Na Lucas Mboje, Dar es Salaam;
KATIBU Mkuu Wizara ya Mambo ya
ndani ya Nchi, Meja Jenerali Projest Rwegasira(pichani) amewataka
Maafisa na Askari wote wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama katika Wizara ya
Mambo ya ndani ya Nchi kudumisha nidhamu wanapokuwa wakitekeleza
majukumu ya kazi za kila siku.
Meja Jenerali Rwegasira ameyasema
hayo leo katika hafla ya ufungaji Mafunzo ya Uongozi wa ngazi za juu kwa
Maafisa wa Jeshi la Magereza yaliyofanyika katika Chuo cha Taaluma ya
Urekebishaji Ukonga, Dar es Salaam.
"Katika muda mfupi niliofanya
kazi katika Wizara hii nimeambiwa kuna watumishi wanakataa kwenda
kwenye vituo vipya kwasababu ya kutopatiwa fedha za uhamisho, huo ni
utovu wa nidhamu," Alisema Jenerali Rwegasira.
Alisisitiza
Mtumishi anapopatiwa uhamisho ndani ya Jeshi jambo la kwanza ni Utii
kwanza wa Utekelezaji wa Amri hiyo na siyo sababu au madai mengine
ambayo ni kinyume na Utendaji wa Taasisi za Kijeshi.
Kwa upande
wake Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza nchini, CGP. John Casmir
Minja alisema Jeshi hilo limeitikia wito wa kubana matumizi kama
inavyosisitizwa na Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Mhe. Joseph
Pombe Magufuli ndiyo maana katika hafla hiyo imehusisha Maafisa wachache
wa Gwaride ili kupunguza gharama zisizo za Msingi.
"Katika
Sherehe za kufunga Mafunzo ya Uongozi kwa mwaka huu Gwaride limepunguzwa
kwa kujumuisha Maafisa na Askari wachache zaidi na pia hata Wageni
Waalikwa utaona wamekua ni wachache sana ili kuitikia wito wa Rais wa
Awamu ya tano kama anavyosisitiza kupunguza matumizi yasiyoyalazima"
Alisema Kamishna Jenerali John Casmir Minja.
Aidha, alisema Chuo
hicho kina changamoto kadhaa ikiwa ni pamoja na uchakavu wa Miundombinu
baada ya kupewa hadhi ya kuwa Chuo cha Taaluma ya Urekebishaji na kwamba
anaamini Serikali ya awamu ya tano itazifanyia kazi changamoto hizo.
Hata
hivyo Kamishna Jenerali Minja aliwapongeza wahitimu hao kwa kuchangia
Tsh. Milioni 2.4 kwaajili ya kuboresha miundombinu ya chuo hicho kwa
ridhaa yao ambapo walichangishana fedha hiyo ili kuboresha hali ya chuo
hicho.
Jumla ya Wahitimu 98 wa Mafunzo ya Uongozi ngazi za Juu
wamehitimu Kozi hiyo na kutunukiwa cheo cha Mrakibu Msaidizi wa Magereza
ambapo Idadi hiyo inajumuisha Wahitimu 93 kutoka Tanzania Bara ikiwa
Wanaume ni 83 na Wanawake 10 pamoja na Wahitimu 05 kutoka Vyuo vya
Mafunzo Zanzibar ambao ni Wanaume 04 na Mwanamke 01.