Banner

Banner

Tuesday, February 4, 2020

NIPENI USHIRIKIANO - KAMISHNA JENERALI MPYA WA MAGEREZA, SULEIMAN MZEE

Na ASP Lucas Mboje, DSM
KAMISHNA Jenerali mpya wa Magereza nchini, Suleiman Mzee (pichani) amewataka Maofisa na askari wote wa Jeshi la Magereza kumpa ushirikiano katika uongozi wake ili aweze kusimamia vyema maelekezo mbalimbali yaliyotolewa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa Jeshi hilo ikiwemo jukukumu la kujitegemea kwa chakula cha wafungwa magerezani.
Akizungumza na Maofisa, askari na watumishi raia wa Jeshi hilo katika Ofisi ndogo za Makao Makuu ya Magereza, jijini Dar es Salaam, Kamishna Jenerali Suleiman Mzee amesema kuwa anayomatarajio makubwa ya kuhakikisha kuwa Jeshi la Magereza linakuwa na miradi mingi ya uzalishaji mali ili kuwezesha kujitegemea badala ya kutegemea bajeti kuu ya Serikali.
“Ni lazima tuzalishe kwa wingi na kila gereza lizalishe kulingana na fursa zilizopo ikiwa tunataka kujiwekea mazingira ya kuaminika. Pia, tuhakikishe kuwa utaalam wetu katika nyanja mbalimbali lazima uwe na manufaa Jeshini”, amesisitiza Jenerali Mzee.
Aidha, Kamishna Jenerali Mzee ameongeza kuwa ni vyema maofisa na askari wa Jeshi hilo wakazingatia utii, uaminifu pamoja na uhodari katika kazi ili kuyafikia matarajio hayo makubwa ndani ya Jeshi.
“Mkizingatia utii, uaminifu pamoja na uhadari katika kazi naamini matokeo chanya yataonekana katika muda mfupi kwani upo uwezekano wa kufanya mambo makubwa ambayo yataliletea heshima na sifa Jeshi letu la Magereza”, amesema Jenerali Mzee.
Kuhusu mafunzo mbalimbali kwa maafisa na askari, amesema kuwa atapitia mitaala ya mafunzo ili kuona kama inaendana na mazingira yaliyopo pamoja na kuifanyia maboresho mbalimbali kwani mafunzo ni nguzo muhimu katika kujenga nidhamu kwa maafisa na askari.
Kwa upande wake aliyekuwa Kamishna Jenerali wa Magereza nchini, Phaustine Kasike(sasa Balozi Mteule) alimpongeza Jenerali Mzee kwa kuteuliwa na Rais kushika nafasi hiyo na alibainisha baadhi ya changamoto ambazo zinalikabili Jeshi hilo ikiwemo uchakavu wa makazi ya askari.
“Nafurahi kuwa naliacha Jeshi la Magereza likiwa na nidhamu ya hali ya juu pamoja na kuwa na baadhi ya changamoto mbalimbali ikiwemo makazi duni ya askari, naamini changamoto hizo utazifanyia kazi kwani tayari tulikwishaanza kuchukua hatua”, amesema Mhe. Balozi Kasike.
Jeshi la Magereza linamiliki ardhi yenye ukubwa wa ekari 326,205 Tanzania Bara, kati ya hizo ekari 151,350 zinafaa kwa shughuli za kilimo na mifugo. Eneo linalotumika kwa shughuli za kilimo kwa sasa ni ekari 20,580 pekee sawa na asilimia 13.60 ya eneo linalofaa kwa shughuli za kilimo. Jeshi hilo likijipanga kimkakati linaweza kujilisha, kuongeza pato serikalini pamoja na kufanya mapinduzi makubwa ya kilimo hapa nchini.

