Na
Lucas Mboje - Jeshi la Magereza;
Mkuu
wa Jeshi la Magereza nchini, Kamishna Jenerali Dkt. Juma Malewa,
amesema Jeshi hilo limeanza kufanyia kazi agizo la Rais John Magufuli la kuhakikisha
wanajitosheleza kwa chakula na kulisha wafungwa.
Amesema
hatua hiyo itaondoa utaratibu wa wafungwa kupelekewa chakula kutoka nje, kwa
kuwa watakuwa wanakula wanachokizalisha wakiwa magerezani.
Jenerali
Dkt. Malewa alisema hayo katika mkutano wa maafisa waandamizi wa Jeshi la
Magereza kutoka maeneo mbalimbali kuweka mkakati wa namna ya kufanikisha agizo
hilo la Rais alilolitoa akiwa mkoani Dodoma hivi karibuni.
Rais
Magufuli alilitaka jeshi hilo kuhakikisha linawatumia wafungwa kuzalisha chakula
kwa ajili ya kuwalisha badala ya kutegemea ruzuku ya serikali kwa chakula.
Alisema
kwa sasa Jeshi hilo lina uwezo wa kujitosheleza kwa chakula kwa asilimia 30,
kutokana na vifaa vichache vilivyopo, lakini wanatarajia kupokea na kuongeza
vifaa zaidi yakiwamo matrekta ili kuongeza nguvu zaidi ya uzalishaji na kufikia
asilimia 100 ya kujitosheleza kwa chakula.
“Zoezi
hili halitawezekana kutekelezwa kwa haraka sana, itatuchukua kama miaka miwili
hadi mitatu kulifanikisha, lakini kwa kutumia nguvu kazi tuliyonayo na vifaa,
tutamudu kulitekeleza,” alisema Kamishna Jenerali wa Magereza.
Malewa
alibainisha mkakati wa kuhakikisha Magereza inatumika kama chuo cha mafunzo kwa
kuwafundisha wafungwa mbinu mbalimbali za kilimo ili wote watumike vyema na kwa
ufanisi katika kuboresha sekta ya kilimo.
Hata
hivyo, alikiri kuwapo changamoto ya nguvu kazi kama baadhi ya wafungwa wakiwamo
waliohukumiwa kunyongwa na mahabusu ambao kisheria hawapaswi kuwa nje ya
Magereza, ingawa wanakula magerezani.
Kuhusu
agizo la Rais la kuitaka Magereza kuwa sehemu ya ukuzaji wa uchumi kupitia
sekta ya viwanda, alisema hilo wameanza kulitekeleza kivitendo kwa kuanzisha
kiwanda cha sukari katika Gereza la Mbigiri, kinachojengwa kwa ubia kwa
kushirikiana na mashirika ya Hifadhi za taifa ya NSSF na PPF pamoja na kiwanda
cha viatu kilichopo Magereza Karanga mkoani Kilimanjaro na kwamba kinajengwa
kingine hivyo kuwa viwili eneo moja.
“Tumeshapata
oda za ndani na nje ya nchi, na tukishafunga mashine zaidi za kisasa,
tutazalisha viatu kwa wingi sana,” Alisema Dkt. Malewa.
Mkuu
wa Magereza Mkoa wa Morogoro, SACP. Ramadhani Nyamka, alisema wamejipanga
kutekeleza agizo la Rais kwa kuzalisha kwa wingi, kwani Morogoro ina Magereza
12 na mengi yanajihusisha na uzalishaji wa mazao ya kilimo.
SACP.
Nyamka alisema kutokana na kuwa na ardhi yenye rutuba, maji mengi na
miundombinu yote muhimu ya kilimo, wanaamini wataweza kufanikiwa.
“Katika
Magereza ya Morogoro niseme nguvu kazi inajitosheleza, kwani hatuna wafungwa
waliohukumiwa kunyongwa, kwa hiyo tutatumia fursa ya Morogoro kama ghala la
Taifa la chakula kulima kwa bidii tujitosheleze na ziada tuhudumie maeneo
mengine, yakiwamo mashule,” alisema SACP. Nyamka.
Mrakibu
Mwandamizi wa Magereza, Ramadhani Mkele ambaye ni Mkuu wa Gereza Kuu la Arusha,
alisema pamoja na kutegemea kilimo cha jembe la mkono kwa kuwatumia wafungwa,
wakipata vitendea kazi kama matrekta
wanaweza kupanua zaidi shughuli za kilimo katika gereza hilo.
Kamishna wa Fedha na
Utawala wa Magereza, Gaston Sanga akitoa neno fupi kabla ya kumkaribisha
Kamishna Jenerali wa Magereza kufungua rasmi kikao kazi hicho.
Kamishna
Jenerali wa Jeshi la Magereza, Dkt. Juma Malewa akiongoza Kikao Maalum cha
kujadili mikakati ya utekelezaji wa Jeshi la Magereza kujitosheleza kwa
chakula.
Wajumbe
wa Kikao hicho ambao ni Maafisa Waandamizi wa Jeshi la Magereza wakifuatilia
kwa makini maelekezo kutoka kwa Kamishna Jenerali wa Magereza, Dkt. Juma
Malewa(hayupo pichani).
Washiriki
wa Kikao kazi ambao ni Maafisa Waandamizi wa Jeshi la Magereza wakifanya
maadiliano mbalimbali katika vikundi kama inavyoonekana katika picha.
Kamishna Jenerali wa
Magereza, Dkt. Juma Malewa(katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Wakuu wa
Magereza Mikoa yote Tanzania Bara(waliosimama mstari wa nyuma) mara baada ya
ufunguzi rasmi wa kikao maalum cha kujadili mikakati ya utekelezaji wa Jeshi la Magereza kujitosheleza
kwa chakula. Kikao hicho kimefanyika
kwa siku moja 17 Machi, 2018 Mkoani Morogoro.
Kamishna
Jenerali wa Jeshi la Magereza, Dkt. Juma Malewa, akisalimiana na Kamishna wa Utawala na Fedha wa Magereza, Gaston Sanga mara baada ya kuwasili kwenye viwanja vya
Nanenane, Mkoani Mororogoro tayari kwa Kikao Maalum cha Maafisa Waandamizi wa
Jeshi hilo. Kikao hicho kimefanyika kwa siku moja 17 Machi, 2018 Mkoani
Morogoro.