Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Meja Jenerali Projest
Rwegasira(katikati) katika Jukwaa akipokea Salaam kutoka kwa Gwaride la
Wahitimu wa Mafunzo ya Awali ya Uaskari Magereza(hawapo pichani) katika
hafla ya kufunga Mafunzo hayo leo Julai 9, 2016 Chuo cha Magereza,
Kiwira Mbeya. Kushoto ni Kamishna Jenerali wa Magereza, CGP- John Casmir
Minja.
Mgeni rasmi
ambaye ni Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Meja Jenerali
Projest Rwegasira akikagua Gwaride la Wahitimu wa Mafunzo ya Awali ya
Uaskari Magereza, Kozi Na. 28 ya Mwaka 2016.
Wahitimu wa Mafunzo ya Awali ya Uaskari Magereza, Kozi Na. 28 ya Mwaka
2016 wakila kiapo cha Utii kwa Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi
na Usalama ambaye ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kama
inavyoonekana katika picha wakiwa wakakamavu.
Mgeni rasmi akimkabidhi cheti cha sifa mmoja wa Askari Wahitimu ambaye
amefanya vizuri zaidi katika nyanja ya Nidhamu katika kipindi chote cha
Mafunzo hayo.
Gadi Maalum ya Gwaride la kunyakua iliyoundwa na Wahitimu wa Mafunzo ya
Awali ya Uaskari Magereza wakitoa heshima mbele ya Jukwaa la Mgeni rasmi
ambaye ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi(hayupo
pichani).
Maafisa Waandamizi wa Jeshi la Magereza wakifuatilia kwa karibu Maonesho
mbalimbali katika Uwanja wa Gwaride kwenye hafla ya kufunga Mafunzo
hayo.
Wakufunzi kutoka Kikosi Maalum cha Kutuliza Ghasia Magerezani(KMKGM)
wakionesha onesho la kijasiri kama inavyoonekana katika picha.
Kamishna Jenerali
wa Magereza, CGP - John Casmir Minja akitoa maelezo mafupi kabla ya
kumkaribisha Mgeni rasmi kutoa hotuba yake ya kufunga rasmi kwa Mafunzo
ya Awali ya Uaskari Magereza katika Chuo cha Magereza, Kiwira Mbeya.
Kamishna Jenerali wa Magereza, CGP - John Casmir Minja(wa
pili kulia)akiwa ameongozana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani
ya Nchi(wa pili kushoto) mara baada ya sherehe za kufunga Mafunzo ya
Awali ya Uaskari Magereza, Chuo cha Magereza, Kiwira Mbeya(wa kwanza
kulia) ni Mkuu wa Chuo cha Magereza - Kiwira, SACP. Stanford
Ntirundura(Picha zote na Lucas Mboje wa Jeshi la Magereza).
Na; Lucas Mboje, Rungwe
JUMLA
ya Wahitimu 1364 wa Mafunzo ya Awali ya Uaskari Magereza wamehitimu
kuwa Askari kamili wa Jeshi hilo ambapo kati yao wanaume ni 977 na
wanawake 377, Mafunzo hayo yamefungwa rasmi Julai 9, 2016 katika Chuo
cha Magereza Kiwira, Wilayani Rungwe Mkoani Mbeya.
Akizungumza
katika sherehe za kufunga Mafunzo hayo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo
ya Ndani ya Nchi, Meja Jenerali Projest Rwegasira amesema Askari wote wa
Jeshi la Magereza nchini wanatakiwa kufanya kazi kwa kuzingatia Misingi
ya Haki za Binadamu na Utawala Bora kila wakati wanapotekeleza majukumu
yao ya kazi.
Aidha,
Meja Jenerali Rwegasira amewataka Askari wahitimu wakazingatie elimu
waliyopewa wakati wa mafunzo ili kuwezesha kuongezeka kwa ufanisi katika
majukumu ya Jeshi la Magereza.
Sambamba
na hilo, amewaasa kudumisha nidhamu mahala pa kazi kwani nidhamu ndiyo
msingi wa kufanikisha utendaji kazi mahala pa kazi hususani katika
Taasisi za Kijeshi.
"Hivyo
ili kudumisha utendaji wenu wa kazi, mnapaswa kuzingatia nidhamu katika
utekelezaji wenu wa majukumu yenu kulingana na maelekezo mtakayokuwa
mnapewa". Alisisitiza Meja Jenerali Rwegasira.
Akizungumza
kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi Kamishna Jenerali wa Magereza nchini,
John Casmir Minja amesema kuwa changamoto nyingi ambazo kwa kiasi
fulani zimeathili utekelezaji wa majukumu ya Jeshi hilo ni pamoja na
ufinyu wa bajeti, makazi duni ya maafisa na askari, uhaba wa vitendea
kazi na uchakavu wa vyombo vya usafiri.
Kamishna
Jenerali Minja ameongeza kuwa tayari Jeshi hilo limechukua hatua
mbalimbali za kufanya maboresho kwa lengo la kufanya Jeshi la Magereza
kuwa la kisasa katika kutekeleza majukumu yake kisayansi na kwa ufanisi
unaotarajiwa.