MAPOKEZI YA KAMISHNA JENERALI MPYA WA MAGEREZA OFISI NDOGO YA MAKAO MAKUU YA MAGEREZA, JIJINI DAR

Kamishna Jenerali mpya wa Magereza, Suleiman Mzee akipokea salaam ya heshima toka  Gwaride Maalum lililoandaliwa na Maofisa na askari wa Jeshi la Magereza(hawapo pichani) kwa ajili yake kwa heshima katika Ofisi ndogo ya Makao Makuu ya Magereza, Jijini             Dar es Salaam.

Kamishna Jenerali  mpya wa Magereza, Suleiman Mzee akikagua Gwaride Maalum lililoandaliwa na Maofisa na askari wa Jeshi la Magereza kwa ajili yake kwa heshima kama inavyoonekana katika picha.

Kamishna Jenerali  mpya wa Magereza, Suleiman Mzee  akisalimiana na aliyekuwa Kamishna Jenerali wa Magereza, Phaustine Kasike (sasa Balozi mteule) alipowasili Makao Makuu ya Jeshi hilo baada ya kuapishwa rasmi kuwa Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza, Ikulu Jijini Dar es Salaam Februari 3, 2020. Kulia ni Kamishna wa Utawala na Rasilimali Watu wa Jeshi hilo, Uwesu Ngarama.

Kamishna Jenerali  mpya wa Magereza, Suleiman Mzee akifanya mahojiano maalum na wanahabari baada ya kuwasili katika Ofisi ndogo za Makao Makuu ya Jeshi la Magereza jijini Dar es Salaam.

Kamishna Jenerali  mpya wa Magereza, Suleiman Mzee akiongea na Maafisa, Askari na Watumishi raia wa Jeshi la Magereza baada ya kutoka kuapishwa kuwa Kamishna Jenerali wa Jeshi hilo, Ikulu Jijini Dar es Salaam Februari 3, 2020.

Baadhi ya Maafisa na Askari wa Jeshi la Magereza wakimsikiliza Kamishna Jenerali mpya wa Ma gereza, Suleiman Mzee mara baada ya kutoka kuapishwa kuwa Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza leo, Ikulu Jijini Dar es Salaam Februari 3, 2020                         (Picha zote na Jeshi la Magereza).

Thursday, January 2, 2020

JESHI LA MAGEREZA LAJIPANGA KIMKAKATI KUZALISHA CHAKULA CHA WAFUNGWA KWA MWAKA 2020



Kamishna Jenerali wa Magereza, Phaustine Kasike akiongoza Baraza Maalum la kufunga mwaka 2019 na kuukaribisha mwaka mpya 2020. Baraza hilo limehudhuriwa na Maafisa na Askari kutoka Ofisi ya Makao Makuu ya Magereza Dodoma pamoja na vituo mbalimbali vya Magereza Mkoani humo. Baraza hilo limefanyika  Desemba 31, 2019 katika Ukumbi wa Gereza Kuu Isanga, Dodoma.

Na ASP Lucas Mboje, Dodoma;

JESHI la Magereza limejipanga kwa mwaka 2020 kuendelea na utekelezaji wa jukumu la uzalishaji wa chakula cha kutosha cha wafungwa kwa kutumia rasilimali zilizopo katika Jeshi hilo ili kufikia adhma ya Serikali ya awamu ya tano kuhusu kujitosheleza kwa chakula cha wafungwa magerezani.

Akizungumza na Maafisa na askari wa Jeshi hilo katika Baraza Maalum la kufunga mwaka 2019 na kuukaribisha mwaka mpya 2020 leo jijini Dodoma, Kamishna Jenerali wa Magereza nchini, Phaustine Kasike amesema kuwa Jeshi hilo tayari limejiwekea mkakati maalum wa kujitosheleza kwa chakula cha wafungwa magerezani.

Katika kulifanyia kazi suala hilo, Kamishna Jenerali Kasike amesema kuwa mavuno yameongezeka katika msimu wa kilimo 2018/2019 ambapo Jeshi hilo limeweza kuzalisha chakula cha wafungwa katika magereza kumi(10) ya kimkakati(Songwe, Mollo, Ludewa, Arusha, Pawaga, Idete, Kitete, Isupilo, Kitai na Kitengule).

