Banner

Banner

Tuesday, October 4, 2016

SHIRIKA LA MAGEREZA NA MFUKO WA PPF WAINGIA UBIA WA UJENZI WA KIWANDA KIPYA CHA VIATU HAPA NCHINI

Kamishna Jenerali wa Magereza, CGP- John Casmir Minja(kulia) akizungumza katika hafla fupi ya utiwaji saini wa Mkataba wa wa Uwekezaji  wa Kiwanda cha Viatu cha Gereza Karanga, Moshi baina ya Shirika la Magereza na Mfuko wa Jamii wa PPF(kushoto) ni Mkurugenzi Mkuu wa PPF Bw. William Erio, Oktober 4, 2016.
Mkurugenzi Mkuu wa PPF Bw. William Erio(kushoto) na Kamishna Jenerali wa Magereza, CGP- John Casmir Minja(kulia) kwa pamoja wakisaini Mkataba wa Uwekezaji baina ya Taasisi hizo mbili katika Ukumbi wa Mkao Makuu ya Jeshi la Magereza, Jijini Dar salaam, Oktoba 4, 2016.
Kamishna Jenerali wa Magereza, CGP- John Casmir Minja(kulia) na Mkurugenzi Mkuu wa PPF Bw. William Erio  wakibadilishana nyaraka mbalimbali za Makubaliano katika Mkataba huo kama inavyoonekana katika picha.
Mkurugenzi Mkuu wa PPF Bw. William Erio na Kamishna Jenerali wa Magereza, CGP- John Casmir Minja(kulia) wakionesha nyaraka mbalimbali baada ya hafla fupi ya utiwaji saini wa Mkataba wa ujenzi wa Kiwanda kipya cha Viatu.
Maafisa Waandamizi kutoka Makao Makuu ya Mfuko wa Jamii wa PPF wakifuatilia utiwaji saini wa Mkataba wa Uwekezaji.
Maafisa Waandamizi wa Jeshi la Magereza wakishuhudia utiwaji wa Mkataba huo kama inavyoonekana katika picha
(Picha zote na Lucas Mboje wa Jeshi la Magereza).

Na Lucas Mboje wa Jeshi la Magereza,
Jeshi la Magereza nchini kupitia Shirika lake la uzalishaji mali (Prisons Corporation Sole) limeingia Makubaliano na Mfuko wa Jamii wa PPF katika ujenzi na uboreshaji wa mradi wa Kiwanda cha Viatu cha Gereza Kuu Karanga – Moshi, Mkoani Kilimanjaro.
 
Makubaliano hayo yamefanyika leo Jumanne 04 Oktoba, 2016 katika Ukumbi wa Mikutano ulioko Makao Makuu ya Jeshi la Magereza Jijini Dar es salaam.
 
Akizungumza na Maafisa Waandamizi wa Jeshi la Magereza pamoja na Wanahabari, Kamishna Jenerali wa Magereza nchini, John Minja amesema uhirikiano huo unalenga kuliimarisha Shirika la Magereza ili liweze kujiendesha kibiashara pamoja na kuchangamkia fursa mbalimbali za kibiashara.
 
Kamishna Jenerali Minja ameongeza kuwa uwekezaji katika kiwanda hicho utalisaidia Jeshi la Magereza kufikia kiu ya kuzalisha bidhaa za ngozi zenye ubora wa hali ya juu na zinazochochea ushindani katika soko la ndani na nje.
 
“Naamini uwekezaji huu wa Kiwanda kipya cha Viatu cha Karanga Moshi ni ishara tosha ya kuunga mkono dhamira ya dhati ya Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli ya kutaka Tanzania mpya ya Viwanda inawezekana hivyo kutimiza malengo na Dira ya Taifa ya Uchumi wa Viwanda ifikapo mwaka 2025”. Alisema Kamanda Minja.
 
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Jamii wa PPF, Bw. William Erio amesema kuwa PPF ipo tayari kwa dhati kushirikiana na Shirika la Magereza katika mradi huo wa ujenzi wa Kiwanda cha Viatu kwani yapo mahitaji makubwa ya bidhaa hiyo ya ngozi hapa nchini.

“Makubaliano haya yanahusisha ujenzi wa Kiwanda kipya cha viatu pamoja na uwekezaji wa mashine za kisasa za kutengenezea bidhaa za ngozi katika Kiwanda cha Viatu cha Karanga Moshi kinachomilikiwa na Jeshi la Magereza”. Alisema Bw. Erio
 
Pia, aliongeza kuwa uwekezaji huo utawezesha Vyombo vyote vya Ulinzi na Usalama hapa nchini kununua sare za viatu na vifaa vingine vya bidhaa za ngozi zitakazozalishwa katika Kiwanda hicho badala ya kuagiza nje ya nchi.
 
Mkakati wa Jeshi la Magereza hivi sasa ni kuendelea kuboresha maeneo mbalimbali pamoja na kuchangamkia fursa zilizopo ili kuhakikisha kuwa linafikia ufanisi unaotarajiwa katika utekelezaji wa majukumu yake.