Na ASP Lucas Mboje, DSM
KAMISHNA Jenerali mpya wa Magereza
nchini, Suleiman Mzee (pichani) amewataka
Maofisa na askari wote wa Jeshi la Magereza kumpa ushirikiano katika uongozi
wake ili aweze kusimamia vyema maelekezo mbalimbali yaliyotolewa na Rais Dkt.
John Pombe Magufuli kwa Jeshi hilo ikiwemo jukukumu la kujitegemea kwa chakula
cha wafungwa magerezani.
Akizungumza
na Maofisa, askari na watumishi raia wa Jeshi hilo katika Ofisi ndogo za Makao
Makuu ya Magereza, jijini Dar es Salaam, Kamishna Jenerali Suleiman Mzee amesema
kuwa anayomatarajio makubwa ya kuhakikisha kuwa Jeshi la Magereza linakuwa na
miradi mingi ya uzalishaji mali ili kuwezesha kujitegemea badala ya kutegemea
bajeti kuu ya Serikali.
“Ni
lazima tuzalishe kwa wingi na kila gereza lizalishe kulingana na fursa zilizopo
ikiwa tunataka kujiwekea mazingira ya kuaminika. Pia, tuhakikishe kuwa utaalam
wetu katika nyanja mbalimbali lazima uwe na manufaa Jeshini”, amesisitiza Jenerali
Mzee.
Aidha,
Kamishna Jenerali Mzee ameongeza kuwa ni vyema maofisa na askari wa Jeshi hilo
wakazingatia utii, uaminifu pamoja na uhodari katika kazi ili kuyafikia
matarajio hayo makubwa ndani ya Jeshi.
“Mkizingatia
utii, uaminifu pamoja na uhadari katika kazi naamini matokeo chanya yataonekana
katika muda mfupi kwani upo uwezekano wa kufanya mambo makubwa ambayo yataliletea
heshima na sifa Jeshi letu la Magereza”, amesema Jenerali Mzee.
Kuhusu
mafunzo mbalimbali kwa maafisa na askari, amesema kuwa atapitia mitaala ya
mafunzo ili kuona kama inaendana na mazingira yaliyopo pamoja na kuifanyia
maboresho mbalimbali kwani mafunzo ni nguzo muhimu katika kujenga nidhamu kwa maafisa
na askari.
Kwa
upande wake aliyekuwa Kamishna Jenerali wa Magereza nchini, Phaustine
Kasike(sasa Balozi Mteule) alimpongeza Jenerali Mzee kwa kuteuliwa na Rais
kushika nafasi hiyo na alibainisha baadhi ya changamoto ambazo zinalikabili
Jeshi hilo ikiwemo uchakavu wa makazi ya askari.
“Nafurahi
kuwa naliacha Jeshi la Magereza likiwa na nidhamu ya hali ya juu pamoja na kuwa
na baadhi ya changamoto mbalimbali ikiwemo makazi duni ya askari, naamini
changamoto hizo utazifanyia kazi kwani tayari tulikwishaanza kuchukua hatua”,
amesema Mhe. Balozi Kasike.
Jeshi
la Magereza linamiliki ardhi yenye ukubwa wa ekari 326,205 Tanzania Bara, kati
ya hizo ekari 151,350 zinafaa kwa shughuli za kilimo na mifugo. Eneo
linalotumika kwa shughuli za kilimo kwa sasa ni ekari 20,580 pekee sawa na
asilimia 13.60 ya eneo linalofaa kwa shughuli za kilimo. Jeshi hilo likijipanga
kimkakati linaweza kujilisha, kuongeza pato serikalini pamoja na kufanya
mapinduzi makubwa ya kilimo hapa nchini.