Banner

Banner

Friday, July 3, 2015

Jeshi la Magereza laibuka mshindi wa kwanza katika utengenezaji wa samani maonesho ya 39 ya biashara kimataifa,"Sabasaba", mwaka 2015

Muonekano wa Samani za Ofisi ambazo hutengenezwa kwa Ustadi mkubwa katika Viwanda mbalimbali vinavyoendeshwa na Jeshi la Magereza zikiwa tayari zimekamilika kwa matumizi ya kiofsi kama inavyoonekana katika picha.


Na; Lucas Mboje wa Jeshi la Magereza

Jeshi la Magereza limeibuka Mshindi wa kwanza kwa upande wa Utengenezaji bidhaa za Samani kwenye Maonesho ya 39 ya Biashara ya Kimataifa yanayoendelea Jijini, Dar es Salaam Maarufu "SABASABA" kwa Mwaka huu 2015.

Akizungumzia ushindi huo Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza Nchini, John Casmir Minja amesema kuwa anajivunia ushindi huo kwani kulikuwa na ushindani mkubwa wa Makampuni mengi yanayoshiriki katika Maonesho haya ya Kibiashara yanayoendelea.

"Nachukua fursa hii kwa dhati kuwapongeza sana Maafisa wote washiriki katika Banda letu la Jeshi la Maonesho kwa kazi nzuri iliyowezesha ushindi huo wa kwanza kwa upande wa Utengenezaji wa Samani Bora". Alisema Jenerali Minja.

Aidha, Jenerali Minja amewaomba Wananchi kutoka maeneo mbalimbali ndani na nje ya Jiji la Dar es Salaam watembelee Banda la Jeshi la Magereza ili waweze kujipatia bidhaa bora pia kuona na kujifunza namna bora ya utengenezaji wa bidhaa mbalimbali.

Kwa upande wao Maofisa wa Jeshi la Magereza wanaoshiriki katika Maonesho haya wameushukru Uongozi wa Jeshi la Magereza kwa kuwawezesha kushiriki kikamilifu hususani kufanikisha maandalizi yote muhimu ya kushiriki katika Maonesho haya ya Biashara yanayoendelea Jijini Dar es Salaam.

Jeshi la Magereza Tanzania limepiga hatua kubwa ya Maboresho juu ya utengenezaji wa bidhaa bora za Samani hivyo kupelekea kuibuka mara kwa mara Mshindi wa kwanza katika Maonesho mbalimbali ya Kibiashara hapa nchini.