Banner

Banner

Friday, December 4, 2015

Magereza kuhamasisha utalii wa ndani katika miaka 54 ya uhuru wa Tanganyika

Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza John Minja akiwasilia katiki viwanja vya Magereza Mkoa wa Kilimanjaro kwa ajili ya hafla ya kukabishi bendera kwa watumishi 39 wa Jehi hilo wanaotarajia kuadhimisha miaka 54 ya Uhuru wa Tanganyika kwa kupanda Mlima Kilimanjaro.
Kamishna Jenerali wa Magereza John Minja akikabidhi bendera ya Magereza kwa kiongozi wa Msafara Kamishna Msaidizi wa Magereza Alexander Mmasy leo tarehe 04/12/2015 wakiwa wanajiandaa kupanda Mlima tarehe 06/12/2015 ili ifikapo tarehe 09 siku ya Uhuru wa Tanganyika wawe kileleni
Kamishna Jenerali  wa Jeshi la Magereza John Minja akitoa nasaha kwa wapanda mlima wa Jeshi la Magereza (Hawapo pichani)
Baadhi ya wadau wa Magereza Utalii Klabu walio tayari kupanda Mlima Kilimanjaro wakisikiliza kwa makini nasaha za Kamishna Jenerali wa Magereza John Minja katika hafla ya kukabidhiwa bendera ya Jeshi hilo kuipeleka katika Kilele cha Mlima huo.
Baadhi ya wadau wa Magereza Utalii Klabu walio tayari kupanda Mlima Kilimanjaro wakiimba nyimbo za hamasa baada ya kupokea bendera kutoka kwa Kamishna Jenerali wa Magereza John Minja katika hafla ya kukabidhiwa bendera ya Jeshi hilo kuipeleka katika Kilele cha Mlima huo.
Wapanda Mlima Kilimanjaro wa Jeshi la Magereza wakiwa katika picha ya pamoja na Mkuu wa Jeshi la Magereza  John Minja (Katikati),wa tatu kulia ni Mkuu wa Magereza Mkoa wa Arusha SACP Hamis Nkubasi, na Mkuu wa Magereza Mkoa wa Kilimanjaro SACP Venant Kayombo,  wa tatu kushoto ni Mnadhimu Mkuu wa Magereza Mkoa
Baadhi ya wapanda mlima Kilimanjaro walipojumuika na watumishi wa Magereza Mkoa wa Kilimanjaro katika kupata kifungua kinywa katika hafla fupi ya kukabidhiwa bendera kwa watumishi hao wanaotarajia kupanda mlima ifikapo tarehe 06/12/2015
Mmoja wa waongozaji utalii Mkoani Kilimanjaro akitoa maelezo mafupi kwa wapanda Mlima ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya awali kabla ya kupanda.
Wadau wa Magereza Utalii Klabu wakiwa katika mazoezi mbalimbali ya kukimbia na kutembea katika viunga vya mji wa Moshi ikiwa ni maandalizi ya kuelekea katika kilele cha Mlima Kilimanjaro ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha miaka 54 ya Uhuru wa Tanganyika sambamba na kuamasisha utalii wa ndani.
Baada ya mazoezi ya kutembea na kukimbia hufuatiwa na mazoezi ya viuongo ikiwa ni maandalizi ya kuelekea katika kilele cha Mlima Kilimanjaro ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha miaka 54 ya Uhuru wa Tanganyika sambamba na kuamasisha utalii wa ndani.



Picha zote na Mrakibu Msaidizi wa Magereza Deodatus Kazinja na Koplo Mfaume Abdalah wa Jeshi la Magereza

Na Deodatus Kazinja
Katika kuadhimisha miaka 54 ya uhuru wa Tanganyika tarehe 9 Desemba  watumishi  wapatao 39 Jeshi la Magereza wakiwa katika uwiano wa wanaume 30 na wanawake 9  wataadhimisha siku hiyo kwa kupanda mlima Kilimanjaro na kutembelea Mamlaka ya Hifadhi ya Bonde la Ngorongoro.

Washiriki hawa wanatoka katika vituo vya Makao Makuu ya Magereza, Chuo cha Taaluma ya urekebishaji Ukonga Dar es salaam,  Kikosi Maalum cha Kutuliza Gasia Magereza (KMKGM), Pwani, Dar es salaam, Iringa, Mbeya, Mara, Tabora, Tanga, Kilimanjaro na Arusha ambao kwa gharama zao wameamua kuadhimisha miaka 54 ya uhuru wa Tanganyika kwa kufanya utalii wa ndani.

