Banner

Banner

Friday, November 9, 2018

KAMISHNA JENERALI WA MAGEREZA AASA JAMII KUACHA KUTENDA UHALIFU ILI KUPUNGUZA MSONGAMANO MAGEREZANI


Na Lucas Mboje, Iringa;

KAMISHNA Jenerali wa Jeshi la Magereza Magereza nchini, Phaustine Kasike ametoa rai kuwa ili kupunguza msongamano magerezani ni vema jamii ikaacha kufanya matukio mbalimbali ya uhalifu hapa nchini.

Rai hiyo imetolewa leo na Kamishna Jenerali Kasike wakati akitoa ufafanuzi mbele ya wanahabari wa Mkoani Iringa kuhusu madai ya uwepo wa msongamano wa wafungwa katika magereza mbalimbali yaliyopo nchini ambapo ameeleza kuwa si kweli kwamba magereza yote yana msongamano bali msongamano uliopo magerezani ni kwenye baadhi ya magereza yenye kuhifadhi mahabusu.

Amesema suala la msongamano limekuwa ni tatizo kubwa ambapo takwimu za Jeshi la Magereza zinaonesha kuwa idadi ya mahabusu waliopo magerezani ni wengi na hali hiyo inatokana na wingi wa matukio ya uhalifu kwenye eneo husika na kule ambako hakuna uhalifu mwingi basi nako kwenye magereza hakuna msongamano mkubwa wa wafungwa/mahabusu.

Ameongeza kuwa Jeshi la Magereza litaendelea kushirikiana na vyombo vya haki jinai ikiwemo Jeshi la Polisi, Mahakama na Ofisi ya DPP ili kuhakikisha kuwa kunakuwa na usukumaji wa kesi mbalimbali za mahabusu waliopo magerezani.

“Tutajitahidi kuendelea kushirikiana kwa pamoja katika jukwaa letu la haki jinai ili kuangalia namna bora zaidi ya kuweza kutatua tatizo la ucheleweshaji wa kesi za mahabusu waliopo magerezani”. Amesema Jenerali Kasike.

Kuhusu uhamisho wa Gereza Iringa kwenda eneo la la Mlolo, Kamishna Jenerali Kasike amesema tayari Jeshi hilo limekwishaanza kutekeleza maelekezo ya Serikali ambapo hivi sasa lipo katika mchakato wa kuhamishwa kadri hali ya kibajeti itakavyoruhusu.

“Tumekwishaanza ufyatuaji wa tofali za ujenzi wa nyumba za maafisa na askari sambamba na ujenzi wa mabweni ya wafungwa unaendelea katika eneo hilo hivyo Gereza Iringa litahamishiwa katika eneo la Mlolo ili kupisha huduma za kijamii”. Amesisitiza Jenerali Kasike.

Mkuu wa Jeshi la Magereza nchini, CGP. Phaustine Kasike yupo mkoani Iringa  kwa ziara ya kikazi ambapo leo ametembelea magereza ya Iringa na Pawaga. Ziara hizi ni mwendelezo wa ziara zake  za kikazi zenye lengo la kukagua magereza yote Tanzania Bara na kuzungumza na Maafisa na askari pamoja na kujua changamoto mbalimbali wanazokutana nazo wakati wakitekeleza majukumu yao.
Kamishna Jenerali wa Magereza, Phaustine Kasike akiwasili katika Gereza la Iringa leo Novemba 9, 2018 tayari kwa ziara yake ya kikazi yenye lengo la kukagua shughuli mbalimbali za uendeshaji wa Jeshi hilo.

Kamishna Jenerali wa Magereza, Phaustine Kasike akikagua moja la ghala la kuhifadhia mpunga unaozalishwa katika Gereza la Kilimo Pawaga.

. Kamishna Jenerali wa Magereza, Phaustine Kasike akizungumza na Mahabusu na Wafungwa wa Gereza Iringa(hawapo pichani) alipofanya ziara ya kikazi leo Novemba 9, 2018.

Kamishna Jenerali wa Magereza, Phaustine Kasike akikagua maandalizi ya shamba ya kilimo cha mpunga katika eneo la Gereza la Pawaga Mkoani Iringa. Gereza Pawaga limepewa malengo ya kulima ekari 375 za mpunga ili kuwezesha mpango wa kujitosheleza kwa chakula cha wafungwa.

Mkuu wa Magereza Mkoa wa Iringa, Kamishna Msaidizi wa Magereza, Hassan Mkwanda akimuongoza Kamishna Jenerali wa Magereza, Phaustine Kasike kutembelea maeneo mbalimbali ya Gereza la Wilaya Iringa.

Askari wa vyeo mbalimbali wa Gereza Pawaga wakifuatilia kwa makini maelekezo ya Kamishna Jenerali wa Magereza alipotembelea gereza hilo leo Novemba 9, 2018.

