Banner

Banner

Monday, April 11, 2016

Jeshi la Magereza na Suma-JKT wakabidhiwa jukumu la kutengeneza madawati yenye thamani ya bilioni 6, jijini Dar

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli akionesha mfano wa hundi aliyokabidhiwa na Ofisi ya Bunge leo Ikulu, Jijini Dar es Salaam ambapo fedha hizo ameelekeza zitumike kutengenezea madawati ya shule hapa nchini(kulia)ni Naibu Spika wa Bunge la Tanzania, Dkt. Tulia Ackson.

Muonekano wa Madawati ambayo yanatarajiwa kutengenezwa na yaliyoidhinishwa na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kama yanavyoonekana katika picha.
Kamishna Jenerali wa Magereza nchini, CGP John Casmir Minja(kushoto) akiwa na Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa, Bregedia Jenerali, Michael Isamuhyo(katikati) wakifuatilia hotuba ya Rais Magufuli(kulia) ni Mtendaji Mkuu wa SUMA - JKT, Bregedia Jenerali C.Yateri.
Kamishna Jenerali wa Magereza nchini, CGP John Casmir Minja akiongea na Wandishi wa Habari kuhusu namna Jeshi hilo lilivyojipanga kutekeleza jukumu lililopewa.
Kamishna Jenerali wa Magereza nchini, CGP John Casmir Minja akisalimiana na Katibu wa Bunge, Dkt. Thomas Kashilila wakipokutana katika Viwanja vya Ikulu, Jijini Da es Salaam(Picha zote na Lucas Mboje wa Jeshi la Magereza).


Na; Lucas Mboje wa Jeshi la Magereza,
JESHI LA MAGEREZA nchini pamoja na Jeshi la Kujenga Taifa limepewa jukumu la kutengeneza madawati yenye thamani ya Bilioni 6 ambayo yatasambazwa katika Mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar.

Jukumu hilo kwa Vyombo vya Ulinzi na Usalama limetolewa leo Aprili 11, 2016 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, katika hafla fupi ya makabidhiziano ya mfano wa hundi ya Bilioni 6 za pesa ya kitanzania kutoka Sekretarieti ya Bunge ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania pesa ambazo zimepatikana kufuatia kubana matumizi ya uendeshaji wa Ofisi hiyo.

Rais Magufuli amesema kuwa Ofisi ya Bunge pamoja na Watendaji wake wameonesha moyo wa kizalendo kwa Taifa lao kwani wametekeleza kwa vitendo maelekezo ya kubana matumizi ya fedha za Serikali hivyo kuokoa kiasi hicho cha Bilioni 6 ambazo wamezikabidhi ili zitumike katika kutatua changamoto ya uhaba wa Madawati katika shule nyingi hapa nchini.

“Nikupongeze sana Dkt. Thomas Kashilila, Watendaji wote wa Ofisi ya Bunge kwa moyo wenu wa upendo, uzalendo mkaamua kiasi hiki cha fedha Bilioni 6 zikafanye kazi ya maendeleo kwani mngeweza kuzitumia fedha hizi katika matumizi mengine hata Mhe. Spika asingejua". Alisema Rais Magufuli.

Aidha, Rais Magufuli amewataka Makatibu Wakuu wote wa Wizara pamoja na Watendaji Wakuu wote wa Taasisi za Umma/Serikali kuiga mfano huo wa kizalendo aliouonesha Katibu wa Bunge, 
Dkt. Thomas Kashilila kwani huo ndio mwelekeo anaoutaka katika Serikali yake ya Awamu ya Tano.
Awali akiongea kabla ya Makabidhiano ya hundi hiyo Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Tulia Ackson amesema kuwa kiasi hicho cha fedha kimepatikana kufuatia kubana matumizi katika maeneo mbalimbali ikiwemo kupunguza safari za nje, gharama za machapisho mbalimbali, gharama za viburudisho na chakula, matibabu kwa wabunge, mafuta na uendeshaji wa mitambo nk.

Akizungumzia utekelezaji wa jukumu la utengenezaji wa madawati hayo Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza Nchini, John Casmir Minja amesema kuwa Jeshi la Magereza lipo tayari kutekeleza agizo la Rais  na amejipanga kutumia nguvu kazi ya Wafungwa waliopo magerezani pamoja na Maafisa na Askari wa Jeshi hilo ili kukamilisha kazi hiyo kwa wakati kama ilivyokusudiwa.

"Mhe. Rais ametoa maelekezo ya kwenda kufanya kazi hiyo kama operesheni maalum hivyo sisi kwa upande wa Jeshi letu tupo tayari kuifanya kazi hiyo kama ilivyoelekezwa kwa kuzingatia maelekezo ya Mhe. Rais". Alisema Jenerali Minja.
Jeshi la Magereza Tanzania limepiga hatua kubwa ya Maboresho juu ya utengenezaji wa bidhaa bora za Samani hivyo kupelekea kuibuka mara kwa mara Mshindi wa kwanza katika Maonesho mbalimbali ya Kibiashara hapa nchini.