MSAMAHA
WA RAIS KWA WAFUNGWA KATIKA KUADHIMISHA MIAKA 54
YA
MUUNGANO WA TANZANIA TAREHE 26 APRILI, 2018
Katika kuadhimisha Miaka
54 ya Muungano wa Tanzania tarehe 26 Aprili, 2018 Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa
kutumia madaraka aliyopewa chini ya Ibara ya 45(1)(d) ya Katiba ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania ametoa msamaha kwa wafungwa wafuatao:-
(i) Wafungwa wote wapunguziwe
robo (1/4) ya adhabu zao baada ya punguzo la kawaida la moja
ya tatu (1/3) linalotolewa
chini ya Kifungu 49(1) cha Sheria ya Magereza Sura ya 58, wafungwa hao sharti wawe wametumikia robo (1/4)
ya adhabu zao gerezani isipokuwa wafungwa walioorodheshwa katika Ibara ya 2(i –
xxi).
(ii)
Wafungwa wagonjwa
wenye magonjwa kama UKIMWI, Kifua kikuu (TB) na Saratani (Cancer) ambao wako
kwenye “terminal stage”. Wafungwa
hawa wathibitishwe na Jopo la Waganga chini ya Uenyekiti wa Mganga Mkuu wa Mkoa/Mganga Mkuu wa Wilaya.
(iii)
Wafungwa wazee wenye
umri wa miaka sabini (70) au zaidi. Umri
huo uthibitishwe na Jopo la Waganga chini ya Uenyekiti wa Mganga Mkuu wa Mkoa/Mganga Mkuu wa Wilaya.
(iv)
Wafungwa wa kike
walioingia na mimba gerezani, pamoja na wale walioingia na watoto wanaonyonya
na wasionyonya.
(v)
Wafungwa wenye
ulemavu wa mwili na akili (Physical
disability and mental disability). Ulemavu huo uthibitishwe na Jopo la
Waganga chini ya Uenyekiti wa Mganga
Mkuu wa Mkoa/Mganga Mkuu wa Wilaya.
2. Aidha,
Msamaha wa Mheshimiwa Rais hautawahusu wafungwa wafuatao:-
(i)
Wafungwa
waliohukumiwa adhabu ya kunyongwa au kwa makosa ya kujaribu kuua (attempt to murder).
(ii) Wafungwa
waliohukumiwa adhabu ya kunyongwa na adhabu hiyo kubadilishwa kuwa kifungo cha
maisha au kifungo gerezani.
(iii)
Wafungwa
waliohukumiwa kifungo cha maisha gerezani.
(iv) Wafungwa wanaotumikia
kifungo kwa makosa ya kujihusisha na usafirishaji na matumizi ya madawa ya
kulevya kama vile cocaine, heroin,
bhangi n.k.
(v) Wafungwa wanaotumikia
kifungo kwa makosa ya kujihusisha na uombaji na upokeaji au utoaji rushwa.
(vi) Wafungwa wanaotumikia
kifungo kwa makosa ya unyang’anyi na unyang’anyi wa kutumia silaha au kujaribu
kutenda makosa hayo (robbery with
violence, armed robbery and attempted robbery).
(vii) Wafungwa wanaotumikia
kifungo kwa makosa ya kupatikana na silaha, risasi au milipuko isivyo halali (fire arms, ammunitions and explosives).
(viii)
Wafungwa wanaotumikia
kifungo kwa makosa ya shambulio la aibu, kunajisi, kubaka na kulawiti, ukatili dhidi
ya watoto au kujaribu kutenda makosa hayo.
(ix)
Wafungwa
waliopatikana na hatia na kuhukumiwa kifungo kwa kosa la kuwapa mimba wanafunzi
wa Shule za Msingi na Shule za Sekondari na ambao walitenda kosa hilo wakiwa na
umri wa miaka kumi na nane (18) na kuendelea.
(x)
Wafungwa wanaotumikia
kifungo kwa makosa ya wizi wa magari na pikipiki, uharibifu wa miundombinu au
kujaribu kutenda makosa hayo.
(xi)
Wafungwa wanaotumikia
kifungo chini ya Sheria ya Bodi ya Parole (Act. No. 25/1994), Sheria ya Huduma
kwa Jamii (Act. No. 6/2002) na Kifungo cha Nje {The Prisons (Extra Mural Penal
Employment) Regulation}.
(xii) Wafungwa
waliopatikana na hatia na kuhukumiwa kifungo kwa makosa ya kutumia vibaya
madaraka yao na kuhujumu uchumi.
(xiii) Wafungwa waliowahi
kupunguziwa kifungo na Msamaha wa Mhe. Rais na bado wangali wanaendelea
kutumikia sehemu ya kifungo kilichobaki.
(xiv) Wafungwa
waliopatikana na hatia na kuhukumiwa kwa kosa la kuzuia watoto kupata masomo.
(xv) Wafungwa
waliopatikana na hatia na kuhukumiwa kwa kosa la utekaji wa watoto, kupoka na
kufanya biashara ya binadamu (Human Trafficking).
(xvi) Wafungwa
waliopatikana na hatia na kuhukumiwa kwa kosa la kukutwa na viungo vya
binadamu.
(xvii)
Wafungwa wanaotumikia
vifungo kwa makosa ya kujihusisha kwa namna yoyote ile na nyara za Serikali na
ujangili (poachers).
(xviii) Wafungwa wanaotumikia
vifungo kwa makosa ya wizi/ubadhirifu wa fedha za Serikali.
(xix) Wafungwa wanaotumikia vifungo kwa
makosa ya kutoroka au kujaribu kutoroka chini ya ulinzi halali au kusaidia
kutendeka kwa makosa hayo na bado wangali wanatumika adhabu hizo.
(xx)
Wafungwa walioingia gerezani baada ya
tarehe 7 Aprili, 2018.
(xxi)
Wafungwa waliowahi kufungwa gerezani
(warudiaji) na wale wenye makosa ya kinidhamu gerezani.
3. Wafungwa
3,319 watafaidika na Msamaha huu
ambapo 585 wataachiliwa huru tarehe
26 Aprili, 2018 na 2,734 watabaki
gerezani kumalizia sehemu ya kifungo kilichobaki baada ya kupewa msamaha huu.
Ni mategemeo ya Serikali kwamba watarejea tena katika jamii kushirikiana na
wenzao katika ujenzi wa Taifa na kwamba watajiepusha kutenda makosa ili
wasirejee tena gerezani.
Maj.
Jen. Projestus Rwegasira
KATIBU
MKUU - WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI
26 Aprili, 2018