Banner

Banner

Saturday, December 31, 2016

KAIMU KAMISHNA JENERALI WA MAGEREZA DKT. JUMA MALEWA AWAASA MAOFISA MAGEREZA KUTIMIZA WAJIBU WAO KWA UFANISI

 
Na Lucas Mboje, Dar es Saam
KAIMU Kamishna Jenerali wa Magereza nchini, Dkt. Juma Malewa(pichani) amewaasa Maafisa na Askari wa Jeshi la Magereza  nchini kuzingatia  kuwa utendaji wao wa kazi za kila siku uende sambamba na kasi ya Serikali ya Awamu ya tano ili kuleta ufanisi unaotarajiwa.
 
KAIMU Kamishna Jenerali, Dkt. Malewa ameyasema hayo jana wakati wa Baraza la Kufunga Mwaka 2016 na kuukaribisha Mwaka 2017 lililowahusisha baadhi ya Maafisa na Askari kutoka Ofisi ya Makao Makuu ya Jeshi la Magereza, Chuo cha Taaluma ya Urekebishaji Ukonga, Kikosi Maalum cha Kutuliza Ghasia Magerezani pamoja na Magereza ya Mkoa wa D'Salaam.

Aidha, amewataka Maofisa na Askari wa Jeshi hilo kudumisha nidhamu wanapokuwa wakitekeleza majukumu yao ya kazi  ikiwemo kutekeleza mara moja Amri mbalimbali zinazotolewa na Viongozi wao wa Jeshi.
 
"Kila mmoja wenu atimize wajibu wake katika eneo lake la kazi kwa bidii, ari na moyo wa kujituma ili kuliwezesha Jeshi letu kupata ufanisi unaotarajiwa". Alisisitiza Kaimu Jenerali Dkt. Malewa.
 
Wakati huo huo Kaimu Kamishna Jenerali wa Magereza nchini, Dkt. Juma Malewa  pia ametumia fursa hiyo kuelezea baadhi ya mafanikio mbalimbali yaliyopatikana kwa Mwaka uliopita 2016 ambapo Jeshi la Magereza limeweza kupata jumla ya leseni 102 za uchimbaji wa madini ya ujenzi kama vile chokaa, mawe, kokoto, mchanga na Murram katika maeneo mbalimbali ya magereza. Pia katika mwaka 2016 Jeshi limeweza kujenga nyumba 129 kwa njia ya kujitolea ambapo nyumba 231 zipo katika hatua mbalimbali ya ukamilishaji.
 
Aidha, Ujenzi wa nyumba 320 za makazi ya askari katika eneo la Gereza Ukonga maandalizi ya ujenzi yanaendelea na ujenzi wa nyumba hizo ni kufuatia ziara ya Rais Magufuli  Novemba 29 mwaka huu  ambapo alipokea taarifa ya uhaba wa nyumba za kuishi askari wa jeshi hilo na akaagiza Jeshi la Magereza lipatiwe Tsh. bilioni 10 haraka ili kupunguza tatizo hilo.
 
Shirika la Magereza na Mfuko wa hifadhi ya Jamii wa PPF wameingia Makubaliano ya Mkataba wa ubia katika mradi wa ujenzi wa Kiwanda kipya cha kusakata ngozi pamoja na uwekezaji wa mashine za kisasa za kutengnezea bidhaa za ngozi katika Kiwanda cha Viatu cha Gereza Karanga, Moshi.
Chuo cha Maafisa Magereza Ukonga kimepata Ithibati na hivyo kuwa na hadhi ya kuwa Chuo cha Taaluma ya Urekebishaji na mapema mwakani kinatarajia kudahili wanafunzi 30 katika fani ya Taaluma ya Urekebishaji ngazi ya cheti. 
 
Pamoja na Mafanikio hayo, Kaimu Kamishna Jenerali Dkt. Malewa ameelezea changamoto mbalimbali zinazolikabili Jeshi hilo ikiwemo ufinyu wa bajeti, makazi duni ya maofisa na askari, uhaba wa vitendea kazi, ukosefu wa pembejeo pamoja na madeni ya wabuni na watumishi wa jeshi hilo.
 
