Na Lucas Mboje, Dodoma
VYAMA vya ushirika
nchini vimetakiwa kuendelea kutoa elimu ya ushirika mara kwa mara kwa wanachama
wake ili kujenga uelewa wakutosha kuhusu sheria, kanuni na masharti mbalimbali
ya ushirika.
Akizungumza
katika Mkutano Mkuu wa sita wa mwaka wa Chama cha Ushirikia wa Akiba na Mikopo
cha Watumishi wa Jeshi la Magereza nchini, Kaimu Mrajisi wa Vyama vya Ushirika
nchini, Bw. Philemon Chilewa ametoa rai hiyo kwa vyama vya ushirika nchini
kuendelea kutoa elimu ya ushirika kwani ni muhimu katika uendeshaji wa shughuli
za chama.
Amesema
kuwa elimu ya ushirika isitolewe tu kwa watendaji na viongozi wa chama bali
itolewe kwa wanachama wa ushirika ili wajue uendeshaji wake na kunufaika na
huduma zitolewazo na chama.
“Vyama
vingi vya ushirika hapa nchini vimekufa kwa kukosa elimu ya ushirika, niwaombe
sana wasimamizi wa ushirika muendelee kutoa elimu kwa wanachama”. Amesisitiza
Kaimu Mrajis Chilewa.
Aidha,
Kaimu Mrajis Chilewa amewaasa Magereza SACCOS pamoja na Saccos zote nchini
kufanya shughuli zake kwa kufuata sheria ya ushirika pamoja na kuheshimu na
kusikiliza maoni ya wanachama kwani wao ndo wenye mali.
Ameongeza
kuwa kwakuwa Mkutano huo utahusisha uchaguzi wa mjumbe mmoja wa Bodi, Bw.
Philemon Chilewa pia amewaasa wajumbe wa Mkutano huo kuwa makini katika
uchaguzi huo kwa kuchagua mtu mwenye weledi na mwenye mapenzi ya dhati na
ushiriki wao ili aweze kutimiza majukumu yanayokusudiwa.
Awali,
akimkaribisha Mgeni rasmi katika Mkutano huo, Mlezi wa Magereza Saccos, ambaye
ni Kamishna Jenerali wa Magereza nchini – CGP Phaustine Kasike amesema kuwa
idadi ya wanachama imeongezeka hadi kufikia wanachama zaidi ya 13,000 ikiwa na
mtaji wa zaidi ya bilioni 20 hivi sasa.
Pia,
Mlezi wa Magereza Saccos, CGP Kasike ameongeza kuwa pamoja na changamoto za
mabadiliko ya kiuchumi, kumekuwa na ushindani mkubwa wa Taasisi za kifedha
katika kutoa huduma za mikopo kwa wanachama.
Chama
cha Ushirikia wa Akiba na Mikopo cha Watumishi wa Jeshi la Magereza nchini
kilianzishwa mwaka 2005 kwa lengo la kupunguza umasikini na kuinua hali ya
maisha ya watanzania hususani watumishi wa Jeshi la Magereza.