Banner

Banner

Thursday, July 28, 2016

WAZIRI MKUU MAJALIWA AKABIDHI HUNDI YA TSH. 85 MILIONI KWA JESHI LA MAGEREZA ZITAKAZOTUMIKA KUTENGENEZEA MADAWATI, JIJINI DAR‏

Waziri Mkuu wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa akimkabidhi mfano wa hundi Afisa Mwandamizi wa Jeshi la Magereza, SACP. John Masunga(kushoto) leo Julai 28, 2016 katika Viwanja vya Shule ya Msingi Chamazi. Waziri Mkuu amelekeza Fedha hizo zitumike kutengeneza madawati ya shule za msingi Majimatitu na Mbande zilizopo Wilayani Temeke.
Waziri Mkuu wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa akiwa ameketi kwenye madawati yaliyotolewa kwa Msaada wa Ubalozi wa Kuwait Nchini Tanzania kama inavyoonekana katika picha(Picha na Lucas Mboje wa Jeshi la Magereza).

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa(Mb) amekabidhi hundi ya Tsh. 85 Milioni kwa Uongozi wa Jeshi la Magereza  ili litengeneze jumla ya madawati  1,703 yatakayotumika katika Shule za Msingi za Majimatitu na Mbande zilizopo Wilaya ya Temeke, Jijini Dar es Salaam.

Hafla ya makabidhiano hayo  yamefanyika  leo tarehe 28 Julai, 2016 katika Viwanja vya Shule ya Msingi Chamazi iliyopo Wilaya ya Temeke, Jijini Dar es salaam ambapo Waziri Mkuu Majaliwa  amekabidhi madawati katika Shule ya Msingi Chamazi yaliyotolewa na Ubalozi wa Kuwait nchini Tanzania na Jumuiya ya Mabohora Tanzania kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri Mkuu Majaliwa  amewashukuru na kuwapongeza Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa kutoa mchango huo na pia amewapongeza wadau wengine ambao wameitikia wito wa Rais Magufuli wa kuchangia madawati kwa lengo la kuondoa tatizo la wanafunzi kukaa chini.

Waziri Mkuu Majaliwa  amesema baada ya kuanza kutekeleza ahadi ya kuondoa ada kwa shule za msingi na sekondari, idadi ya wanafunzi waliojiandikisha kuanza darasa la kwanza katika shule mbali mbali imeongezeka hali iliyosababisha upungufu wa madawati lakini tatizo hilo limetatuliwa kwa kiasi kikubwa hapa nchini.

Aidha,  amelitaka na Jeshi la Magereza kutengeneza madawati hayo mapema iwezekanavyo ili yakamilike haraka na kuanza kutumika katika Shule za Msingi Majimatitu na Mbande kwani shule hizo zinakabiliwa na idadi kubwa ya Wanafunzi hapa Jijini Dar es Salaam.

Hafla hiyo imehudhuriwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Augustine Mahiga, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Ramadhani Mwinyi, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Paul Makonda, Wakuu wa Wilaya zote za Mkoa wa Dar es Salaam, Wakurugenzi wote wa Halmashauri za Mkoa wa Dar es Salaam, Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Dar es Salaam, Wananchi pamoja na wanafunzi wa Shule ya msingi Chamazi.

Lucas Mboje, Mrakibu Msaidizi wa Magereza,
Afisa Habari wa Jeshi la Magereza,
Makao Makuu ya Jeshi la Magereza,
28 Julai, 2016.