Kuhusu maeneo yatakayopewa kipaumbele kwa Mwaka mpya 2017 ni kuwa Jeshi la Magereza litaendeleza jitihada za kuimarisha na kuongeza uzalishaji kwenye miradi ya uzalishaji wa mazao ya Kilimo na mifugo lengo ikiwa ni kujitosheleza kwenye chakula cha wafungwa, kuhakikisha wafungwa wanafanya kazi za uzalishaji mali kwa kiwango chenye tija badala ya kukaa tu magerezani pia kuendeleza mikakati ya kupunguza msongamano magerezani.
 
Baraza la kufunga Mwaka na kuukaribisha Mwaka unaofuata ni utamaduni wa siku nyingi ambao unaenziwa na Viongozi Wakuu wa Jeshi la Magereza ambapo Baraza la aina hii hufanyika kila Mwaka ili Kamishna Jenerali wa Magereza nchini aweze kuongea na Watumishi wote wa Jeshi la Magereza nchini kupitia Baraza hilo lengo ikiwa ni kufanya tathmini ya yale yaliyojiri katika Jeshi kwa kipindi cha Mwaka unaisha kwa kuzungumzia mafanikio na changamoto zilizojitokeza na  kutazama matarajio ya Mwaka mpya.

Friday, December 30, 2016

KAIMU KAMISHNA JENERALI WA MAGEREZA AHUTUBIA BARAZA LA KUFUNGA MWAKA 2016 NA KUUKARIBISHA MWAKA MPYA 2017 JIJINI DAR

Kaimu Kamishna Jenerali wa Magereza, Dkt. Juma Malewa akitoa hotuba yake fupi ya kufunga mwaka 2016 na kuukaribisha mwaka mpya 2017 kwenye Baraza la Maafisa na Askari kutoka vituo mbalimbali vya Magereza Mkoani Dar es Salam Desemba 30, 2016 katika Bwalo Kuu la Maafisa Magereza Ukonga.
Naibu Kamishna wa Magereza, Edith Mallya akimkaribisha Kaimu Kamishna Jenerali wa Magereza, Dkt. Juma Malewa(katikati aliyeketi) kabla ya kuongea na Maafisa na Askari wa Jeshi la Magereza Mkoa wa Dar es Salaam katika Baraza Maalum la kufunga mwaka 2016 na kuukaribisha mwaka mpya 2017(kushoto) ni Mkuu wa Magereza Mkoa wa D ar es Salaam, SACP. Augustine Mboje. Baraza hilo limefanyika Bwalo Kuu la Maafisa Magereza Ukonga, Dar es Salaam Desemba 30, 2016.
Kaimu Kamishna Jenerali wa Magereza, Dkt. Juma Malewa akijibu kero mbalimbali zilizoulizwa na Maafisa na Askari wa Jeshi la Magereza Mkoa wa Dar es Salaam(hawapo pichani) katika Baraza Maalum la kufunga mwaka 2016 na kuukaribisha mwaka mpya 2017
Askari wa Jeshi la Magereza kutoka vituo mbalimbali vya Magereza ya Mkoa wa Dar es Salaam wakisikiliza hotuba ya Kaimu Kamishna Jenerali wa Magereza, Dkt. Juma Malewa(hayupo pichani) katika Baraza Maalum la kufunga mwaka 2016 na kuukaribisha mwaka mpya 2017.
Afisa Utumishi wa Jeshi la Magereza, Mrakibu wa Magereza Elmas Mgimwa akitolea ufafanuzi kuhusiana na masuala ya kiutumishi yaliyoulizwa na Maafisa na Askari wa Jeshi la Magereza Mkoa wa Dar es Salaam(hawapo pichani) katika Baraza hilo.
Baadhi ya Maafisa Waandamizi wa Jeshi la Magereza wakifuatilia kwa umakini mkubwa hotuba ya Kaimu Kamishna Jenerali wa Magereza, Dkt. Juma Malewa kwenye Baraza hilo. 

(Picha zote na Lucas Mboje wa Jeshi la Magereza).

