Banner

Banner

Thursday, February 27, 2025

WAFUNGWA 118 KUNUFAIKA NA MPANGO WA PAROLE


Mwenyekiti wa Bodi ya Taifa ya Parole  Mhe. Balozi Khamis Kagasheki Feberuari 20, 2025 aliongoza kikao cha 52 cha  Bodi ya Taifa ya Parole kilichofanyika kwa muda wa siku mbili katika Ukumbi wa Corridor Springs Hotel jijini Arusha ambapo 
wajumbe wamejadili na kupendekeza wafungwa ambao wana sifa ya kunufaika na mpango wa Sheria ya Parole.

Pia Mhe. Kagasheki alisema kuwa wafungwa waliojadiliwa wameshatumikia sehemu ya kifungo chao gerezani na kifungo kilichobaki wataenda kumalizia wakiwa na familia zao na jamii kama Sheria ya Parole inavyotaka.

''Bodi imepitia kwa umakini majalada 132 na kuona kama vigezo, Kanuni, taratibu na Sheria zimefuatwa  hivyo basi Bodi imeamua kuwa wafungwa 118 wanastahili kunufaika na mpango huo wa Parole'' Alisema Kagasheki.

Kwa upande wake Mkuu wa Jeshi la Magereza nchini (CGP) Jeremiah Yoram Katungu ametoa rai kwa jamii na wananchi kwa ujumla kushirikiana kwa pamoja na Jeshi la Magereza kuwapokea Wafungwa ambao wanatarajia kutoka gerezani kwa mpango wa Parole, nakusema kuwa Wafungwa hawa wamejirekebisha kitabia na mienendo yao wakiwa gerezani.

Pamoja na mambo mengine CGP Katungu alisema kuwa utaratibu wa Parole umewekwa kwa mujibu wa Sheria na umeainisha vigezo ambavyo vinatakiwa kuzingatiwa ili mfungwa aweze kunufaika na mpango huo, akivitaja vigezo hivyo ikiwemo urefu wa kifungo chake, tabia na mwenendo wake akiwa gerezani, lakini kama jamii nayo iko tayari kumpokea, hayo yote yanazingatiwa wakati Bodi inamjadili mfungwa huyo ili aweze kupendekezwa kwa utaratibu wa Parole.

Kikao hicho cha 52 cha Bodi ya Taifa ya Parole kimejadili jumla ya majalada 132, na majalada 118 yamekidhi vigezo vya mpango huo.