Na Mwandishi Wetu
Jeshi la Magereza nchini limeokoa jumla ya Shilingi Bilioni 11, ikiwa
ni gharama ya chakula cha wafungwa tangu lianze kujitegemea kwa
chakula ikiwa ni maelekezo ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli ya
kulitaka jeshi hilo litumie nguvu kazi ya wafungwa ilionao kuzalisha
chakula.
Akizungumza leo katika ziara ya Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya
Nchi,iliyofanyika katika Makao Makuu Mapya ya Jeshi hilo ,Msalato
jijini Dodoma, Kamishna Jenerali wa Magereza, Suleiman Mzee amesema
walikuwa wanatumia Shilingi Bilioni Moja kila mwezi kulipa wazabuni wa
chakula waliokuwa wanaliuzia chakula jeshi hilo.
“Sasa hivi tunajitegemea asilimia kubwa kwa chakula, Serikali kabla ya
mwezi wa tatu mwaka jana kila mwezi kulikua kuna deni la Bilioni Moja,
lakini baada ya mwezi huo wa tatu sasa tunaokoa kiasi hicho cha fedha
shilingi bilioni moja na mpaka sasa tuna miezi kumi na moja
tunajilisha wenyewe kupitia shirika la magereza” alisema CGP Mzee
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Naibu Waziri, Khamis Hamza Chilo
alilipongeza Jeshi la Magereza kwa kutekeleza vyema agizo la Rais
Magufuli ikiwa sambamba na ujengaji wa kiwanda kikubwa cha samani
ambapo mpaka kukamilika kwake kitagharimu shilingi Bilioni
1,101,743,123/=
“Niwapongeze kwa hatua mbalimbali za maendeleo ambazo zingine
nimeshuhudia mwenyewe,lakini kubwa kuweza kujitegemea kwa chakula cha
wafungwa hali iliyopelekea kuokoa kiasi kikubwa cha fedha ambacho
kinabaki humu humu ndani na mnakitumia kwa shughuli zingine za
maendeleo hongereni sana” alisema Naibu Waziri Chilo
Kamishna Jenerali wa Magereza Mej. Jen. S.M Mzee akielezea jambo kwa Naibu Waziri wa mambo ya ndani ya Nchi Mh. Khamis Hamza Chilo (MB) wakati wa Ziara ya Kikazi Makao Makuu ya Jeshi la Magereza Jijini Dodoma jana tarehe 15 Jan, 2021.
Kamishna Jenerali Suleiman M. Mzee (kushoto akimpa taarifa fupi Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani Mh. Khamis Hamza Chilo alipotembelea Makao Makuu ya Magereza Jijini Dodoma.
Naibu waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mh. Khamis Hamza Chilo (MB) akipanda Mti mbele ya Ofisi ya Ofisi ya Makao Makuu Ya Magereza eneo la Msalato Jijini Dodoma.
Naibu waziri wa Mambo ya Ndani Mh. Khamis Chilo akitoa maelekezo alipotembelea Makao Makuu ya Magereza sehem ya Kiwanda cha Samani Msalato jijini Dodoma.
Mrakibu msaidizi wa Magereza Malima akifafanua jambo mbele ya Naibu waziri wa Mambo ya ndani ya Nchi Mh. Khamis Chilo katika Mashine za Kiwanda cha Samani Msalato jijini Dodoma.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mh. Khamis Chilo (kushoto,mbele) akipokewa na Mwenyeji wake Kamishna Jenerali wa Magereza Mej. Jen. Suleiman Mzee ( kulia, mbele) alipotembelea Makoa Makuu ya Magereza katika ziara ya kikazi jijini Dodoma jana.
Naibu waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mh. Khamis Chilo akikagua gwaride la heshima lilioandalia kwa ajili yake wakati wa Ziara ya kikazi Makao makuu ya Magereza Jijini Dodoma.