Saturday, December 24, 2016

WAZIRI MKUU AKAGUA ENEO LA UJENZI WA MAKAZI YA ASKARI MAGEREZA JIJINI DAR, AMPONGEZA KAIMU KAMISHNA JENERALI WA MAGEREZA NAMNA ALIVYOJIPANGA KUSIMAMIA UJENZI

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa(Mb)  akisalimiana na Kaimu Kamishna Jenerali wa Magereza, Dkt. Juma Malewa kabla ya kuongea na Maafisa na askari wa Jeshi la Magereza Mkoa wa Dar es Salaam alipofanya ziara ya kikazi ya kukagua maandalizi ya ujenzi wa nyumba 320 za makazi ya Maafisa na askari wa Jeshi hilo katika eneo la Gereza Kuu Ukonga, Jiji la Dar es Salaam Disemba 24, 2016(wa kwanza kushoto) ni Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni (Mb).
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa(Mb) akikagua Gwaride Maalum la heshima lililoandaliwa na Maofisa na askari wa Jeshi la Magereza kabla ya kukagua eneo la ujenzi wa nyumba 320 za makazi ya Maafisa na askari wa Jeshi hilo katika eneo la Gereza Kuu Ukonga, Jiji la Dar es Salaam Disemba 24, 2016.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa(Mb) akipokea Salaam ya heshima kutoka Gwaride Maalum la heshima lililoandaliwa na Maofisa na askari wa Jeshi la Magereza kabla ya kukagua eneo la ujenzi wa nyumba 320 za makazi ya Maafisa na askari wa Jeshi hilo katika eneo la Gereza Kuu Ukonga, Jiji la Dar es Salaam Disemba 24, 2016.
Kaimu Kamishna Jenerali wa Magereza, Dkt. Juma Malewa akitoa maelezo mafupi kwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim(hayupo pichani) namna Jeshi hilo lilivyojipanga katika kuhakikisha kuwa ujenzi wa nyumba hizo ambazo zinatarajiwa kujengwa katika eneo la Gereza Kuu Ukonga, Jijini Dar es Salaam unakamilika ipasavyo.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa akitoa hotuba fupi kwa  Maafisa na askari wa Jeshi la Magereza  alipofanya ziara ya kikazi ya kukagua maandalizi ya ujenzi wa nyumba 320 za makazi ya askari katika eneo la Gereza Kuu Ukonga, Jiji la Dar es Salaam Disemba 24, 2016.
Baadhi ya Maafisa na askari wa Jeshi la Magereza wakimsikiliza Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa alipofanya ziara ya kikazi ya kukagua maandalizi ya ujenzi wa nyumba 320 za makazi ya askari katika eneo la Gereza Kuu Ukonga, Jiji la Dar es Salaam Disemba 24, 2016.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa akiteta jambo na Naibu Waziri wa Mambo ya ndani ya nchi, Mhandisi Hamad Masauni(kulia).
Meneja Ujenzi wa Mamlaka ya Majengo nchini – TBA, Arch. Humphrey Killo akitoa maelezo ya kitalaam kwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa alipofanya ziara ya kikazi ya kukagua maandalizi ya ujenzi wa nyumba 320 za makazi ya askari katika eneo la Gereza Kuu Ukonga, Jiji la Dar es Salaam Disemba 24, 2016.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa akikagua eneo la ujenzi wa nyumba hizo za makazi ya askari kama inavyoonekana katika picha.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa akiwa katika picha ya pamoja na Maafisa Waandamizi wa Jeshi la Magereza alipofanya ziara ya kikazi ya kukagua maandalizi ya ujenzi wa nyumba 320 za makazi ya askari katika eneo la Gereza Kuu Ukonga, Jiji la Dar es Salaam

(Picha zote na Lucas Mboje wa Jeshi la Magereza).

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametembelea gereza la Ukonga jijini Dar es Salaam na kukagua eneo la ujenzi wa makazi ya askari wa Magereza unaotarajiwa kuanza baada ya wiki tatu zijazo.

