Na ASP. Lucas Mboje, Dar es Salaam
JUMLA ya Wafungwa
5,533 katika magereza mbalimbali nchini walionufaika na msamaha wa Rais wakati
wa maadhimisho ya miaka 58 ya Uhuru
wameachiliwa huru magerezani.
Akizungumza
na wanahabari leo jijini Dar es Salaam, Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza,
Phaustine Kasike amesema kuwa utekelezaji wa zoezi la kuwaachiliwa huru
wafungwa wote walionufaika na msamaha wa Rais umekamilika nchi nzima.
“Ni
matarajio yangu kuwa wafungwa walioachiliwa wamejutia makosa yao na wataacha
kutenda uhalifu hivyo kujihusisha na shughuli halali kwa maendeleo yao, familia
zao, jamii na taifa kwa ujumla”, amesisitiza Jenerali Kasike.
Aidha,
Kamishna Jenerali Kasike ameelezea manufaa mbalimbali ya msamaha huo; mosi
kupungua kwa msongamano magerezani, pili, wanufaika wa msamaha kujumuika na
familia zao, tatu, kichocheo cha urekebishaji magerezani kwani msamaha huo
utasaidia kuimarika kwa nidhamu na kurejesha matumaini kwa wanaobakia
magerezani pamoja na wanufaika wa wamsamaha huo kupata fursa ya kujishughulisha
na shughuli za maendeleo uraiani.
“Zipo
changamoto zilizojitokeza katika utekelezaji wa zoezi hili ambapo baadhi ya wafungwa
walionesha kuwa hawako tayari kuungana na jamii zao pamoja na waliosamehewa
kurejea kutenda makosa mara baada ya kuachiwa huru. Hata hivyo nitoe wito kwa
jamii nchini kuwapokea wafungwa hao na kuacha kuwanyanyapaa”, amesema Jenerali
Kasike.
Wakati
huo huo, Kamishna Jenerali Kasike amemshukru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Dkt. John Pombe
Magufuli kwa kutoa msamaha huo ambao ni wa kihistoria hapa nchini. Pia
amewapongeza wanahabari wote nchini kwa namna walivyoshiriki kutoa habari za
zoezi la msamaha huo katika ngazi ya Mkoa na wilaya.
Kwa
mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 45(1) (d) imempa
mamlaka Rais kutoa msamaha kwa wafungwa waliopo magerezani. Kwa kutumia Ibara
hiyo Rais Dkt. John Pombe Magufuli alitoa msamaha kwa wafungwa wakati wa
maadhimisho ya miaka 58 ya Uhuru ambapo kilele chake kilifanyika Mkoani Mwanza
Desemba 9, 2019.