Banner

Banner

Tuesday, October 30, 2018

SACOSS NCHINI ZAASWA KUENDELEA KUTOA ELIMU YA USHIRIKA KWA WANACHAMA


Na Lucas Mboje, Dodoma

VYAMA vya ushirika nchini vimetakiwa kuendelea kutoa elimu ya ushirika mara kwa mara kwa wanachama wake ili kujenga uelewa wakutosha kuhusu sheria, kanuni na masharti mbalimbali ya ushirika.

Akizungumza katika Mkutano Mkuu wa sita wa mwaka wa Chama cha Ushirikia wa Akiba na Mikopo cha Watumishi wa Jeshi la Magereza nchini, Kaimu Mrajisi wa Vyama vya Ushirika nchini, Bw. Philemon Chilewa ametoa rai hiyo kwa vyama vya ushirika nchini kuendelea kutoa elimu ya ushirika kwani ni muhimu katika uendeshaji wa shughuli za chama.

Amesema kuwa elimu ya ushirika isitolewe tu kwa watendaji na viongozi wa chama bali itolewe kwa wanachama wa ushirika ili wajue uendeshaji wake na kunufaika na huduma zitolewazo na chama.

“Vyama vingi vya ushirika hapa nchini vimekufa kwa kukosa elimu ya ushirika, niwaombe sana wasimamizi wa ushirika muendelee kutoa elimu kwa wanachama”. Amesisitiza Kaimu Mrajis Chilewa.

Aidha, Kaimu Mrajis Chilewa amewaasa Magereza SACCOS pamoja na Saccos zote nchini kufanya shughuli zake kwa kufuata sheria ya ushirika pamoja na kuheshimu na kusikiliza maoni ya wanachama kwani wao ndo wenye mali.

Ameongeza kuwa kwakuwa Mkutano huo utahusisha uchaguzi wa mjumbe mmoja wa Bodi, Bw. Philemon Chilewa pia amewaasa wajumbe wa Mkutano huo kuwa makini katika uchaguzi huo kwa kuchagua mtu mwenye weledi na mwenye mapenzi ya dhati na ushiriki wao ili aweze kutimiza majukumu yanayokusudiwa.

Awali, akimkaribisha Mgeni rasmi katika Mkutano huo, Mlezi wa Magereza Saccos, ambaye ni Kamishna Jenerali wa Magereza nchini – CGP Phaustine Kasike amesema kuwa idadi ya wanachama imeongezeka hadi kufikia wanachama zaidi ya 13,000 ikiwa na mtaji wa zaidi ya bilioni 20 hivi sasa.

Pia, Mlezi wa Magereza Saccos, CGP Kasike ameongeza kuwa pamoja na changamoto za mabadiliko ya kiuchumi, kumekuwa na ushindani mkubwa wa Taasisi za kifedha katika kutoa huduma za mikopo kwa wanachama.

Chama cha Ushirikia wa Akiba na Mikopo cha Watumishi wa Jeshi la Magereza nchini kilianzishwa mwaka 2005 kwa lengo la kupunguza umasikini na kuinua hali ya maisha ya watanzania hususani watumishi wa Jeshi la Magereza.