Banner

Banner

Friday, June 8, 2018

KAMISHNA JENERALI WA MAGEREZA AWAVISHA VYEO MAOFISA WAANDAMIZI TISA WA JESHI LA MAGEREZA JIJINI DAR

Jenerali wa Magereza, Dkt. Juma Malewa(kulia) akimvalisha cheo akimvalisha cheo Naibu Kamishna wa Magereza, Tusekile Mwaisabila kuwa Kamishina wa Magereza katika hafla fupi iliyofanyika kwenye viwanja wa Chuo cha Taaluma ya Urekebishaji, Ukonga jijini Dar es salaam Juni  8, 2018.
Kamishna Jenerali wa Magereza, Dkt. Juma Malewa(kulia) akimvalisha cheo Mkuu wa Magereza Mkoani Tanga, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Magereza, John Masunga kuwa  Naibu wa Magereza katika hafla fupi iliyofanyika kwenye uwanja wa Chuo cha Taaluma ya Urekebishaji, Ukonga jijini Dar es salaam Juni  8, 2018.
Makamishina na Manaibu Kamishna wa Magereza wakisoma Tamko la Ahadi ya Uadilifu kwa Viongozi wa Umma baada ya kuvalishwa vyeo na Kamishna Jenerali wa Magereza, Dkt. Juma Malewa katika hafla fupi  iliyofanyika kwenye viwanja wa Chuo cha Taaluma ya Urekebishaji, Ukonga jijini Dar es salaam leo Juni 2, 2018.
Kamishna Jenerali wa Magereza, Dkt Juma Malewa akikagua gwaride maalum katika hafla ya uvishaji vyeo kwa Maafisa Waandamizi wa Jeshi la Magereza.
Baadhi ya Maafisa Wastaafu na waliopo sasa wa Jeshi la Magereza wakifuatilia hafla fupi ya uvishaji vyeo kama inavyoonekana katika picha. 
Kamishna Jenerali wa Magereza, Dkt. Juma Malewa(wa tatu kulia) akiwa katika picha ya pamoja na Maofisa Waandamizi wa Jeshi la Magereza waliowavalisha vyeo hivyo kwa niaba ya Rais John Pombe Magufuli ambapo hafla hiyo imefanyika katika viwanja vya Chuo cha Taaluma ya Urekebishaji, Ukonga jijini Dar es salaam Juni, 8, 2018
(Picha zote na Jeshi la Magereza)

Na Mwandishi wetu,

KAMISHNA Jenerali wa Magereza nchini, Dkt. Juma Malewa, kwa niaba ya Amiri jeshi mkuu Rais John Magufuli amewavisha vyeo maafisa wa ngazi ya juu 9 wa Jeshi la Magereza waliopandishwa vyeo hivyo hivi karibuni na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Miongoni mwa maafisa 9 waliovishwa vyeo ni manaibu kamishna wa magereza - DCP wanne wa Jeshi hilo ambao wamepandishwa vyeo na kuwa Makamishna wa magereza, huku makamishna wasaidizi waandamizi wa Magereza -SACP watano wakipandishwa vyeo kuwa Manaibu Kamishna - DCP wa Jeshi hilo.

Waliovishwa vyeo kuwa Makamishna wa Magereza ni Naibu Kamishna wa Magereza Uwesu Ngarama, Boharia Mkuu wa Jeshi la Magereza, Naibu Kamishna wa Magereza Tusekile Mwaisabila, Mkuu wa Divisheni ya Huduma za Urekebishaji, Naibu Kamishna wa Magereza Augustine Mboje, Mkuu wa Magereza Mkoa wa Dar es Salaam pamoja na Naibu Kamishna wa Magereza Gideon Nkana ambaye ni  Mkuu wa Chuo cha Taaluma ya Urekebishaji Ukonga, Dar es Salaam.

Wengine waliovishwa vyeo kuwa Manaibu Kamishna wa Magereza ni  Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Magereza, Julius Sang’udi, Mkuu wa Magereza Mkoa wa Dodoma, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Magereza, Afwilile Mwakijungu, Mkuu wa Magereza Mkoa wa Iringa, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Magereza, John Masunga, Mkuu wa Magereza Mkoa wa Tanga, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Magereza, Phaustine Kasike, Mkuu wa Kitengo cha Parole pamoja na Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Magereza, Jeremiah Katungu ambaye ni Katibu Ofisi ya Kamishna Jenerali wa Magereza.

