Mkuu wa Jeshi la Magereza Nchini (CGP Yoram Katungu Novemba 23, 2024 alifanya kikao kazi na wakuu wa Magereza Mikoa yote Tanzania bara na kuwataka wakuu hao kutokuwa na makundi, mivutano na migongano mahala pa kazi na kuhimiza Umoja, Ushirikiano na Upendo ili kuwa na mwelekeo mmoja kama Jeshi.
CGP. Katungu, alisisitiza masuala mbalimbali ya kiutendaji ikiwemo programu za mfungwa anapoingia gerezani afanyiwe tathmini ya kina ili kugundua uwezo wake na kumpangia program ya kumfaa katika kufanikisha suala la Urekebishaji kwa mfungwa husika na pindi anapokaribia kumaliza kifungo chake, aandaliwe kisaikolojia namna bora ya kwenda kuishi na jamii ukizingatia kwasasa Jeshi linafanya mapitio ya Sheria ya kuwafuatilia wafungwa pindi wanapokuwa wamemaliza vifungo vyao.
Kwa upande wake Mkuu wa Divisheni ya Fedha na Mipango Kaimu Kamishna wa Magereza (DCP) Chacha Bina, alipongeza wakuu wa Magereza kwa jitihada zao za kuhakikisha maduhuli ya serikali yanapatikana kwa wakati na kuvuka malengo ya kukusanya maduhuli hayo akisisitiza kuwa maduhuli si takwa la Mkuu wa Jeshi, bali ni agizo la Serikali.
Katika kikao kazi hicho wakuu wa Divisheni, Vitengo na Sehemu waliwasilisha mada mbalimbali.