Kitalu cha mbegu za mpunga ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya Kilimo mpunga katika eneo la Gereza la Pawaga Mkoani Iringa. Gereza Pawaga limepewa malengo ya kulima ekari 375 za mpunga ili kuwezesha mpango wa kujitosheleza kwa chakula cha wafungwa. (Picha na Jeshi la Magereza).

MKUU WA JESHI LA MAGEREZA NCHINI, CGP PHAUSTINE KASIKE AANZA ZIARA YA KIKAZI MKOANI IRINGA

Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Iringa, ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Iringa Mjini, Mhe. Richard Kasesela akisalimiana na Mkuu wa Jeshi la Magereza nchini (CGP) Phaustine Kasike walipokutana  Mkoani Iringa alipotembelea Ofisi za Mkuu wa Mkoa kabla ya kuendelea na ziara yake ya kikazi, leo Novemba 8, 2018.

   Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Iringa, ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Iringa Mjini, Mhe. Richard  Kasesela(watatu toka kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na  Kamishna Jenerali wa Magereza nchini, Phaustine Kasike(wa tatu toka kulia) pamoja na wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Iringa.


Mkuu wa Jeshi la Magereza nchini (CGP) Phaustine Kasike (kushoto) akizungumza na Mkuu wa Magereza Mkoa wa Iringa,  Kamishna Msaidizi wa Magereza (ACP) Hassan Mkwanda na Maafisa wengine wa Magereza Mkoani Iringa, muda mfupi alipowasili leo Novemba 8, 2018 Mkoani humo. CGP Kasike yupo mkoani humo kwa ziara ya kikazi yenye lengo la kukagua magereza yote ya Mkoa wa Iringa na kuzungumza na Maafisa na askari pamoja na kujua chamgamoto mbalimbali wanazokutana nazo wakati wakitekeleza majukumu yao.
Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Iringa wakisalimiana na Mkuu wa Jeshi la Magereza Nchini (CGP) Phaustine Kasike walipokutana  Mkoani Iringa alipotembelea Ofisi za Mkuu wa Mkoa kabla ya kuendelea na ziara yake ya kikazi.
Baadhi ya Askari wa Gereza la Wilaya Iringa wakifuatilia maelekezo katika Baraza lililoongozwa na  Kamishna Jenerali wa Magereza nchini, Phaustine Kasike ambapo askari hao wameelezea changamoto zao kiutendaji leo Novemba 8, 2018.
Mkuu wa Magereza Mkoa wa Iringa,  Kamishna Msaidizi wa Magereza (ACP) Hassan Mkwanda  akimkaribisha Kamishna Jenerali wa Magereza Nchini (CGP) Phaustine Kasike(katikati meza kuu) ili azungumze na baadhi ya Maafisa na askari wa Gereza Iringa(hawapo pichani, leo Novemba 8, 2018 . Kulia ni  ACP. Josephine Semwenda ambaye hivi karibuni ameteuliwa kuwa Mkuu wa Magereza Mkoa  wa Lindi ( Picha na Jeshi la Magereza).


Wednesday, November 7, 2018

KAMISHNA JENERALI WA MAGEREZA - CGP. PHAUSTINE KASIKE AFANYA MABADAILIKO MAKUBWA YA WAKUU WA MAGEREZA MIKOA TANZANIA BARA

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Katika kuboresha utendaji kazi ndani ya Jeshi la Magereza Kamishna Jenerali wa Magereza nchini, Phaustine Martin Kasike amefanya mabadiliko makubwa  ya kiuongozi kwa kuwateua  Wakuu wa Magereza wa Mikoa Tanzania Bara(RPOs) 19 wapya na saba (7) kuwabakiza katika nyadhifa zao.

Katika mabadiliko hayo  Kamishna Jenerali Kasike ameteuwa na kuthibitisha maafisa sita (6) kuwa Wakuu wa Vyuo vya Magereza  na kuwabadilisha maafisa wengine watatu (3) katika vitengo muhimu ndani ya Jeshi hilo.

Aidha, Kamishna Jenerali Kasike katika mabadiliko hayo  kwa mara ya kwanza amewateua Wakuu wa  Magereza wa Mikoa katika mikoa ya Katavi, Songwe, Njombe, Simiyu na Geita ambayo ilikuwa haina uongozi wa kimagereza katika ngazi ya mikoa hiyo.

Katika mabadiliko hayo ni pamoja na aliyekuwa RPO (DSM) SACP. Hamis Nkubasi ambaye amehamishiwa Makao Makuu ya Magereza kitengo cha Ujenzi na nafasi yake kuchukuliwa na SACP. Julius Ntambala, SACP. Salum Hussein RPO (Dodoma) amebakia katika kituo chake na aliyekuwa Mkuu wa Chuo Kiwira SACP. Luhende Makwaia anakwenda kuwa RPO (Mbeya) na nafasi yake kuchukuliwa na ACP. Mathias Mkama na aliyekuwa RPO (Mbeya) SACP. Kijida Mwakingi amehamishiwa Makao Makuu, Kitengo cha TEHAMA.

