WAZIRI MKUU MAJALIWA: KAMILISHENI UJENZI WA MAGEREZA YA WILAYA MPYA
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameuagiza uongozi wa Jeshi la Magereza nchini ukamilishe mkakati wa ujenzi wa magereza za wilaya kwa wilaya zisizokuwa na magereza.
Ametoa agizo hilo leo (Jumatatu, Juni 3, 2019) wakati akifungua Gereza la wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi. Uzinduzi huo umefanyika kwenye viwanja vya gereza hilo.
Amesema uwepo wa magereza katika wilaya zote nchini utasaidia kumaliza tatizo la msongamano wa wafungwa na mahabusu kwenye magereza ya jirani.
“Kutokuwepo kwa magereza ya wilaya kunasababisha msongamano wa wafungwa na mahabusu katika magereza ya jirani, pamoja na kuchelewesha upatikanaji wa haki.” Amesema Majaliwa.
Majaliwa amesema kwamba ufunguzi wa gereza la Ruangwa utatatua tatizo la msongamano wa wafungwa na mahabusu katika Gereza la wilaya ya Nachingwea
Awali wakazi wa wilaya hiyo waliokabiliwa na tuhuma mbalimbali au waliohukumiwa vifungo walikuwa wakipelekwa katika Gereza la wilaya ya Nachingwea.
Amesema kitendo cha kupelekwa Nachingwea kilikuwa kikiwanyima wafungwa na mahabusu fursa ya kuonana na ndugu au mawakili wao kutokana na umbali uliokuwepo.
“Mbali na ndugu na jamaa kushindwa kwenda kuwaona ndugu zao pia Jeshi la Polisi lilikuwa likilaumiwa kuwa linawachelewesha mahubusu kuja kusikiliza mashauri yao.”
Waziri Mkuu amesema uwepo wa gereza hilo katika wilaya ya Ruangwa umeipunguzia Serikali gharama za kuwasafirisha mahabusu na wafungwa kwenda Nachingwea.
Awali, Waziri waMambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola amesema Gereza la Wilaya ya Ruangwa ni nyenzo muhimu katika kuimarisha ulinzi na usalama wa wilaya hiyo.
Amesema gereza hilo ni chachu ya kuimarika kwa uchumi wa wilaya hiyo kwa kupitia sekta ya kilimo kwani kutakuwa na kambi za kilimo, hivyo wananchi nao watajifunza.
“Wananchi msilione gereza hili kama adui kwenu, halijaja kuwafunga bali lipo kwa ajili ya kuimarisha amani, ulinzi na usalama wa wilaya yetu pamoja na kutoa elimu mbalimbali.”
Kwa upande wake, Kamishna Jenerali wa Magereza Phaustine Kasike amesema ujenzi huo umefanywa na kikosi cha ujenzi cha Magereza kwa kutumia nguvukazi ya wafungwa.
Amesema awamu ya kwanza ya ujenzi wa gereza hilo imekamilika na imegharimu sh. bilioni 1.5 hivyo umekamilisha uwepo wa magereza katika wilaya zote za mkoa wa Lindi.
Kamishna huyo amesema ujenzi huo ungefanywa na mkandarasi wa nje ungegharimu sh. bilioni 2.226, hivyo kwa kutumia kikosi cha Magereza wameokoa sh. milioni 635.675.
Amesema kwa sasa gereza hilo lina uwezo wa kuwahifadhi wahalifu 250 hadi 280 na likikamilika itakuwa na uwezo wa kuwahifadhi wahalifu 500.
Kamishna Kasike amesema gereza hilo lina ardhi yenye ukubwa wa ekari 80, ambapo ekari saba zitatumika kwa ajili ya majengo ya gereza, maegezo ya magari na karakana.
“Ekari 56 zitatumika kwa ajili ya ujenzi wa nyumba 100 za makazi, ekari sita ujenzi wa majengo ya huduma kama zahanati na ekari nane zitatumika katika kilimo cha bustani.”
Baadhi ya wananchi waliohudhuria ufunguzi huo wameishukuru Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli kwa kuboresha huduma za jamii.
Mmoja wa wananchi hao Zena Selemani amesema kabla ya ujenzi wa gereza hilo walikuwa wanashindwa kuwatembelea ndugu zao walofungwa katika gereza la Nachingwea.