungo cha maisha gerezani.

(iv)    Wafungwa wanaotumikia kifungo kwa makosa ya kujihusisha na usafirishaji na matumizi ya madawa ya kulevya kama vile cocaine, heroin, bhangi n.k.

(v)    Wafungwa wanaotumikia kifungo kwa makosa ya kujihusisha na uombaji, upokeaji au utoaji rushwa.

(vi)    Wafungwa wanaotumikia kifungo kwa makosa ya unyang’anyi na unyang’anyi wa kutumia silaha au kujaribu kutenda makosa hayo (robbery with violence, armed robbery and attempt robbery).

(vii)    Wafungwa wanaotumikia kifungo kwa makosa ya kupatikana na silaha, risasi au milipuko isivyo halali (firearms, ammunitions and explosives).

(viii)    Wafungwa wanaotumikia kifungo kwa makosa ya shambulio la aibu, kunajisi, kubaka na kulawiti, au kujaribu kutenda makosa hayo.

(ix)    Wafungwa waliopatikana na hatia na kuhukumiwa kifungo kwa kosa la kuwapa mimba wanafunzi wa Shule za Msingi na Shule za Sekondari na ambao walitenda kosa hilo wakiwa na umri wa miaka kumi na nane (18) na kuendelea.

(x)    Wafungwa wanaotumikia kifungo kwa makosa ya wizi wa magari na pikipiki au kujaribu kutenda makosa hayo.

(xi)    Wafungwa wanaotumikia kifungo chini ya Sheria ya Bodi ya Parole (Act. No. 25/1994) na Sheria ya Huduma kwa Jamii (Act. No. 6/2002).

(xii)    Wafungwa waliopatikana na hatia na kuhukumiwa kifungo kwa makosa ya kutumia vibaya madaraka yao.

(xiii)    Wafungwa waliowahi kupunguziwa kifungo na Msamaha wa Mheshimiwa Rais na bado wangali wanaendelea kutumikia sehemu ya kifungo kilichobaki.

(xiv)    Wafungwa waliopatikana na hatia na kuhukumiwa kwa kosa la kuzuia watoto kupata masomo.

(xv)    Wafungwa waliopatikana na hatia na kuhukumiwa kwa kosa la utekaji wa watoto, kupoka na kufanya biashara ya binadamu (Human Trafficking).

(xvi)    Wafungwa waliopatikana na hatia na kuhukumiwa kwa kosa la kukutwa na viungo vya binadamu.

(xvii)     Wafungwa wanaotumikia vifungo kwa makosa ya kujihusisha na  usafirishaji wa nyara za Serikali na ujangili (Poachers).

(xviii)    Wafungwa wanaotumikia kifungo kwa makosa ya        wizi/ubadhirifu wa fedha za Serikali.

(xix)    Wafungwa wanaotumikia vifungo kwa makosa ya kutoroka au kujaribu kutoroka chini ya ulinzi halali.

(xx)    Wafungwa walioingia gerezani baada ya tarehe 9/10/2016.


3.    Wafungwa wapatao 5,678 watafaidika na msamaha huu baada ya kupunguziwa 1/6 ya vifungo vyao ambapo 1,340 wataachiliwa huru na wafungwa 4,338 watanufaika na kubaki gerezani wakitumikia sehemu ya kifungo kilichobaki. Ni mategemeo ya Serikali kwamba watakaoachiliwa huru watarejea tena katika jamii kushirikiana na wenzao katika ujenzi wa Taifa na kwamba watajiepusha kutenda makosa ili wasirejee tena gerezani.

Imesainiwa na;
Meja Jenerali  Projest  Rwegasira
KATIBU MKUU WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI
9/12/2016