Aliyekuwa RPO (Mtwara) SACP. Ismail Mlawa amehamishiwa Makao Makuu ya Magereza Kitengo cha Mipango na nafasi yake kuchukuliwa na ACP. Varisanga Msuya aliyekuwa Kaimu Bohari Mkuu wa Jeshi ambapo nafasi yake inachukuliwa na ACP. Robert Masali ambaye anakuwa Boharia Mkuu wa Jeshi la Magereza. Aliyekuwa RPO (Mwanza) SACP. Athuman Kitiku amehamishiwa Makao Makuu ya Magereza sehemu ya Utumishi na nafasi yake kuchukuliwa na SACP. Hamza Hamza aliyekuwa RPO Tabora.

Aidha, ACP. Joseph Mkude anakuwa RPO (Tabora) na aliyekuwa  RPO (Kagera) SACP. Boyd Mwambingu amehamishiwa Makao Makuu Kitengo cha Utawala na nafasi yake inachukuliwa na ACP. Rymond Mwampashe. Aliyekuwa RPO (Lindi) SACP. Rajabu Bakari  amehamishiwa Makao Makuu Kitengo cha Mawasiliano na Usafirishaji na nafasi yake kuchukuliwa na ACP. Josephine Semwenda.

Aliyekuwa RPO (Rukwa) SACP. Benno Hunja amehamishiwa Makao Makuu sehemu ya Kilimo, Mifugo na Mazingira na nafasi yake  inachukuliwa na ACP. Jail Mwamgunda na aliyekuwa RPO (Kilimanjaro) SACP. Hassan Mkwiche amehamishiwa Makao Makuu kuwa Mkuu wa Kitengo cha Afya, Tiba na Lishe na nafasi yake kuchukuliwa na ACP. Rajab Igongi. Aliyekuwa Mkuu wa Kitengo cha Afya, Tiba na Lishe ACP. Wilson Rugamba anakuwa RPO (Shinyanga).

 Pia, Aliyekuwa RPO (Morogoro) SACP. Mzee Nyamka amehamishiwa Makao Makuu kuwa Mkuu wa Kitengo cha Utafiti na Takwimu na nafasi yake inachukuliwa na ACP. Stylvester Mrema. Aliyekuwa Kaimu RPO (Mara) ACP. Benezeth Bisibe amehamishiwa Makao Makuu kuwa Mdhibiti wa Fedha (FC) na nafasi yake inachukuliwa na ACP. Hospitius Adrian. Mkuu wa Mkuu wa Chuo KPF ACP. Lazaro Nyanga anabakia katika nafasi hiyo, ACP. Anthony Sogoseye anabakia kuwa Mkuu wa Shule ya Sekondari Bwawani. Aliyekuwa Msaidizi wa Mkuu wa chuo Ruanda SSP. Enock Mwanguku anakuwa Mkuu wa Chuo hicho.

Aidha, waliokuwa Kaimu RPOs, Vyuo na maeneo mengine ambao sasa wamethibitishwa ni kama ifuatavyo:- ACP. Hasseid Mkwanda (Iringa), ACP. Anderson Kamtearo (Arusha), ACP. Emmanuel Lwinga (Tanga), ACP. Masudi Kimolo (Manyara), ACP. Joel Matani (Mkuu wa Chuo cha Taaluma ya Urekebishaji), ACP. Rehema Ezekiel (Pwani), ACP. Msepwa Omary (Singida), na SP. Ally Uwesu (Mkuu wa Kikosi Maalum cha Magereza).

Walioteuliwa kuwa RPOs katika mikoa mipya ni ACP. Alexander Mmassy (Katavi), ACP. Lyzecky Mwaseba (Songwe), ACP. Festo Ng’umbi (Njombe), ACP. Robert Rumanyika (Geita) na ACP. Andulile Mwasampeta (Simiyu). Wakati huo huo ACP. Alexander Nyefwe anakuwa RPO (Ruvuma) na ACP. Leonard Burushi anakuwa RPO (Kigoma) kufuatia waliokuwa RPO katika mikoa hiyo kustaafu kazi kwa mujibu wa sheria.


Maafisa wengine waandamizi walioko Makao Makuu ambao wamepangiwa majukumu mengine ni SACP. Bertha Minde anakuwa Mkuu wa Kitengo cha Parole na SACP. Chacha Jackson ambaye anakuwa Mkuu wa Kitengo cha Huduma za Mahabusu.


Kwa mujibu wa Kamishna Jenerali Kasike Maafisa wote waliohamishiwa Makao Makuu wanatakiwa kuripoti Makao Makuu ya Jeshi la Magereza jijini Dodoma.



Imesainiwa na; Mrakibu Msaidizi wa Magereza, Deodatus Kazinja – Ofisa Habari,
Makao Makuu ya Jeshi la Magereza,
DAR ES SALAAM,
07 Novemba, 2018.