Akizungumza mara baada ya kuwavisha vyeo Maafisa hao wa magereza(Ijumaa, Juni 8, 2018) katika hafla ya kuwavisha vyeo hivyo iliyofanyika kwenye viwanja vya Chuo cha Taaluma ya Urekebishaji Tanzania (TCTA), Ukonga, jijini Dar es Salaam,  Kamishna Jenerali wa Magereza, Dkt. Juma Malewa amewataka makamishna hao wa Jeshi la magereza wa ngazi zote kuendelea kufanya kazi kwa weledi, uadilifu  sambamba na kusimamia haki na usawa katika utekelezaji wa majukumu yao kila siku.

Aidha, Jenerali Malewa amemshukru Amiri jeshi mkuu Rais John Magufuli kwa kuwapandishwa vyeo maafisa hao ambao watajaza nafasi mbalimbali za juu za uongozi ndani ya Jeshi la Magereza kwani kwa muda mrefu safu ya juu ya uongozi ilikuwa na upungufu mkubwa wa kada ya maafisa wa vyeo hivyo hali iliyopelekea kuathiri utendaji kazi wa Jeshi hilo.

Maafisa hao kabla ya kuvishwa vyeo hivyo walivyotunukiwa  na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kuanzia Juni 02, 2018, walipata fursa ya kula kiapo cha Tamko la Ahadi ya Uadilifu kwa Viongozi wa Umma mbele ya katibu wa sekretarieti ya maadili ya viongozi wa umma.

Tuesday, April 24, 2018

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI


MSAMAHA WA RAIS KWA WAFUNGWA KATIKA KUADHIMISHA MIAKA 54
YA MUUNGANO WA TANZANIA TAREHE 26 APRILI, 2018

Katika kuadhimisha Miaka 54 ya Muungano wa Tanzania tarehe  26 Aprili, 2018 Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutumia madaraka aliyopewa chini ya Ibara ya 45(1)(d) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ametoa msamaha kwa wafungwa wafuatao:-

(i)      Wafungwa wote wapunguziwe robo (1/4) ya adhabu zao baada ya punguzo la kawaida la moja ya tatu (1/3) linalotolewa chini ya Kifungu 49(1) cha Sheria ya Magereza Sura ya 58, wafungwa hao  sharti wawe wametumikia robo (1/4) ya adhabu zao gerezani isipokuwa wafungwa walioorodheshwa katika Ibara ya 2(i – xxi).

(ii)        Wafungwa wagonjwa wenye magonjwa kama UKIMWI, Kifua kikuu (TB) na Saratani (Cancer) ambao wako kwenye “terminal stage”. Wafungwa hawa wathibitishwe na Jopo la Waganga chini ya Uenyekiti wa Mganga Mkuu wa Mkoa/Mganga Mkuu wa Wilaya.

(iii)       Wafungwa wazee wenye umri wa miaka sabini (70) au zaidi.  Umri huo uthibitishwe na Jopo la Waganga chini ya Uenyekiti wa Mganga Mkuu wa Mkoa/Mganga Mkuu wa Wilaya.

(iv)       Wafungwa wa kike walioingia na mimba gerezani, pamoja na wale walioingia na watoto wanaonyonya na wasionyonya.

(v)         Wafungwa wenye ulemavu wa mwili na akili (Physical disability and mental disability). Ulemavu huo uthibitishwe na Jopo la Waganga chini ya Uenyekiti wa Mganga Mkuu wa Mkoa/Mganga Mkuu wa Wilaya.

2.      Aidha, Msamaha wa Mheshimiwa Rais hautawahusu wafungwa wafuatao:-

(i)              Wafungwa waliohukumiwa adhabu ya kunyongwa au kwa makosa ya kujaribu kuua (attempt to murder).

(ii)       Wafungwa waliohukumiwa adhabu ya kunyongwa na adhabu hiyo kubadilishwa kuwa kifungo cha maisha au kifungo gerezani.

