Banner

Banner

Friday, March 11, 2016

Ziara ya Kamishna Jenerali wa Magereza nchini mkoani Kagera

Kamishna Jenerali wa Magereza John C. Minja( wa pili kushoto) akikagua maeneo mbalimbali ya Gereza Bukoba alipofanya ziara ya kikazi leo Machi 11, 2016 (wa kwanza kushoto) ni Mkuu wa Magereza Mkoa wa Kagera, SACP. Omari Mtiga (wa pili kulia) ni Mkuu wa Gereza Bukoba, ACP. Benizeth Bisibe.
Kamishna Jenerali wa Magereza John C. Minja (wa nne kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na Maofisa Waandamizi wa Jeshi la Magereza Mkoani Kagera mara baada ya kutembelea Gereza la Wilaya ya Bukoba 
Mkuu wa Mkoa wa Kagera Mhe. John Mongella akiongea ofisini kwake na Kamishna Jenerali wa Magereza John C. Minja na ujumbe wake (hawapo pichani)
Mkuu wa Mkoa wa Kagera Mhe. John Mongella akiongea ofisini kwake na Kamishna Jenerali wa Magereza John C. Minja na ujumbe wake kama inavyoonekana katika picha.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba Mhe. Sivangilwa Mwangesi Akisalimiana na Kamishna Jenerali wa Magereza John C. Minja alipomtembelea ofisini kwake

(Picha na Lucas Mboje wa Jeshi la Magereza).


Kamishina Jenerali wa Mageraza nchini John Carmir Minja afanya ziara ya kikazi  Mkoani Kagera yenye lengo la kutembelea na kukagua Magereza ya Mkoa wa Kagera pamoja na kujionea miradi ya uzalishaji inayosimamiwa na Jeshi hilo.

Akiwa Mkoani hapa Kamishna Jenerali Minja alifika ofisini kwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera Mhe. John Mongella na kufanya naye mazungumzo kuhusu utendaji kazi na ufanisi wa Jeshi la Magereza Mkoani hapa katika kuimarisha ulinzi na usalama.

Aidha katika mazungumzo hayo walizungumzia  changamoto ya  msongamano wa Mahabusu katika Gereza la Wilaya ya Muleba ambalo hivi sasa linatumika kuhifadhi Mahabusu wa Wilaya ya Muleba na Wilaya ya Chato Mkoani Geita ambayo haina Gereza la Wilaya.

Kamishna Jenerali wa Mageraza nchini John Carmir Minja pia alitembelea Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba na kufanya mazungumzo na Jaji Mfawidhi wa Mahakama hiyo Mhe. Sivangilwa Mwangesi juu ya namna ya kuongeza kasi ya usikilizwaji wa kesi mbalimbali za watuhumiwa ili kuondoa msongamano Magerezani.

Vilevile Kamishna Jenerali Minja alitembelea Gereza la Wilaya la Bukoba na kuongea na wafungwa na Mahabusu wa Gereza  hilo pia na kukagua mradi wa ujenzi wa jengo la zahanati ambalo lipo katika hatua za mwisho kukamilishwa ili liweze kutoa huduma za afya kwa wafungwa na watumishi wa Jeshi hilo pamoja na wananchi wanaoishi jirani na zahanati hiyo.

Kamishna Jenerali Minja yupo Mkoani Kagera kwa siku 7 kuanzia tarehe 10 hadi 16 Machi, 2016 ambapo lengo la ziara hiyo ni kutembelea na kukagua Magereza ya Mkoa wa Kagera pamoja na kujionea miradi ya uzalishaji inayosimamiwa na jeshi hilo.


Thursday, March 10, 2016

Kamishna Jenerali wa Magereza atembelea gereza Biharamulo pamoja na eneo linakojengwa gereza la wiliya ya Chato mkoani Geita