Akizungumza na askari wa magereza kabla ya kufanya ukaguzi huo leo (Jumamosi, Desemba 24, 2016) Waziri Mkuu amesema ziara aliyoifanya leo, ni ufuatiliaji wa maagizo ya Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli aliyoitoa wakati alipoenda kukagua gereza hilo.

Novemba 29, mwaka huu, Rais Magufuli alifanya ziara kwenye gereza hilo na kupokea taarifa ya uhaba wa nyumba za kuishi askari wa jeshi hilo zipatazo 9,500 na akaagiza zitafutwe sh. bilioni 10 haraka ili kupunguza tatizo hilo.

Akizungumzia kuhusu ujenzi huo, Waziri Mkuu amesema amefarijika kukuta Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) wako eneo la kazi na wameanza kusafisha eneo hilo.

“Nimefarijika kukuta TBA wako kazini na nimeelezwa hatua inayofuata ni upimaji wa sampuli za udongo kabla hawajaanza kujenga msingi. Nawapongeza TBA kwa kazi nzuri wanazofanya za ujenzi wa nyumba zenye viwango na kwa haraka kama tulivyoona kule Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na nyumba za Magomeni Kota,” amesema.

Waziri Mkuu amesema Serikali inatambua mchango uliofanywa na Serikali ya awamu ya nne katika suala la makazi ya askari kama vile wa Jeshi la Wananchi (JWTZ) na Jeshi la Polisi. “Nia ya Serikali ni kuhakikisha makamanda wote wanapata nyumba nzuri ili waendelee kufanya kazi zao kwa weledi mkubwa wakiwa na uhakika familia zao zimetulia kwenye makazi bora”.

Amesema katika ziara alizozifanya kwenye mikoa mbalimbali, alitembelea magereza ya Isanga, Msalato (Dodoma), Lindi, Singida na Keko (Dar es Salaam) alikuta nyumba za askari hazina viwango na kama zipo zimechakaa sana.

Mapema, akitoa taarifa kuhusu ujenzi wa nyumba hizo, Kaimu Kamishna Jenerali wa Magereza, Juma Malewa alisema wanamshukuru Mheshimiwa Rais kwa kuwapatia fedha za ujenzi wa makazi ya askari na kwamba jeshi hilo litafanya kazi zote zisizo za kitaalamu ili kuokoa fedha za Serikali na badala ya kulipwa watu binafsi, fedha hizo zitatumika kuongeza nyumba zaidi.

“Tumekubaliana na TBA kazi zote zisizohitaji utalaamu kama kufyatua matofali, kubeba mizigo au kufyeka zitafanywa na askari wetu pamoja na wafungwa ili tuokoe gharama zote hizo na badala ya kulipa watu binafsi, fedha hizo zitumike kujenga nyumba nyingine 80,” alisema huku akishangiliwa.

Alisema wamejipanga kufanya kazi hizo kwa saa 24 kila siku ili kuokoa muda ambao TBA walikuwa wameuweka wa kukamilisha ujenzi ndani ya miezi minane.

Alisema wako tayari kuanzisha kambi za ujenzi kwa kutumia wafungwa na askari ili wafanye kazi zisizohitaji utaalamu na fedha zitakazopatikana, badala ya kuwalipa watu binafsi zitumike kujenga nyumba zaidi za askari.

Naye mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa TBA, Bw. Baltazar Kimangano alisema wanataraji kuanza ujenzi ndani ya wiki tatu baada ya kupokea matokeo ya uchunguzi wa sampuli za udongo kutoka taasisi ya BICO ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Alisema wanataraji kujenga majengo (block) manne ya ghorofa sita kila moja ambayo kwa ujumla yatakuwa na nyumba 240 zenye ukubwa wa vyumba viwili vya kulala. Pia watajenga majengo (block) mengine mawili ya ghorofa sita kila moja ambayo yatakuwa na nyumba 80 zenye ukubwa wa vyumba vitatu vya kulala.





IMETOLEWA NA:

OFISI YA WAZIRI MKUU,


2 MTAA WA MAGOGONI,

L. P. 3021,

11410 – DAR ES SALAAM

JUMAMOSI, DESEMBA 24, 2016