Naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Waziri wa Nishati, Mhe. Dotto Biteko (Mb), ametoa Wito kwa Wahitimu wa Kozi ya Uongozi wa Ngazi ya Juu (GO'S) Jeshi la Magereza, kutumia maarifa waliyopata kuboresha utendaji kazi, kudumisha nidhamu, sambamba na kuleta magaeuzi chanya ndani ya jeshi.
Mhe. Biteko amezungumza hayo katika hafla ya kufunga Kozi namba 27 ya Uongozi wa juu iliyofanyika katika viwanja vya Chuo Cha Taaluma ya Sayansi ya Urekebishaji Tanzania (TCTA) jijini Dar es Salaam, Machi 28, 2025 ambapo aliwapongeza wahitimu kwa hatua waliyoifikia na kuwakumbusha kuwa kupandishwa cheo ni ishara ya kuongezewa majukumu makubwa zaidi.
"Serikali inatarajia kuona mnakuwa chachu ya mabadiliko katika Jeshi la Magereza kwa kufanya kazi kwa bidii, uadilifu, na kuhakikisha haki inatendeka kwa mujibu wa Sheria," alisema Mhe. Biteko.
Naibu Waziri Mkuu, Alisisitiza kuwa Jeshi la Magereza lina jukumu kubwa la kuwahudumia watu waliokosea, lakini lengo kuu ni kuwasaidia kurekebisha tabia zao ili wawe raia wema wanaporejea kwenye jamii. Aliwataka wahitimu kuhakikisha wanazingatia utu, weledi na kuzingatia Sheria, taratibu na kanuni za kazi.
Kwa Upande wake, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Daniel Sillo amesisitiza dhamira ya Serikali ya kuleta mageuzi katika Taasisi za Haki Jinai kama sehemu ya juhudi za kuboresha mifumo ya utoaji haki nchini.
Aliongeza kuwa hatua hiyo inatokana na maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye aliunda Tume Maalum ya Kuboresha Taasisi za Haki Jinai ili kutathmini changamoto zilizopo na kupendekeza njia bora za kuimarisha Sekta hiyo.
Naye, Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza (CGP) Jeremiah Katungu, amesema kuwa, Jeshi kwa kushirikiana na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) lilizindua mpango wa kurasimisha ujuzi wa wafungwa, ambapo jumla ya wafungwa 201 wamepatiwa vyeti rasmi. Lengo la mpango huo ni kuhakikisha ujuzi walioupata Magerezani unatambulika rasmi ili kuwawezesha kupata ajira au kujiajiri mara baada ya kumaliza vifungo vyao.