Kamishna Jenerali wa Magereza - CGP John Casmir Minja akisalimiana na Mkuu wa Gereza Kuu Butimba, Mwanza Kamishna Msaidizi wa Magereza, Jaili Mwamugunda alipowasili katika Uwanja wa Ndege wa Mwanza kabla ya kuanza ziara yake ya kikazi Mkoani Kagera ambapo leo Machi 10, 2016 ametembelea eneo kunakojengwa Gereza la Wilaya ya Chato lililopo Mkoani Geita pamoja na Gereza la Wilaya ya Biharamulo(wengine) ni Maofisa wa Jeshi la Magereza kutoka Ofisi ya Magereza Mkoani Mwanza.
Kamishna Jenerali wa Magereza, John Casmir Minja akifurahia jambo pamoja na Luteni Jenerali Mstaafu Samuel Ndomba walipokutana katika Kivuko cha Busisi kabla ya kuendelea na safari kuekelea Mkoani Kagera(kulia) ni Mkuu wa Magereza Mkoani Mwanza, Goleha Masunzu.
Mkuu wa Wilaya ya Chato, Mhe. Shaban Ntarambe(kushoto) akiwa na Kamati yake ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya wakielekea eneo linakojengwa Gereza la Wilaya ya Chato mara baada ya Kamishna Jenerali wa Magereza kuwasili Wilayani Chato kabla ya kuelekea Mkoani Kagera.
Mkuu wa Magereza Mkoani Kagera, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Magereza, Omar Mtiga(wa pili kushoto) akimuonesha Kamishna Jenerali wa Magereza, John Casmir Minja(wa tatu kulia) nyumba mbili za Askari wa Jeshi la Magereza ambazo tayari zimekamilika katika eneo linakojengwa Gereza la Wilaya ya Biharamulo(wa pili kulia) ni Mkuu wa Wilaya ya Chato, Mhe. Shaaban Ntarambe.
Kamishna Jenerali wa Magereza, John Casmir Minja(suti nyeusi) akiwa na Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Chato wakiaangalia moja ya Bweni la kulala Wafungwa/Mahabusu ambalo tayari limekamilika katika eneo linakojengwa Gereza la Wilaya ya Chato Mkoani Geita. Kukamilika kwa Gereza hilo kutasaidia kutatua tatizo la Msongamano wa Wafungwa na Mahabusu katika Magereza ya Biharamulo na Gereza Muleba.
Kamishna Jenerali wa Magereza John Casmir Minja akisaini katika kitabu cha Wageni alipotembelea Gereza la Wilaya ya Biharamulo katika ziara yake ya kikazi leo Machi 10, 2016.
Mkuu wa Gereza la Biharamulo, Mrakibu Mwandamizi wa Magereza, Gidion Kakulu akimuonesha Kamishna Jenerali wa Magereza maeneo mbalimbali ya Gereza hilo katika ziara yake ya Kikazi leo Machi 10, 2016. Wengine ni Maafisa Waandamizi wa Jeshi hilo ambao wameambatana na Kamishna Jenerali wa Magereza katika ziara yake ya kikazi.




Wednesday, March 9, 2016

Tangazo la kuitwa chuoni

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI

(Jeshi la Magereza)
TANGAZO LA KUITWA CHUONI
Kamishna Jenerali wa Magereza Tanzania Bara anawatangazia wafuatao kuwa wamechaguliwa kujiunga na Jeshi la Magereza baada ya Usaili kufanyika katika kambi mbalimbali za JKT.  Usaili huu ulihusu vijana waliohitimu Shahada ya Kwanza, Stashahada, Astashahada, Kidato cha Sita na Kidato cha Nne.

Wahusika wote wanatakiwa kuripoti katika Ofisi za Wakuu wa Magereza Mikoa mara wapatapo taarifa hii tayari kwa safari ya kwenda Chuo cha Mafunzo ya Awali kilichopo Kiwira Tukuyu Mkoani Mbeya.

Mafunzo yanategemewa kuanza tarehe 12 Machi, 2016 hivyo mwisho wa kuripoti chuoni ni tarehe 14 Machi, 2016.  Yeyote atakayeshindwa kuripoti kwa tarehe iliyotamkwa kwenye tangazo hili hatapokelewa.

Wahusika wanatakiwa kuzingatia mambo yafuatayo:-

1.          Walete vyeti halisi vya masomo na vya kuzaliwa, vikiwa na pamoja na nakala 5 za kila cheti.

2.          Picha (Passport size) za rangi 5 za hivi karibuni.

3.         Chandarua cheupe cha duara ft 31/2, shuka nyeupe mbili, mto wenye foronya nyeupe zisizo na maua/maandishi.

4.           Fedha taslimu Tshs.90,000/=.

5.           Kalamu za wino,  za risasi na madaftari ya kutosha.

6.           Cheti cha afya kutoka kwa hospitali ya Serikali.

7.           Nguo za kiraia za kutosha sweta, raba (Brown au nyeusi) na soksi

8.           Kwa wale wenye kadi za Bima waje nazo na

9.           Kila mwanafunzi atajitegemea kwa nauli ya kwenda.

Tangazo hili linapatikana kwenye mbao za matangazo zilizopo Ofisi za Magereza, tovuti ya Magereza kwa anwani ya www.magereza.go.tz sanjari na blog ya Magereza kwa anwani ya www.magereza.blogspot.com

Imetolewa na Kamishna Jenerali wa Magereza.

SIGNED
Dr. J. A. Malewa  -  CP
Kny:  KAMISHNA JENERALI WA MAGEREZA