(iii)           Wafungwa waliohukumiwa kifungo cha maisha gerezani.

(iv)    Wafungwa wanaotumikia kifungo kwa makosa ya kujihusisha na usafirishaji na matumizi ya madawa ya kulevya kama vile cocaine, heroin, bhangi n.k.

(v)     Wafungwa wanaotumikia kifungo kwa makosa ya kujihusisha na uombaji na upokeaji au utoaji rushwa.

(vi)      Wafungwa wanaotumikia kifungo kwa makosa ya unyang’anyi na unyang’anyi wa kutumia silaha au kujaribu kutenda makosa hayo (robbery with violence, armed robbery and attempted robbery).

(vii)    Wafungwa wanaotumikia kifungo kwa makosa ya kupatikana na silaha, risasi au milipuko isivyo halali (fire arms, ammunitions and explosives).

(viii)        Wafungwa wanaotumikia kifungo kwa makosa ya shambulio la aibu, kunajisi, kubaka na kulawiti, ukatili dhidi ya watoto au kujaribu kutenda makosa hayo.

(ix)           Wafungwa waliopatikana na hatia na kuhukumiwa kifungo kwa kosa la kuwapa mimba wanafunzi wa Shule za Msingi na Shule za Sekondari na ambao walitenda kosa hilo wakiwa na umri wa miaka kumi na nane (18) na kuendelea.

(x)             Wafungwa wanaotumikia kifungo kwa makosa ya wizi wa magari na pikipiki, uharibifu wa miundombinu au kujaribu kutenda makosa hayo.

(xi)           Wafungwa wanaotumikia kifungo chini ya Sheria ya Bodi ya Parole (Act. No. 25/1994), Sheria ya Huduma kwa Jamii (Act. No. 6/2002) na Kifungo cha Nje {The Prisons (Extra Mural Penal Employment) Regulation}.

(xii)   Wafungwa waliopatikana na hatia na kuhukumiwa kifungo kwa makosa ya kutumia vibaya madaraka yao na kuhujumu uchumi.

(xiii)     Wafungwa waliowahi kupunguziwa kifungo na Msamaha wa Mhe. Rais na bado wangali wanaendelea kutumikia sehemu ya kifungo kilichobaki.

(xiv)     Wafungwa waliopatikana na hatia na kuhukumiwa kwa kosa la kuzuia watoto kupata masomo.

(xv)     Wafungwa waliopatikana na hatia na kuhukumiwa kwa kosa la utekaji wa watoto, kupoka na kufanya biashara ya binadamu (Human Trafficking).

(xvi)    Wafungwa waliopatikana na hatia na kuhukumiwa kwa kosa la kukutwa na viungo vya binadamu.

(xvii)      Wafungwa wanaotumikia vifungo kwa makosa ya kujihusisha kwa namna yoyote ile na nyara za Serikali na ujangili (poachers).

(xviii)    Wafungwa wanaotumikia vifungo kwa makosa ya wizi/ubadhirifu wa fedha za Serikali.

(xix)   Wafungwa wanaotumikia vifungo kwa makosa ya kutoroka au kujaribu kutoroka chini ya ulinzi halali au kusaidia kutendeka kwa makosa hayo na bado wangali wanatumika adhabu hizo.

(xx)          Wafungwa walioingia gerezani baada ya tarehe 7 Aprili, 2018.

(xxi)        Wafungwa waliowahi kufungwa gerezani (warudiaji) na wale wenye makosa ya kinidhamu gerezani.

3.      Wafungwa 3,319 watafaidika na Msamaha huu ambapo 585 wataachiliwa huru tarehe 26 Aprili, 2018 na 2,734 watabaki gerezani kumalizia sehemu ya kifungo kilichobaki baada ya kupewa msamaha huu. Ni mategemeo ya Serikali kwamba watarejea tena katika jamii kushirikiana na wenzao katika ujenzi wa Taifa na kwamba watajiepusha kutenda makosa ili wasirejee tena gerezani.


Maj. Jen. Projestus Rwegasira
KATIBU MKUU - WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI
26 Aprili, 2018