Akiongea na waandishi wa habari Kamishna Jenerali wa Magereza nchini John Casmir Minja katika hafula fupi ya kuwakabidhi bendera watumishi hao katika viwanja vya Magereza Mkoa wa Kilimanjaro amesema amefurahishwa mno na uamuzi wa askari hao kwa vile unalitangaza Jeshi la Magereza nje ya mipaka yake.

Kamishna Minja alisema pia mbali na kulitangaza Jeshi la Magereza unawaweka timamu watumishi hao katika kufanya kazi  zao vizuri ikiwa ni kuunga kauli mbiu ya serikali ya Awamu ya Tano ya Hapa Kazi tu.

Aidha Kamishna  huyo alitumia fursa hiyo kuishukuru serikali kwa namna ambavyo imekuwa ikijitolea kulisaidia Jeshi la Magereza ambapo alitoa taarifa kuwa tayari mikataba ya kununuliwa magari yapatayo 905 na ujenzi wa nyumba za watumishi zipatazo 9500 imesainiwa na magari yataanza kuingia mapema Januari 2016.

Kwa upande wake mwenyekiti wa Magereza Utalii Klabu ambaye pia ni Mhasibu Mkuu wa Jeshi la Magereza Ndugu Estomih Hamis mbali na kumshuruku Kamishna Minja akwa namna ambavyo amejitolea katika kufanikisha uanzishwaji wa Klabu hiyo kuelezea dhima nzima ya utalii huo.

 “ Tumeamua kuadhimisha miaka 54 ya uhuru wa Tanganyika kwa mfumo huu  kwa sababu kadhaa. Mosi , ni kuunga mkono jitihada za serikali  za muda mrefu za kuhamasisha utalii wa ndani ambacho ni chanzo kimojawapo cha kuongeza mapato ya ndani ya serikali”

“Pili, ni kuleta mwamko kwa  watumishi wa umma na watanzania kwa ujumla katika kutembelea vivutio vya utalii vya ndani kuliko ilivyo sasa ambapo sehemu kubwa ya watalii ni wageni kutoka nje ya Tanzania”

Aidha, ndugu Hamis aliongeza kuwa zoezi  la upandaji mlima Kilimanjaro ni zuri kwa kuimarisha afya za watumishi hivyo kujiepusha na magonjwa kama vile kisukari, shinikizo la damu na utimamu wa mwili na hasa kwa askari wanaotakiwa kuwa hivyo muda wote.

Tukio la watumishi wa Magereza kupanda mlima Kilimanjaro  litakuwa ni la pili kwa mwaka huu ambapo mara ya mwisho walipanda mlima tarehe 6 March, 2015 wakiwa ni jumla ya watumishi 20 ambapo 16 walifanikiwa kufika kileleni na wanne kurudia njiani kwa sababu mbalimbali.

Zoezi la upandaji mlima lililopita lilifanyika kwa mafanikio makubwa kiasi cha kuibua hoja y wa unndwaji wa chombo cha pamoja kinachoweza kuratibu shughuli za utalii ndani ya Jeshi la Magereza kwa kuwaunganisha watumishi wote.

Hoja hiyo ilifanikiwa kwa kuundwa kwa Klabu ya Utalii ya Magereza, klabu ambayo iko katika hatua za mwisho za usajili. Tayari Klabu hiyo inao viongozi wakiongozwa na Mwenyikiti ndugu Hamis, katibu wake akiwa ni Mkaguzi wa Magereza Dominick Mshana na Mweka Hazina ni Mrakibu Msaidizi wa Magereza Erasto Kipingu.

Nani analipa gharama za utalii huo?
Akijibu swali hilo katibu wa Klabu hiyo Mkaguzi Mshana alisema kwa hivi sasa watumishi hao wanapanda kwa gharama zao wenyewe kutoka katika mishahara yao ambapo karibu kila mshiriki amechanga wastani wa shilingi 300,000.

Mshana amesema ni matumaini yake kuwa katika siku za mbeleni kama watapatikana wadhamini gharama hizo zinaweza kupungua sana kutoka mifukoni mwa washiri.

Aidha amesema gharama za kupanda mlima na kutembelea vivutio vingine kwa ujumla ni kubwa kwa mtu mmoja mmoja lakini kunakuwa na unafuu mkubwa watu wakipanda kama kikundi.