“Kupitia Shirika la Uzalishaji Mali la Magereza(SHIMA), Jeshi limeweza kulisha unga wa mahindi kwa wahalifu magerezani kwa kipindi cha mwaka mzima katika mikoa ya Lindi, Ruvuma, Mtwara, Rukwa, Njombe na Katavi. Aidha, katika mikoa mingine Shirika limeweza kulisha unga kwa miezi mitatu hadi sita”, amesema Kamishna Jenerali Kasike.

Ameongeza kuwa kuna mkakati wa muda mrefu wa kuanzisha kilimo cha umwagiliaji kwa kutumia vyanzo vya maji vilivyopo katika maeneo mbalimbali ya magereza ambapo Jeshi hilo tayari limekamilisha andiko linalohusu mapindizi ya kilimo na tayari limewasilishwa serikalini katika hatua mbalimbali za ngazi ya maamuzi.

Akizungumzia mafanikio mengi ya kujivunia kwa mwaka 2019 Kamishna Jenerali Kasike amesema kuwa kumekuwa na mwitikio mkubwa miongoni mwa maafisa na askari katika kuishi na ajenda mahususi ya Jeshi hilo kuhusu umuhimu wa kubadilika kimtizamo, kifikra na utendaji kama nguzo ya mabadiliko katika Jeshi hilo.

“Naomba nisistize kuwa bado tuendelee kuishi na ajenda hii ya mabadiliko ya kimtizamo na kifikra katika mwaka mpya 2020 tunaoutarajia kuuanza muda mfupi ujao kwa kufanya kazi kwa weledi, ubunifu katika maeneo yetu ya kazi. Tradition die hard”, amesisitiza Kamishna Jenerali Kasike.

Mafanikio mengine aliyoyaainisha ni pamoja na utekelezaji wa agizo la Serikali kuhusu kujitosheleza kwa chakula cha wafungwa, ujenzi wa nyumba za watumishi wa Jeshi hilo katika maeneo mbalimbali nchini kwa njia ya ubunifu, udhibiti wa uingizaji wa vitu visivyoruhusiwa magerezani kwa kufunga CCTV camera katika baadhi ya magereza. Aidha, katika kuhakikisha kuwa wafungwa waliopo magerezani wanafanya kazi, Jeshi kupitia Shirika lake limefanikiwa kupata  leseni ya usajili ya kuwatumia wafungwa katika kandarasi mbalimbali ikiwemo kufanya usafi katika Barabara zilizopo nchini na shughuli nyinginezo za kuweza kuliingizia faida Shirika hilo.

“Shirika la Magereza limefanikisha utaratibu wa kuingiza miradi yake yote katika mfumo wa kielektroniki wa ukusanyaji wa mapato ya Serikali(GePG) na hivyo kuziba mianya ya upotevu wa mapato ya Serikali. Pia, Shirika hilo limeweza kutoa mchango wake Serikalini kiasi cha Tsh. Milioni mia moja na therasini kwa mwaka 2019”, ameainisha Kamishna Jenerali Kasike.

Aidha, pamoja na mafanikio hayo Kamishna Jenerali Kasike amebainisha changamoto zinazolikabili Jeshi hilo ikiwemo ufinyu wa bajeti, uhaba wa vitendea kazi mbalimbali kama vile magari, vyombo vya mawasiliano, pia changamoto za makazi na uchache wa nguvu kazi ya maafisa na askari katika Jeshi hilo.

Kamishna Jenerali wa Magereza nchini, Phaustine Kasike amehitimisha hotuba yake leo jijini Dodoma kwa kuwatakia heri ya mwaka mpya 2020 maafisa, askari pamoja na watumishi wote wa Jeshi hilo na amewataka kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia misingi ya kazi, Dira na Dhima ya Jeshi hilo.