Tuesday, December 6, 2016

MAGEREZA YAPATA MSAADA WA VIFAA VYA MICHEZO

Kaimu Kamishna Jenerali wa Magereza nchini, Dkt. Juma Malewa(wa pili kulia) akipokea vifaa vya michezo kutoka kwa Kaimu Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya SAN LAM Life Insurance, Bw. Samuel Mika(wa pili kushoto) ni Kamishna wa Fedha na Utawala wa Jeshi hilo, Kamishna Gaston Sanga(wa kwanza kushoto) ni Afisa Uhusiano wa Kampuni ya SAN LAM, Bw. Rishia Kileo. Vifaa hivyo vitatumiwa na Maafisa na Askari wa Jeshi la Magereza katika Mashindano ya Kijeshi yanayotarajiwa kufanyika Zanzibar mwezi huu Desemba, 2016.
Kaimu Kamishna Jenerali wa Magereza nchini, Dkt. Juma Malewa akitoa neno la shukrani kwenye hafla fupi ya makabidhiano ya vifaa vya michezo vilivyotolewa na Kampuni ya SAN LAM Life Insurance. Hafla hiyo imefanyika leo Desemba 06, 2016 katika Ukumbi wa Makao Makuu ya Jeshi la Magereza, Jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Kamishna wa Fedha na Utawala wa Jeshi hilo, Kamishna wa Magereza Gaston Sanga(kulia) ni Kaimu Mtendaji Mkuu wa Kampuni SAN LAM Life Insurance, Bw. Samuel Mika.
Kaimu Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya SAN LAM Life Insurance, Bw. Samuel Mika akitoa maelezo mafupi kabla ya kukabidhi vifaa vya michezo kwa Jeshi la Magereza leo Desemba 06, 2016 katika Ukumbi wa Makao Makuu ya Jeshi la Magereza, Jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Kamati ya Michezo ya Jeshi la Magereza, SACP. Gideon Nkana akitoa utambulisho mfupi katika hafla ya kukabidhi vifaa vya michezo kwa Jeshi la Magereza leo Desemba 06, 2016 katika Ukumbi wa Makao Makuu ya Jeshi la Magereza, Jijini Dar es Salaam.
Kaimu Kamishna Jenerali wa Magereza Nchini, Dkt. Juma Malewa(katikati walioketi) akiwa katika picha ya pamoja na Maafisa Waandamizi wa Jeshi la Magereza pamoja na Wawakilikilishi wa Kampuni ya SAN LAM Life Insurance(waliosimama). hafla hiyo ya makabidhiano ya vifaa vya michezo imefanyika leo Desemba 06, 2016 katika Ukumbi wa Makao Makuu ya Jeshi la Magereza, Jijini Dar es Salaam.

Friday, December 2, 2016

ZIARA YA RAIS MAGUFULI MAGEREZA MKOA WA DAR ES SALAAM

Amiri Jeshi Mkuu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt John Pombe Joseph Magufuli akiweka saini kitabu cha wageni akiwa na  Kamishna Jenerali wa Magereza John Casmir Minja kabla ya kuongea na Maafisa na askari wa Jeshi la Magereza Mkoa wa Dar es Salaam alipofanya ziara ya kustukiza katika Jiji la Dar es Salaam Novemba 29, 2016.
Kamishna Jenerali Magereza, John Casmir Minja(Kushoto) akiteta jambo na Amiri Jeshi Mkuu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt John Pombe Joseph Magufuli katika Bwalo Kuu la Maafisa Magereza Ukonga kabla ya kuongea na Maafisa na askari wa Jeshi la Magereza Mkoani Dar es Salaam alipofanya ziara ya kustukiza katika Jiji la Dar es Salaam Novemba 29, 2016.
Amiri Jeshi Mkuu Rais Dkt John Pombe Joseph Magufuli akiongea na baadhi ya Maafisa na askari wa Jeshi la Magereza Mkoani Dar es Salaam alipofanya ziara ya kustukiza katika Jiji la Dar es salaam Novemba 29, 2016.
Kamishna Jenerali wa Magereza John Casmir Minja akimkaribisha Amiri Jeshi Mkuu Rais Dkt John Pombe Joseph Magufuli ili aongee  na Maafisa na askari wa Jeshi la Magereza alipofanya ziara ya kustukiza Jijini Dar es salaam Novemba 29, 2016
Amiri Jeshi Mkuu Rais Dkt John Pombe Joseph Magufuli akichukua maelezo kutoka kwa  Maafisa na askari wa Jeshi la Magereza alipofanya ziara ya kustukiza Jijini Dar es Salaam Novemba 29, 2016.
Baadhi ya Maafisa na askari wa Jeshi la Magereza wakimsikiliza Amiri Jeshi Mkuu Rais Dkt. John Pombe Magufuli alipofanya ziara ya kustukiza jijini Dar es salaam  Novemba 29, 2016.
Amiri Jeshi Mkuu Rais Dkt John Pombe Joseph Magufuli akiwa katika picha ya pamoja na Maafisa Waandamizi wa Jeshi la Magereza alipofanya ziara ya kustukiza Jijini Dar es salaam  Novemba 29, 2016.

(Picha zote na Lucas Mboje wa Jeshi la Magereza)